MAKALA MAALUM

MAKALA MAALUM YA SHOMARI KAPOMBE IMEANDALIWA NA  ANDREW CHALE

Yatima aliyefunika tuzo za Taswa 2011 Dar
*Alikuwa muokota mipira Jamhuri Moro

 
USIKU wa kuamkia Juni 15, utabaki kuwa wa kihistoria kwa kiungo chipukizi wa Simba na timu ya soka ya Tanzania , Taifa Stars, Shomari  Salum Kapombe.
 
Ni usiku ambao Kapombe alimwaga machozi, baada ya kutangazwa kuwa mwanasoka bora wa 2011 wa Chama cha Waandishi wa Habari za Michezo Tanzania (Taswa).
Usiku huo, mbali ya Kapombe kutwaa tuzo hiyo ya jumla, pia alibeba tuzo ya mwanasoka bora chipukizi wa mwaka huo kutokana na mchango mkubwa kwa timu yake ya Simba, akiwapiku Salum Aboubakar wa Azam FC.
 
Ni tuzo aliyostahili kutokana na mchango wake kwa timu yake ya Simba iliyomaliza msimu huo mabingwa wa Ligi Kuu ya Bara iliyofikia tamati Mei 6.
Wengi waliokuwepo kwenye ukumbi wa Diamond Jubilee, jijini Dar es Salaam na waliokuwa kifuatikia kupitia luninga, walipigwa butwaa kuona Kapombe akilia.
Kilichowashangaza wengi, ni kuona chipukizi huyo akilia katika mazingira ya furaha, akiitwa mbele kwenda kupokea tuzo yake.
 
Wakati wengine hicho kilikuwa kipindi cha furaha kwa Kapombe ikawa kinyume chake, akiwa kwenye wakati mgumu akirejesha hisia zake kwa wazazi wake waliotangulia mbele za haki kama ilivyo kwa aliyekuwa rafiki yake mkubwa katika klabu ya Simba, Patrick Mafisango.
Kuhusu wazazi, Kapombe alifiwa na baba yake mzazi (Salum Kapombe) wakati yeye akiwa na umri wa miaka mitatu.
 
Hiyo ikamfanya kwa kiasi kikubwa kulelewa na mama yake mzazi (Ester Shomari), hivyo kukosa mapenzi ya baba.
Zaidi ya hapo, shujaa huyu akiwa na umri wa miaka 10, mama yake naye akafariki.
Hiyo ikamfanya Kapombe alelewe na ndugu zake, akiwemo bibi yake Hilda Emilian, aliyekuwa akiishi Mafiga, Morogoro.
Hata hivyo, Kapombe akiwa na umri wa miaka 14, bibi yake huyo mzaa mama, naye akafariki.
Hiyo ikamlazimu Kapombe kulelewa na dada zake, Halima na Aisha Kapombe; wote wakiwa watoto yatima.
Baada ya Kapombe kuyatafakari magumu aliyopitia katika maisha yake akiwa yatima na mafanikio mbali ya wazazi wake, Kapombe anasema, kingine kilichomfanya alie, ni kuyakumbuka maneno ya rafiki yake Patrick Mutesa Mafisango.
Anasema, Mafisango nyota wa kimataifa wa Rwanda aliyefariki Mei 17, alikuwa mtu wake wa karibu akimtia moyo, ajitume zaidi kusaka mafanikio.
“Nilipowakumbuka wazazi wangu waliofariki, ndipo nilipojisikia huzuni kubwa, kama wangekuwa hai, wangeshuhudia nikipata tuzo,” anasema Kapombe.
Kapombe aliyetua Simba msimu uliopita akitokea timu ya Polisi Morogoro, wakati huo ikiwa Ligi Daraja la Kwanza , anasema alipomkumbuka Mafisango, alishindwa kuvumilia.
“Mafisango alikuwa mtu wangu wa karibu, alikuwa msaada mkubwa kwangu, akinipa ushauri wa kujituma zaidi, ili nifanikiwe,” anasema Kapombe.
Hata hivyo, kuna kitu yawezekana si wengi wanaokijua, kilichowafanya Mafisango na Kapombe wawe marafiki zaidi wakiwa Simba; wote ni watoto yatima.
Kapombe anasema, Mafisango alikuwa akimtia moyo akimtaka ajitume na kutokata tamaa, ili afanikiwe huku akimtolea magumu aliyokuwa amepitia hadi anatua Simba.
Ingawa ni raia wa DR Congo , alibadili uraia wake na kuwa Mrwanda ili aweze kufanikiwa katika malengo yake ya soka.
Hata ubini Mafisango, si jina la baba yake mzazi, bali mkwe wake. Alifanya hivyo kupata urahisi wa kuishi Rwanda kwenye harakati za kusaka mafanikio ya soka.
 
