Dec 30, 2015

MSAADA WA MAREKANI NA UCHAGUZI WA ZANZIBAR na Ibrahim Haruna Lipumba
MSAADA WA MAREKANI NA UCHAGUZI WA ZANZIBAR
Moja ya mafanikio makubwa ya Rais Kikwete ni kuimarisha uhusiano wa Tanzania na mataifa makubwa hususan Marekani na China. Rais Kikwete alifanikisha Tanzania kupata msaada mkubwa wa Millennium Challenge Corporation – MCC wa dola milioni 698 kutoka serikali ya Marekani uliogharamia miradi mingi ya sekta ya usafiri, nishati na maji katika kipindi cha miaka 5 kati ya 2008 – 2013.

Naunga mkono azma ya Rais Magufuli ya kupunguza na hatimaye kuondoa kabisa nchi yetu kuwa tegemezi wa misaada ya nje. Pamoja na lengo hilo ni muhimu kuyalinda na kuyatumia kwa manufaa ya taifa matunda ya diplomasia ya JK.

Serikali ya awamu ya nne ilifanikisha maandalizi ya kupata msaada wa pili wa dola milioni 472.8 ambao utajikita katika kuimarisha sekta ya nishati ili kuhakikisha kupatikana kwa umeme wa uhakika. Uamuzi wa kuweka kipaumbele sekta ya nishati ulitokana na utafiti wa vikwazo vya uchumi uliobainisha kuwa ukosefu wa umeme wa uhakika ni kikwazo kikubwa kinachozuia ukuaji wa uchumi.

Msaada huu wa pili unaojumuisha dola milioni 58.6 zitakazotumiwa kuimarizha ZECO na sekta ya umeme Zanzibar uko hatarini kusambaratika ikiwa maamuzi ya wananchi wa Zanzibar katika uchaguzi mkuu wa Oktoba 25 2015 hayataheshimiwa.

Serikali imeandaa mpango kabambe wa kurekebisha sekta ya umeme – Electricity Supply Industry Reform Strategy and Roadmap. Mpango wa pili wa MCC umejielekeza kusaidia kutekeleza mpango huu wa serikali. Utekelezaji wa mpango huu pia unalenga kuunganisha wateja wapya 300,000 wapate umeme wa uhakika. Msaada huu pia unatarajia kurekebisha sekta ya umeme ya Zanzibar na kuanzisha ufuaji wa umeme wa MW 5 kutumia jua au upepo.

Tarehe 17 Septemba 2015, Bodi ya MCC ilikutana katika kikao chake cha kila robo mwaka na ikatoa taarifa ya mjadala wake wa msaada wa pili kwa Tanzania wa dola milioni 472.8. Bodi iliunga mkono msaada huo kwani una lengo la kuboresha upatikanaji wa umeme wa uhakika Tanzania. Msaada huu utaimarisha utendaji wa asasi zinazosimamia ufuaji na ugawaji wa umeme – TANESCO kwa upande wa Tanzania Bara na ZECO kwa upande wa Zanzibar. 

Hata hivyo Bodi ya MCC ilikuwa na wasiwasi kuhusu rushwa na ufisadi nchini Tanzania. Ilisisitiza kwamba Tanzania lazima ifaulu kigezo cha kupambana na rushwa kabla ya kuamua kupitisha msaada huo. Bodi pia ilieleza kuwa ina matumaini ya uchaguzi Mkuu wa Tanzania wa tarehe 25 Oktoba 2015 utakuwa huru na haki kwa kuwa MCC inaamini haki za kidemokrasia ni sehemu muhimu ya utawala bora.

Tarehe 26 Septemba MCC ilitoa tamko kuwa kufuatana na taarifa za kigezo cha kupambana na rushwa kinachotolewa na Benki ya Dunia katika chapisho lao la Worldwide Governance Indicators, Tanzania imefaulu kigezo hiki. Kwa hiyo Tanzania imefaulu vigezo vyote vya kitakwimu vinavyotumiwa na Bodi katika maamuzi yake. Tamko la MCC liliendelea kusisitiza matumaini yake kuwa uchaguzi wa tarehe 15 Oktoba 2015 utakuwa huru na wa haki.

Pamoja na mapungufu ya uchaguzi mkuu, Watazamaji wengi wa ndani na nje waliutathmini mchakato mzima wa uchaguzi kwa ujumla wake na kuridhishwa kwamba ulikuwa huru na wa haki, Tanzania Bara na Zanzibar. Watazamaji hawa walistushwa na kustajabishwa na uamuzi wa Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar kufuta uchaguzi wote wa Zanzibar. Ikumbukwe Zanzibar wamefanya uchaguzi wa Rais wa Muungano, Wabunge, Rais wa Zanzibar, Wawakilishi na Madiwani. Uchaguzi huu umetumia Daftari la Wapigakura la ZEC na vituo vya kupigia kura vilivyoandaliwa na ZEC. Itakuwaje matokeo ya uchaguzi wa Rais wa Muungano na Wabunge ukubaliwe, lakini Uchaguzi wa Zanzibar ufutwe?

