Aug 27, 2013

Dada yake Freeman Mbowe achukua rasmi kadi ya uanachama CCM



DADA wa Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Grace Mbowe, amejiunga na Chama Cha Mapinduzi ( CCM) akitokea Chadema, kwa kile alichodai haoni jambo jipya katika chama hicho.

Grace amesema amehama kutokana na kuwepo propaganda zisizotekelezeka. Hata hivyo, amesisitiza kwamba kuwepo kwake katika Chadema, siyo kwa sababu ya familia.

Alikabidhi kadi hiyo jana kwenye ofisi za CCM Wilaya ya Hai. Alisema itikadi za kisiasa, zisihusishe masuala ya kifamilia, kwani upendo wao uko pale pale.

Alisema kilichomfanya kujiunga na chama hicho ni utashi wake. Alidai CHADEMA wanafanya propaganda za
kuwadanganya wananchi.

Alisema itikadi za chama, haziwezi kuingilia masuala ya kifamilia, hivyo kwake siyo ajabu kuondoka CHADEMA, kwani kila mtu ana utashi wake wa kisiasa.

“Nimeamua kwa hiari yangu mwenyewe bila kushawishiwa na mtu, ndio maana nimetoka Dar es Salaam kuja Hai kwa ajili ya kurejesha kadi ya CHADEMA na kujiunga na CCM, suala la itikadi lisihusishe masuala ya kifamilia kwani upendo wetu upo palepale,”alisema Mbowe.

Alisema, “kuwapo kwangu CHADEMA siyo kwa sababu ya familia, hivyo hakuna wa kunizuia, natoka kwa utashi wangu, na tutaendelea kuheshimiana na mdogo wangu Freeman Mbowe katika masuala ya kifamilia.”

“Freeman Mbowe ni mdogo wangu wa kuzaliwa kabisa, hakunishawishi kuingia CHADEMA, hivyo sioni haja ya kuendelea kubaki huku wakati sioni jambo jipya, mimi tangu naifahamu CCM iko vile vile, bali propaganda za upinzani ndizo zinawalaghai wananchi,” alisema.
 
chanzo na timesfc tz