Sep 21, 2013

Mbeya City yapiga hodi Simba

http://www.mwananchi.co.tz/image/view/-/2001462/highRes/583777/-/maxw/600/-/7uuqu2z/-/mbeya.jpg
KIKOSI CHA MBEYA CITY

Sosthenes Nyoni, Vicky Kimaro, Mwananchi Dar es Salaam. : Simba inashuka leo kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam kukabiliana na Mbeya City , lakini inafahamu kwamba inahitaji pointi tatu ili iweze kujiimarisha kileleni mwa msimamo wa Ligi Kuu soka Tanzania Bara.
Wekundu hao wa Msimbazi, wanakamata usukani wa ligi hiyo wakiwa na pointi 10, lakini wanasakamwa kwa karibu na JKT Ruvu iliyoko nafasi ya pili na pointi tisa, sawa na ndugu zao
Ruvu Shooting ambao pia wana pointi tisa lakini wakitofautiana kwa idadi ya mabao ya kufunga na kufungwa.
Kama itafanikiwa kuvuna pointi tatu kwenye mchezo wa leo, Simba itafikisha pointi 13 huku mabingwa watetezi, Yanga watajiuliza upya mbele ya Azam kesho baada ya kuandamwa
na mdudu wa sare katika mecvhi tatu mfululizo.
Hata hivyo, ushindi wa pointi tatu haitakuwa rahisi kwa Simba bila jitihada za dhati, kwani Mbeya City nayo imethibitisha kwamba haitishiki kwa ukongwe hasa baada ya kuivimbia
Yanga kwa kutoka nayo sare ya bao 1-1.
Mbeya City ambayo imefuzu kucheza Ligi Kuu kwa mara ya kwanza msimu huu imeng’ang’ania katika nafasi ya saba ikiwa na pointi sita, huku ikiwa haijapoteza mchezo hata mmoja.
Kocha wa Simba, Abdallah Kibadeni”King” ambaye mchezo wa mwisho alichekelea ushindi mnono wa mabao 6-0 dhidi ya Mgambo JKT amejitapa kuifundisha soka Mbeya City kwa
kuibuka na ushindi kwenye kipute cha leo.
Naye Kocha wa Mbeya City, Juma Mwambusi amedai kutotishika na maneno ya mpinzani wake baada ya kusema yupo tayari kwa vita na kuibuka mbabe.
Katika hatua nyingine, Uongozi wa Simba umesema hauna matatizo na Mbeya City na kutaka timu hiyo iimarishiwe ulinzi zaidi.


Ofisa Habari wa Simba, Ezekiel Kamwaga alisema jana kuwa kuna kikundi cha watu ambao wamejipanga kuvaa jezi nyekundu na kufanya vurugu kwenye mchezo wao wa leo ili
kulipiza kisasa.
“Kuna mamluki wa Yanga ambao wamejipanga kuvaa jezi nyekundu na kuwafanyia vurugu Mbeya City, tungeomba jeshi la Polisi chini ya Kamanda Kova, kuimarisha zaidi ulinzi,”
alisema Kamwaga.
“Wasituchanganye sisi vyovyote, iwe tufungwe, tutoke sare kwetu ni matokeo na tutajipanga kwa mechi nyingine na kama kuna watu wanataka kulipiza kisasa wasubiri ikifika zamu yao,
tunaomba jeshi la Polisi liimarishe ulinzi hasa kwa Mbeya City.
Utamu wa ligi hiyo utakolezwa na mechi zingine tatu zitakazopigwa sehemu tofauti ikiwaemo Bukoba, ambako Kagera Sugar itakuwa nyumbani kwenye Uwanja wa Kaitaba kuumana na Ashanti, wakati 

Mgambo itakuwa nyumbani kwenye Uwanja wa Mkwakwani, Tanga kupimana ubavu na Rhino Rangers, hali kadhalika Prisons itakuwa mwenyeji wa Mtibwa Sugar kwenye Uwanja wa Sokoine, Mbeya.

 CHANZO NA MWANANCHI

0 Weka maoni yako hapa:

Post a Comment

COMMENT HAPA