Msemaji & Waziri Kivuli, Sheria, Katiba na Utawala Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, Tundu Antiphas Mughwai Lissu.
MAONI YA MSEMAJI MKUU WA KAMBI RASMI YA UPINZANI BUNGENI, WIZARA YA KATIBA NA SHERIA,
MHESHIMIWA TUNDU A.M. LISSU (MB.)
KUHUSU
MPANGO NA MAKADIRIO YA MAPATO NA MATUMIZI YA FEDHA YA WIZARA YA KATIBA NA SHERIA KWA MWAKA 2013/2014
(Kanuni ya 99(9) ya Kanuni za Kudumu za Bunge, 2013)
UTANGULIZI
Mheshimiwa Spika,
Ofisi ya Waziri wa Katiba na Sheria imeanzishwa kwa mujibu wa kipengele
cha 12 cha Nyongeza ya Waraka wa Rais uliochapishwa kama Tangazo la
Serikali Na. 494 la tarehe 17 Desemba 2010. Majukumu ya Ofisi hii
yameainishwa katika Tangazo la Ukasimishaji wa Majukumu ya Kiuwaziri la
mwaka 2010 (The Ministers [Assignment of Ministerial Functions] Notice,
2010) lililochapishwa katika Gazeti la Serikali kama Tangazo la Serikali
Na. 494A la tarehe 17 Desemba 2010. Kwa mujibu wa Nyongeza ya Pili ya
Tangazo hilo, pamoja na mengine, Ofisi ya Waziri wa Katiba na Sheria
imekasimiwa majukumu ya masuala ya kikatiba, uendeshaji na utoaji wa
haki, uendeshaji mashtaka na haki za binadamu. Kwa sababu ya matukio ya
hivi karibuni yanayohusu utendaji wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba katika
mchakato wa Katiba Mpya na kwa kuzingatia umuhimu wake katika
mustakbala wa taifa letu, tunaomba kuanza na masuala yanayoihusu Tume na
uendeshaji wake wa mchakato huo.
TUME YA MABADILIKO YA KATIBA NA MCHAKATO WA KATIBA MPYA
Mheshimiwa Spika,
Katika mwaka wa fedha 2012/2013, Tume ya Mabadiliko ya Katiba
iliidhinishiwa jumla ya shilingi bilioni 33.944 kwa ajili ya utekelezaji
wa majukumu yake kwa mujibu wa Sheria ya Mabadiliko ya Katiba, Sura ya
83 ya Sheria za Tanzania. Kwa mujibu wa Maelezo ya Makadirio ya Matumizi
Mengineyo kwa Mwaka wa Fedha 2013/2014 yaliyoletwa mbele ya Kamati ya
Katiba, Sheria na Utawala mwezi uliopita, hadi kufikia tarehe 25
Februari, 2013 Tume ilishapokea shilingi bilioni 18.473 kutoka Hazina na
ilikwishatumia shilingi bilioni 14.968, sawa na 81% ya fedha
zilizopokelewa. Kwa mujibu wa Maelezo hayo, shilingi bilioni 3.504
ambazo hazijatumika zimetengwa kwa ajili ya kulipia madeni kutokana na
huduma za uchapishaji wa Mwongozo wa Mabaraza ya Katiba, uratibu wa
mchakato wa kupatikana Wajumbe wa Mabaraza ya Katiba na gharama nyingine
za uendeshaji wa Ofisi.
Maelezo ya Tume yanaonyesha kwamba
shillingi bilioni 15.471 ambazo hazijatolewa na Hazina zitatumika kwa
ajili ya kusambaza nakala milioni moja za Rasimu ya Katiba Mpya
(shilingi bilioni 3.848); elimu kwa umma juu ya Rasimu ya Katiba Mpya
(shilingi milioni 400); kuratibu na kuendesha Mabaraza ya Katiba kwa
nchi nzima (shilingi bilioni 4.734); na shilingi bilioni 6.488 kwa ajili
ya matumizi mengine pamoja na ‘stahili za Wajumbe na Sekretarieti.’
Mheshimiwa Spika,
Katika Maoni yetu ya mwaka jana, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni
ililalamikia kile ilichokiita “... matumizi yasiyoelezeka na
yasiyokubalika ya fedha za umma hasa hasa katika mazingira ambayo
wananchi wanahubiriwa na watawala kwamba miradi ya maendeleo yao ya
kiuchumi na kijamii haitekelezeki kwa sababu ya ufinyu wa bajeti ya
Serikali.” Aidha, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni ilidai kwamba shilingi
bilioni 14.633 zilizotengwa kwa ajili ya kuwalipa wajumbe na watendaji
wa Tume posho mbali mbali zilikuwa zinatishia kuigeuza “heshima ya
kutumikia waliyopewa wajumbe wa Tume kuwa hongo ya Serikali.” Madai ya
Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni kuitaka Serikali ieleze Bunge hili
tukufu gharama zote za kila Mjumbe wa Tume, Sekretarieti na watumishi
wengine wote wa Tume “ili Wabunge na wananchi wa Tanzania wafahamu kodi
wanazolipa zinavyotumika katika mchakato wa Katiba Mpya” yalikataliwa na
Serikali kwa hoja kwamba taarifa hizo ‘ni siri kati ya mwajiri na
mwajiriwa.’
Mheshimiwa Spika,
Bunge lako tukufu
linaombwa kuidhinisha shilingi bilioni 33.944, kiasi kile kile
kilichoidhinishwa mwaka jana, kwa ajili ya matumizi ya Tume kwa mwaka wa
fedha 2013/14. Kiasi hiki ni pamoja na shilingi bilioni 12.193 kwa
ajili ya “... kulipia posho za vikao kwa Wajumbe wa Tume 34 na
Sekretarieti 160 ...”; shilingi bilioni 1.728 ambazo “... zitalipia
posho ya kujikimu kwa ajili ya Wajumbe na Sekretarieti wanaposafiri
ndani ya nchi kikazi”; na shilingi bilioni 1.650 kwa ajili ya “...
kulipa gharama za nyumba za Wajumbe na Sekretarieti wanaotoka nje ya Dar
es Salaam.”
Aidha, kuna shilingi milioni 18 zinazoombwa “...
kwa ajili ya kugharamia chakula kwa Wajumbe wa Tume na Sekretarieti
watakaokuwa wamepata maambukizi ya ukimwi”; shilingi milioni 60 kwa
ajili ya usafiri wa ndani; shilingi milioni 50 kwa ajili ya gharama za
malazi kwa Wajumbe wa Tume na Sekretarieti ‘wanaposafiri kikazi’;
shilingi milioni 423 kwa ajili ya ‘chai na vitafunwa’; na shilingi
milioni 50 kwa ajili ya “... wahudumu wanaosaidia kazi za Tume wakiwa
mikoani wakati wa kushiriki kwenye Mabaraza ya Katiba na zoezi la
upigaji kura ya maoni.”
Vile vile, Mheshimiwa Spika, Bunge lako
tukufu linaombwa kuidhinisha shilingi milioni 60 ya kulipia maji kwa
matumizi ya ofisi za Tume; shilingi milioni 30 “... kwa ajili ya kulipia
gharama za usafiri wa basi na taxi kwa Wajumbe na Sekretarieti
watakaposafiri ndani ya nchi kikazi”; na shilingi milioni 103 kwa ajili
ya kulipia gharama za simu za mikononi.
Mheshimiwa Spika,
Bunge lako tukufu linaombwa kuidhinisha posho na ulaji zaidi ya huu kwa
ajili ya wajumbe na Sekretarieti ya Tume. Ulaji huu mwingine
unajumuisha shilingi milioni 604 “... kwa ajili ya posho kwa Wajumbe wa
Tume na Sekretarieti wakati wa Bunge Maalum la Katiba.” Maelezo ya Tume
yamejaribu kuhalalisha matumizi ya fedha hizi za ziada kwa kuzibatiza
jina la ‘hardship allowances’, yaani ‘posho ya mazingira magumu’, wakati
vikao vya Bunge Maalum la Katiba vitafanyika Dar es Salaam au hapa
Dodoma!
Vile vile, katika ulaji huu mpya zipo shilingi milioni
266 zinazoombwa “... kwa ajili ya chakula na viburudisho wakati wa vikao
vya Bunge Maalum la Katiba”; shilingi milioni 12 nyingine “... kwa
ajili ya huduma za chakula na viburudisho kwa shughuli zinazohusiana na
Tume”; na shilingi milioni 185 kwa ajili ya kulipia “... usafiri wa basi
na taxi....” Aidha, kuna shilingi milioni 30 za “... utengenezaji wa
T-shirts na kofia kwa Wajumbe wa Tume na Sekretarieti wakati wa
kushiriki kwenye zoezi za uhamasishaji kuelekea upigaji wa kura ya
maoni”; shilingi milioni 40 nyingine kwa ajili ya “... utengenezaji wa
sare wakati wa maadhimisho mbali mbali ya kitaifa”; na shilingi milioni
12 “... kwa ajili ya posho za kujikimu kwa watumishi wa Tume
watakaohudhuria kwenye maadhimisho mbali mbali ya kitaifa....” Zaidi ya
hayo, kuna shilingi bilioni 1.307 zinazoombwa kwa ajili ya “... posho za
kujikimu kwa ajili ya Wajumbe na Sekretarieti ya Tume wanaposafiri
ndani ya nchi wakati wa kushiriki kwenye zoezi la upigaji wa kura ya
maoni”; na shilingi milioni 218 kwa ajili ya “... ununuzi wa mafuta ya
magari ya Tume wakati wa kushiriki zoezi la uhamasishaji kuelekea
upigaji wa kura ya maoni.”
Kwa ujumla, Mheshimiwa Spika, Bunge
lako tukufu linaombwa kuidhinisha jumla ya shilingi bilioni 19.039 kwa
ajili ya posho za aina mbali mbali na malipo mengine yanayowahusu
Wajumbe na Sekretarieti ya Tume kwa mwaka wa fedha 2013/14. Hii ni zaidi
ya 56% ya bajeti yote inayoombwa kwa ajili ya Tume. Kwa ulinganisho,
posho na malipo mengine yanayowahusu Wajumbe na Sekretarieti ya Tume
yalikuwa shilingi bilioni 14.633 au 43% ya bajeti yote ya mwaka wa fedha
uliopita. Hii ina maana kwamba gharama za moja kwa moja za Wajumbe na
Sekretarieti ya Tume zitaongezeka kwa zaidi ya shilingi bilioni 4.406 au
zaidi ya 30% ya gharama za mwaka jana kama Bunge lako tukufu
litaidhinisha maombi haya!
