Jan 3, 2014

BAADA YA KUSIKIA KILIO SERIKALI IMEONGEZA MUDA WA KUNUNUA (EFDs) HADI MWEZI UJAO

Serikali juzi ilitangaza kukubali maombi ya wafanyabiashara nchini ya kuongeza muda wa kununua Mashine za Kielektroniki za kutolea Risiti za manunuzi (EFDs) hadi mwezi ujao.

Muda huo umeongezwa kwa wafanyabiashara ambao walikuwa hawajazinunua mashine hizo.


Hatua hiyo ilitangazwa na Naibu Waziri wa Fedha, Saada Mkuya, akiwa amefuatana na Waziri wa Viwanda na Biashara, Dk. Abdallah Kigoda.


Mkuya alisema serikali imechukua hatua hiyo ya kuongeza muda huo ambao ni takribani siku 30, baada ya kufanya mazungumzo na baadhi ya wafanyabiashara na maofisa wa TRA.


Naibu Waziri alifafanua kuwa serikali imeamua kufanya hivyo, baada ya kusikiliza malalamiko ya wafanyabiashara ili kuwapa muda wale ambao walikuwa hawajanunua mashine hizo waweze kufanya hivyo.


Hata hivyo, alisema iwapo muda huo utamalizika wakiwa bado hawajanunua, wataongezewa siku 14 za mwanzo za kuwaonya na siku nyingine saba kama hawatatekeleza, na baada ya hapo sheria itachukua mkondo wake.


Aidha, Mkuya aliwaasa baadhi ya maofisa wa TRA na Polisi kuacha mara moja tabia ya kuwabughudhi wafanyabiashara kwa madai ya kwamba wamekuwa wakiwahujumu.


Kwa upande wake, Kamishna wa Kodi wa TRA, Patrick Kassera, alisema hatua zitakazochukuliwa kwa wafanyabiashara watakaoshindwa kununua mashine hizo ni pamoja kukatwa asilimia tano ya mapato kwa kosa la kwanza, na la pili ni asilimia 10 huku kosa la tatu ni kufungiwa biashara kwa siku saba na iwapo wataendelea kukaidi mbali na kutozwa faini hizo, watapelekwa mahakamani ambako watahukumiwa kifungo cha mwaka mmoja ama faini.


Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Wafanyabiashara, Sued Chemchem, aliishukuru serikali kwa kauli hiyo ya kuwachukulia hatua polisi ambao walikuwa wanajihusisha na vitendo hivyo.


Tangu TRA itangaze matumizi ya mashine hizo, wafanyabiashara kutoka mikoa mbalimbali nchini kama vile Mbeya, Dar es Salaam, Mwanza na Lindi wamekuwa wakiendesha migomo kwa kufunga maduka yao na kusitisha biashara zao wakipinga matumizi ya mashine hizo kwa madai ya kuuzwa kwa bei kubwa na kuwaingizia hasara.


Kitendo hicho cha wafanyabiashara hao kufunga maduka kushinikiza kuangaliwa upya kwa utaratibu wa mashine hizo za EFDs, kwa hakika kilikuwa kinadhoofisha uchumi wa nchi.


Aidha, kitendo hicho kilikuwa ni kero kubwa kwa wananchi na wafanyabiashara wengine wadogo wadogo ambao tegemeo lao ni maduka ya wafanyabiashara hao wakubwa.


Kwa mfano, kwa wakazi wa Jiji la Dar es Salaam, walishuhudia adha kubwa iliyojitokeza baada ya wafanyabiashara wa maeneo ya Kariakoo kugoma kufungua maduka yao.


Hali kama hiyo pia ilishuhudiwa kwa wananchi wa majiji ya Mbeya na Mwanza.


Hata hivyo, tunapenda kutumia fursa hii kuipongeza serikali kwa uamuzi wake huu wa kuwaongezea muda zaidi wafanyabiashara kununua mashine hizo kwani ni dhahiri imeonyesha kwamba ni sikivu ingawa kwa kiasi fulani imechelewa kuchukua hatua.


Lakini wakati tukiipongeza serikali kwa kuchukua hatua hiyo stahiki, tungependa pia kuwasisitiza wafanyabiashara ambao bado hawajanunua mashine hizo za EFDs, wawe waungwana na kuutumia vema muda huo kwa kuhakikisha kwamba unapomalizika wawe tayari wamenunua.


Kwa ujumla, haitapendeza kama muda huo ulioongezwa na serikali utafika halafu baadhi ya wafanyabiashara watoe visingizio vingine.


Inatarajiwa kwamba muda huu utawasaidia wafanyabiashara kujipanga vizuri na kuhakikisha kwamba wananunua mashine hizo ili kuepuka misuguano ya mara kwa mara na isiyo na tija na maofisa wa TRA.


Ikumbukwe kwamba malumbano kati ya wafanyabiashara, maofisa wa TRA na polisi, hayatawasaidia wananchi zaidi ya kufifisha juhudi zao za kujiletea maendeleo.


SOURCE: NIPASHE

0 Weka maoni yako hapa:

Post a Comment

COMMENT HAPA