Dec 16, 2013

Njama ya mapinduzi yatibuka Sudan Kusini

 https://fbcdn-sphotos-e-a.akamaihd.net/hphotos-ak-prn1/1525619_702312286454106_424011002_n.jpg

Rais wa Sudan Kusini Salva Kiir,amesema kuwa jeshi limetibua njama ya mapinduzi dhidi ya serikali yake. 

Rais Kiir amewalaumu wanajeshi wanaomuunga mkono aliyekuwa naibu wake Riek Machar ambaye alifutwa kazi, kwa mapigano yaliyozuka kati ya wanajeshi wake Jumapili usiku. Amesema kuwa serikali sasa imedhibiti hali.
Kiongea na waandishi wa habari, Bwana Kiir alisema serikali imedhibiti hali huku ikitangaza sheria ya kutotoka nje nyakati za usiku.

Wanajeshi mahasimu, walipigana vikali kwa masaa kadhaa na inaarifiwa kuna majeruhi kadhaa huku mamia wakitoroka mji wa Juba..

Kwa sasa milio ya risasi imekwisha. Kumekuwa na hali ya taharuki nchini Sudan Kusini tangu mwezi Julai wakati Rais Kiir alipowafuta kazi mawaziri wake akiwemo bwana Machar.

Wito wa utulivu

Awali Umoja wa Mataifa ulitoa wito wa utulivu nchini Sudan Kusini baada ya kuzuka mapigano kati ya vikosi vya jeshi katika mji mkuu Juba.

Umoja huo pia ulisema kuwa ni jukumu la Viongozi nchini humo kuitisha utulivu.

Kwa mujibu wa mwakilishi maalum wa katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa, Hilde Johnson, pande zinazozana zimetakiwa kusitisha mapigano haraka iwezekanavyo.

Alisema amekuwa akishauriana na viongozi wa taifa hilo wakiwemo viongozi mkuu kuhakikisha kuna utulivu.
Milio ya risasi ilisikika usiku kucha hadi asubuhi ya leo katika mji mkuu wa Sudan Kusini Juba kwa mujibu wa maafisa wa balozi na wengine waliohsuhudia tukio hilo.

Inaarifiwa mapigano hayo yametokea kati ya walinzi wa Rais wa Sudan Kusini Salva Kiir.
Mapigano yanasemekana yalianza saa nne usiku wa kuamkia leo katika kambi kuu kuu za jeshi mjini Juba na kuendelea kuwa makali kwa karibu saa moja kabla ya kundi moja kufurushwa.

Milio ya risasi ilisikika usiku kucha na kusababisha hali ya taharuki huku wananchi wakizuiwa kutoka nje.

Kwa mujibu wa shirika la habari la AFP, taarifa kutoka katika balozi za Marekani na Uingereza mjini Juba, zimetaka raia wa nchi zao kujizuia na kutoka nje.

Ubalozi wa Marekani umesema kuwa duru mbali mbali zinaarifu mapigano makali ya ufyatulinaji wa risasi yamesikika katika sehemu mbali mbali mjini Juba.

Mwandishi wa habari wa shirika la AFP amesema kuwa aliona wanajeshi waliokuwa wamejihami vikali wakishika doria katika barabara za Juba mapema asubuhi ya leo makabiliano makali yakiendelea katika kambi za jeshi.

Hata hivyo hakuna taarifa rasmi kutoka kwa jeshi kwani huduma za simu zimesemekana kutatizika.

Duru za kiijeshi zilisema kuwa makabiliano yalizuka kati ya kikosi cha jeshi cha Tiger, wakati moja ya kikosi ambacho kina wanajeshi wengi wa kabila la Nuer kushuku kuhusu muundo wa kikosi kingine cha jeshi ambacho wanajeshi wake wengi ni wa kabila la Dinka na hivyo kuanza kugombana kiasi cha kuanza kufyuatuliana risasi.

Inaarifiwa wanajeshi hao wa Nuer wamewafukuza wenzao wa Dinka ambao wengi wao walifuzu hivi karibuni na kuajiriwa katika serikali ya Rais Kiir.

chanzo na http://www.bbc.co.uk/swahili

0 Weka maoni yako hapa:

Post a Comment

COMMENT HAPA