Mheshimiwa Spika,
Maombi
haya ya mabilioni ya fedha za wananchi yanatoa uvundo na harufu mbaya ya
ufisadi, na hayaelezeki na wala kukubalika kwa misingi ya kisheria, na
kwa rekodi ya utendaji kazi wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba. Kwanza
kabisa, kwa mujibu wa kifungu cha 7(1) cha Sheria ya Mabadailiko ya
Katiba, Tume ina Wajumbe wasiozidi thelathini pamoja na Mwenyekiti na
Makamu Mwenyekiti wake.
Kwa maana hiyo, Kambi Rasmi ya Upinzani
Bungeni inataka kujua uhalali wa maombi ya shilingi bilioni 12.193 kwa
ajili ya posho za vikao kwa Wajumbe 34 wa Tume wanaotajwa katika
kijifungu 210321 cha kasma 210300 kwenye randama ya Fungu 08 linalohusu
Tume. Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inataka kujua Wajumbe hawa wanne
wa ziada ni akina nani na wameteuliwa lini kuwa Wajumbe wa Tume? Aidha,
Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inataka kuelezwa, inakuwaje Tume iwe na
Wajumbe 34 wakati Sheria iliyoiunda inataka Tume yenye Wajumbe wasiozidi
thelathini?
Pili, kwa mujibu wa kazi za Tume kama
zilivyoainishwa katika kifungu cha 9 cha Sheria; na kwa mujibu wa
utaratibu wa utendaji kazi wa Tume kama ulivyofafanuliwa katika Sehemu
ya Nne ya Sheria; na kwa kuzingatia masharti ya kifungu cha 22(1) cha
Sheria hiyo, Wajumbe na Sekretarieti ya Tume sio wajumbe wa Bunge Maalum
la Katiba. Badala yake, uhusiano pekee wa kisheria uliopo kati ya Tume
na Bunge Maalum ni ule uliotajwa katika vifungu vya 20(3), 20(4) na
25(2) vya Sheria vinavyomruhusu Mwenyekiti wa Tume kuwasilisha Rasimu ya
Katiba Mpya kwenye Bunge Maalum, na kuwaruhusu Mwenyekiti na wajumbe
“... kutoa ufafanuzi utakaohitajika wakati wa majadiliano katika Bunge
Maalum.”
Hii ina maana kwamba mara baada ya kuwasilisha Rasimu
ya Katiba Mpya, Mwenyekiti wa Tume anakuwa functus officio, yaani hana
kazi nyingine yoyote ya kufanya kwenye Bunge Maalum. Aidha, Mwenyekiti
na Wajumbe wa Tume hawana kazi nyingine yoyote ya kufanya katika Bunge
Maalum hadi hapo watakapohitajika na Bunge Maalum kwa ajili ya kutoa
ufafanuzi wa jambo lolote linalohusu Rasimu ya Katiba Mpya.
Wakishatoa ‘ufafanuzi utakaohitajika’ walioitiwa, nao pia wanakuwa
functus officio. Kwa sababu hizo, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni
inataka kujua uhalali wa shilingi bilioni 1.055 ambazo Bunge lako tukufu
linaombwa kuziidhinisha kwa ajili ya posho, chakula na viburudisho na
usafiri wa basi na taxi kwa Wajumbe wa Tume na Sekretarieti wakati wa
vikao vya Bunge Maalum la Katiba.
Tatu, kwa mujibu wa kifungu
cha 33(2) cha Sheria ya Mabadiliko ya Katiba, jukumu pekee la Tume
katika hatua ya uhalalishaji wa Katiba Mpya ni “... kutoa elimu ya uraia
na uhamasishaji juu ya Katiba inayopendekezwa kwa muda usiozidi siku
thelathini kuanzia siku ya kuchapishwa katika Gazeti la Serikali.” Kwa
kazi ya mwezi mmoja tu Wajumbe na Sekretarieti ya Tume wanaombewa
shilingi bilioni 1.307 kwa ajili ya posho za kujikimu. Kwa mahesabu
hayo, kila Mjumbe wa Tume, Katibu na Naibu Katibu pamoja na wakuu wa
vitengo saba vya Tume na madereva wa kila mmoja wao watalipwa wastani wa
shilingi milioni 16.756 kwa mwezi huo mmoja, au shilingi 558,547 kama
posho ya kujikimu kwa kila siku moja!
Mheshimiwa Spika,
Katika nchi ambayo wauguzi katika hospitali za umma wanalipwa mshahara
wa kuanzia wa takriban shilingi 360,000 kwa mwezi; na walimu wa shule za
msingi wanaanzia shilingi laki mbili na nusu na wale wa sekondari
shilingi 325,000 kwa mwezi, malipo haya kwa Tume ya Mabadiliko ya Katiba
yana uvundo na harufu mbaya ya rushwa kwa Wajumbe wa Tume!
Hivyo basi, kwa vile kifungu cha 14(2) cha Sheria ya Mabadiliko ya
Katiba kinatamka kwamba Wajumbe wa Tume na Sekretarieti “watalipwa kwa
mujibu wa sheria na kanuni za nchi”, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni
inaitaka Serikali hii ya CCM iliambie Bunge lako tukufu ni sheria na
kanuni zipi za nchi yetu ambazo zimetumika kuhalalisha malipo haya
makubwa kwa Wajumbe na Sekretarieti ya Tume.
Aidha, Kambi Rasmi
ya Upinzani Bungeni inaitaka Serikali hii ya CCM itoe kauli rasmi mbele
ya Bunge lako tukufu kama kuna uhalali wowote wa kutumia fedha za
wananchi wa Tanzania ili kununua ‘chakula maalum’ (special foods) kwa
ajili ya Wajumbe na Sekretarieti ya Tume watakaopata ukimwi kwa sababu
ya kuendekeza ngono zembe na starehe zao binafsi wakati wanatakiwa
wafanye kazi ya Tume! Vinginevyo, Bunge lako tukufu lielezwe kwa ufasaha
ni kwa namna gani mchakato huu wa Katiba Mpya unatazamiwa kusababisha
maambukizi ya ukimwi kwa Wajumbe na Sekretarieti ya Tume!
Kwa
Serikali kujificha nyuma ya pazia la ‘siri ya mwajiri na mwajiriwa’
hakutoshi tena, kwani ni kulizuia Bunge lako tukufu kutekeleza wajibu
wake kikatiba wa kuisimamia Serikali chini ya ibara ya 63(2) ya Katiba
ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Sura ya 2 ya Sheria za Tanzania.
Aidha, ni haki kwa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni kujua uhalali wa
malipo haya kwani, kwa mujibu wa ibara ya 63(3)(a) ya Katiba, Bunge lako
tukufu “laweza kumuuliza Waziri yeyote swali lolote kuhusu mambo ya
umma katika Jamhuri ya Muungano ambayo yako katika wajibu wake....”
Mheshimiwa Spika,
Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inataka kujua shilingi milioni 218 kwa
ajili ya ununuzi wa mafuta ya magari ya Tume zitatumikaje ndani ya
kipindi cha siku thelathini za uhamasishaji na kuelimisha wananchi
kupiga kura ya maoni kwa Katiba Mpya. Hii ina maana kwamba hata kama
kila Mjumbe wa Tume, Katibu, Naibu Katibu na wakuu wa vitengo saba vya
Tume watapewa gari moja kwa kila mmoja wao kwa kipindi hicho, kila gari
itatumia wastani wa shilingi 186,325 kwa siku kwa ajili ya mafuta tu!
Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inataka kujua ni safari zipi hizo za
Tume ambazo zitalazimu matumizi ya full tank ya mafuta kila siku kwa
mwezi mzima? Huu, kama Baba wa Taifa Mwalimu Nyerere alivyowahi kusema,
ni ‘wizi mtupu’!
Mheshimiwa Spika,
Amlipaye mpiga
zumari ndiye achaguaye wimbo. Baada ya Tume kulipwa mabilioni yote
tuliyoyapigia kelele kwenye Maoni yetu ya mwaka jana, kuna ushahidi
kwamba Tume imekuwa inacheza wimbo uliochaguliwa na CCM na Serikali
yake. Mwezi Februari ya mwaka huu, Tume ilichapisha Mwongozo Kuhusu
Muundo, Utaratibu wa Kuwapata Wajumbe wa Mabaraza ya Katiba ya Wilaya
(Mamlaka za Serikali za Mitaa) na Uendeshaji Wake.
Mwongozo huo
ulisainiwa na Mwenyekiti wa Tume Jaji Joseph Sinde Warioba na ulianza
kutumika tarehe 1 Machi, 2013. Ingawa Tume imedai kwamba Mwongozo huo
ulitolewa kwa kuzingatia matakwa ya Sheria ya Mabadiliko ya Katiba,
Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inaamini kwamba Mwongozo ulitolewa
kinyume na matakwa ya Sheria hiyo na kwa lengo la kuinufaisha CCM na
washirika wake.
Mheshimiwa Spika,
Kifungu cha 17(8)
cha Sheria kinailazimu Tume kubuni “... utaratibu unaofanana ambao
utatumika katika kila upande wa Jamhuri ya Muungano katika ukusanyaji na
uchambuzi wa maoni ya wananchi, uendeshaji wa mabaraza na uandaaji wa
ripoti.” Katika utekelezaji wa majukumu yake, Tume inatakiwa kufuata
msingi huu mkuu “isipokuwa kama mazingira yatahitaji vinginevyo....”
Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inatambua kwamba, kwa kiasi kikubwa,
Tume iliweka utaratibu unaofanana ambao ulitumika katika hatua ya
ukusanyaji wa maoni ya wananchi katika kila upande wa Jamhuri ya
Muungano.
Kwanza, Tume haikuweka utaratibu wowote wa maana wa
kutoa elimu kwa wananchi juu ya masuala yote yanayohusu Katiba Mpya ili
kuwaandaa wananchi kuchangia maoni yao kwa Tume wakiwa na uelewa wa
kutosha. Badala yake, wakati wa mikutano ya Tume ya kupokea maoni ya
wananchi, wajumbe wa Tume walipewa jukumu la kuwaeleza wananchi juu ya
Katiba Mpya kwa muda usiozidi nusu saa. Hii ilifanyika katika mikutano
yote ya Tume katika kila upande wa Jamhuri ya Muungano.