Tarehe 16 Disemba, Bodi ya MCC ilikutana na ikamua kutopitisha msaada wa pili kwa Tanzania. Hoja kubwa iliyoifanya Bodi isipitishe msaada wa dola milioni 472.8 ni kufutwa kwa matokeo ya uchaguzi wa Zanzibar baada ya kufanyika uchaguzi mzuri na wa amani. Hoja ya pili ni matumizi mabaya ya sheria ya Makosa ya Jinai ya Mtandao wakati wa uchaguzi mkuu ambapo kuna baadhi ya watazamaji waliosajiliwa na Tume ya Uchaguzi walikamatwa na polisi kwa kutumia sheria hii. 

Ni wazi kabisa kama matokeo ya uchaguzi wa Zanzibar hayataheshimiwa, msaada wa pili wa MCC utafutwa.

Ikiwa msaada wa pili wa MCC utafutwa utaathiri utekelezaji wa mpango wa serikali wa kurekebisha sekta ya umeme na pia kuhujumu mpango wa Rais Obama wa Power Africa kwa upande wa Tanzania. Ziara ya Rais Obama nchini Tanzania iliambatana na uzinduzi wa Power Africa mpango wa Marekani kusaidia nchi za kiafrika kuongeza uzalishaji na usambazaji wa umeme. Tanzania ilikuwa miongoni mwa nchi 6 za mwanzo kufaidika na mpango huu. Marekebisho ya sekta ya umeme yatakayofadhiliwa na MCC yalitarajiwa kuwa motisha kwa wawekezaji wa sekta binafsi. Kwa mfano kampuni ya Symbion ambayo ilitekeleza baadhi ya miradi ya msaada wa kwanza wa MCC, ina mpango wa kuwekeza ufuaji wa umeme wa MW 600, mjini Mtwara na kuunganisha Mtwara na gridi ya taifa kupitia Songea. Mradi huu utagharimu zaidi ya dola bilioni 1. Ikiwa msaada wa MCC utafutwa mradi huu utakuwa mashakani kutekelezwa.

Ilani ya uchaguzi ya CCM inalenga kuongeza uwezo wa kufua umeme kwa karibu mara tatu, kutoka MW 1308 za sasa mpaka kufikia MW 4915 mwaka 2020. Kuunganisha mikoa yote kwenye gridi ya taifa na kuhakikisha asilimia 60 za kaya zote zinatumia umeme. Haya ni malengo makubwa sana yaliyojikita katika utekelezaji wa Mpango Kabambe wa serikali wa sekta ya umeme utakaosaidiwa na msaada wa MCC.
Kutoyakubali matokeo ya uchaguzi wa Zanzibar kutaathiri mahusiano yetu na nchi nyingine hasa za Jumuiya ya Ulaya. Hata Jamhuri ya Watu wa China inataka nchi yetu iwe na amani na utulivu wa kisiasa. Suala la Zanzibar la kuheshimu matokeo ya uchaguzi siyo la kusalimu amri ya Mataifa mengine bali la kuheshimu uamuzi wa Wazanzibari waliofanya kwenye uchaguzi ambao kwa ujumla wake ulihesabiwa kuwa ni huru na wa haki

Dr Ali Mohamed Shein, Rais aliyechaguliwa katika uchaguzi wa 2010 ana ufunguo wa tatizo hili. Akubali matokeo ya uchaguzi wa 2015 ya Zanzibar yakamilishwe na kutangazwa na Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar. Ajiulize suala la msingi anataka kuleta vurugu za kisiasa Zanzibar? Anataka kuwapa fursa watu wenye siasa kali inayopinga demokrasia kuhamasisha vijana wa Zanzibar? Anataka kuharibu matunda ya diplomasia ya JK aliyoshiriki kuyaleta kama Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzaania? Anataka kuvuruga uhusiano wa Tanzania na Marekani na mataifa mengine? Anataka kumuhujumu Rais Obama asifanikishe Mpango wake wa Power Afrika kabla hajan’gatuka mwaka 2016? Anataka kumuharibia Rais Magufuli asitekeleze sera zake za kupambana na rushwa na kujenga uchumi wa viwanda unaoongeza ajira na kutokomeza umasikini bali ashughulikie matatizo ya kisiasa na kiusalama ya Zanzibar na kushutumiwa kuwa anavunja haki za binadamu za Wazanzibari? Anataka Watanzania wa Bara tufanye maandamano ya kumshutumu kuwa anatuvurugia nchi na kuhujumu utekelezaji wa sera za Rais Magufuli?

Pamoja na mapungufu yetu, Tanzania inatazamwa kuwa nchi ya mfano kwa amani na utulivu na ujenzi wa demokrasia katika eneo letu la Afrika ya Mashariki na nchi za Maziwa Makuu. Tunategemewa kusaidia kusuluhisha migogoro ya nchi za jirani. Rais Magufuli na Waziri wa Mambo ya Nje, Dr Mahiga watawezaje kusuluhisha migogoro ya nchi za jirani ikiwa Zanzibar italipuka kwa sababu ya Dr Shein kukataa matokeo ya uchaguzi?

