Makamo wa kwanza wa Rais Zanzibar Maalim Seif Sharif akizungumza na
Waandishi wa habari katika ukumbi wa Zanzibar Ocein View Hotel iliopo
Kilimani
Waheshimiwa Waandishi wa habari
Kwanza kabisa hatuna budi kumshukuru Mwenyezi Mungu Mtukufu kwa
kutuweka katika hali ya uzima hadi kukutana tena leo kuzungumzia
utendaji na majukumu yetu tuliyokabidhiwa na wananchi wa Zanzibar katika
serikali yetu, hasa hii ya awamu ya saba ya uongozi ambayo imetimiza
muda wa miaka mitatu sasa.
Mkutano huu ni mwendelezo wa uamuzi wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar
ya awamu ya saba yenye mfumo wa Serikali ya Umoja wa Kitaifa,
unaowataka viongozi wa juu na taasisi zote za serikali wawe wanajiwekea
utaratibu wa kuzungumza na waandishi wa habari baada ya kila muda
waliojipangia.
Pili natoa shukurani zangu za dhati kabisa kwenu nyinyi wanahabari
mliotenga muda wenu na kuja kuhudhuria kwa wingi na kuja kuitikia wito
wetu wa kutusikiliza, ambapo baadaye mtapata fursa ya kuuliza, ili mpate
ufafanuzi wa masuala mbali mbali yanayohusu maendeleo ya nchi yetu
katika nyanja za kiuchumi, kisiasa na mambo yote yanayogusa jamii ya
Wazanzibari kwa ujumla.
Waheshimiwa Waandishi wa habari
Katika hotuba yangu nakusudia kugusia angalau kwa ufupi baadhi ya
mambo muhimu yanayoendelea na kujitokeza katika nchi yetu hivi sasa, na
katika siku za hivi karibuni. Kisha nitajikita zaidi kutoa maelezo kwa
yale maeneo yaliyowekwa chini ya usimamizi wa Ofisi ya Makamu wa Kwanza
wa Rais.
Kama mjuavyo ofisi hii naiongoza mimi nikisaidiwa na Waziri wa Nchi
makini, mchapakazi na muadilifu, Mheshimiwa Fatma Abdulhabib Fereji.
Waziri wa Nchi ndiye msimamizi wa siku kwa siku wa shughuli zote za
ofisi hii. Lakini pia nina Katibu Mkuu makini mjuzi na mzoefu wa
taratibu za serikali, ambaye ndiye anayenishauri mimi na Waziri wa Nchi
kuhusu masuala ya kitaalam, mbali kuwa Mtendaji Mkuu wa shughuli zote
zilizochini ya ofisi hii. Huyo ni Dk. Omar Shajak akisaidiwa na Naibu
Katibu Mkuu, Dk. Islam Seif Salum, pamoja na Wakurugenzi na Watendaji
Wakuu wa Kamisheni zilizo chini ya ofisi hii. Wote hao nawashukuru kwa
msaada mkubwa walionipa na wanaoendelea kunipa, muda wote huu.
Waheshimiwa waandishi wa habari
Katika kipindi hiki cha muda wa miaka mitatu tunaendelea kushuhudia
nchi yetu ya Zanzibar ikiendelea kuwa katika hali ya amani, utulivu na
mshikamano miongoni mwa wananchi wake. Hali hii imetuwezesha kuendelea
kutekeleza majukumu yetu Serikalini na kwa wananchi wote katika hali ya
utulivu.
Kutokana na hali hiyo ndio maana hivi sasa ushiriki wa wananchi wote
katika shughuli za kimaendeleo, kijamii na kisiasa umeendelea kuwa
mkubwa, ambapo wamekuwa wakiiunga mkono Serikali yao katika mambo yote,
ikiwemo yale mambo muhuimu ya Kitaifa tunayoendelea nayo hivi sasa. Kati
ya mambo hayo ni Maadhimisho ya miaka 50 ya Mapinduzi Matukufu ya
Zanzibar, ambayo yanafikia kilele chake Januari 12 mwakani. Ni matumaini
yangu kuwa wananchi wote bila ya kujali itikadi zao za kisiasa,
watashiriki kwa ukamilifu katika maadhimisho hayo.