Pili,
muda uliowekwa na Tume wa kukusanya maoni ya wananchi ulikuwa mdogo sana
ukilinganisha na ukubwa wa nchi yetu na wingi wa Watanzania. Katika
Majimbo karibu yote ya uchaguzi, Tume iliendesha wastani wa mikutano
saba kwa kila jimbo kwa lengo la kukusanya maoni ya wananchi. Lakini huu
ni wastani tu, katika majimbo mengi, Tume ilifanya mikutano minne au
mitano tu. Hili pia lilifanyika katika kila upande wa Jamhuri ya
Muungano.
Tatu, katika mikutano yote ya ukusanyaji maoni,
wananchi walitakiwa kutoa maoni yao kuhusu Katiba Mpya kwa muda wa
dakika tano kila mmoja na mikutano yenyewe ilichukua muda wa masaa
matatu ikiwa ni pamoja na muda wa kutambulishana wajumbe wa Tume na
mambo mengine yaliyo nje ya kuchukua maoni ya wananchi. Hii ilifanyika
hata kwa Wabunge wakati Tume ilipokuja kuchukua maoni ya Wabunge hapa
Dodoma. Utaratibu huu ulitumika katika kila upande wa Jamhuri ya
Muungano. Aidha, utaratibu unaofanana katika kila upande wa Jamhuri ya
Muungano ulitumika pia kukusanya maoni ya makundi maalum kama vile vyama
vya siasa, taasisi zisizokuwa za kiserikali, mashirika ya kidini na
hata taasisi za kiserikali na viongozi wake, wa sasa na waliostaafu.
Mheshimiwa Spika,
Wakati Tume iliweka utaratibu unaofanana katika kila upande wa Jamhuri
ya Muungano wakati wa zoezi la kukusanya maoni ya wananchi, Tume hiyo
hiyo iliweka utaratibu tofauti na wa kibaguzi katika hatua ya kuunda
Mabaraza ya Katiba ya Wilaya. Kwanza, Tume iliweka ngazi mbili za
uchaguzi wa wajumbe wa Mabaraza kwa upande wa Tanzania Bara wakati kwa
upande wa Zanzibar Tume iliweka ngazi moja tu ya uchaguzi.
Hivyo, kwa mfano, aya ya 6.1.4 ya Mwongozo wa Tume imeweka Mkutano Mkuu
Maalum wa Kijiji au Mtaa “ambao utakuwa na agenda moja tu ya
kuwapendekeza kwa kuwapigia kura watu wanne ambao majina yao
yatawasilishwa kwenye Kamati ya Maendeleo ya Kata.” Hii ni ngazi ya
kwanza ya uchaguzi wa wajumbe wa Mabaraza kwa upande wa Tanzania Bara na
kazi yake ni kupendekeza tu.
Baada ya hapo majina ya watu
walioshinda katika uchaguzi wa ngazi ya Kijiji au Mtaa yatawasilishwa
kwa Afisa Mtendaji wa Kata “ambaye ataitisha Kikao Maalum cha Kamati ya
Maendeleo ya Kata, ambacho ... kitachagua majina manne ...” ya wajumbe
wa Baraza la Katiba la Wilaya. (aya ya 6.1.8, 6.1.9 na 6.1.10) Hii ni
ngazi ya pili na ndiyo inayoamua nani awe mjumbe wa Baraza la Katiba la
Wilaya kwa upande wa Tanzania Bara na nani asiwe.
Kwa upande wa
Zanzibar, ngazi ya uchaguzi ni moja tu, Mkutano wa Shehia ambao, kwa
mujibu wa aya 6.3.4 ya Mwongozo wa Tume, “... utakuwa na agenda moja tu
ya kuwapigia kura ya siri watu watatu ... ambao majina yao
yatawasilishwa kwa Mkurugenzi wa Baraza la Manispaa au Katibu wa
Halmashauri ya Mji au Wilaya ambapo Shehia hiyo ipo.” Kwa utaratibu huu,
wajumbe wa Mabaraza ya Katiba ya Wilaya kwa upande wa Tanzania Bara
wamechaguliwa na watu wanne au watano tu ambao ni wajumbe wa WDC wakati
wajumbe wa Mabaraza ya hayo kwa upande wa Zanzibar wamechaguliwa na watu
wote walioshiriki katika Mkutano wa Shehia.
Wajumbe wa
Mabaraza ya Katiba ya Wilaya kwa upande wa Zanzibar wana uhalali wa
kisiasa kwa sababu wanawakilisha matakwa ya wananchi waliowachagua moja
kwa moja bila mchujo, wakati wajumbe wa Mabaraza ya Katiba ya Wilaya kwa
upande wa Tanzania Bara hawana uhalali wowote wa kisiasa kwa sababu
wanawakilisha maslahi ya CCM ambayo ndiyo inayotawala asilimia zaidi ya
themanini ya WDC zote ambazo ndio zilizowachuja wajumbe hao.
Mheshimiwa Spika,
Eneo la pili linalothibitisha kwamba utaratibu wa Tume ni wa kibaguzi
ni katika uendeshaji wa mikutano ya uchaguzi wa wajumbe wa Mabaraza ya
Katiba ya Wilaya. Kwa mujibu wa aya ya 6.1.4 ya Mwongozo wa Tume, kwa
upande wa Tanzania Bara Mkutano Maalum wa Kijiji au Mtaa “...
utaendeshwa na Mwenyekiti wa Kijiji au Mtaa, ambapo Afisa Mtendaji wa
Kijiji au Mtaa atakuwa Katibu wa Mkutano na ndiye atakayewasilisha
majina ya wananchi walioomba kuingia kwenye Baraza la Katiba la Wilaya.”
Hata hivyo, kwa upande wa Zanzibar kwa mujibu wa aya ya 6.3.5 ya
Mwongozo wa Tume, “Mkutano wa Shehia utachagua Mwenyekiti na Katibu wa
Mkutano huo kutoka miongoni mwa wananchi waliohudhuria Mkutano. Katibu
ndiye atakayewasilisha kwenye Mkutano majina ya wananchi wote walioomba
kuwa wajumbe wa Mabaraza ya Katiba ya Wilaya....” Karibu Maafisa
Watendaji wa Vijiji na Mitaa wote wa Tanzania Bara ni wanachama na
makada wa CCM, ilhali zaidi ya 90% ya Wenyeviti wa Vijiji na Mitaa wote
ni wanachama na makada wa chama hicho.
Kwa maana hiyo, mikutano
ya uchaguzi wa Mabaraza ya Katiba ya Wilaya kwa upande wa Tanzania Bara
imeendeshwa na makada wa CCM wakati kwa upande wa Zanzibar mikutano
imeendeshwa na viongozi waliochaguliwa na wananchi walioshiriki katika
mikutano hiyo bila kujali itikadi au uanachama wao katika vyama vya
siasa. Ndiyo maana, karibu nchi nzima ukiacha Zanzibar, kwa mujibu wa
taarifa ilizo nazo Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, wananchi wengi
wasiokuwa wanachama wa CCM ambao walipata kura nyingi katika kura za
mikutano ya uchaguzi ya Vijiji na Mitaa walienguliwa kwenye michujo
iliyofanyika katika Kamati za Maendeleo za Kata zilizowekwa kwa mujibu
wa Mwongozo wa Tume.
Mheshimiwa Spika,
Hata mahali
ambapo wananchi wasiokuwa wanaCCM walifanikiwa kupenyeza katika
chekecheke la mchujo wa WDC wamefanyiwa mizengwe na wanaCCM ili
waondolewe katika orodha ya wajumbe wa Mabaraza ya Katiba ya Wilaya.
Mfano mzuri ni yaliyomkuta Bw. Beatus Kipeya aliyechaguliwa mjumbe wa
Baraza la Katiba la Wilaya ya Arusha Mjini kwa kupitia Kata ya
Sombetini. Mara baada ya Bw. Kipeya kuchaguliwa kwenye kikao cha Kamati
ya Maendeleo ya Kata ya Sombetini cha tarehe 8 Aprili, 2013, siku hiyo
hiyo Katibu wa CCM Wilaya ya Arusha Allan G. Kingazi alimwandikia Mkuu
wa Wilaya ya Arusha barua ya malalamiko juu ya kuchaguliwa kwa Bw.
Kipeya.
Pamoja na kumpa Mkuu wa Wilaya ‘salaam za Chama’ chao,
Katibu wa CCM Kingazi alilalamika kwamba Afisa Mtendaji wa Kata ya
Sombetini amemruhusu “... raia wa Burundi Bwana Beatus Ndanyahubwi Kipea
(ambaye katika kugombea ametumia jina la Beatusi Kipea ili asijulikane
kama ni Mrundi – ila mtu wa Kigoma yaani Muha) kugombea nafasi ya Ujumbe
wa Baraza la Katiba la Wilaya na akashinda, kinyume na maagizo ya Tume
ya Katiba, kwamba Mjumbe ni lazima awe Raia wa Tanzania.”
Baada
ya maelezo mengi kuhusu ‘Urundi’ wa Bw. Kipeya, Katibu wa CCM Kingazi
anamwambia Mkuu wa Wilaya yafuatayo: “... (N)ashauri matokeo ya Uchaguzi
wa Wajumbe wa Baraza la Katiba ufutwe na utangazwe upya. Aidha, Afisa
Mtendaji huyo achukuliwe hatua za kinidhamu kwa kuvuruga kwa makusudi
Uchaguzi wa Muundo wa Baraza la Katiba la Wilaya.”
Mheshimiwa Spika,
Kitu cha kwanza cha kushangaza kuhusu barua ya Katibu wa CCM Kingazi ni
kwamba aliyetumiwa malalamiko ni Mkuu wa Wilaya ambaye, kwa mujibu wa
ibara ya 42(3), 44(3) na 46(3) ya Katiba ya CCM Toleo la 1982, Mkuu wa
Wilaya ni mjumbe wa Mkutano Mkuu wa CCM Wilaya, Halmashauri Kuu ya CCM
Wilaya na Kamati ya Siasa ya Halmashauri Kuu ya CCM Wilaya. Kwa mujibu
wa Sheria ya Mabadiliko ya Katiba na Mwongozo wa Tume, Mkuu wa Wilaya
hana mamlaka yoyote kushughulikia jambo lolote linalohusu uchaguzi wa
Wajumbe wa Mabaraza ya Katiba ya Wilaya. Kwa maana hiyo, sababu pekee ya
Mkuu wa Wilaya ya Arusha kuandikiwa malalamiko haya ni kwa sababu ni
kada wa CCM!