Hatari kubwa zaidi kwa Zanzibar na Tanzania kwa ujumla ni vijana kuamini kuwa hatuwezi kuleta mabadiliko kwa njia za kidemokrasia. Watu wenye itikadi kali zisizoamini mfumo wa demokrasia watapata mwanya wa kuendeleza itikadi hizo na kupata wafuasi hasa vijana. Dr Shein jiulize unataka kutupeleka huko?

Tuwashukuru na kuwapongeza Wazanzibari kwa kuendelea kuwa watulivu na kuwa na matumaini ya kupatikana ufumbuzi wa haki. Lakini tuelewe uvumilivu wa Wazanzibari una kikomo. Kutangaza rasmi kurudia uchaguzi kunaweza kuwa chanzo cha vurugu za kisiasa zinazoweza kuleta maafa makubwa. Nani atakayesimamia uchaguzi huo ikiwa taarifa ya Mwenyekiti wa ZEC kuwa wajumbe wake wanadundana itakubaliwa kuwa ni ya kweli? Kama Tume na Sekretariati yake imeharibu uchaguzi wa Oktoba 2015 watawezaje kusimamia uchaguzi mwingine? Kama uchaguzi wa Zanzibar umeharibika kwa nini uchaguzi wa Wabunge na Rais wa Jamhuri ya Muungano kwa upande wa Zanzibar uhesabiwe kuwa ni halali wakati ulifanyika siku moja kwa kutumia daftari la ZEC na vituo vya kupigia kura vilivyoandaliwa na ZEC? Uchaguzi wa Zanzibar umekamilika. Matokeo yapo. Mchakato wake ukamilishwe na yatangazwe. 

Watanzania hasa viongozi wa dini na madhehebu mbalimbali, viongozi wa asasi za kiraia, viongozi wastaafu, vyombo vya habari na wapenda haki tusilifumbie macho tatizo la kisiasa la Zanzibar. Tumshauri Dr Shein akubali mchakato wa kutangaza matokeo ukamilishwe. Ni aibu kuulizwa na Marekani kuwa uchaguzi wa Zanzibar ulikuwa shwari na wa amani kwanini matokeo yake yamefutwa? Kama CCM aiheshimu maamuzi ya Wapiga kura wa Zanzibar itaheshimu maamuzi ya Watanzania wote ikiwa itashindwa uchaguzi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano?

Imetolewa na
Ibrahim Haruna Lipumba
Mwenyekiti Mstaafu
 30 Disemba 2015

Dec 29, 2015

TAMKO LA CUF BAADA YA TANKO LA CCM KUHUSU MSTAKABALI WA ZANZIBARKufuatia taarifa iliyotolewa na Chama Cha Mapinduzi (CCM) baada ya kikao cha Kamati Maalum ya Halmashauri Kuu ya Taifa ya chama hicho iliyokutana Zanzibar juzi, tarehe 27 Desemba, 2015, waandishi wengi wa habari wametupigia simu wakitaka kujua Chama Cha Wananchi (CUF) kimepokea vipi taarifa ile.
Vikao vya CCM ni vikao vya CCM. Si kawaida yetu kutolea taarifa maamuzi ya vikao vya vyama vyengine. Hata hivyo, tunaelewa ni kwa nini kumekuwepo na shauku ya kusikia CUF inasema nini kwa sababu yale yaliyokuwemo kwenye taarifa hiyo yaligusia pia mazungumzo yanayofanyika Ikulu Zanzibar yanayolenga kupata ufumbuzi wa mgogoro wa uchaguzi uliofanyika tarehe 25 Oktoba, 2015.

Baada ya kuipitia taarifa ya CCM na mengine yaliyoelezwa na Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM Zanzibar wakati akitoa ufafanuzi wa yale yaliyomo kwenye taarifa hiyo, CUF tunapenda kuwaeleza Wazanzibari na Watanzania kwa ujumla haya yafuatayo:

1. Taarifa yenyewe haionekani kama imeandaliwa na watu makini wala haioneshi kama walioitoa wanajua nini kilichopo. Hilo liko wazi kutokana na taarifa yenyewe kuwa na maudhui yanayopingana ambayo yamekuja kukorogwa zaidi na maelezo yaliyotolewa na Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM Zanzibar mbele ya waandishi wa habari na kuoneshwa katika vituo kadhaa vya televisheni:

(a) Taarifa inawataka wanachama wa CCM wajiandae na uchaguzi wa marudio lakini papo hapo inaeleza kwamba kikao kimeridhia mazungumzo yanayoendelea Ikulu Zanzibar. Taarifa haisemi iwapo maamuzi ya vikao vya mazungumzo hayatakuwa na suala la kurudiwa uchaguzi, upi ni mwelekeo wa CCM.