Waheshimiwa Wana Habari
Serikali ya Mapinduzi Zanzibar ya Awamu ya Saba yenye mfumo wa
Kitaifa imeendelea kutekeleza malengo ya Mapinduzi katika nyanja zote,
zikiwemo za kiuchumi, kijamii, kisiasa na kiutamaduni.
Katika kipindi hichi cha miaka mitatu ya Serikali ya Mapinduzi yenye
mfumo wa Serikali ya Umoja wa Kitaifa, yapo mafanikio kadhaa
yaliyopatikana. Kwanza ni kuwa Serikali imechukua hatua kadhaa za
kuimarisha uchumi wetu, lengo likiwa ni kuwaongezea kipato wananchi
wetu.
Yapo mafanikio makubwa yaliyopatikana katika kipindi hiki cha miaka
mitatu ya Serikali ya Awamu ya Saba. Miongoni mwa hatua hizo ni
kupandisha bei ya karafuu. Wakulima wetu wamepata afueni kubwa ya bei,
ikilinganishwa na hali ilivyokuwa huko nyuma. Hali hiyo imewapa mwamko
mkubwa wakulima wetu, lakini pia kuwa na mwamko wa kuziuza karafuu zao
kunakohusika. Hadi jana jumla ya tani 1,540 tayari zimenunuliwa kwa
kiasi cha shilingi bilioni 21,560,805,000.
Kupandishwa bei ya karafuu kumewafanya wananchi wengi, hasa katika
vijiji vya Pemba, kujenga nyumba bora zaidi na hivyo kuwafanya kuishi
katika mazingira bora.
Halikadhalika, Serikali imechukua hatua za makusudi kabisa
kumuendeleza mkulima, mfugaji na mvuvi. Katika hili Serikali imepunguza
kwa kiwango kikubwa bei za pembejeo za kilimo, kama mbolea, dawa za
kuulia magugu na wadudu, mbegu na kupunghuza gharama za kulimia kwa
kutumia matrekta.
Serikali pia imechukua hatua za kutoa elimu kwa wakulima na wafugaji,
kwa nia ya kutumia njia za kisasa za ukulima na ufugaji. Jumla ya
wavuvi wadogo 59 wamepelekwa China kujifunza njia za kisasa za ufugaji
wa samaki. Pia Maafisa watatu wa Wizara ya Uvuvi na Ufugaji walipelekwa
nchini Korea maalum kusomea ufugaji wa samaki.
Hatua hizi zote lengo lake ni kuwasaidia wananchi. Pia tumeona kwamba
katika dhana hiyo hiyo ya kujaribu kuleta huduma kwa wananchi, serikali
imekuwa ikijitahidi sana kuhakikisha kuwa huduma za afya zinapata
unafuu. Serikali pamoja na ufinyu wa bajeti yake inahakikisha kuwa zile
dawa ambazo ni muhimu “essential drugs” zinapatikana katika hospitali
zetu.
Kwa upande wa madaktari bado tuna upungufu, lakini juhudi za
kuwasomesha watu wetu zinaendelea, vijana kadhaa wanapata mafunzo katika
skuli ya udaktari ya Zanzibar yaani ‘Zanzibar Medical School’ na vijana
hao watakapomaliza mwaka huu au mwakani, tutapata kwa mpigo mmoja
madaktari 34. Hatua hiyo itaweza kupunguza sana pengo la upungufu wa
madaktari katika nchi yetu.
Vile vile juhudi zinachukuliwa kuwataka wale madaktari ambao wanasoma
nchi nyengine warudi, ili tumalize kabisa tatizo la uhaba wa wataalamu
wa kada hii.
Serikali hii ya Umoja wa Kitaifa vile vile imekuwa ikipambana na tatizo
la upungufu wa maji kwa kushirikiana na wahisani na makampuni mengine ya
nje. Tumekuwa na miradi mikubwa ya maji katika nchi na bado jitihada
zinafanyika katika kupunguza tatizo hili.
Kwa mfano hivi sasa tumekubaliana na nchi ya Ras El Khaima kutusaidia
katika suala la kuchimba visima kwa mintaaraf ya kupunguza tatizo la
uhaba wa maji.