TUZO YA TASWA
 
 
Kutokana na mchango wake mkubwa kwa timu yake ya Simba tena akiwa chipukizi wa umri wa miaka 18, Kapombe amekuwa gumzo kubwa ndani na nje ya Simba.
Mchango wake kwa Simba, ndio ukamshawishi aliyekuwa Kocha Mkuu wa timu ya soka ya Tanzania , Taifa Stars, Jan Poulsen kumwita.
 
Mechi ya kwanza kwa Kapombe akiwa Stars, ilikuwa mechi ya kuwania nafasi ya kupangwa kwenye makundi ya kusaka tiketi ya fainali za Kombe la Dunia za mwaka 2014.
 
Stars wakianzia ugenini Novemba 11, 2011, licha ya ugeni wake kwenye kikosi hicho, Kapombe  alipangwa kikosi cha kwanza.
 
Katika mechi hiyo ambayo iliisha kwa Stars kushinda 2-1, Kapombe alionesha uwezo mkubwa ambao umemwezesha kuwamo hadi sasa chini ya Kocha Kim Poulsen.
 
Vitu vyake vya uhakika akiwa na timu yake na Simba na Stars, vyote hivyo vimemfanya awe kivutio kwa kila mpenda maendeleo ya soka.
 
Kwa uwezo wake dimbani na mchango wake kwa Simba na Stars, hata jina lake lilipotajwa kama chipukizi bora, hakuna aliyeshangaa.
 
Aidha, hata jina lake lilipotajwa kuwa mshindi wa jumla wa Tuzo ya Mwanamichezo Bora wa Chama 
cha Waandishi wa Habari za Michezo (Taswa), hakuna aliyesema hakustahili.
AMETOKEA WAPI KISOKA
 
Kapombe anasema, alianza kupenda soka tangu akiwa na miaka mitano, wakati huo akicheza chandimu mtaani kwao Mafiga, Morogoro.
Anasema, timu yake ya kwanza ni Santos FC, iliyokuwa ikishiriki michuano mbalimbali, akipata nafasi ya kujifunza mengi ya soka.
 
Kati ya michuano aliyowahi kucheza akiwa na Santos FC, ni ‘Serve Access Game’ iliyokuwa ikiandaliwa na taasisi ya kuibua vipaji ya  Morogoro Youth Academy .
 
KUOKOTA MIPIRA UWANJANI
 
Mbali ya kucheza Santos FC, pia Kapombe alikuwa kwenye timu iliyokuwa ikiundwa na vijana waokota mipira kwenye uwanja wa Jamhuri, Morogoro iliyojulikana kwa jina la ‘Jamhuri Ball Boys FC.
 “Nilipitia timu nyingi katika utoto wangu, Mafiga FC, Santos, Jamhuri Ball Boys, hadi nikaonwa na kituo cha Moro Youth Academy,” anasema Kapombe.
Anasema, kote alikopitia kisoka kwenye utoto wake, ndoto yake ilikuwa ni kufika mbali kisoka, hivyo kutwaa tuzo ya Taswa, ni mwanzo kwake.
“Nikiwa Ball Boys pale uwanja wa Jamhuri, nilikuwa na shauku kubwa ya kucheza timu kubwa kama 
 
Mtibwa Sugar, Simba, Yanga na nyinginezo nilizokuwa naziona Jamhuri.
“Nilijipa moyo, nikiongeza juhudi zangu katika mazoezi kutimiza ndoto hizo, kweli zimeanza kutimia,” anasema Kapombe.
 