(b) Taarifa inazungumzia uchaguzi wa marudio lakini papo hapo Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM Zanzibar anasema CCM haina imani na Tume ya Uchaguzi iliyopo na kwa hivyo uchaguzi huo wa marudio lazima ufanyike chini ya Tume mpya. Baada ya hapo hasemi Tume iliyopo ambayo muda wa utumishi wa Makamishna wake unalindwa kikatiba itaondolewa vipi na Tume mpya itapatikana vipi.

(c) Taarifa inawataka wanachama wa CCM wajiandae na uchaguzi wa marudio lakini Katibu wa itikadi na Uenezi anasema hata usiporudiwa ndani ya siku 90, bado Dk. Ali Mohamed Shein ataendelea kuwa Rais.


Nukta hizi tatu ambazo haziwezi zote kusimama kwa pamoja bila ya kupingana moja dhidi ya nyengine zinaonesha tu ni kwa kiasi gani viongozi wa CCM Zanzibar wamepoteza mwelekeo na hawana uhakika wa nini kitatokea katika kuondokana na mgogoro huu wa kutengenezwa.


2. Taarifa ya CCM haiwasaidii wanachama wa CCM wala wananchi wa Zanzibar kwa kuwapa matumaini ya kumalizika kwa mgogoro wa kutengenezwa wa uchaguzi wa Zanzibar na badala yake inaonekana imelenga kuwachanganya zaidi wananchi kwa maelezo yanayopingana.

3. Taarifa inaonyesha ni jinsi gani CCM kilivyopoteza mvuto kwa kujiweka mbali na wananchi. Taarifa hiyo inapongeza eti kuwepo kwa maendeleo ya kiuchumi na kijamii wakati wananchi wa Zanzibar, bila ya kujali itikadi zao za kisiasa, siyo tu wanumia kutokana na sera mbovu za CCM lakini sasa wanazidi kuteketea na maisha yao kuwa magumu zaidi kutokana na fadhaa (tension) na taharuki iliyopo katika nchi kutokana na kutokuwepo kwa Serikali yenye ridhaa yao. Harakati za maisha zimeathirika sana huku bidhaa vikiwemo vyakula vikipanda bei. Viongozi wa CCM hawaonekani kujali hali hii mradi wao yao yanawaendea. Tabia hii ya CCM kutowajali wananchi wanyonge wa nchi hii ndiyo iliyopelekea wananchi kukiadhibu chama hicho katika uchaguzi mkuu na kupelekea mgombea wake wa Urais wa Zanzibar na wagombea Uwakilishi kushindwa vibaya kwa tofauti ya zaidi ya kura 25,831

.
4. Taarifa inaendeleza utamaduni wa unafiki wa kisiasa kwa eti kuwapongeza viongozi wa CCM na jumuiya zake kwa kazi ya kukiimarisha chama chao huku wakijua kwamba viongozi wao hasa wale walioongoza Kamati ya Kitaifa ya Kampeni za CCM Zanzibar walishindwa kazi na kupoteza mwelekeo. Matokeo ya kazi mbovu ya Kamati ya Kampeni ya CCM Zanzibar ni kukisababishia chama hicho kipigo kikubwa katika uchaguzi huo kilichopelekea kushindwa katika nafasi ya Urais wa Zanzibar kwa zaidi ya kura 25,831 na kupoteza viti tisa (9) vya Uwakilishi kisiwani Unguja mbali ya kutopata hata kiti kimoja kisiwani Pemba. Viongozi hao walishindwa kuwajibika licha ya kutumia mabilioni ya fedha walizopewa kwa ajili ya kampeni.
 Baada ya uchambuzi huo wa taarifa ya Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM Zanzibar, CUF inapenda kuwaeleza Wazanzibari yafuatayo:


1. Waipuuze taarifa hiyo ya Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM Zanzibar kwani haina lolote jipya zaidi ya kutaka kufunika kombe kutokana na hali ngumu inayotokana na hoja za viongozi wa ngazi za chini na wanachama wa CCM wanaotaka maelezo ya kwa nini chama hicho licha ya kutumia mabilioni ya shilingi kimeshindwa vibaya katika uchaguzi mkuu.

2. Wazanzibari wasubiri taarifa rasmi ya matokeo ya mazungumzo yanayowahusisha viongozi wakuu wa kisiasa yanayofanyika Ikulu Zanzibar ambayo yamo katika hatua za mwisho kumalizika.


3. Wampe nafasi Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dk. John Pombe Magufuli, ambaye anaendelea na juhudi katika ngazi za juu kabisa za kuhimiza kupatikana ufumbuzi wa haraka wa mgogoro wa uchaguzi wa tarehe 25 Oktoba, 2015.


4. CUF inawahakikishia Wazanzibari kwamba haitotetereka na itasimamia kwa dhati maamuzi yao waliyoyafanya kwa njia za kidemokrasia kupitia uchaguzi mkuu wa tarehe 25 Oktoba, 2015 na italinda chaguo lao la Rais wa Zanzibar, Wawakilishi na Madiwani wao.