Tatizo la Umeme limepungua kwa kiasi kikubwa kutokana na mradi wa MCC
unaofadhiliwa na Marekani. Tunafahamu bado umeme unakatika katika
kutokana na sababu tafauti. Lakini azma ya Serikali ni kulimaliza tatizo
hili kabisa.
Ukiangalia sekta ya elimu, hivi sasa watoto karibu wote waliofikia
umri wa kwenda skuli wanapatiwa fursa hiyo. Hivi sasa takriban kila
Shehia ina angalau skuli moja, na zile Shehia chache ambazo bado
hazijawa na skuli juhudi zinaendelea kufanywa, ili kuhakikisha kuwa kila
Shehia inakuwa na skuli.
Serikali inaendelea kuwavutia wawekezaji wa ndani na nje ya nchi,
kuwekeza katika sekta mbali mbali, miradi ya kiuchumi imekuwa
ikiongezeka. Kwa mfano mwaka jana pekee jumla ya miradi sita mipya na
programu 18 mpya zilianzishwa. Ni azma ya Serikali ya Mapinduzi Zanzibar
kushirikiana na sekta binafsi kuzidi mkuleta maendeleo.
Jengine ni kwamba tumeweza kuongeza maslahi ya wafanyakazi wa Serikali
ya Mapinduzi ya Zanzibar. Katika mwaka 2010/2011 mishahara ya
wafanyakazi wa Serikali iliongezwa. Huko nyuma ilikuwa muda mrefu
hawajapata nyongeza zao wala kupandishwa vyeo. Kwa kuwa katika mwaka
2011/2012 Serikali ilishughulikia suala la kupanga “Scheme of service”,
kwa Wizara na Taasisi zote za Serikali ili kila mmoja ajijue yuko wapi.
Lengo la Serikali ni kupandisha tena mishahara katika mwaka huu wa fedha
2013/2014.
Mengine ni Serikali hii kuona umuhimu wa sekta ya mifugo na uvuvi,
Mhe. Rais ameunda Wizara Maalum inayoshughulikia Mifugo na Uvuvi. Kwa
vile bado tuna changamoto, hatujaendeleza uvuvi katika bahari kuu na
bado hatujawaendeleza ipasavyo wakulima wetu na hasa wafugaji, Wizara
imepewa jukumu hilo kuona kuwa sekta ya uvuvi inakua sambamba na sekta
ya ufugaji.
Pia tumefanya mabadiliko ya hapa na pale, sasa hivi sasa ipo Wizara
maalum inayoshughulikia utalii, ambayo inaelekeza azma ya Serikali
kuifanya sekta ya utalii kuwa sekta kiongozi katika uchumi wa Zanzibar.
Chini ya Uongozi wa Rais Shein Serikali imebuni dhana ya utalii kwa
wote, kwa min ajili ya kuwawezesha Wazanzibari wote washiriki katika
kuundeleza utalii na kuweza kupata manufaa kutokan na utalii wenyewe.
Mafanikio haya pamoja na juhudi nyengine tunazoendelea kuzichukua,
ikiwemo za kuliinua zao la Karafuu kwa kujali zaidi maslahi ya wakulima,
yametuwezesha kukuza matumaini ya kuimarika kwa uchumi wa Zanzibar
ambao umeweza kukua kutoka asilimia 6.7 mwaka 2011hadi asilimia 7.0
mwaka jana.
Hayo ni kwa ufupi tu, lakini yapo mafanikio mengine makubwa ambayo
yamepatikana katika kipindi hicho na hasa chini ya Serikali hii yenye
mfumo wa Umoja wa Kitaifa.
Changamoto
Lazima tukiri kuwa pamoja na mafanikio hayo makubwa bado tunazo
changamoto ambazo tunapaswa tusizifumbie macho. Kwa mfano ni kweli
tumeeneza skuli, lakini kwa sababu yale mahitaji ya elimu au mahitaji ya
skuli ni makubwa, ukweli ni kwamba ule ubora wa elimu bado haujafikiwa
kwa kiwango cha kuridhisha. Zamani darasa lilikuwa na wanafunzi kati ya
24 na 30, lakini sasa hivi si ajabu kukuta darasa lina wanafunzi 80 hadi
100. Sasa katika hali kama hiyo, ukweli mwalimu anakuwa na kazi pevu.
Pia kuna upungufu wa walimu wa Hesabu, Sayansi, Kingereza na Jographia.