Mheshimiwa Spika,
Ukiacha Afisa Uhamiaji
wa Mkoa wa Arusha, watu wengine wote walionakiliwa barua ya malalamiko
ya Katibu wa CCM Kingazi ni makada wa CCM. Hivyo basi, nakala za
malalamiko hayo zinaonyeshwa kupelekwa kwa Katibu Mkuu wa CCM Taifa,
Katibu wa CCM Mkoa, Mkuu wa Mkoa (ambaye pia ni mjumbe wa vikao vyote
vya kikatiba vya CCM katika ngazi ya mkoa), Afisa usalama wa Taifa na
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Jiji la Arusha. Wote hawa
hawahusiki kisheria kwa namna yoyote ile katika mchakato wa uundaji wa
Mabaraza ya Katiba ya Wilaya. Chombo pekee ambacho kinahusika kisheria
na mchakato wa kuunda Mabaraza hayo na ambacho kilitoa Mwongozo wa namna
ya kuyaunda, yaani Tume, haikuandikiwa wala kunakiliwa barua ya
malalamiko ya Katibu wa CCM Kingazi!
Mheshimiwa Spika,
Mara tu baada ya Afisa Uhamiaji Mkoa wa Arusha Bw. R. Gowelle kupata
nakala yake, alimwandikia Bw. Kipeya barua ya ‘wito wa kufika ofisi ya
uhamiaji Mkoa wa Arusha’, ambapo alimtaka kufika ofisini kwake ‘bila
kukosa wala kutuma mwakilishi.’ Cha kushangaza ni barua hiyo imenakiliwa
kwa Afisa Mtendaji Kata ya Sombetini, Mwenyekiti wa Mtaa wa Kirika A,
Sombetini na Balozi wa Mtaa wa Zurich, Sombetini. Mbali na Afisa
Mtendaji Kata ambaye alikuwa mlalamikiwa, wengine wote walionakiliwa
barua ya Afisa Uhamiaji Mkoa ni makada wa CCM na, kwa taarifa za Kambi
Rasmi ya Upinzani Bungeni, ndio walikuwa chanzo cha malalamiko ya Katibu
wa CCM Kingazi.
Kwa taarifa za Kambi Rasmi ya Upinzani
Bungeni, Bw. Kipeya ni raia halali wa Tanzania anayetoka katika Jimbo la
Muhambwe katika Wilaya ya Kasulu ya Mkoa wa Kigoma. Dhambi pekee na
kubwa aliyoifanya na kustahili kusumbuliwa na Idara ya Uhamiaji ni
kugombea na kuchaguliwa kuwa mjumbe wa Baraza la Katiba la Wilaya ya
Arusha wakati yeye sio mwanachama wa CCM.
Mheshimiwa Spika,
Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni ina ushahidi unaoonyesha kwamba njama
za kuhakikisha kwamba wanaCCM pekee ndio watakaochaguliwa kuwa wajumbe
wa Mabaraza ya Katiba ya Wilaya kwa upande wa Tanzania Bara zilipangwa
katika ngazi za juu kabisa za CCM. Mnamo tarehe 3 Machi, 2013, siku
mbili tu baada ya Mwongozo wa Tume kuanza kutumika, Katibu wa NEC ya
CCM, Uhusiano wa Kimataifa Dr. Asha-Rose Migiro alituma barua pepe kwa
wajumbe na watendaji wa Sekretarieti ya NEC ya CCM yenye kichwa cha
habari: ‘MUHIMU!! MABARAZA YA KATIBA YA WILAYA.’
Barua pepe ya
Dr. Asha-Rose Migiro inasema: “Naandika kuhimiza kazi ya kuwatia hamasa
Makatibu wa Mikoa wasimamie kikamilifu mchakato wa kuundwa kwa Mabaraza
ya Wilaya ya Katiba. Kama mnavyofahamu Tume ya Katiba imeshatoa taarifa
rasmi kwenye vyombo vya habari ... kuhusu zoezi hili muhimu. Sambamba na
hatua za awali tulizochukua baada ya kupata rasimu ya mwanzo ya
Mwongozo wa Tume, hivi sasa tunatakiwa tuongeze juhudi za ushiriki wetu
na kutayarisha makundi husika kama tulivyokwishaongea.”
Baada
ya kuagiza ‘mawasiliano kati ya SUKI na Makatibu wa Mikoa’ kuhusu mambo
ya kufanya, Dr. Asha-Rose Migiro alimalizia barua yake kwa maneno
yafuatayo: “Tafadhali wanakaliwa msisite kutoa maoni, ushauri na mbinu
bora zaidi za kutimiza azma yetu katika suala hili muhimu.” ‘Wanakiliwa’
wa barua pepe ya Dr. Asha-Rose Migiro ni pamoja na Mh. Mwigulu Nchemba,
Mh. Zakhia Meghji, Mh. Muhamed Seif Khatib na Bw. Nape Nnauye, Katibu
Mwenezi wa NEC ya CCM.
Siku moja baadaye, Nape Nnauye
aliwaandikia ‘wanakiliwa’ wenzake kama ifuatavyo: “NASHAURI ikiwezekana
kwa sababu ya unyeti wa swala hili tupate taarifa kila siku/au walau
siku tatu ya HALI HALISI inavyoendelea katika kila mkoa, ni vizuri idara
ikaandaa checklist ya mambo muhimu ya kupima kama mchakato unakwenda
vizuri au la! Mfano ... idadi ya walioandaliwa kugombea katika kila
eneo, idadi ya waliohamasishwa kuhudhuria na kupiga kura, n.k.”
Mheshimiwa Spika,
Njama za CCM kuteka nyara mchakato wa Katiba Mpya zinahusu pia mchakato
wa uhalalishaji wa Katiba Mpya kwenye kura ya maoni. Mnamo tarehe 18
Desemba mwaka jana, Katibu wa Sekretarieti ya Halmashauri Kuu ya Taifa
ya CCM, Francis K. Mwonga, aliwaandikia barua Makatibu wote wa CCM wa
Mikoa kuwapa ‘Maelekezo ya Kikao cha Sekretarieti ya Halmashauri Kuu ya
Taifa na Makatibu wa CCM wa Mikoa Kilichofanyika Dar es Salaam Tarehe
10/12/2012.’
Sehemu ya Maelekezo hayo inasema: “Wakati wa
kupiga kura ya maoni kuhusu Katiba Mpya ya Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania mawasiliano yafanywe na wahusika ili vituo vya kupigia kura
visiwe mbali sana na wananchi.” Maneno haya yameandikwa hata kabla Tume
haijamaliza zoezi la kukusanya maoni ya wananchi na tayari Sekretarieti
ya Halmashauri Kuu ya CCM inawaelekeza makada wake mikoani kufanya
mawasiliano na ‘wahusika’ juu ya namna ya kupanga vituo vya kupigia
kura.
Mheshimiwa Spika,
Kwa mujibu wa kifungu cha
56(a) cha Sheria ya Taifa ya Uchaguzi, Sura ya 343 ya Sheria za
Tanzania, mamlaka inayohusika kupanga vituo vya kupigia kura ni
Msimamizi wa Uchaguzi, yaani Mkurugenzi wa Jiji, Mkurugenzi wa Manispaa,
Mkurugenzi wa Mji na Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya.
Wasimamizi hawa wa uchaguzi wamelalamikiwa kwa miaka mingi na vyama vya
upinzani kwa kupendelea CCM na wagombea wake katika chaguzi mbali mbali.
Hawa ndio wanaotakiwa wawasiliane na Makatibu wa CCM Mikoa ili wapange
vituo vya kupigia kura ya maoni juu ya Katiba Mpya!
Mheshimiwa Spika,
Mawasiliano haya ya viongozi wa ngazi za juu za CCM yanathibitisha
kwamba mchakato wa Katiba Mpya umeiingiliwa na kuhujumiwa kwa kiasi
kikubwa na CCM. Aidha, mawasiliano haya yanathibitisha kauli iliyotolewa
mbele ya Bunge lako tukufu na Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani
Bungeni wakati wa mjadala wa hoja ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwamba
“...viongozi wa kiserikali kama vile Wakuu wa Wilaya na wa Mikoa
waliwahamasisha wenyeviti wa vijiji, mitaa na madiwani kuhakikisha
kwamba wagombea wote wasiokuwa wa CCM, hasa wa CHADEMA, wanaenguliwa
katika chaguzi za vijiji, mitaa au kata.” Aidha, mawasiliano haya
yanathibitisha kauli ya Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni kwamba Mabaraza
ya Katiba ya Wilaya yaliyochaguliwa kwa utaratibu “...ni mabaraza ya CCM
na sio mabaraza ya katiba ya Watanzania wote.”
Mheshimiwa Spika,
Yote ambayo tumeyasema hapa yanathibitishwa pia na Tume yenyewe. Tarehe
29 Aprili, 2013 Mwenyekiti wa Tume Jaji Warioba alikiri kwenye mkutano
wa waandishi habari kwamba “... sehemu kubwa ya matatizo yaliyojitokeza
yalisababishwa na misukumo na misimamo ya kisiasa na kidini.” Mwenyekiti
Warioba amekiri kwamba kuna wajumbe wamejazwa katika Mabaraza ya Katiba
ya Wilaya: “‘Hao waliojazana kwenye mabaraza wanadhani wanakuja kupiga
kura, hapana.... Tume inazingatia uzito wa hoja zilizotolewa na wananchi
na si idadi ya watu waliotoa maoni.’”
Kwingineko, Mwenyekiti
Warioba amekaririwa na vyombo vya habari akikiri kwamba kulikuwa na
rushwa katika mchakato wa uchaguzi wa Mabaraza ya Katiba ya Wilaya. Hata
hivyo, licha ya kukiri kuwepo kwa matatizo makubwa kama haya katika
mchakato wa kuunda Mabaraza hayo, Mwenyekiti Warioba na Tume yake
wamekataa madai ya kufutwa kwa matokeo ya uchaguzi wa Mabaraza kwa hoja
kwamba kufanya hivyo kutachelewesha kupatikana kwa Katiba Mpya!