5. Mwisho kabisa, inaendelea kuwapongeza Wazanzibari kwa kuonesha ukomavu wa hali ya juu wa kisiasa na kuendelea kutunza amani na utulivu wakati wakisubiri matokeo ya kazi kubwa waliyoifanya tarehe 25 Oktoba, 2015 ambayo inaashiria ujenzi wa Zanzibar Mpya.


HAKI SAWA KWA WOTE
ISMAIL JUSSA
KAIMU MKURUGENZI WA HABARI NA MAWASILIANO NA UMMA – CUF
29 DESEMBA, 2015

Dec 18, 2015

MATOKEO YA MTIHANI WA DARASA LA SABA 2015

  


 Jumla ya wanafunzi 503,914 kati ya 518,034 waliofaulu mtihani wa kumaliza elimu ya msingi,wamechaguliwa kujiunga na kidato cha kwanza,katika shule za sekondari za serikali katika awamu ya kwanza.Idadi hiyo ni sawa na asilimia 97.3 ya wanafunzi waliofaulu na wenye sifa ya kujiunga na kidato cha kwanzaDec 11, 2015

Video Mpya : Belle 9 – Burger Movie Selfie

http://www.hassbabytz.com/wp-content/uploads/2015/12/Belle-9-Burger-Movie-Selfie.png
                                                     

Dec 8, 2015

TAARIFA KWA UMMA JUU YA UENDELEZAJI WA UFUKWE WA OYSTERBAYUfukwe wa Oysterbay unaanzia katika eneo la Police Officers Mess hadi Barabara ya Kenyatta, upande wa Mashariki wa Barabara ya Toure. ambapo ndani ya ufukwe huo kuna eneo maarufu linaloitwa Coco Beach.
Kwa muda mrefu sana, ufukwe huo umekuwa ukitumiwa na wananchi wengi wa Jiji la Dar es Salaam kwa ajili ya kujipumzisha, kuogelea na wakati mwingine kufanyia mazoezi ya viungo ikiwamo mazoezi ya kutembea.

Hivi karibuni kumeibuka taarifa potofu katika vyombo mbali mbali vya habari kuwa Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni imeuza Ufukwe wa Oysterbay.

Ukweli ni kuwa katika kuiboresha fukwe hiyo, mnamo mwaka 2007 Halmashauri iliingia mkataba na Kampuni ya Q-Consult iliyopewa masharti ya kuiendeleza fukwe hiyo, lakini ilishindwa kutimiza masharti ya uendelezaji, hali iliyopelekea Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni kusitisha mkataba huo
.
Baada ya kusitishwa kwa mkataba, Kampuni hiyo ya Q-Consult ilifungua shauri Mahakama Kuu Kitengo cha Ardhi, na Mahakama ikampa ushindi Q-Consult
.
Kwa kutoridhishwa na uamuzi huo, Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni ilianza taratibu za kukata rufaa Mahakama ya Rufani, kwa kuwasilisha nyaraka za awali kama notisi ya kukata rufaa, kuwasilisha nyaraka za kuomba kibali cha kukata rufaa na kuandika barua ya kuomba kupatiwa nyaraka zote za kukata rufaa, ikiwa ni pamoja na hukumu na mwenendo wa shauri.

DHAMIRA YA HALMASHAURI:

Katika lengo hilo hilo la kuiendeleza fukwe hiyo Halmashauri, kwa kushirikiana na Benki ya TIB wameshaandaa michoro inayoonyesha namna ufukwe huo utakavyokuwa baada ya kutengenezwa.
Ni mchoro unaonyesha kuwa itakuwa ni Open Beach (Ufukwe wa Wazi) kwa wananchi wenye vipato tofauti tofauti kwenda kupumzika, kustarehe na hata kufanya mazoezi mbali mbali.

Ili kutimiza azma ya kuifanya kama ni Open Beach, Halmashauri itagharamia sehemu ya ujenzi huo hasa maeneo ya wazi, pia itashirikisha wadau mbali mbali katika kugharamia ujenzi huo.

Napenda kuwahakikishia wananchi wote kuwa mpango wa uendelezaji wa ufukwe huo nishirikishi na unamtaka kila mdau kutoa maoni yake ili kuondoa dhana potofu kuwa Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni imeuza ufukwe wa Coco Beach ambayo ni sehemu ya ufukwe wa Oysterbay.

Imetolewa na
Eng. Mussa B. Natty
Mkurugenzi wa Manispaa
Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni

CUF YAKOSOA MAAZIMIO YA KIKAO CHA KAMATI KUU YA CCM


 

Kushindwa kutoa Kauli dhidi ya Ubakwaji ya Demokrasia uliofanywa na ZEC chini ya Salim Jecha 

Kushindwa kutoa Maelekezo kwa Rais Magufuli kuhusiana na Pesa za Account ya Tegeta Escrow 

Kushindwa Kuunga Mkono Matamko ya Waangalizi wa Ndani na Wa Nje, Balozi na Mashirika Mbali mbali Kuhusu Uchaguzi wa Zanzibar. 

