HIKI NDICHO ALICHOKISEMA MNYIKA BAADA YA CHENGE KUSEMA KODI YA (SimCardTax) NI SAHIHI
Chenge
(Mb) amesema kodi ya kadi za simu (SimCardTax) ni sahihi kwa utafiti
wao; aulizwe kupitia 0754782577 atoe maelezo zaidi na vielelezo vya
ziada
Leo tarehe 25 Julai 2013 chombo kimoja cha habari
kimemnukuu Mwenyekiti wa Kamati ya Bajeti Andrew Chenge (Mb) akisema
kwamba uamuzi kuhusu kodi/tozo ya kadi/laini za simu haukuwa wa
kubahatisha. Chenge amesema kwamba kamati yake ilifanya utafiti wa kina
na kisha kufikia uamuzi wa kuona tozo hiyo ni sahihi.
Ni muhimu
akatakiwa kupitia namba yake 0754782577 atoe maelezo zaidi kuhusu
usahihi wa tozo hiyo na aeleze ni wapi wananchi na wadau mbalimbali
wanaweza kupata vielelezo vya utafiti walioufanya.
Aidha, wenye
maswali kuhusu nini hasa kilijiri kwenye kamati ya bajeti mpaka kamati
hiyo ikakataa jedwali la marekebisho nililowasilisha tarehe 27 Juni 2013
kabla ya muswada wa sheria ya fedha kupitishwa bungeni tareheb 28 Juni
2013 kwa kuwa yeye ambaye ndiye msemaji wa kamati ameanza kutoa majibu.
Pia, aeleze iwapo yupo tayari kumshauri Spika aruhusu kamati ya bajeti
ikutane kwa dharura wiki ijayo kufanya kazi ya kupitia matumizi ya
Serikali kwa lengo la kuanisha maeneo ambayo Serikali inaweza kubana
matumizi kwa haraka kufidia pengo la bilioni 178 zinazotafutwa kwenye
tozo hiyo ya simu. Hatua hii itawezesha kodi hiyo kuacha kutozwa bila ya
kulazimika hata kuongeza vyanzo vingine vya fedha iwapo Serikali
inasuasua kupanua wigo wa mapato.
Izingatiwe kuwa katika
kuwawakilisha wananchi kuepusha kutozwa kodi ya kumiliki kadi ya simu na
nyingine zenye kuongeza gharama za maisha kwa wananchi, kabla ya
kupitishwa kwa muswada wa sheria ya fedha nilichukua hatua kuanzia
bungeni katika mkutano uliopita wa Bunge.
Niliwasilisha kwa
Bunge kupitia ofisi ya Katibu wa Bunge jedwali la marekebisho ya sheria
hiyo kwa mujibu wa Kanuni ya 86 (11) ambapo pamoja na mapendekezo
mengine nilitaka kifungu katika jedwali la marekebisho la Serikali
kilichopendekeza kuanzisha ushuru huo kiondolewe.
Ikumbukwe
kwamba kwamba katika mchango wangu kwa kuzungumza bungeni nilisema
muswada wa sheria ya fedha wa mwaka 2013 ni “muswada wa majanga” ambao
utaleta athari za ongezeko la bei ya bidhaa na huduma muhimu.
Hata hivyo, Kamati ya Bajeti chini ilikataa mapendekezo hayo, hata hivyo
kwa kuwa masharti ya kanuni za kudumu za Bunge yanakataza mbunge
mwingine kutoa taarifa za majadiliano ya ndani ya kamati sitaeleza kwa
undani yaliyojiri katika kikao cha kamati tajwa.
Hivyo taarifa
rasmi na sababu za mapendekezo hayo kukataliwa zinaweza kutolewa na
mwenyekiti wa kamati hiyo Mh. Andrew Chenge (Mb) kwa kuulizwa kupitia
namba yake ya simu ya mkononi/kiganjani (0754782577).
Uongozi
bora na uraia mwema wenye uwajibikaji ni chimbuko na chachu ya ukuaji
endelevu wa uchumi wa nchi na ustawi wa maisha ya wananchi.
Kwa
ufupi nilielelezwa kwamba tayari chanzo hicho cha mapato na vingine
vilishaingizwa katika bajeti ya Serikali kwa ajili ya matumizi ya
kawaida na ya miradi ya maendeleo kwa mwaka wa fedha 2013/2014 na
kupigiwa kura ya ndio na wabunge wengi kabla ya muswada huo wa sheria ya
fedha kujadiliwa. Hivyo nilitakiwa kuwasilisha mapendekezo ya vyanzo
mbadala vya kuziba pengo litakalotokana na kufuta ushuru huo na kodi
zingine nilizopendekeza zifutwe au zipunguzwe.
Katika muktadha
huo kwa upande wa sekta ya mawasiliano pekee, nilipendekeza vyanzo
mbadala vyenye jumla ya zaidi ya bilioni 400 za kitanzania ambazo ni
zaidi ya lengo lililowekwa na Serikali bila ya kuongeza mzigo wa gharama
kwa wananchi wa kawaida. Nilitoa ushuhuda wa kitakwimu kutoka nchi ya
Ghana ambayo makampuni ya simu yanachangia asilimia 10 ya mapato ya nchi
hiyo bila kuongeza mzigo mkubwa wa gharama kwa watumiaji wa kawaida wa
huduma za simu ya kiganjani/mkononi.
Kati ya mapendekezo
niliyotoa ni pamoja na kutaka marekebisho ya Sheria ya Mawasiliano ya
njia Kieletroniki na Posta ya mwaka 2009 ili kuipa uwezo wa kutosha
Mamlaka ya Udhibiti wa Mawasiliano Tanzania (TCRA) kufanya ukaguzi wa
uwekezaji unaofanywa na makampuni ya simu. Hata hivyo, mapendekezo hayo
yalikataliwa na kamati ya fedha chini ya uenyekiti wa Andrew Chenge
(Mb).
Ifahamike kuwa kwa kurejea masharti ya Kanuni ya 109 (2)
niliwasilisha pia katika ofisi kwa Katibu wa Bunge kabla mjadala kuhusu
muswada huo kufungwa mapendekezo ya ziada ya vyanzo mbadala vya mapato
vya kuziba pengo lililotokana na marekebisho niliyotaka yafanyike kwa
lengo la kupunguza mzigo wa gharama za maisha kwa wananchi kutokana na
ongezeko la kodi.
Marekebisho hayo yangechangia katika
kudhibiti udanganyifu unaofanywa na makampuni mengi ya simu juu ya
uwekezaji na faida wanayoipata. Marekebisho hayo yangewezesha pamoja na
mambo mengine makampuni mengi kuorodheshwa katika soko la hisa la Dar
Es Salaam na pia kudhibiti usajili wa makampuni katika nchi zenye mfumo
wa kuwezesha ukwepaji kodi (Tax Heavens).
John Mnyika (Mb)
25 Julai 2013
0 Weka maoni yako hapa:
Post a Comment
COMMENT HAPA