Halikadhalika tuna upungufu wa zana za kufundishia, hasa kwa masomo ya
Sayansi.
Vile vile kwa sababu ya kupanuka kwa huduma, uwezo wetu wa kiuchumi
bado ni mdogo, hata huduma za afya hazijawa za kutosheleza. Wakati
mwengine tunakabiliwa na upungufu wa dawa hasa dawa ambazo ni muhimu
zaidi, upungufu wa wafanyakazi hasa madaktari na wafanyakazi wengine wa
sekta ya afya, kuna upungufu wa zana au vitendea kazi vya kutibia, Hizi
ni baadhi ya changamoto ambazo tunapambana nazo.
Serikali katika awamu zote imekuwa zikichukua hatua mbali mbali katika kupunguza matatizo hayo ambayo yanatukabili.
Changamoto nyengine ambayo imejitokeza katika siku za hivi karibuni
katika nchi yetu ni hili suala la vitendo vya hujuma, ikiwemo watu
kumwagiwa tindikali na hujuma za aina nyengine.
Napenda kusema kuwa haya ni mambo ya kusikitisha kabisa, kwa sababu sisi Wazanzibari tumezoweya kuwa nchi yetu ni nchi ya amani.
Haya mambo ya raia kutumia risasi au mashambulizi kwa kutumia tindikali
kwa Zanzibar ni mageni. Sisi ustaarabu wetu Wazanzibari, Utamaduni wetu
na dini zetu, masuala haya ya ukatili na hujuma sio mambo yetu kabisa.
Mambo haya yananisononesha na kunisikitisha sana, hasa kipindi hiki
ambacho tuna maridhiano katika nchi. Kama mambo haya yangetokea wakati
ule wa tofauti za kisiasa, tungesema ni hujuma za kisiasa, lakini leo
tunayo serikali ya pamoja. Kila chama ambacho kina viti katika Baraza la
Wawakilishi kinashirikishwa katika serikali hii ya Umoja wa Kitaifa.
Suala la kujiuliza kwanini jambo hili lizuke sasa? Ukweli ni mtihani
mkubwa kwetu.
Sisi Wazanzibari tumekuwa ni watu wa dini mbali mbali kwa muda mrefu.
Tokea enzi na enzi kiwango cha uvumilivu wa kidini ni kikubwa Zanzibar,
mimi nadhani hakuna duniani kuliko Zanzibar. Hapa inajulikana kabisa
kwamba asilimia 98 ni Waislamu. Lakini lazima wananchi wajue kwamba
Ukristo katika Afrika Mashariki na Kati, mlango wake uliopitia kwenda
huko ni Zanzibar.
Waheshimiwa Waandishi wa Habari
Jambo jengine zito linalotukabili katika kipindi hichi cha Serikali
ya Awamu ya Saba ni mchakato wa kupata Katiba Mpya ya Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania.
Mchakato huo unatokana na dhana na fikra za Rais wa Jamhuri ya Muungano
wa Tanzania, Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete. Yeye kwa busara zake ameona
kwamba sasa hivi miaka 50 imepita tangu Uhuru wa Tanganyika. Hivyo
tunahitaji kuandika Katiba Mpya ambayo itawashirikisha wananchi wenyewe.
Kwa hivyo mimi nimpongeze kwa dhati Rais Jakaya Kikwete kuona umuhimu
huu wa kuwashirikisha Watanzania wenyewe kuandika Katiba mpya. Yeye
alisema wazi kwamba baada ya miaka 50 lazima tuwe na katiba ambayo
inakidhi mahitaji ya wakati huu. Katiba ambayo angalau itatuchukua miaka
50 mingine. La msingi zaidi ni kuwa wananchi washirikishwe kikamilifu.
Ni uamuzi mzuri aliochukua Rais ingawa kuna changamoto zake. Hivi
sasa tumemaliza hatua ya Tume kukusanya maoni ya wananchi, pamoja na ili
hatua ya Mabaraza ya Katiba kuchambua Rasimu ya Kwanza ya Katiba hiyo.