Cuf Chama cha Wananchi kimekosoa Maazimio ya Kikao cha Kamati Kuu ya CCM nakusema kwamba, Kikao hicho hakikujadili mambo ya Msingi yanayolikabili Taifa letu kwa kuzingatia Hali ya kisiasa. Taifa lipo katika kipindi ambacho Macho na Masikio ya Watanzania waliopo Nchini na Nje ya Nchi wakielekeza kwenye Mgogoro wa Kikatiba Zanzibar kufuatia tamko la kufutwa kwa Uchaguzi wa Zanzibar lililotolewa na Mwenyekiti wa ZEC bila kua na uhalali wa Kikatiba. Ni jambo la kushangaza, kusikitisha na kufedhesha kwa Kikao cha Kamati Kuu kuketi na bila kujadili na hatimae kutoa Kauli juu Ya suala Hilo. CCM imekua ikijinasibu kua inaongoza Nchini yetu kwa Mujibu wa Katiba na Sheria, imekua inajinasibu kufuata misingi ya Demokrasia na Utawala Bora.

 Lakini kwa kinachoendelea Zanzibar sio tu ni Uvunjaji wa Katiba Lakini pia Kuna hatari ya kuturudisha kwenye matukio ya January 26 na 27 Mwaka 2001. Kwa Chama makini na chenye kujali Maisha ya Raia wake, kwa vyovyote vile kingejadili Mgogoro wa Zanzibar. Kingefanya hivyo kwakua kinachoendelea Sasa ni Viashiria vya yale tuliosameheana baada ya matukio ya January 26 na 27. Ni dhahiri kwamba CCM imeshasahau Matukio hayo. Na kwa mantiki hiyo kilichofanywa na ZEC kina Baraka za Kamati Kuu ya CCM. 

CCM imeshindwa hata Kuunga Mkono matamko Ya Waangalizi wa Uchaguzi wa Ndani na Nje kuhusiana na Uchaguzi wa Zanzibar na hata kujibalaguza kwa kutoa tamko la Kisiasa tu ili waweze kujitautisha na ZEC. Ama kweli la kuvunda halina ubani. 

Kikao hicho cha Kamati Kuu kimeshindwa kumuongoza Rais Magufuli kuhusiana na Makada wake waliochota Mabilioni ya Fedha za Escrow. Kashfa ya Fedha za Escrow ambayo iliibuliwa Bungeni ina uthibitisho mzuri toka Ofisi ya CAG na hata Taarifa za Kamati ya Bunge inayoshughulika na Ukaguzi wa Hesabu za Mashirika ya Umma. Kutokulizungumzia jambo hilo ni kufunga Mdomo Rais Magufuli juu ya dhamira yake ya kusimamia Mapato na Matumizi ya Fedha za Umma. 

Cuf Chama cha Wananchi kinalichukulia Tamko Hilo kama hadaa kwa Watanzania na halina uzito wowote utokanao na utekelezaji wa llani ya CCM. Cuf Chama cha Wananchi kinawataka na kuwaomba Watanzania kuendeleza Agenda ya upatikanaji wa Katiba mpya ili kuweza kua na uhakika wa Demokrasia Pana kwa Maslahi ya Taifa letu 

Lakini pia Ni vyema kwa Rais Magufuli kuangalia Hali ya Kisiasa kwa Upande wa zanzibar sio tu kujipa nafasi nzuri ya kutumbua Majipu Lakini pia kuepusha yale ya January 26 na 27 Mwaka 2001.
Suala la Tegeta Escrow Ni muhimu kwakua Hilo halihitaji tochi katika kulishughulikia.
Mambo hayo kwenye Kikao cha Kamati Kuu ya CCM haya kua na u muhimu.

KAMATI KUU CCM YARIDHISHWA NA KASI YA SERIKALI YA AWAMU YA TONA CHIDI YA DK MAGUFURIJana tarehe 07/12/2015 Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya CCM Taifa ilifanya kikao chake cha kawaida mjini Dar es salaam kwa siku moja. Kikao hicho kiliongozwa na Mwenyekiti wa CCM, Rais mstaafu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete.

Kamati Kuu pia ilipokea taarifa juu ya utendaji wa Serikali katika utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2015-2020. Kwa ujumla na kwa kauli moja Kamati Kuu ya CCM Taifa iliipongeza Serikali ya Awamu ya Tano chini ya uongozi wa Rais Dkt. John Pombe Magufuli, Makamu wa Rais Mheshimiwa Samia Suluhu na Waziri Mkuu Mhe. Kassim M. Majaliwa kwa kasi nzuri waliyoanza nayo katika utekelezaji wa Ilani hiyo.