Mheshimiwa Spika,
Kauli ya Mwenyekiti wa Tume ni ya kinafiki na ya kujikosha kutokana na
makosa ya Tume yenyewe. Hii ni kwa sababu Tume yake ilitahadharishwa
mapema juu ya uwezekano mkubwa wa matatizo hayo kujitokeza. Chama cha
Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kiliitahadharisha Tume mapema mwezi
Februari ya mwaka huu kwamba rasimu ya Mwongozo wa Tume itazaa mabaraza
ya kiCCM na italeta manung’uniko mengi ya wadau ambao wataenguliwa
kwenye ngazi ya WDC ambazo zinatawaliwa na CCM kwa kiasi kikubwa.
CHADEMA iliishauri Tume iachane na mapendekezo ya kuziweka WDC kuwa ni
kikao cha uchaguzi wa wajumbe wa Mabaraza ya Katiba ya Wilaya na badala
yake wajumbe wa Mabaraza wachaguliwe moja kwa moja na wananchi kama
ilivyopendekezwa kwa upande wa Zanzibar. Jaji Warioba na Tume yake
walikataa kata kata mapendekezo haya ya CHADEMA. Kama alivyosema
Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni: “... (L)icha ya Tume ya
Mabadiliko ya Katiba kupatiwa maoni ya wadau kwamba utaratibu huo
utaharibu mchakato wa Katiba Mpya, Tume ilikataa kata kata kuubadilisha
Muundo wa Mabaraza haya. Ni wazi kwamba Tume inafahamu inachokifanya. Ni
wazi vile vile kwamba Tume inafahamu matokeo ya hicho inachokifanya,
yaani kuundwa kwa Mabaraza ya Katiba ya Wilaya ambayo ni ya wanaCCM.”
Mheshimiwa Spika,
Jaji Warioba na Tume yake hawawezi wakasikika sasa hivi wakisema kwamba
vyama vya kisiasa na taasisi za kidini ndio zenye makosa kwa kuvurugika
kwa mchakato wa Mabaraza ya Katiba ya Wilaya! Aidha, Tume
iliyotengeneza Mwongozo uliosababisha wanachama wa CCM ‘kujazana’ katika
Mabaraza ya Katiba ya Wilaya haiwezi sasa ikalalama na kudai kwamba
haitaangalia idadi ya waliotoa maoni bali itaangalia uzito wa hoja!
Katika hili Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inaitaka Serikali iwaeleze
Watanzania kama kuna uhalali wowote kutumia shilingi bilioni 4.734 kwa
ajili ya kuratibu na kuendesha Mabaraza ambayo Tume imesema maoni ya
wengi katika Mabaraza hayo hayatafuatwa.
Zaidi ya hayo, kukataa
kwa Tume kufuta matokeo ya uchaguzi wa Mabaraza ambayo Tume yenyewe
inakiri umevurugwa ni uthibitisho tosha kwamba ndivyo Tume
ilivyodhamiria tangu mwanzoni. Mabaraza haya ya kiCCM ni matunda ya moja
kwa moja ya Tume kukiuka utaratibu uliowekwa na kifungu cha 18(3) cha
Sheria ulioilazimu Tume kuunda Mabaraza ambayo “... yatashirikisha na
kuwakutanisha wawakilishi toka makundi mbali mbali ya wananchi katika
jamii.”
Mheshimiwa Spika,
Kambi Rasmi ya Upinzani
Bungeni inaitaka Serikali itoe kauli mbele ya Bunge lako tukufu kama CCM
au viongozi na makada wake wamefanya mawasiliano yoyote na vyombo
vitakavyosimamia kura ya maoni juu ya Katiba Mpya kama zinavyoashiria
nyaraka za CCM ambazo tumezielezea hapa. Aidha, Kambi Rasmi ya Upinzani
Bungeni inaitaka Serikali hii ya CCM itoe kauli juu ya uhalali wa
mawasiliano haya wakati mchakato wa kutengeneza Katiba Mpya
haujakamilika na wala sheria husika za uchaguzi hazijafanyiwa
marekebisho ili kuruhusu kura ya maoni kufanyika kihalali, hasa kwa
upande wa Tanzania Bara.
Mheshimiwa Spika,
Kifungu cha
10 cha Sheria ya Mabadiliko ya Katiba kinafafanua kwamba “Tume itakuwa
na mamlaka na uhuru kwa kadri itakavyokuwa muhimu kwa ajili ya
utekelezaji wa majukumu na mamlaka yake chini ya Sheria hii na
haitaingiliwa na mtu au mamlaka yoyote.” Nyaraka za CCM ambazo
tumezielezea hapa zinaonyesha dhahiri kwamba CCM imeingilia uhuru na
mamlaka ya Tume. Kwa uchache kabisa, nyaraka hizi zinaonyesha viongozi
wa ngazi za juu kabisa wa Sekretarieti ya NEC ya CCM wamefanya makosa ya
kula njama kutwaa mamlaka ya Tume kwa kuwatumia Makatibu wa Mikoa wa
CCM ‘kusimamia kikamilifu mchakato wa kuundwa kwa Mabaraza ya Wilaya ya
Katiba.’ Kwa mujibu wa kifungu cha 21(2)(b) cha Sheria, “mtu yeyote ...
atakayejifanya kuwa mjumbe wa Tume au Sekretarieti ... atakuwa ametenda
kosa.” Kifungu cha 21(3) kinaelekeza adhabu ya faini isiyopungua
shilingi milioni mbili na isiyozidi shilingi milioni tano au kifungo kwa
muda usiopungua mwaka mmoja na usiozidi miaka mitatu au adhabu zote
mbili, kwa mtu yeyote atakayepatikana na hatia na kosa hilo. Kambi Rasmi
ya Upinzani Bungeni inaitaka Serikali hii ya CCM itoe kauli mbele ya
Bunge hili tukufu kama iko tayari sasa kuwachukulia hatua tajwa za
kisheria Dr. Asha-Rose Migiro, Mh. Mwigulu Nchemba, Mh. Zakia Hamdani
Meghji, Mh. Muhamed Seif Khatib, Nape Nnauye na wengine wote waliotajwa
katika nyaraka za CCM kwa uhalifu walioufanya dhidi ya Sheria ya
Mabadiliko ya Katiba.
Mheshimiwa Spika,
Baada ya
ushahidi wote huu, hakuwezi kuwa na ubishi kwamba utaratibu mzima wa
kuundwa kwa Mabaraza ya Katiba ya Wilaya ni haramu. Hakuwezi kuwa na
ubishi tena kwamba uharamu huu una lengo moja tu: kuhakikisha kwamba
Katiba Mpya itakayopatikana kwa mchakato huu haramu “... itakuwa ni
Katiba Mpya kwa jina tu, mambo mengine ya msingi yatabaki vile vile
(yalivyo katika Katiba ya sasa). Kwa maneno mengine, itakuwa ni Katiba
ile ile, ya watu wale wale, wa chama kile kile.”
Kama
alivyosema Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni: “Katika mwaka wa
kwanza wa mchakato wa upatikanaji Katiba mpya, Tume ya Mabadiliko ya
Katiba imethibitisha hofu tuliyokuwa nayo toka mwanzo kwamba lengo la
mchakato wa Katiba Mpya uliowekwa kwa mujibu wa Sheria ya Mabadiliko ya
Katiba ni kuhakikisha kwamba mabadiliko pekee yakayokuwepo ni yale yenye
kulinda matakwa ya CCM na Serikali yake au yale pekee yatakayokuwa na
baraka za “‘status quo.’”
Mheshimiwa Spika,
Katika
Maoni ya Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni kuhusu hoja ya
Ofisi ya Waziri Mkuu, tulitangaza kwamba CHADEMA itajitoa ushiriki wake
katika mchakato wa Katiba Mpya endapo mambo yafuatayo hayatapatiwa
ufumbuzi hadi kufikia mwisho wa mwezi huu, yaani tarehe 30 Aprili, 2013:
1. Kufutwa kwa uchaguzi wa wajumbe wa mabaraza ya wilaya ya Katiba
uliofanywa na Kamati za Maendeleo za Kata, na badala yake wajumbe wa
mabaraza ya katiba ya wilaya wachaguliwe moja kwa moja na wananchi wa
Kata husika bila kuchujwa na WDC;
2. Serikali ilete mbele
ya Bunge hili tukufu Muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria ya
Mabadiliko ya Katiba yatayofanyia maeneo yafuatayo marekebisho:
(a) Vifungu vyote vinavyohusu uwakilishi katika Bunge Maalum la Katiba
wa taasisi zilizoainishwa katika Sheria ya Mabadiliko ya Katiba ili
kuweka wazi namna wawakilishi wa taasisi hizo watakavyopatikana kutoka
kila taasisi na idadi yao kwa kila taasisi;
(b) Vifungu
vyote vinavyohusu ushirikishi wa wajumbe wa Bunge Maalum la Katiba
kutoka Zanzibar katika mijadala inayohusu mambo yasiyokuwa ya muungano
ya Tanzania Bara ili kuhakikisha kwamba wajumbe wa Zanzibar ambao
hawatakuwa pungufu ya theluthi moja ya wajumbe wote watashiriki katika
mijadala inayohusu mambo ya Muungano tu na sio mambo ya Tanzania Bara
yasiyokuwa ya Muungano;
(c) Vifungu vyote vinavyohusu
mamlaka ya Rais kuitisha tena Bunge Maalum la Katiba baada ya Bunge hilo
kuwa limeshapitisha Rasimu ya Katiba Mpya kwa lengo la kufanya
marekebisho katika Rasimu kabla haijapelekwa kwenye kura ya maoni ili
kumwondolea Rais uwezo wa kubadilisha maamuzi yaliyopitishwa na Bunge
Maalum;
(d) Vifungu vyote vinavyohusu mamlaka ya kikatiba
na ya kisheria yatakayoiwezesha Tume ya Taifa ya Uchaguzi kuendesha na
kusimamia kura ya maoni ili kurekebisha hali ya sasa ambayo Katiba na
Sheria za Uchaguzi za nchi yetu hazitambui uwepo wa kura za maoni na
utaratibu wa namna ya kuiratibu, kuisimamia na kuiendesha;
Mheshimiwa Spika,
Madai ya Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni hayajatimizwa hadi tunatoa
Maoni haya. Mwenyekiti wa Tume Jaji Warioba amesema wazi wazi kwamba
uchaguzi wa Mabaraza ya Katiba ya Wilaya, ambayo Tume inakiri ulivurugwa
na mivutano ya kisiasa na kidini, hautarudiwa na Mabaraza hayo
yataendelea. Aidha, Mwenyekiti wa Tume amewaasa wale wanaolalamikia
uchaguzi wa Mabaraza hayo wapeleke malalamiko yao kwenye Tume ili
yashughulikiwe. Ushauri huu wa Tume hauna maana yoyote kwa sababu
Mwongozo uliotolewa na Tume yenyewe haujaweka utaratibu wowote wa
kufungua na kushughulikia malalamiko yoyote yanayotokana na uchaguzi wa
Mabaraza hayo!
