KUFUATIA GAZETI LA NIPASHE KOTOA HABARI HII YA KUMUHUSISHA NA UASI MAKAMBA AJIBU
Gazeti
la leo la Nipashe, katika ukurasa wa mbele, lina picha yangu na kichwa
cha habari kinachosema "Waziri Adaiwa Kuchochea Uasi: wananchi wavamia
kiwanda; aahidi kuwawekea wakili dhidi ya mwekezaji". Habari hii ina
nusu ukweli.
Ni kweli wana Bumbuli tumechoshwa na
mbia/mwekezaji katika kiwanda chetu cha chai na uongozi wa Chama cha
Wakulima wa Chai. Hali hii ilidhihirika wazi kwenye mkutano wangu na
wakulima wa chai siku ya Jumapili. Kwa miaka tisa sasa, wananchi
wamekuwa wanalalamika kuhusu kudhulumiwa, kunyanyaswa na kuonewa na
kutonufaika na zao lao la Chai. Nimefanya juhudi mbalimbali za kumaliza
tatizo hili, ikiwa ni pamoja na vikao zaidi ya vitatu kati yangu,
mwekezaji, viongozi wa wakulima, pamoja na Bodi ya Chai. Mwaka juzi,
niliongoza kikao cha wadau wa Chai Kanda ya Kaskazini na kupigania
kupandishwa bei ya chai kutoka shilingi 110 hadi 206. Hata hivyo, malipo
kwa wakulima yamekuwa yanacheleweshwa na taarifa za mapato na matumizi zimekuwa hazitolewi na mbia/mwekezaji.
Pia wapo viongozi wanaonufaika na dhuluma hizi, ikiwa ni pamoja na
kulipwa mshahara na mbia kila Mwezi pasipo kufanya shughuli yoyote.
Wakulima, ambao ni wamiliki wa kiwanda, sasa wamechoka. Wamechoshwa na
mbia wao na wamechoshwa na viongozi wao. Nami niko nao na nawaunga
mkono. Kama kuwaunga mkono watu wangu ni uasi, naikubali label hiyo.
Tutapigana hadi tupate haki yetu. Nitaweka wakili ili tutafute haki yetu
kisheria.
Niweke baadhi ya mambo sahihi:
1. Hakujatokea vurugu wala machafuko yoyote. Wananchi wameamua wenyewe kwenda kukaa nje ya kiwanda kulinda mali yao.
2. Tofauti na ilivyoripotiwa, hakuna uharibifu wowote wa mali
uliofanyika. Polisi wameenda kuangalia na kukuta kila kitu salama na
kuondoka.
3. Tunafanya jitihada mbalimbali kwa kushirikiana na
Bodi ya Chai ili wakulima wapate sehemu nyingine ya kuuza chai yao
wakati tunatafuta suluhu.
4. Wapo wanasiasa uchwara wanaodai
tuwe na amani na tukubali unyonyaji kisa tu kwamba siku zote tumekuwa
wapole tangu enzi za mababu. Watuache tudai haki yetu.
5.
Uamuzi huu ni wa wakulima wenyewe. Kusema eti wanachochewa ni
kuwatukana, kana kwamba ni wajinga ambao hawajui kipi sawa na kipi si
sawa.
0 Weka maoni yako hapa:
Post a Comment
COMMENT HAPA