Kamati Kuu kwa niaba ya Chama imeunga mkono hatua kadhaa zinazochukuliwa na Serikali ya Awamu ya Tano katika kuhakikisha Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya 2015-2020 inatekelezwa kwa ufanisi. Aidha, inapongeza na kuunga mkono juhudi kubwa zinazofanywa na Serikali katika maeneo ya:-
(1) Kusimamia vyanzo vya mapato ya Serikali:

Kamati Kuu inapongeza na kuunga mkono juhudi kubwa zinazofanywa na Serikali ya Awamu ya Tano katika kuhakikisha kuwa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) na Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA) zinasimamia ukusanyaji wa kodi za Serikali ipasavyo. Juhudi hizi za Serikali ya Awamu ya Tano kwa muda mfupi zimezaa matunda yanayoonekana wazi. Aidha, Kamati Kuu inawataka wahusika mbalimbali kwenye maeneo hayo ya udhibiti wa vyanzo vya mapato kuhakikisha wanatoa ushirikiano kwa Serikali ili lengo liweze kutimia.

(2) Kudhibiti matumizi ya Serikali:
Kama ilivyoagizwa na Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya 2015-2020, Serikali ya Awamu ya Tano imeanza vizuri na kwa kasi kusimamia udhibiti wa matumizi yasiyo ya lazima katika Serikali, ili kutumia fedha hizo kwenye utoaji wa huduma kwa wananchi. Kamati Kuu inaunga mkono juhudi hizi na kuwataka wote wanaohusika kwa namna moja ama nyingine na udhibiti wa matumizi hayo wamuunge mkono Rais Dkt. John Pombe Magufuli na Serikali yake katika jitihada hizi.

(3) Uhimizaji wa wananchi katika kufanya kazi kwa bidii:
Kamati Kuu inawataka wanaCCM na wananchi wote kwa ujumla nchini kumuunga mkono Rais na Serikali yake kwa kuitikia wito wa kufanya kazi kwa bidii, kwa maarifa na uzalendo. Kamati Kuu inawahimiza watu wote kwenye maeneo yao ya kazi kujituma na kuchapa kazi ili kujenga nchi yetu na kumuunga mkono Rais Magufuli.

(4) Kusimamia na kuhimiza uwajibikaji katika Serikali, Taasisi na Mashirika yake:
Kamati Kuu pia inapongeza na kuunga mkono juhudi zinazoendelea za kuhakikisha kunakuwa na uwajibikaji mkubwa Serikalini ili kuongeza kasi na ubora wa utoaji huduma. Katika kipindi cha muda mfupi matunda yake yameanza kuonekana na hivyo kuweka msingi mzuri wa kuboresha huduma kwa umma kwa njia endelevu.

(5) Juhudi na jitihada hizi za Serikali ya Awamu ya Tano chini ya Uongozi wa Rais Dkt. Magufuli zimeleta matumaini mapya kwa sehemu kubwa ya wananchi na kukuza imani kwa Serikali yao. Hivyo, kila Mtanzania ana wajibu wa kuunga mkono jitihada hizi.

Pamoja na kuunga mkono na kupongeza kasi waliyoanza nayo Rais Magufuli, Makamu wa Rais na Waziri Mkuu, Kamati Kuu inawataka Viongozi wengine wote kuiga mfano huu mzuri na kuhakikisha wanatimiza wajibu wao ipasavyo ili kutekeleza kwa haraka zaidi Ilani ya Uchaguzi ya CCM na kuleta maendeleo nchini.
Aidha, Kamati Kuu inawatakia Watanzania wote kheri ya Krismas na mwaka mpya wa 2016, na inaamini mwaka ujao utakuwa wa kuchapa kazi na wenye mafanikio zaidi.

Imetolewa na:-
Abdulrahman O. Kinana,
KATIBU MKUU WA CCM 08/12/2015

Nov 27, 2015

KAMISHNA MKUU WA TRA, RISHED BADE ASIMAMISHWA KAZI  KAMISHNA MKUU WA TRA, RISHED BADE ASIMAMISHWA KAZI

Rais Dk Magufuli amemsimamisha kazi Kamishna Mkuu wa mamlaka ya mapato Tanzania ( TRA) Rished Bade na kumteua Philiph Mpango kukaimu nafasi hiyo

Taarifa kutoka ikulu zimesema kuwa uamuzi huo wa Rais Magufuli umefuatia ziara ya waziri mkuu bandarini iliyobaini upotevu wa makontena 349.

Aidha Rais Magufuli amemtaka Rished Bade kutoa ushirikiano kwa Philiph Mpango wakati uchunguzi ukiendelea.

May 12, 2015

Ndugu ya Adebayor aomba msamahaNdugu wa mshambuliaji wa klabu ya Tottenham Emmanuel Adebayor ameomba msamaha baada ya nyota huyo kumshtumu katika mtandao wa facebook na watu wengine wa familia yake.

Rotimi Adebayor ameiambia BBC kwamba anaomba msamaha kwa makosa aliyofanya,na kwamba angependelea nduguye arudi katika familia.

Emmanuel Adebayor ambaye pia anaichezea Togo alisema wiki iliopita kwamba mzigo wa kifedha wa kuisadia familia yake pamoja na ugomvi katika familia yake umemuahiribia kazi yake.