Akiwa na umri wa miaka 14, wakati huo akiichezea Ball Boys, alipewa uhahodha katika michuano ya WINOME Cup na Serve Access Games.
Baada ya kung’ara, ndipo akatwaliwa na kituo Moro Youth, hivyo kupata nafasi ya kujifunza mengi zaidi.
 
WALIOCHANGIA MAFANIKIO
 
Kapombe anamtaja Kocha Yahya Belin aliyemnoa katika timu ya Jamhuri Ball Boys, akisema alikuwa akimpa mbinu nyingi na kumtaka asichague namba.
 
“Kocha Belin, alinipa siri kucheza namba nyingi uwanjani ili kupangwa mara nyingi, pia kuweza kuhama namba moja hadi nyingine kulingana na mazingira ya mchezo kuisaidia timu.”
Kutokana na uwezo wake mkubwa kiuchezaji, licha ya kuwa na umri wa miaka 15, alipandishwa kikosi cha vijana wa umri wa chini ya miaka 17 cha kituo hicho.
 
Akiwa kwenye timu hiyo, ndipo alipoteuliwa kwenye kikosi cha mkoa cha vijana wa chini ya miaka 17, kilichoshiriki michuano ya Copa Coca Cola mwaka 2008, huko nako akiwa nahodha.
Anasema, katika mashindano hayo walitolewa hatua ya robo fainali na Kigoma ambayo ilikuja kuwa mabingwa.
 
Kapombe anasema, baada ya michuano
hiyo, yeye na  Zahor Zeirani kutoka kikosi cha Morogoro, waliteuliwa kwenye timu ya Coca Cola Dream Team iliyokwenda Brazil .
 
Lakini, yeye Kapombe hakuungana na Kombaini hiyo ya Dream Team kutokana na kuwa mgonjwa, hivyo akarudi Morogoro na kujiunga na timu ya Polisi Morogoro.
Anasema, alikuwa ni kati ya nyota sita kutoka Kombaini ya Morogoro waliokuwa wametwalia na Polisi Morogoro, hivyo akapata nafasi ya kuonesha kipaji chake.
Akiwa kikosi cha pili cha Polisi Morogoro, mwaka 2009, Kapombe alishiriki michuano ya vijana wa timu za Ligi Kuu ‘Uhai Cup.
 
Kutokana na uwezo wake mkubwa, Kapombe alipandishwa hadi kikosi cha kwanza cha timu hiyo, kilichokuwa kikishiriki Ligi Kuu Tanzania Bara.
“Nakumbuka kulikuwa na mechi kati yetu na timu moja ya Arusha, katika mechi ile, alikuwepo Kocha Jamhuri Kihwelo ‘Julio.’
 
“Aliridhishwa na uwezo wangu, akanieleza ningekuwemo kwenye kikosi cha timu ya taifa ya vijana chini ya miaka 23, ndipo nilijiunga na kikosi hicho,” anasema.
Akiwa na U-23, Kapombe anasema alishiriki  kwenye hatua ya kuwania nafasi ya kucheza
Michuano ya All African Games na fainali za Olimpiki, akicheza mechi dhidi ya Cameroon , Nigeria na Uganda , hivyo kuzidi kupata uzoefu.
 
ALITUA VIPI SIMBA?
Anasema, Simba walimwona katika mechi ya kimataifa dhidi ya Cameroon kwenye uwanja wa Taifa, jijini Dar es Salaam .
 
Anasema, baada ya filimbi ya mwisho, alifuatwa na viongozi wa Simba wakimtaka ajiunge nayo, naye hakusita kwani ni kitu ambacho hakuwa amekitaraji katika umri wa miaka 17.
 
“Naikumbuka mechi baina ya U-23 dhidi ya Cameroon , mchezo uliochezwa kwenye dimba la Taifa, siku hiyo viongozi wa Simba walinifuata na kunitaka nijiunge nayo,” anasema.
 