Mheshimiwa Spika,
Kwa upande wa
Serikali, Waziri Mkuu aliahidi – wakati wa kuhitimisha hoja ya Ofisi ya
Waziri Mkuu – kwamba Serikali italeta Muswada wa Marekebisho ya Sheria
ya Mabadiliko ya Katiba kabla ya mwisho wa Mkutano huu wa Bajeti. Kambi
Rasmi ya Upinzani Bungeni imetafakari sana ahadi hii ya Waziri Mkuu.
Pamoja na kwamba ni ahadi ya maneno tu, kama ilivyokuwa ahadi ya
Mheshimiwa Rais Dokta Jakaya Mrisho Kikwete kwamba marekebisho yote
yanayohitajika katika Sheria hiyo yatakamilika hadi kufikia Novemba
2012, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni imeona ni vema iipe muda Serikali
wa kuleta marekebisho tajwa ndani ya Mkutano huu wa Bunge la Bajeti.
Kipindi hiki pia kitaenda sambamba na Tume kutoa Rasimu ya Kwanza ya
Katiba Mpya kwa ajili ya kuanza kujadiliwa na Watanzania.
Mheshimiwa Spika,
Endapo hadi kufikia mwisho wa kipindi hicho Serikali itakuwa haijaleta
Muswada wa marekebisho yanayotakiwa; au endapo Muswada utakaoletwa
hautakidhi matakwa ya kuboresha mchakato wa upatikanaji wa Katiba Mpya,
basi CHADEMA itawaalika wanachama, wafuasi na mashabiki wake Tanzania
nzima, pamoja na taasisi za kiraia na za kidini, vyama vya siasa na
Watanzania wote wenye nia njema na taifa hili kuhamasisha Watanzania
kuikataa Rasimu ya Katiba Mpya kwenye kura ya maoni itakayofanyika kwa
ajili ya kuihalalisha Katiba hiyo.
Mheshimiwa Spika,
Nchi ya Kenya imepata Katiba Mpya mwezi Agosti 2010 baada ya mchakato
uliochukua zaidi ya miaka kumi na moja. Kwa mujibu wa Dr. Patrice L.O.
Lumumba aliyekuwa Katibu wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba ya Kenya,
kwanza Serikali ya KANU chini ya Rais Daniel arap Moi, na baadaye
Serikali ya NARC chini ya Rais Mwai Kibaki, zilijaribu kuteka nyara
mchakato wa Katiba Mpya ya Kenya kwa kuandaa Rasimu ya Katiba Mpya
ambayo ilipopelekwa kwenye kura ya maoni mwaka 2005 ilikataliwa na
wananchi wa Kenya.
Kama inavyojulikana, baadaye Kenya ilifanya
Uchaguzi Mkuu wa Desemba 2007 kwa mujibu wa Katiba ya zamani ya Kenya ya
mwaka 1969. Matokeo ya uchaguzi huo chini ya Katiba ya zamani
yaliingiza Kenya katika machafuko makubwa ya kisiasa yaliyosababisha
mauaji ya maelfu ya Wakenya. Kwa sababu ya machafuko hayo, Kenya
imeingia katika vitabu vya historia kuwa nchi ya pili katika Bara la
Afrika, baada ya Hassan al-Bashir wa Sudan, yenye Rais na Naibu Rais
walioko madaraka lakini wanakabiliwa na mashtaka ya uhalifu dhidi ya
ubinadamu (crimes against humanity) katika Mahakama ya Kimataifa ya
Jinai.
Mheshimiwa Spika,
Jamhuri ya Zimbabwe nayo
imepata Katiba Mpya mwezi Februari ya mwaka huu baada ya mchakato
uliochukua zaidi ya miaka kumi na sita. Mwaka 2000, Chama tawala cha
ZANU PF cha Rais Robert Mugabe kiliwapelekea wananchi wa Zimbabwe Rasimu
ya Katiba Mpya iliyotokana na mchakato uliotawaliwa na chama hicho
kuanzia mwanzo hadi mwisho. Katika kura ya maoni iliyofanyika mwaka huo,
Rasimu hiyo ya Katiba Mpya ilikataliwa kwa kura nyingi na wananchi wa
Zimbabwe.
Matokeo yake, Zimbabwe iliingia katika giza kuu la
machafuko ya kisiasa na kijamii yaliyopelekea ukiukwaji wa kutisha wa
haki za binadamu na hatimaye Zimbabwe kutengwa kimataifa kwa kufukuzwa
katika Jumuiya ya Madola na kuwekewa vikwazo vya kiuchumi na
kidiplomasia. Baadaye, ZANU PF iliyofikiria kwamba inaweza kutawala kwa
mabavu ya kijeshi, ilipoteza wingi wake Bungeni na hatimaye ililazimika
kufanya maridhiano na vyama vya upinzani na makundi mengine ya kijamii
yaliyopelekea kusainiwa kwa Makubaliano Makuu ya Kisiasa (Global
Political Agreement). Chini ya Makubaliano hayo, Bunge la Zimbabwe
liliunda Kamati ya Katiba ya Bunge iliyokuwa na wajumbe sawa kwa kila
kimoja cha vyama vikuu vya kisiasa vya nchi hiyo.
Kamati hiyo
ya Bunge, iliyokuwa na Wenyeviti Wenza Watatu, Makamu Wenyeviti Wenza
Watatu na wajumbe tisa kwa kila chama, ndiyo iliyoandaa Rasimu ya Katiba
Mpya ya Jamhuri ya Zimbabwe iliyopigiwa kura ya maoni na kupitishwa na
wananchi wa Zimbabwe mwezi Februari ya mwaka huu. Baadhi ya wabunge wa
Bunge lako tukufu walishiriki katika kura ya maoni hiyo kama sehemu ya
ujumbe wa waangalizi wa Chama cha Mabunge ya SADC.
Mheshimiwa Spika,
Mifano ya Kenya na Zimbabwe inatosha kuwaonyesha kwamba wanajidanganya
wale wote wanaodhani kwamba kuwa chama tawala chenye wabunge wengi na
mabavu ya kijeshi inatosha kubaki madarakani hata kwa hila na
uchakachuaji. Saa ya mabadiliko inapogonga, hakuna mabavu ya kijeshi
wala usalama wa taifa wala mapesa mengi wala ukatili wa aina yoyote
unaoweza kuzuia wimbi la mabadiliko hayo! Bunge lako tukufu litafanya
vema kujifunza kutokana na historia ya wenzetu.
HIFADHI YA HAKI ZA BINADAMU
Mheshimiwa Spika,
Katiba ya nchi yetu inatambua na kuhifadhi haki za binadamu na wajibu
muhimu. Sehemu ya Tatu ya Katiba yetu imefafanua haki hizo kwa kirefu.
Kama sehemu ya jumuiya ya kimataifa, Tanzania vile vile imeridhia
mikataba mbali mbali ya haki za binadamu kama vile Tangazo la Ulimwengu
la Haki za Binadamu (Universal Declaration of Human Rights – UDHR),
1948; Mkataba wa Kimataifa wa Haki za Kiraia na Kisiasa (International
Covenant on Civil and Political Rights – ICCPR), 1966 na Mkataba wa
Kimataifa wa Haki za Kiuchumi, Kijamii na Kiutamaduni (International
Covenant on Economic, Social and Cultural Rights – ICESCR), 1966. Aidha,
Tanzania ni mwanachama wa Mkataba wa Afrika wa Haki za Binadamu na za
Wananchi (African Charter on Human and Peoples Rights – ACHPR), 1981.
Mheshimiwa Spika,
Licha ya kuwepo kwa msingi huu wa kikatiba na kisheria, hali ya haki za
binadamu imezidi kuzorota kwa kiasi kikubwa katika nchi yetu kama
ambavyo Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni imeelezea mara nyingi katika
Bunge lako tukufu. Kwenye Maoni haya, Mheshimiwa Spika, tunaomba tufanye
marejeo ya taarifa rasmi za kitafiti za mamlaka za umma za kiserikali
na za taasisi zisizokuwa za kiserikali kuhusiana na matumizi ya nguvu za
vyombo vya dola na jinsi ambavyo zinahatarisha haki za binadamu
zilizohifadhiwa na Katiba yetu. Taarifa hizi rasmi zinahusu uchunguzi wa
kifo au mauaji ya mwandishi wa habari Daudi Mwangosi katika Kijiji cha
Nyololo, Wilaya ya Mufindi, mkoani Iringa mnamo tarehe 2 Septemba, 2012,
wakati akifanya kazi ya kukusanya habari kwa niaba ya Kituo cha
Televisheni cha Channel Ten katika mkutano wa ndani ulioandaliwa na
Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA).
Mheshimiwa Spika,
Ibara ya 18(b) na (d) ya Katiba inahifadhi haki ya kila mtu “...
kutafuta, kupokea na kutoa habari bila ya kujali mipaka ya nchi”; na
“... haki ya kupewa taarifa wakati wowote kuhusu matukio mbali mbali
muhimu kwa maisha na shughuli za wananchi na pia kuhusu masuala muhimu
ya jamii.” Aidha, kwa mujibu wa ibara ya 22(1) inatamka bayana kwamba
“kila mtu anayo haki ya kufanya kazi.” Kwa misingi hii ya kikatiba,
Marehemu Daudi Mwangosi alikuwa na haki zote kisheria kukusanya habari
katika mkutano wa CHADEMA katika Kijiji cha Nyololo siku alipouawa.