Amesema kuwa anazitaka familia nyangine barani afrika kupata funzo kutoka kwake.

Mar 30, 2015

MSAFARA WA CUF WASHAMBULIWA ZANZIBAR

Wanachana wa Chama cha wananchi CUF wamevamiwa na kujeruhiwa na watu wasiojulikana.

Kitendo hicho cha uvamizi wa msafara huo uliokua ukitokea katika mkutano wa hadhara makunduchi.
Watu hao walivamia msafara huo maeneo ya fuoni meli tano na kujeruhi watu kadhaa.

 
Hawa ni baadhi ya majeruhi 

Tunapenda kuwapa pole walikutwa na matatizo haya ila tunawashauri Wazanzibari waachane na siasa za uhasama hizi

Mar 25, 2015

Jumuiya ya Vijana ya CUF (JUVICUF) haikubaliani na Muswada wa kuanzishwa kwa Baraza la Vijana la Taifa

Jumuiya ya Vijana ya CUF (JUVICUF) haikubaliani na Muswada wa kuanzishwa kwa Baraza la Vijana la Taifa kutokana na Muswada huo kubeba ajenda ya kulitaka baraza hilo kuwa ni Asasi ya Kiserikali ambayo itakua inafanaya kazi zake bega kwa bega na serikali huku serikali ikipewa meno zaidi katika baraza hilo.

JUVICUF tunakubaliana moja kwa moja na wazo la kuanzisha baraza la taifa la Vijana. Ingawa pia tunaona kuwa kama taifa tumechelewa sana kwani hata Umoja wa Afrika ulishapitisha azimio la kuanzishwa kwa Baraza ya Vijana kwa Nchi wanachama miaka sita iliyopita na Rais wetu Mh. Jakaya Kikwete alisaini Uwamuzi huo.

Lakini kwakua Baraza hilo ni chombo cha vijana ambacho kitakua huru na akitafungamana na aina yoyote ya Itikadi za kisiasa, Jumuiya ya Vijana ya CUF haikubaliani na muswada huo kwakua unakiuka lengo na mantiki ya kuwa na baraza huru la vijana ambalo lengo kuu litakua ni platform huru ya vijana wa Tanzania, Jumuiya inaona muswada huo haufai kupitishwa na Bunge kwani umejaa makosa ya kimantiki na kidhamira kama ifuatavyo.

1. Bado Baraza hilo litaendelea kuwa tegemezi zaidi kwa serikali kwa kuwa kila jukum la msingi linalotaka kufanywa litakua linasuburi kibali kutoka kwa Waziri husika.

2. Uteuzi wa Mwenyekiti na Katibu kuwa chini ya Waziri bado ni kulifanya baraza kuwa ni Taasisi ya kiserikali. Kama waziri anateua na pia anaweza kufuta uteuzi wa Mwenyekiti kwaiyo huyu mwenyekiti anakwenda kuwa mtumwa wa Waziri ambae pia ni Mwanasiasa kutoka chama cha siasa. Tunatakiwa kuhama katika zama za Uteuzi, uteuzi na kuhamia zama za ushindani zaidi , kama vijana tunapaswa kuwa mfano katika hili.

3. Muswada unapingana wenyewe katika baadhi ya vifungu. Huku unataka siasa isiingie katika baraza, wakati vifungu vingine vinawapa uhalali wanasiasa kuteua viongozi wa Baraza. Waziri ni nani kwa mujibu wa katika ya sasa ya Tanzania. Is a typical political person of which is difficult for him/her to hide or withstand his or her political affiliation while is in office because most of them are still holding important and big political positions within their political party. (Eg. Mwigulu Nchema, Membe, Makamba, Migiro,etc)

4. Muswada huu ni sawa na katiba inayopendekezwa tu, umefanywa kwa kukurupuka zaidi. Baraza ni kitu ambacho vijana wengi wa Tanzania wamekua wakitamani kuwa nacho tangu enzi hizo. Ninamkumbuka hapa Mwalimu wangu Israel Ilunde na wenzake namna walivyo pambana tangu kitambo bila mafanikio na wenzake akina Mchimbi wakaishia mikononi mwa polisi. Tatizo serikali inaogopa kivuli chake kwaiyo wanataka kulifanya baraza kuwa ni chanzo cha habari na kuwa kama nguzo ya kuendeleza political regime ili chama kilichopo madarakani kiendelee kutanua madarakani kwa kutumia Baraza bovu la vijana litakalo undwa.


Ushauri.

Vijana na watanzania kwa ujumla tuusome muswada huo kwa umakini ili tuweze kushirikiana katika kuupinga na kuiomba serikali ikajipange katika hili.


Serikali iache kuogopa kivuli chake yenyewe, vijana tunataka Baraza huru la Vijana.

Wabunge wazalendo wa Nchi yetu nzuri ya Tanzania wasikubali kuupitisha mswada huo usio na faida kwa taifa .

Ahsanteni sana
Hamidu Bobali,
Mwenyekiti wa JUVICUF
25/03/2015.