CUF YATOA MKONO WA TANZIA KUTOKANA NA KIFO CHA MHE. SENGODO MVUNGI
THE CIVIC UNITED FRONT CUF,
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
13-11-2013
MKONO WA TANZIA KUTOKANA NA KIFO CHA
MHE. SENGODO MVUNGI
Chama cha Wananchi – CUF kimepokea kwa mshituko na majonzi makubwa
taarifa ya kifo cha Dr. Sengodo Mvungi, Kiongozi mwandamizi wa NCCR –
Mageuzi, Mjumbe wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba na Makamu Mkuu wa Chuo
Kikuu cha Bagamoyo.
Kifo cha Dr. Mvungi kimeishtua Tanzania
nzima hasa kwa vile tulitazamia kuwa angeishi kwa muda mrefu zaidi.
Kifo hicho kinazidi kusikitisha kwa vile kimetokana na kushambuliwa
kikatili na watu wasiojulikana wanaodaiwa kuwa ni majambazi.
Mwenyekiti wa Taifa wa Chama cha Wananchi CUF, mimi mwenyewe na viongozi
waandamizi wa CUF walimjua vizuri sana Marehemu Dr. Mvungi kwani
tukifanya kazi naye kwa karibu.
Dr. Mvungi alikuwa mpambanaji jasiri
asiyeyumba katika mapambano ya kuiletea Tanzania mfumo wa kidemokrasia
halisi unaolenga kulinda haki za kila Mtanzania bila ya ubaguzi wa aina
yoyote ile. Dr. Mvungi alichukia uonevu, manyanyaso, ukandamizaji na
dhulma dhidi ya binadamu yoyote.
Dr. Mvungi tulishirikiana
naye kwa karibu katika mchakato wa kudai Katiba mpya ya Tanzania na pale
vyama vya siasa vilipounda kamati ya kufanya rasimu ya Katiba mpya
Marehemu Dr. Mvungi ndiye aliyekuwa Mwanasheria wa Kamati hio. Alitoa
mchango mkubwa katika kuandaa na kukamilisha rasimu hio.
Wengi
tulifarijika pale alipoteuliwa kuwa miongoni mwa Wajumbe wa Tume ya
Mabadiliko ya Katiba ya Tanzania. Tulijua uwezo wake, umahiri wake,
utendahi kazi makini wake na dhamira yake ya kuona Tanzania inapata
Katiba nzuri kwa masilahi ya wananchi wote bila kujali itikadi za vyama.
Dr. Mvungi alikuwa ni Wakili mahiri, msomi makini na kiongozi shupavu.
Alikuwa jasiri hasa katika kuwatetea wanyonge na katika kutoa mawazo
yake. Alikuwa ni mchambuzi hodari wa mambo ya kisheria, hasa sheria
inayoambatana na masuala ya Katiba. Halikadhalika alikuwa mchambuzi
aliyebobea katika masuala ya kijamii na ya kisiasa na aliguswa sana na
umuhimu wa kuendeleza elimu bora nchini Tanzania.
Kifo chake
ni pigo zito kwa familia yake, Chama cha NCCR – Mageuzi, Chuo Kikuu cha
Bagamoyo, Tume ya mabadiliko ya Katiba na kwa jamii nzima ya Watanzania.
Kwa niaba ya Profesa Ibrahim Haruna Lipumba, Wajumbe wa Baraza Kuu la
Uongozi la CUF na Wanachama wote wa CUF, na kwa niaba yangu mwenyewe,
tunatoa mkono wa tanzia kwa familia ya Marehemu, Mwenyekiti wa Taifa wa
NCCR – Mageuzi, Wajumbe wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba na wafiwa wote.
Tunamuomba Mwenyeezi Mungu aipumzishe roho ya Marehemu Dr. Mvungi pema peponi, AMIN.
Seif Sharif Hamad
KATIBU MKUU
CHAMA CHA WANANCHI – CUF
ZANZIBAR
0 Weka maoni yako hapa:
Post a Comment
COMMENT HAPA