“Nikamshukuru Mungu, kwangu ulikuwa mwanzo wa safari ya mafanikio kisoka, anasema Kapombe.
Anasema, baada ya kutua Simba, mechi yake ya kwanza ilikuwa dhidi ya timu kutoka Uganda kwenye Simba Day, Uwanja wa Sheikh Amri Abeid, jijini Arusha.
 
Anasema, wakiwa njiani kurejea jijini Dar es Salaam, aliyekuwa Kocha Mkuu wa timu hiyo, Moses Basena, akatangaza nyota 18 huku akimpa jezi namba 15 ya kikosi cha kwanza.
Anasema, mbali ya kupewa jezi, Basena alimsihi kucheza kwa kujiamini na mechi kubwa kwake ilikuwa mechi ya Ngao ya Hisani dhidi ya Yanga, akiingia kutokea benchi.
Kapombe anasema, anashukuru Mungu kumjalia uwezo kisoka kwani msimu wake wa kwanza akiwa Simba, ameweza kupangwa kikosi cha kwanza katika mechi zote.
 
KUITWA TAIFA STARS
 
“Siku nilipoitwa kwenye kikosi cha Stars, nilishangaa, kwa sababu naona kama ni mapema kwangu, lakini namshukuru Mungu,” anasema.
 
HISTORIA KWA UFUPI
 
Kapombe ni mtoto wa mwisho kwenye familia ya watoto watatu wa Mzee Salum Kapombe wa mjini Morogoro, aliyezaliwa Januari 28, 1992. Alipata elimu ya msingi katika shule ya Mwele, kuanzia 2000 hadi 2006 na baadaye elimu ya sekondari ya Lupanga.
Anasema, hiyo ni shule iliyo jirani na Chuo cha Ualimu Kigurunyembe, kuanzia 2007 hadi 2010.
 
SIFA ZA ZIADA
 
Amejaliwa uwezo wa kutumia miguu yote miwili, pia amekuwa akicheza namba zaidi ya moja ikiwemo kudaka.
Kapombe amekuwa akivutiwa na Haruna Moshi ‘Boban,’ akisema ndiye amekuwa akiiga uchezaji wake kwa hapa nchini.
Kimataifa, amekuwa akivutiwa na Tom Cleverley wa timu ya Manchester Utd ya England .
 
SHUKRANI
 
Anasema, hawezi kuwasahau makocha, wazazi wake na wengine wengi wakiwemo Catherine Ntevi, Godfrey Ngatimwa na Dennis Anthony kwani wamekuwa msaada mkubwa akiwa
jijini Dar es Salaam .
Aidha, anawashukuru makocha Belin, Allan Thigo na Rajabu Kindagule wa Moro Youth, John Tamba wa Polisi Morogoro, ‘Julio’, Moses Basena wa Simba Jan Poulsen aliyemwita mara ya kwanza Stars.
 
ASICHOKISAHAU
 
Kapombe anasema, katika maisha yake hatosahu walipokuwa safarini kuelekea mjini Younde , Cameroon , mwanzoni mwa mwaka huu.
Anasema, wakiwa angani, walikumbana na hali mbaya ya hewa hadi ndege kuanza kuyumba, hali ile ilimuweka kwenye wakati mgumu.
“Kwenye hali ile, wachezaji tulikuwa kwenye wakati mgumu sana , wengi wetu tulisema pengine ndiyo ulikuwa mwisho wa uhai wetu; hata hivyo tulifika salama,” anasema Kapombe.
                    
Mwisho
 
DONDOO MUHIMU;
 
JINA KAMILI: Shomari Salum Kapombe.
KUZALIWA: Januari 28, 1992.
MAHALI: Morogoro.
TIMU YA MTAANI: Santos Fc, Mafiga Kids
UTAIFA: Tanzania
ELIMU: Kidato cha nne
Mwandishi wa makala: 0719076376/chalefamily@yahoo.com
 
Mwisho

0 Weka maoni yako hapa:

Post a Comment

COMMENT HAPA