Mheshimiwa Spika,
Katiba yetu pia inatambua na kuhifadhi “... uhuru wa kukutana na watu
wengine kwa hiari yake na kwa amani, kuchanganyika, kushirikiana na watu
wengine, na kwa ajili hiyo kutoa mawazo yake hadharani na kuanzisha na
kujiunga na vyama au mashirika yaliyoanzishwa kwa madhumuni ya kuhifadhi
na kuendeleza imani au maslahi yake au maslahi mengineyo.” (ibara ya
20(1) Ni muhimu kutambua hapa kwamba ‘aya nyakuzi’ (clawback clauses)
zilizokuwa zinaweka masharti na vizingiti vya ‘kwa mujibu wa sheria’
vilivyokuwa vinazuia raia kufaidi haki na uhuru unaotambuliwa na ibara
za 18 na 20 viliondolewa na Sheria ya Marekebisho ya Katiba, Sheria Na. 1
ya 2005. Kwa maana hiyo, hakuna sheria nyingine yoyote inayoweza
kufunga au kupunguza uhuru na haki zilizotolewa na vifungu hivi
isipokuwa masharti yaliyoko kwenye ibara ya 30 ya Katiba yenyewe.
Mheshimiwa Spika,
Sehemu ya Kwanza ya Sura ya Sita ya Katiba inaunda Tume ya Haki za
Binadamu na Utawala Bora na kuipa majukumu na mamlaka ya kuyatekeleza
majukumu hayo. Kwa mujibu wa ibara ya 130(1) ya Katiba, majukumu ya
CHRAGG ni pamoja na kuhamasisha hifadhi ya haki za binadamu na wajibu
kwa jamii; kupokea malalamiko ya uvunjaji wa haki za binadamu na
kuyachunguza; na, kama itabidi, kufungua mashauri mahakamani ili kuzuia
uvunjaji wa haki za binadamu.
Mara baada ya mauaji ya Marehemu
Mwangosi kutokea, Tume ya Haki za Binadamu ilifanya uchunguzi wa
mazingira na sababu za mauaji hayo. Baada ya uchunguzi huo, Tume
iliandaa Taarifa ya Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora ya
Uchunguzi wa Tukio Lililopelekea Kifo cha Daudi Mwangosi Kilichotokea
Septemba 2, 2012 Kijijini Nyololo. Taarifa hiyo ilitolewa hadharani na
kwa vyombo vya habari tarehe 10 Oktoba, 2012.
Mheshimiwa Spika,
Taarifa ya Uchunguzi inaeleza kwamba “... Tume ilizingatia zaidi
masuala ya uvunjwaji wa haki za binadamu na ukiukwaji wa misingi ya
utawala bora. Hivyo basi, Tume ilitilia maanani Katiba ..., sheria mbali
mbali na mikataba ya kimataifa na ya kikanda inayohusu haki za binadamu
ambayo Tanzania imeridhia.” Katika uchunguzi wake Tume ilibaini mambo
yafuatayo:
1) Tarehe 2 Septemba, 2012 CHADEMA kiliruhusiwa na
Kamanda wa Polisi wa Wilaya ya Mufindi kufanya mikutano ya ndani na
kuzindua matawi mapya. Lakini jioni ya tarehe 1 Septemba, 2012 Kamanda
wa Polisi wa Mkoa wa Iringa Michael Kamuhanda alizuia CHADEMA kufanya
mikutano iliyoruhusiwa. Kwa mujibu wa Tume ya Haki za Binadamu, Kamanda
wa Polisi wa Wilaya ndiye ‘“Officer in charge” wa polisi wa eneo husika
kama sheria inavyotaka.’
2) Viongozi wa CHADEMA kilifanya
mazungumzo na Mkuu wa Upelelezi wa Jinai Mkoa wa Iringa “... na
kuruhusiwa kufungua matawi yao bila ya kuwa na mikutano ya hadhara.”
3) Msajili wa Vyama vya Siasa aliwaandikia barua viongozi wa vyama vya
siasa kuwataka kusitisha shughuli zao kwa sababu ya sensa ya watu na
makazi iliyokuwa inafanyika wakati huo.
4) Wakati shughuli ya
uzinduzi wa tawi la Nyololo ukiendelea, Kamanda Kamuhanda alifika eneo
hilo na kuamuru viongozi wa CHADEMA wakamatwe, na wafuasi wa CHADEMA
walipinga kukamatwa kwa viongozi wao.
5) Kamanda Kamuhanda aliamuru
kupigwa kwa mabomu ya machozi ili kuwatawanya wananchi waliokusanyika
katika ofisi za tawi hilo la CHADEMA.
6) Baada ya mabomu ya
machozi kupigwa, wananchi walitawanyika na kukimbia ovyo, lakini
Marehemu Mwangosi “... alizingirwa na askari, aliteswa na hatimaye
inadaiwa alipigwa bomu na kufa papo hapo.
7) Marehemu Mwangosi aliuawa umbali wa takriban mita 100 kutoka ilipo Ofisi ya CHADEMA tawi la Nyololo.
8) Katika tukio hilo wananchi kadhaa walijeruhiwa kwa mabomu, wakiwemo
mwandishi wa habari wa gazeti la Nipashe Godfrey Mushi, Mwenyekiti wa
Jumuiya ya Wanawake CHADEMA Wilaya ya Mufindi, Winnie Sanga, na Mkuu wa
Kituo cha Polisi Mufindi Asseli Mwampamba “aliyekuwa akifanya jitihada
za kumuokoa marehemu Daudi Mwangosi.”
Kwa mujibu wa Taarifa ya
Tume ya Haki za Binadamu, “... Tume imejiridhisha kuwa tukio la
lililopelekea kifo cha Daudi Mwangosi limegubikwa na uvunjwaji wa haki
za binadamu na ukiukwaji wa misingi ya utawala bora.” Taarifa ya Tume
inafafanua kuwa, “... Tume imejiridhisha kuwa Jeshi la Polisi limevunja
haki ... ya kuishi, haki ya kutoteswa na kupigwa, haki ya usawa mbele ya
sheria na haki ya kukusanyika na kutoa maoni.”
Kuhusiana na
amri ya Kamanda Kamuhanda ya kupiga marufuku mkutano wa CHADEMA, Taarifa
ya Tume inasema kwamba katika utekelezaji wa majukumu yake, Kamanda
Kamuhanda “... alikiuka Sheria ya Vyama vya Siasa ... kifungu cha 11(a)
na (b) na Sheria ya (Jeshi la) Polisi ... kwa kuingilia kazi za OCD wa
Mufindi na kutoa amri ya kuzuia shughuli za CHADEMA wakati yeye hakuwa
‘Officer in-charge’ wa polisi eneo husika. Kwa maana hiyo amri aliyoitoa
haikuwa halali kwa kuwa ilitolewa na mtu ambaye hakuwa na mamlaka
kisheria kutoa amri hiyo. Haya ni matumizi mabaya ya madaraka, hivyo ni
ukiukwaji wa misingi ya utawala bora.”
Mheshimiwa Spika,
Tume ya Haki za Binadamu ilihoji pia hatua ya Msajili wa Vyama vya
Siasa John Tendwa kuwaandikia barua viongozi wa vyama vya siasa kuwataka
kusitisha shughuli zao kwa sababu ya sensa. Kwa mujibu wa Taarifa ya
Tume, hatua hiyo “... ilikiuka misingi ya utawala bora kwani maelekezo
yaliyotolewa ndani ya barua hiyo yanakinzana na Sheria ya Takwimu, Na. 1
ya mwaka 2002 inayotoa fursa kwa wananchi kuendelea na kazi zao wakati
wa sense....” Barua hiyo pia “... ni kinyume na Sheria ya Vyama vya
Siasa ... inayotoa fursa kwa vyama vya siasa kufanya shughuli zake bila
kuingiliwa.”
Katika hili ni muhimu kunukuu mapendekezo ya Tume
ya Haki za Binadamu kwa kirefu: “Jeshi la Polisi na Msajili wa Vyama vya
Siasa waepuke kufanya maamuzi au matendo yanayoibua hisia za ubaguzi au
upendeleo miongoni mwa jamii wakati wanapotekeleza majukumu yao
kisheria. Mfano, Jeshi la Polisi lilizuia mikutano ya CHADEMA kwa sababu
ya sensa wakati huo huo ... CCM walikuwa wakifanya uzinduzi wa kampeni
huko Zanzibar. Aidha, rai ya Msajili wa Vyama vya Siasa haikuzingatiwa
kwa upande wa CCM Zanzibar huku CHADEMA walishurutishwa na polisi kutii
rai hiyo.” Aidha, Taarifa ya Tume inasisitiza kwamba “demokrasia ya
mfumo wa vyama vingi iheshimiwe na kulindwa.”
Mheshimiwa Spika,
Sio Tume ya Haki za Binadamu pekee iliyofanya uchunguzi wa mauaji ya
Marehemu Mwangosi. Baraza la Habari Tanzania (MCT) na Jukwaa la Wahariri
Tanzania (TEF), taasisi mbili huru zinazojihusisha na masuala ya habari
Tanzania, nazo zilifanya uchunguzi wa pamoja. Taarifa yao inayojulikana
kama Ripoti ya Timu Maalum ya Uchunguzi Iliyoteuliwa na Baraza la
Habari Tanzania (MCT) na Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF) Kuchunguza
Mazingira Yaliyopelekea Kuuawa kwa Mwandishi wa Habari Daudi Mwangosi
Septemba 2, 2012 Katika Kijiji cha Nyololo, Wilaya ya Mufindi, Mkoani
Iringa, imeunga mkono Taarifa ya Tume ya Haki za Binadamu juu ya jambo
hili.
Kwa mujibu wa Ripoti ya MCT/TEF, matokeo ya uchunguzi wao
“... yanadhihirisha bila wasi wasi kwamba polisi kwa makusudi
waliwavurumisha waandishi waliotoka Iringa wakati wakikusanya habari za
shughuli za CHADEMA katika kijiji cha Nyololo. Zaidi ya hapo, Daudi
Mwangosi mwenyewe aliuawa akiwa mikononi mwa polisi huku wakisimamiwa
moja kwa moja na Kamanda ... Kamuhanda.” Ripoti inakubaliana na Taarifa
ya Tume ya Haki za Binadamu kabla ya Mwangosi kuuawa, “... maelewano
yalifikiwa katika ya RCO na maofisa wa CHADEMA, na kamanda (RCO)
(aliwa)amuru maofisa wake kutotumia nguvu dhidi ya watu waliokusanyika
kwenye ofisi ile.
