Dec 18, 2013

YANGA NA SIMBA KUCHEZA JUMAMOSI BEI YA CHINI KUONA MECHI HII NI TSHS 5000

Mechi ya "Nani Mtani Jembe" kati ya Yanga SC na timu ya Simba SC itafanyika siku ya jumamosi katika dimba la Uwanja wa Taifa huku maandalizi yote yakiwa yamekamilika na Shirikisho la Mpira Miguu nchini  Tanzania (TFF) likitangaza Viingilio vya mchezo huo bei ya juu ni Tshs 40,000/=.


Akiongea na waandishi wa habari makao makuu ya shirikisho Kaimu Katibu Mkuu wa TFF Bw. Boniface Wambura amesema wao kama wasimamizi wa mchezo huo wamehakikisha masuala yote yamekamlika kuelekea mchezo huo na sasa kilichobakia ni timu zenyewe kuonyesha uwezo wao dimbani.


Mchezo huo wa jumamosi utachezeshwa na mwamuzi Ramadhani Ibada kutoka visiwani Zanzibar, huku akisaidiwa na washika vibendera Ferdinand Chacha kutoka Bukoba, Charles Simon kutoka Dodoma, mwamuzi wa akiba ni Israel Nkongo kutoka Dar es salaam na mtathimini wa waamuzi ni Soud Abdi.


Kwa upande wa klabu ya Yanga SC, Afisa Habari wake Baraka Kizuguto amesema maandalizi yote yamekamilika kuelekea mchezo huo, wachezaji wako katika hali nzuri kiafya, kifikra na morali ni ya hali ya juu.


"Wachezaji wetu waliokuwa katika timu za Taifa tayari wameshaungana na wenzao kujianda na mchezo huo, kikubwa tunawaomba wapenzi, wanachama na washabiki wa Yanga kwa ujumla na wadau wa soka kujitokeza kwa wingi kuja kuwashuhudia watoto wa Jangwani wanavyoendeleza ubabe dhidi ya Simba SC" alisema Kizuguto. 


Viingilio vya mchezo wa jumamosi ni:

VIP A Tshs 40,000/,
VIP B Tshs 20,000/=
VIP C Tshs 15,000/=
Rangi ya Chungwa Tshs 10,000/= 
Bluu Tshs 7,000/=
Kijani Tshs 5,000/=



Tiketi za mchezo huo zitaanza kuuzwa siku ya ijumaa saa 3 asubuhi katika vituo vifuatavyo:

1. Shule ya Sekondari  Benjamini Mkapa - Uhuru
2. Sokoni - Kariakoo
3. Steers - Samora Posta
4. Kituo cha mafuta - Buguruni
5. Kituo cha mafuta - Ubungo
6. Dar Live - Mbagala
7. Uwanja wa mpira wa Uhuru
8. BM Saloon - Sinza

0 Weka maoni yako hapa:

Post a Comment

COMMENT HAPA