TAARIFA KUHUSU MRADI WA UWANJA
Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini Francis Kifukwe (katikati) ambaye pia ni mwenyekiti wa mradi wa ujenzi wa uwanja eneo la jangwani akiongea na waandishi wa habari makao makuu ya klabu leo, kushoto ni mzee Jabir Katundu (mwenyekiti wa baraza la wazee) na kulia Lawrence Mwalusako katibu mkuu wa Yanga SC
LEO tungependa kupitia kwenu kutoa
taarifa kuhusu maendeleo ya mradi wetu wa Uwanja wa kisasa wa mpira
katika Jiji la Jangwani kama itakavyojulikana
Mara
ya mwisho tuliongea ama kuonana ilikuwa mwezi wa tatu wakati Ndugu zetu
wa BCEG walipokabizi Concept design ama Usanifu wa awali na kuanzia
sasa tutakuwa tunatoa taarifa za mara kwa mara kuhusu mradi huu. Wahenga
walisema UKICHA KUSEMA HUTATENDA JAMBO lakini pia KUKAA KIMYA SANA
kunajenga hisia mbaya na kutoa nafasi ya upotoshwaji wa habari.
Kwa kifupi napenda kuwakumbusha kuwa Makubalino ya
Awali (Memorandum of Understanding) yalisainiwa 23 Novemba 2012. Pamoja
na mengineyo YANGA inatakiwa:
• Kupata na kuwa na eneo la kutoshereza malengo ya mradi
• Kupata ushauri mzuri, michoro mizuri na mkandarasi mzuri wa mradi
• Kupata na kutenga fedha za kukamilisha usanifu na ujenzi wa mradi
Kwa
upande wa BCEG wajibu wao ni kuwa na utaalamu na uzoefu wa kutosha.
BCEG wameandaa na kukabidhi michoro ya usanifu wa awali kukidhi matakwa
ya YANGA. YANGA tunatakiwa kutoa maoni yetu na na kuingia RASMI mkataba
wa ujenzi.
Kutokana na kukua kwa Jiji la Dar es
Salaam, na katika hali ya kutaka klabu iwe na vitega uchumi klabu
imeonelea ni vyema kama ingekuwa na uwanja wa mpira wa karne ya sasa na
baadaye ambao pamoja na mambo mengine utakuwa na mioundombinu ifuatayo:-
1. Uwanja wa mpira wenye viti 40,000
2. Hostel ya wachezaji na football academy ya vijana
3. Viwanja vya mazoezi
4. Uwanja wa kutosha kuegesha magari
5. Hoteli na sehemu ya makazi
6. Ukumbi wa mikutano
7. Sehemu ya maofisi, benki, zahanati (sports clinic)
8. Maduka, supermarket na sinema
9. Sehemu za kubarizi, kupumzikia (Recretional and Open spaces)
Mara
baada ya azma yetu kukamilika eneo hili litaitwa “Jangwani City” na
kufanya wakazi wa maeneo ya Jangwani na sehemu za jirani wasiende maeneo
ya mbali kutafuta huduma muhimu za kijamii. Eneo hili litaboresha
mandhari nzima ya Jangwani kwa kukuza mazingira na miundombinu. Hii
itahusu pamoja na mambo mengine ujazaji udongo (tuta kubwa), upandaji
miti, bustani za kubarizi, kuboresha mifereji ya majitaka na kudhibiti
mafuriko ya eneo la Jangwani na hivyo kulipatia sura ya kibiashara na
kitalii.
Ili kukamilisha azma ya kuwa na
Jangwani City itakayo kuwa na miundombinu yote hiyo, Uongozi ulipeleka
maombi ya eneo la nyongeza Manispaa ya Ilala na Wizara ya Ardhi, Nyumba
na Maendeleo ya Makazi kwa barua zenye kumbukumbu namba
YASC/ARDHI/MWK/YM/46/2012 na YASC/ARDHI/MWK/YM/47/2012 za 12 Desemba
2012, na mpaka sasa bado maombi yetu hayajajibiwa.
Mwezi
wa saba, Wadhamini/Uongozi wa YANGA walimwandikia Mheshimiwa Mkuu wa
Mkoa wa Dar es Salaam kuomba msaada wake kufanikisha maombi ya nyongeza
ya kiwanja yaliyowasilishwa Manispaa ya Ilala na Wizara ya Ardhi, Nyumba
na Maendeleo ya Makazi.
Klabu ya Yanga ina
kiwanja chenye ukubwa wa hekta 3.59 eneo la Jangwani. Kiwanja hiki kina
hati miliki kwa miaka 99 toka mwaka 1972 na katika eneo hilo, klabu
ilifanikiwa kujenga uwanja wa mpira wa Kaunda na Jengo la klabu la
ghorofa tatu. Jengo hili lilijengwa kwa ufadhili mkubwa sana wa Rais wa
Kwanza wa Zanzibar Marehemu Mzee Abeid Amani Karume (Mungu aiweke roho
yake mahali pema peponi) na michango ya wanachama na wapenzi wa klabu
ambao kila siku wamekuwa wakiamini kuwa haba na haba hujaza kibaba.
Ndugu
Wandishi wa habari kwa kifupi tumefikia hapo, zoezi la kutoa maoni yetu
kuhusu michoro ya usanifu wa awali na kuingia rasmi mkataba wa ujenzi
na BCEG limesimama, likisubiri majibu ya nyongeza la eneo. Ni matumaini
yetu zoezi hili litakamilika hivi karibuni na kuendelea na mradi.
YANGA DAIMA MBELE NYUMA MWIKO
Dar es Salaam, 30 September 2013
Francis Mponjoli Kifukwe
Last Updated ( Monday, 30 September 2013 12:43 CHANZO NA http://www.youngafricans.co.tz
0 Weka maoni yako hapa:
Post a Comment
COMMENT HAPA