Hatua inayoendelea hivi sasa ni Tume ya Mabadiliko ya Katiba kuendelea
kuchambua maoni ya Mabaraza hayo, na hatimaye iweze kupatikana rasimu ya
Pili ambayo ndiyo itapelekwa kwa Rais na yeye Rais kuiwasilisha kwenye
Bunge la Katiba.
Waheshimiwa Waandishi wa Habari
Hata hivyo, pamoja na azma njema ya kuifanya nchi yetu iwe na Katiba
mpya ifikapo mwakani, lazima tukiri kwamba changamoto nyingi zinaendelea
kujitokeza katika suala hili.
Waandishi wa habari mnakumbuka mfululizo wa matukio yaliyojiri, hasa
baada ya Serikali kuamua kuwasilisha Bungeni mswada wa kurekebisha
sheria ya Mabadiliko ya Katiba, pamoja na kadhia nzima ya vurugu
zilizojitokeza Bungeni hivi karibuni na kusababisha baadhi ya Wabunge wa
Upinzani, wakiwemo viongozi wa Kambi hiyo, kulalamika kutotendewa haki
na kuamua kutoka nje.
Baada ya yote yaliyotokea, Rais wa Jamhuri ya Muungano ameona busara
ya kukaa meza moja na viongozi wa vyama vyote vya siasa vilivyo
sajiliwa, ili kuyajadili kwa upeo wake mambo yanayo lalamikiwa. Kati ya
mdai ya msingi ni madai kwamba upande wa Zanzibar haujashirikishwa
katika mabadiliko ya sheria ya Mabadiliko ya Katiba na mambo mengine
mengi, ikiwemo muundo na upatikanaji wa Wabunge wa Bunge Maalum,
wasiokuwa Wabunge na Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi.
Matarajio yangu ni kwamba vikao vilivyofanyika na maazimio ya vikao
hivyo, kati ya Rais na Viongozi wa vyama vya siasa yataweza kuzaa
maafikiano mema, ili hatua zinazofuata katika suala zima la kuandika
Katiba mpya ziweze kuendelea kwa amani na utulkivu na matarajio ya
wananchi walio wengi yaweze kufikiwa.
Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais
Baada ya kueleza kwa kifupi baadhi ya masuala mabli mbali yanayogusa
nchi yetu kwa jumla, sasa naomba niruhusuni kuingia moja kwa moja katika
utendaji wa majukumu ya Idara na Tume zilizopo katika Ofisi yangu. Hizo
ni Tume ya Ukimwi Zanzibar, Tume ya Kuratibu na Kudhibiti Dawa za
Kulevya, Idara ya Mazingira na Idara ya Watu Wenye Ulemavu.
Tume ya Ukimwi
Tume hii ina umuhimu mkubwa na wa kipekee kwa ustawi na afya za
wananchi wa Zanzibar. Ndiyo maana ikapewa majukumu makuu ya kuhakikisha
kwamba Sera na Mikakati ya Taifa ya kupiga vita ukimwi zinaandaliwa na
kutekelezwa ipasavyo, nia ikiwa ni wananchi wetu wabaki salama na
wasiambukizwe Virusi vya Ukimwi.
Mambo mengine yanayotekelezwa kupitia Tume hii ni kutafuta rasilimali
zitakazo tumika katika kutekeleza Muitikio wa Kitaifa wa kupambana na
Ukimwi, kuimarisha uwezo wa wadau katika kufanyia kazi program za ukimwi
pamoja na kuratibu shughuli zao. Aidha majukumu mengine ya Tume ni
kushajiisha utoaji wa huduma za tiba na matunzo kwa watu walioathirika
na kuathiriwa, kufuatilia na kutathmini ufanisi wa mapambano dhidi ya
ukimwi, pamoja na kutoa taarifa zote zinazohusiana na Ukimwi.
Mafanikio makubwa yameweza kupatikana chini ya utendaji wa Tume hii.
