HILI NDIO TAMKO LA WAISLAM MWEMBE YANGA
Leo
Waislamu walikusanyika kwa wingi katika viwanja vya Mwembe Yanga,
Temeke Jijini Dar es Salaam kuwasikiliza masheikh wanatoa tamko gani
kuhusu kadhia ya kujeruhiwa Katibu wa Jumuiya na Taasisi za Kiislamu
Tanzania, Sheikh Ponda Issa Ponda.
Uwanja ulikuwa umefurika waumini waliokuwa na hamu kubwa ya kusikiliza kile kitakachosemwa na viongozi wao.
Tulibahatika kuhudhuria kuanzia mwanzo wa shughuli mpaka mwisho, ingawa
hatukuweza kuwaletea yaliyokuwa yakiendelea moja kwa moja kutoka
uwanjani kutokana na sababu zilizokuwa nje ya uwezo wetu.
Hata
hivyo, muda si mrefu shughuli imekamilika. Mwitikio ulikuwa mkubwa na
watu walikuwa wengi sana, uwanja wa Mwembe Yanga ulifurika hasa.
Sheikh kutoka Morogoro, aliwaelezea tukio zima la kupigwa risasi kwa
Sheikh Ponda, jinsi alivyowatoroka Polisi na kile kilichofanywa na jeshi
hilo katika uficha ukweli.
Baada ya Sheikh kutoka Morogoro,
ilifuatia salamu ya Sheikh kutoka Zanzibar ambaye alielezea kadhia nzima
ya safari ya Sheikh Ponda visiwani Zanzibar na yale aliyoyatamka dhidi
ya dhulma iliyofanywa na serikali ya visiwa hivyo kwa masheikh
mbalimbali. Mpaka sasa kadhaa wapo ndani na huu ni mwezi wa 10
hawajapewa dhamana. Aliwaeleza Waislamu kuwa tayari wana muungano wao,
ambao ni Muuungano wa Uislamu, na hivyo hawahitaji muungano ulioasisiwa
na Mzee Nyerere na Mzee Karume.
Aidha, alisema kuwa muungano wa Uislamu ni imara zaidi kuliko muungano huu unaolazimishwa na watawala.
Pamoja na mambo mengine alizungumzia tukio la kumwagiwa tindikali kwa
wasichana wawili, raia wa Uingereza. Alieleza kuwa, kwa mujibu wa gazeti
la Telegraph la Uingereza, matukio hayo yameongezeka huko nchini
Uingereza, na hivyo kuna uwezekano kuwa wahusika wa tukio hilo wanatoka
huko huko Uingereza.
Baadaya swala ya Alasiri, ilitolewa mada
kuhusu harakati za Sheikh Ponda, msingi na malengo yake, pamoja na kile
kilichompata Sheikh huyo.
Waislamu walikuwa na msisimko na
hamasa ya ajabu mno ambayo muda mwingi watoa mada walilazimika kukatisha
mada zao ili kupisha sauti za Takbirah zilizokuwa zikihanikiza uwanjani
hapo.
Baada ya mada hiyo, uliwadia wakati wa tamko
lililotolewa na Amiri wa Wahadhiri Tanzania, Sheikh Kondo BUngo.
Yafuatayo yalikuwa katika tamko hilo la Mwembe Yanga:
1- Waislamu wanatambua kuwa Sheikh Ponda alipigwa risasi na Polisi kwa lengo la kumuua.
2- Waislamu wanataka Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro awajibishwe,
ikiwa ni pamoja na kupelekwa mahakamani. Hasa ikizingatiwa kuwa wakati
akiongea na vyombo vya habari vya ndani, alikanusha tuhuma za polisi
kutekeleza kitendo hicho, lakini alipoongea na vyombo vya habari vya nje
alikiri kuwa polisi walimpiga risasi Sheikh Ponda, kama ilivyonukuliwa
na vyombo hivyo.
3- Kamanda wa operesheni ya kumkamata na
kumjeruhi Sheikh Ponda, pamoja na askari aliyepigwa risasi wanatakiwa
kuwajibishwa na kushitakiwa.
4- Waziri wa Mambo ya Ndani, Dk. Emmanuel Nchimbi ajiuzulu.
5- Waislamu hawaitaki tume ya polisi, bali wanataka tume huru
itakayochunguza tukio hilo, kwa sababu Polisi ni waongo, na Waislamu
hawana imani nao tena. Aidha, Polisi ni watuhumiwa, hivyo hawawezi
kujichunguza kisha wakatenda haki.
6- Waislamu wanatangaza kuwa
adui yao mkubwa kwa sasa ni serikali ya CCM, na hivyo wanakusudia
kuitia adabu. Kampeni za kuitia adabu zinaanza sasa hivi mpaka mwaka
2015 wakati wa uchaguzi mkuu.
Iwapo hayo hayatatekelezwa,
Waislamu wametangaza kuchukua hatua stahiki itakayoifanya iwe mwisho wa
kudhulumiwa katika nchi hii.
Ndugu wadau, kwa mukhtasari hayo ndiyo yaliyojiri katika Viwanja vya Mwembe Yanga, ambapo sisi wenyewe tulikuwa mashuhuda.
HUU NI UMATI ULIOJITOKEZA JANA
chanzo na page ya islamic forum
https://www.facebook.com/IslamicForumOfTanzania
0 Weka maoni yako hapa:
Post a Comment
COMMENT HAPA