Hata hivyo, hali hiyo maelewano ilibadilika
mara baada ya Kamanda Kamuhanda kufika katika eneo la tukio. Kwa mujibu
wa Ripoti ya MCT/TEF, “mashuhuda wanaeleza kuwa RPC alimwita RCO na
kumuonya wazi kuhusu kushughulikia kwa amani masuala ya CHADEMA katika
eneo la awali la utulivu.” Baada ya hapo, “inaelekea RCO alijitoa
kuelekea eneo la umwagaji damu ... na hivyo usimamizi wa utoaji amri
katika eneo la umwagaji damu ... ulibakia kwa mkuu wake ambaye ni RPC
Michael Kamuhanda.”
Sawa na Taarifa ya Tume, Ripoti ya MCT/TEF
inaweka lawama za vurugu zilizotokea Nyololo kwenye miguu ya Kamanda
Kamuhanda: Vurugu zilianza pale Kamanda Kamuhanda alipoamuru kukamatwa
kwa viongozi wa CHADEMA waliokuwepo. “Kufuatia amri hiyo ... polisi ...
waliingia kwa nguvu katika ofisi ya CHADEMA wakipiga mabomu ya machozi
na kuwaamuru viongozi hao wajisalimishe.” Kwa mujibu wa Ripoti ya
MCT/TEF, viongozi wa CHADEMA walitii amri hiyo na “... kujisalimisha kwa
kuketi na kuinua mikono yao juu.” Hata hivyo, “... wakati makada wa
CHADEMA walitii maagizo ya viongozi wao ya kuketi chini na kuinua mikono
yao juu, polisi walifyatua risasi na mabomu ya machozi, na kuwapiga
makada hao na waandishi kwa virungu.”
Mheshimiwa Spika,
Ripoti ya MCT/TEF inakubaliana na Taarifa ya Tume ya Haki za Binadamu
juu ya jinsi Marehemu Mwangosi alivyouawa. “Alipoangalia nyuma, Daudi
Mwangosi aliona kikundi cha polisi wakimpiga mwandishi mkuu wa gazeti la
Nipashe wa Iringa, Godfrey Mushi.... Wakati mwandishi Godfrey Mushi
akiwa bado anapigwa na polisi, marehemu Mwangosi aliwakimbilia akiwaomba
waache kumdhuru zaidi Mushi kwa kuwa alikuwa mwandishi tu. Polisi
hawakumsikiliza. Badala yake wakamburuta mwandishi huyo ambaye tayari
alikuwa amepoteza fahamu na kumweka kwenye gari lao na wakamgeukia Daudi
Mwangosi mwenyewe, wakampiga kwa nguvu mpaka akapoteza fahamu.”
Hata amri ya Mkuu wa Kituo cha Polisi Mafinga Mwampamba kuwataka askari
polisi waache kumpiga marehemu Mwangosi haikusikilizwa na askari hao.
Ili kujiokoa, marehemu Mwangosi alimkumbatia OCS Mwampamba na “baadaye
kumwangukia miguuni mwake kuepuka kipigo zaidi.” Kwa mujibu wa Ripoti ya
MCT/TEF, “picha za mgando zinaonyesha polisi mmoja akipiga bomu la
machozi tumboni mwa marehemu Mwangosi kwa karibu kabisa.” Bomu hilo
liliusambaratisha mwili wa marehemu Mwangosi aliyekufa papo hapo. Kwa
sababu marehemu Mwangosi alikuwa chini ya miguu ya OCS Mwampamba, “naye
pia alijeruhiwa vibaya.”
Mheshimiwa Spika,
Siku moja
baada ya mauaji ya Daudi Mwangosi, Kamanda Kamuhanda alinukuliwa na
vyombo vya habari akidai kwamba marehemu Mwangosi alifariki “kutokana na
kitu kizito kilichotupwa na waandamanaji.” Aidha, siku iliyofuata
Kamishna wa Operesheni wa Jeshi la Polisi Paul Chagonja alidai kwamba
baada ya ghasia kudhibitiwa, marehemu Mwangosi alikimbilia walipokuwa
polisi na “kitu kama bomu kikarushwa na kundi la watu wanaokimbia hovyo
na kumlipua Mwangosi.”
Madai haya yanakanushwa na Ripoti ya
MCT/TEF inayomnukuu shuhuda mwanamke aliyeshuhudia mauaji hayo na
kubainisha kwamba marehemu Mwangosi “aliuawa chini ya usimamizi wa moja
kwa moja wa RPC Michael Kamuhanda.” Ripoti hiyo pia imeelezea kwa kirefu
jinsi Jeshi la Polisi lilivyotoa taarifa zinazokinzana juu ya kuhusika
kwake na mauaji ya Mwangosi. Hivyo, kwa mfano, wakati Waziri wa Mambo ya
Ndani Mheshimiwa Emmanuel Nchimbi alidai tarehe 4 Septemba 2012 kwamba
marehemu aliuawa na bomu la machozi ambalo ‘halikulipuliwa kitaalamu na
polisi’, Kamanda Kamuhanda alitokea kwenye televisheni siku iliyofuata
“akitangaza habari za kuwatupia lawama wafuasi wa CHADEMA kwa kutupa
kitu kizito kilicholipuka na kumuua Mwangosi....”
Mheshimiwa Spika,
Kwa miaka miwili mfululizo, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni
imezungumzia kwa kirefu vitendo vya mauaji ya raia wasiokuwa na hatia
ambavyo vimekuwa vinafanywa na vyombo vya dola hasa Jeshi la Polisi.
Kama tulivyowahi kusema kwa kunukuu matokeo ya utafiti uliofanywa katika
nchi za Afrika Mashariki na Mradi wa Haki za Binadamu wa Jumuia ya
Madola na kuchapishwa mwezi Juni 2006, ‘“watu wa Tanzania … wanakabiliwa
na tatizo la kuwa na jeshi la polisi ambalo mara nyingi lina sifa ya
ulaji rushwa, matumizi ya mabavu na kuwa na chombo katili cha serikali.”
Kwa mujibu wa utafiti huo, “aina hii ya uendeshaji wa shughuli za
polisi inapingana na madai ya kuwepo kwa demokrasia yanayotolewa na
serikali ya Tanzania.”
Mheshimiwa Spika,
Sasa Taarifa
ya Uchunguzi wa Kifo cha Mwandishi wa Habari wa Channel Ten Bw. Daudi
Mwangosi, iliyoandaliwa na Kamati iliyoundwa na Mheshimiwa Nchimbi na
kuchapishwa tarehe 9 Oktoba 2012 imethibitisha ukweli wa kauli hii na
ukweli wa madai ya Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni juu ya matumizi ya
nguvu ya Jeshi la Polisi. Baada ya kuzunguka huku na huko ikijaribu
kulisafisha Jeshi la Polisi, Taarifa ya Kamati hiyo inasema: “Hapakuwepo
na uhalali wa kutumia Bomu la Kishindo kwani lengo la ulipuaji wake ni
ili watu waogope na kukimbia.”
Aidha, Kamati hiyo iliyoongozwa
na Jaji Mstaafu Stephen Ihema, inakiri kwamba “hapakuwepo umuhimu wa
kutumia Bomu la Kishindo kwa sababu hata ingekuwa ukamataji tayari
askari polisi wapatao sita walikuwepo eneo la tukio.” Kwa misingi hiyo,
“… Kamati imeona kwamba … tukio la kuuawa Bw. Daudi Mwangosi na kuumizwa
baadhi ya askari polisi halikustahili kabisa.”
Mheshimiwa Spika,
Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inaitaka Serikali itoe kauli kama
inakubaliana na matokeo ya taarifa hizi tatu zilizoandaliwa na taasisi
za kiserikali kama vile Tume ya Haki za Binadamu, Kamati ya Jaji Ihema
na MCT/TEF juu ya kuhusika kwa Jeshi la Polisi na mauaji ya marehemu
Daudi Mwangosi. Aidha, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inaitaka Serikali
iteo kauli mbele ya Bunge lako tukufu kama inakubaliana na Taarifa ya
Tume ya Haki za Binadamu kwamba kitendo cha Kamanda Kamuhanda kupiga
marufuku mkutano halali wa CHADEMA kilikuwa ni kinyume cha Sheria ya
Jeshi la Polisi, Sheria ya Vyama vya Siasa na ukiukwaji wa haki za
binadamu na misingi ya utawala bora.
Vile vile, Kambi Rasmi ya
Upinzani Bungeni inaitaka Serikali itoe kauli kama – baada ya ushahidi
wa taarifa hizi tatu - iko tayari kuiomba radhi CHADEMA kwa kuisingizia
kuhusika na kifo cha marehemu Daudi Mwangosi. Na mwisho, Kambi Rasmi ya
Upinzani Bungeni inaitaka Serikali itoe kauli mbele ya Bunge lako tukufu
kama iko tayari kuilipa familia ya marehemu Mwangosi fidia kwa mujibu
wa sheria kwa kitendo cha Serikali kusababisha mauaji yake bila
‘uhalali.’
Mheshimiwa Spika,
Serikali na chama ambacho sera
zake zinakiuka haki za binadamu na misingi ya utawala bora inapoteza
uhalali (legitimacy) ya kuendelea kutawala. Hapa ndipo CCM na Serikali
yake ilikoifikisha nchi yetu: waandishi wa habari wanauawa kwa sababu ya
kufanya kazi yao halali ya kutafuta habari za mambo yanayohusu umma
kama mikutano ya vyama vya siasa. Watanzania hawastahili Serikali ya
aina hii. Kama alivyosema Baba wa Taifa katika kitabu chake Uongozi Wetu
na Hatima ya Tanzania:
“Hatulazimiki kuendelea na uongozi
mbovu wa Chama na Serikali. Wala tukiendelea na hali hii, bila kubadili
uongozi wa Chama na Serikali, sina hakika kama tutafika huko salama.
Masuala muhimu ya nchi yetu hayatashughulikiwa.... Na masuala mengine
muhimu ... yataachwa yajitatue yenyewe. Nasema katika hali kama hiyo
sina hakika kama tutafika salama; na tukifika salama tukiwa na uongozi
huu huu wa Chama na Serikali mbele kutakuwa ni giza tupu. Majuto ni
mjukuu, huja baadaye.”
Mheshimiwa Spika,
Baada ya maelezo haya marefu, naomba kukushukuru na wewe binafsi na naomba kuwasilisha.
---------------------------------------------------------------
Tundu Antiphas Mughwai Lissu
MSEMAJI & WAZIRI KIVULI, SHERIA, KATIBA NA UTAWALA
KAMBI RASMI YA UPINZANI BUNGENI
chanazo na http://www.globalpublishers.info
0 Weka maoni yako hapa:
Post a Comment
COMMENT HAPA