Kwa mfano mwaka jana Tume hii iliweza kusaidia Shehia 22 kuibua Mipango
Mkakati ya kukabiliana na Ukimwi. Aidha, katika juhudi za kuongeza uwezo
wa program za habari na kuchochea mabadiliko ya tabia katika masuala ya
Ukimwi nyumba kadhaa za makaazi ya vijana walioacha dawa za kulevya
‘Sober Houses’ zimesaidiwa kwa kununuliwa televisheni na radio. Dada poa
wapatao 307 na kaka poa 38 na vijana 271 wanaojidunga sindano waliweza
kufikiwa kupatiwa taaluma kupitia waelimishaji rika.
Pia taasisi za Kidini zinaendelea kuhamasisha waumini wao kupitia
katika mikusanyiko ya kidini juu ya mbinu muafaka za kuzuia maambukizi
ya ukimwi, kusaidia upatikanaji wa taarifa za afya ya uzazi na usawa wa
kijinsia.
Tukiwa tumo katika utekelezaji wa Mkakati wa Pili wa Taifa wa
Kupambana na Ukimwi, Mapitio ya Sheria ya Tume ya Ukimwi Nam.3 ya mwaka
2002 yamefanyika na rasimu ya mswada wa marekebisho yake yanatarajiwa
kuwasilishwa katika Baraza la Wawakilishi karibuni.
Hata hivyo, pamoja na mafanikio katika juhudi hizo, bado changamoto
kubwa inatukabili, changamoto hiyo imejitokeza wazi baada ya Utafiti wa
mwisho uliofanywa juu ya Virusi vya Ukimwi na Malaria kuonesha kwamba
kiwango cha maambukizi ya Virusi vya Ukimwi Tanzania kwa mwaka
2011/2012, kwa upande wa Zanzibar kimepanda kutoka asilimia 0.6 hadi
asilimia 1. Taarifa hizi sio nzuri kwetu na nguvu ya pamoja inahitajika
kuhakikisha kwamba maambukizi zaidi yana zibitiwa.
Waheshimiwa Waandishi wa Habari
Tume ya Kuratibu na Kudhibiti Dawa za Kulevya
Kama mnavyoelewa, Zanzibar kama ilivyo kwa nchi nyengine Duniani,
miongoni mwa changamoto kubwa zinazojitokeza ni kuwalinda vijana wake
wasiathiriwe kwa matumizi ya dawa za kulevya, lakini pia kukomesha
uingizwaji na biashara ya dawa hizo kwa jumla.
Suala hili ni changamoto kubwa kwetu. Juhudi kubwa tunazichukua ikiwemo,
kuhakikisha Sheria ya Dawa za Kulevya inatekelezeka, mpango wa
utekelezaji wa sheria hiyo ‘Road Map’ tayari imeandaliwa. Katika mwaka
uliopita jumla ya watu 22 wamekamatwa kwa makosa ya dawa za kulevya,
kati yao wanaume ni 21 na mwanamke mmoja, ambapo jumla ya kesi 22 zipo
mahakamani. Wizara yangu tayari imeandaa rasimu ya kanuni ya Sheria ya
Dawa za Kelevya, ili kuona sheria hiyo inatekelezwa ipasavyo.
Aidha, vipindi vya redio na televisheni vilivyolenga kuinua mwamko wa
jamii juu ya athari za dawa za kulevya vimerushwa hewani kupitia vyombo
mbali mbali vya habari. Vile vile kampeni kubwa inafanyika maskulini,
ambapo kwa mwaka jana wanafunzi wapatao 6,270 Unguja na Pemba walipatiwa
elimu juu ya athari za dawa za kulevya.
Vile vile kwa kutambua mchango wa taasisi zisizokuwa za kiserikali,
katika mapambano dhidi ya dawa za kulevya, Tume imezipatia ruzuku nyumba
tisa za makaazi ya vijana wanaoacha matumizi ya dawa za kulevya (Sober
Houses), kwa ajili ya kusaidia mahitaji yao mbali mbali.
Jambo muhimu la kuzingatiwa katika kupiga vita dawa za kulevya
Zanzibar na kwengineko, ni kuendelea kutoa elimu, ili watu wote wakatae
kutumia dawa za kulevya. Kwani itakapofika pahala ambapo hakuna mtu
anayetaka kutumia, ni wazi kwamba hata yule muingizaji naye atakuwa
haingizi tena kwa sababu hakuna soko.
