Dec 8, 2015

TAARIFA KWA UMMA JUU YA UENDELEZAJI WA UFUKWE WA OYSTERBAYUfukwe wa Oysterbay unaanzia katika eneo la Police Officers Mess hadi Barabara ya Kenyatta, upande wa Mashariki wa Barabara ya Toure. ambapo ndani ya ufukwe huo kuna eneo maarufu linaloitwa Coco Beach.
Kwa muda mrefu sana, ufukwe huo umekuwa ukitumiwa na wananchi wengi wa Jiji la Dar es Salaam kwa ajili ya kujipumzisha, kuogelea na wakati mwingine kufanyia mazoezi ya viungo ikiwamo mazoezi ya kutembea.

Hivi karibuni kumeibuka taarifa potofu katika vyombo mbali mbali vya habari kuwa Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni imeuza Ufukwe wa Oysterbay.

Ukweli ni kuwa katika kuiboresha fukwe hiyo, mnamo mwaka 2007 Halmashauri iliingia mkataba na Kampuni ya Q-Consult iliyopewa masharti ya kuiendeleza fukwe hiyo, lakini ilishindwa kutimiza masharti ya uendelezaji, hali iliyopelekea Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni kusitisha mkataba huo
.
Baada ya kusitishwa kwa mkataba, Kampuni hiyo ya Q-Consult ilifungua shauri Mahakama Kuu Kitengo cha Ardhi, na Mahakama ikampa ushindi Q-Consult
.
Kwa kutoridhishwa na uamuzi huo, Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni ilianza taratibu za kukata rufaa Mahakama ya Rufani, kwa kuwasilisha nyaraka za awali kama notisi ya kukata rufaa, kuwasilisha nyaraka za kuomba kibali cha kukata rufaa na kuandika barua ya kuomba kupatiwa nyaraka zote za kukata rufaa, ikiwa ni pamoja na hukumu na mwenendo wa shauri.

DHAMIRA YA HALMASHAURI:

Katika lengo hilo hilo la kuiendeleza fukwe hiyo Halmashauri, kwa kushirikiana na Benki ya TIB wameshaandaa michoro inayoonyesha namna ufukwe huo utakavyokuwa baada ya kutengenezwa.
Ni mchoro unaonyesha kuwa itakuwa ni Open Beach (Ufukwe wa Wazi) kwa wananchi wenye vipato tofauti tofauti kwenda kupumzika, kustarehe na hata kufanya mazoezi mbali mbali.

Ili kutimiza azma ya kuifanya kama ni Open Beach, Halmashauri itagharamia sehemu ya ujenzi huo hasa maeneo ya wazi, pia itashirikisha wadau mbali mbali katika kugharamia ujenzi huo.

Napenda kuwahakikishia wananchi wote kuwa mpango wa uendelezaji wa ufukwe huo nishirikishi na unamtaka kila mdau kutoa maoni yake ili kuondoa dhana potofu kuwa Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni imeuza ufukwe wa Coco Beach ambayo ni sehemu ya ufukwe wa Oysterbay.

Imetolewa na
Eng. Mussa B. Natty
Mkurugenzi wa Manispaa
Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni

0 Weka maoni yako hapa:

Post a Comment

COMMENT HAPA