Dec 6, 2013

CUF WAOMBOLEZA KIFO CHA MZEE MANDELA

THE CIVIC UNITED FRONT - CUF CHAMA CHA WANANCHI,
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI;
Ijumaa, 06/12/2013 - Dar Es Salaam.

CUF - Chama Cha Wananchi kimesikitishwa na msiba mkubwa uliolikumba taifa la Afrika ya Kusini baada ya mwasisi muhimu wa taifa hilo, rais mwafrika wa kwanza, mzalendo na mpingaji mkubwa wa siasa za ubaguzi, Mzee Nelson Mandela "Madiba" kuaga dunia jana alhamisi majira ya saa 2.50 usiku.

CUF kama chama kinachoamini kuwa dhana ya siasa na mapambano ya kidemokrasia lazima vijikite katika kupigania "HAKI SAWA KWA WOTE", tumeumizwa sana na msiba huu kwani mzee NELSON MANDELA alipigania haki sawa kwa wananchi wa Afrika ya kusini, na aliapa kupigania usawa wa binadamu katika nyanja zote hadi atakapoiaga dunia.

Mzee Mandela alikuwa ni tunu ya dunia, ni kiongozi aliyeweza kuionesha dunia kuwa "Viongozi wa Afrika wanaweza kuibadili dunia kuwa kisiwa cha amani, maendeleo, maridhiano na kutobaguana kwa misingi yoyote ile".

Mimi binafsi nimemfahamu Mzee Mandela kuwa kiongozi wa mfano wa kuigwa aliyetoa maisha yake yote, kukubali kukaa gerezani zaidi ya miongo miwili ilimradi tu aone HAKI INATENDEKA NA UTU WA MWANADAMU UNAHESHIMIKA, jambo ambalo alilifanikisha. Ni wanadamu wachache sana wameweza kujitoa kiasi hiki.

Kwa niaba ya viongozi wote na wanachama wa CUF Tanzania nzima, natoa pole kwa familia ya Mzee Mandela, ndugu jamaa na marafiki, Rais wa sasa wa Afrika ya Kusini na Wananchi wa Afrika ya Kusini, kwa msiba huu na tunawaomba sote kwa pamoja tuyageuze matendo ya kweli ya Mzee wetu Mandela kuwa dira thabiti ya kujenga mazingira ya KUJALI NA KUTEKELEZA HAKI SAWA KWA KILA RAIA bila kujali rangi yake, kipato chake, utaifa wake n.k.

Aidha, CUF itapeperusha bendera zake nusu mlingoti kuanzia leo Ijumaa tarehe 06/12 hadi siku ya jumapili tarehe 08/12/2013 kwa ajili ya kuomboleza na kuenzi mchango wa Mzee Mandela hapa duniani.

"Mzee Mandela amelala kwa amani, lakini matendo yake makuu yamelinda utu wa wanadamu"
Apumzike kwa amani. Amina.

Imetolewa na;
Prof. Ibrahim Haruna Lipumba,
Mwenyekiti wa Taifa,

0 Weka maoni yako hapa:

Post a Comment

COMMENT HAPA