Waheshimiwa Wana Habari
Idara ya Mazingira
Hii nayo ni Idara muhimu sana katika kuhakikisha usalama wa wananchi
na uendelevu wa nchi yao katika suala zima la kuhakikisha mazingira
hayaharibiwi.
Kati ya majukumu makubwa yanayotekelezwa na Ofisi yangu, kupitia Idara
hii ni kukusanya na kuhifadhi taarifa za kimazingira, kwa azma ya
kusaidia utayarishaji na utekelezaji wa mipango na miradi ya
kimazingira. Vile vile kuhamasisha wananchi na wadau wote kuchukua hatua
za kuhifadhi mazingira pamoja na kutoa elimu ya mazingira kwa jamii
yetu.
Mbali na hayo majukumu mengine makubwa yanayosimamiwa chini ya Idara
hii ni kuhakikisha shughuli za kiuchumi na kimaendeleo haziwi chanzo cha
uharibifu wa mazingira. Mwaka jana tuliweza kukagua jumla ya miradi 65
ya mahoteli, miradi 15 ya uwekezaji imefanyiwa tathmini ya Athari za
Kimazingira. Aidha, kiwanda cha Makonyo kilichopo Wawi Pemba kimefanyiwa
ukaguzi wa kimazingira na ripoti yake imekabidhiwa Wizara ya Biashara,
Viwanda na Masoko, ikiwemo mapendekezo yaliyotolewa.
Waheshimiwa Waandishi wa Habari
Kukabiliana na Athari za Mabadiliko ya tabia nchi ni eneo jengine
ambalo nchi yetu inalipa umuhimu wa kipekee, hasa kwa maumbile ya nchi
yetu ikiwa ni ya visiwa vidogo. Kwa kawaida nchi kama hizi huathiriwa
sana na athari za mabadiliko ya tabianchi.
Zanzibar imeendelea kuwa mshirika muhimu katika umoja wa nchi za visiwa
katika Bahari ya Hindi (ISLANDS), na imekuwa ikinufaika kwa njia mbali
mbali na ushiriki huo katika kuandaa na kutekeleza mikakati na program
tafauti za kukabiliana na athari hizo na kuhifadhi mazingira kwa jumla,
pamoja na kwamba hadi sasa sio mwanachama kamili wa jumuiya hiyo.
Miongoni mwa mikakati yetu Zanzibar katika kukabiliana na athari za
mabadiliko ya tabia nchi, ni suala hilo kulihusisha moja kwa moja katika
ngazi za Shehia, ili wananchi wenyewe wahusike kikamilifu. Kamati 10 za
majaribio za usimamizi wa ukanda wa pwani tumezisaidia kuandaa mipango
ya utekelezaji ya usimamizi wa mazingira katika maeneo yao. Miongoni ya
Shehia hizo ni Nungwi, Chwaka, Nyamanzi na Mtende.
Kazi ya kuyatambua maeneo yaliyoingiliwa na maji ya chumvi na hivyo
kuathiri shughuli za kimaendeleo, kijamii na kiuchumi, ikiwemo kilimo
kote Zanzibar inaendelea. Hatua hii itatuwezesha kujua ukubwa wa tatizo
na hatua zinazofaa ziweze kuchukuliwa.
Ofisi yangu imejikita zaidi kuhakikisha kwamba, Sera, Sheria na
Kanuni za Mazingira zinatekelezwa. Kwa mfano kwa mwaka jana jumla ya
operesheni 117 zimefanyika Unguja na Pemba na watu 33 walikamatwa na
kuhukumiwa kwa faini ya TZS 3,280,000 kwa jumla. Operesheni za kudhibiti
mifuko ya plastiki zinaendelea. Mwaka jana kilo 670 za mifuko ya
plastiki ziliteketezwa katika eneo la Maruhubi.
Matarajio yetu ni kupata mafanikio makubwa zaidi katika utekelezaji
wa majukumu yetu, hasa baada ya Serikali kuidhinisha Sera mpya ya
Mazingira na Mpango wa Utekelezaji wa Usimamizi wa Mazingira kuandaliwa
kwa mujibu wa Sera hiyo Mpya ya Mazingira.
Waheshimiwa Wana Habari
Idara ya Watu Wenye Ulemavu
Idara hii yenye majukumu ya kuratibu masuala mbali mbali ya watu
wenye ulemavu Zanzibar, pia ina umuhimu mkubwa na wa kipekee katika
kuhakikisha haki sawa inapatikana miongoni mwa wananchi wote wa Zanzibar
bila ya kuwepo ubaguzi wa aina yoyote ile.
Katika kuhakikisha tunafanikisha hilo la kuleta usawa na kuona watu
wenye ulemavu wanapata fursa zote, ikiwemo za kielimu, kiuchumi na
kushirikishwa kikamilifu katika mambo yote yanayohusu nchi na jamii,
mkazo mkubwa tumeuweka katika kufanya kazi kwa pamoja na jumuiya zote
zilizopo za Watu Wenye Ulemavu.
Miongoni mwa Jumuiya hizo ni Jumuiya ya Wasioona Zanzibar (ZANAB),
Chama cha Viziwi (CHAVIZA), Umoja wa Watu Wenye Ulemavu (UWZ), Jumuiya
ya Maalbino Zanzibar (JMZ), Jumuiya ya Wanawake Wenye Ulemavu (JUWAUZA),
Shirikisho la Watu Wenye Ulemavu (ZADA), Chama Maalum cha Olympic kwa
Watu Wenye Ulemavu (SOZ) na jumuiya nyenginezo.
Hata hivyo lazima tukiri kwamba tuna changamoto kubwa ya uhaba wa
fedha, visaidizi na nyenzo nyengine kwa ajili ya kuweza kutosheleza
mahitaji yote kwa wenzetu Wenye Ulemavu.
Kutokana na hali hiyo, Serikali, taasisi zisizokuwa za kiserikali na
jamii kwa jumla, hatuna budi tushirikiane kwa pamoja katika kuwaandalia
mazingira mazuri zaidi ya kujiletea maendeleo na kuwarahisishia maisha
yao, na hatimaye tuweze kuondoa vikwazo vya aina zote na tujenge jamii
Jumuishi kwa Wote.
Kati ya mikakati yetu pia ni kuhakikisha Watu wote Wenye Ulemavu
Zanzibar wanatambuliwa. Katika kuendeleza usajili wa Watu Wenye Ulemavu
jumla ya Wilaya tisa zimefanyiwa usajili, zikiwemo tano Unguja na nne
Pemba, kwa azma ya kuweza kupata takwimu sahihi na kurahisisha upangaji
wa Sera na Mipango ya Maendeleo kwa Watu Wenye Ulemavu.
Ofisi yangu kupitia Idara hii imeendelea kutoa ruzuku kwa baadhi ya
jumuiya za watu wenye ulemavu, pamoja na kuandaa njia mbali mbali
zitakazowezesha kupunguza changamoto zinazojitokeza. Kati ya juhudi hizo
ni kuanzisha Mfuko wa Maendeleo ya Watu Wenye Ulemavu, ambapo kila
mwenye moyo wa kusaidia anaweza kutumia Mfuko huo kusaidia shughuli za
kimaendeleo kwa Watu Wenye Ulemavu.
Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais itaendelea na juhudi zake za
kuhakikisha Watu Wenye Ulemavu wanapata fursa na haki zote kama ilivyo
kwa wananchi wote. Aidha, Ofisi inatoa shukuruni nyingi na za dhati
kabisa kwa wananchi wote waliojitokeza na wanaoendelea kujitokeza
kusaidia Watu Wenye Ulemavu kwa njia mbali mbali.
Njia hizo ni misaada ya kifedha, matibabu na visaidizi. Miongoni mwa
watu waliotoa misaada hiyo ni pamoja na Wazanzibari wanaoishi nje ya
nchi, mtu mmoja mmoja ndani nchi, pamoja na jumuiya na taasisi mbali
mbali.
Kwa ufupi kabisa hayo ndiyo mambo tunayoyatekeleza.
Ahsanteni.
0 Weka maoni yako hapa:
Post a Comment
COMMENT HAPA