Nov 1, 2012

YANGA YAICHAPA MGAMBO JKT 3-0





Safari imeshika kasi kwa mabingwa watetezi wa kombe la Kagame mara mbili mfululizo timu ya Young Africans, leo wameichapa timu ya Mgambo JKT mabao 3-0 katika mchezo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania bara, mchezo uliofanyika leo katika Uwanja wa Taifa.
 
Yanga ambayo imerudisha makali yake katika kinyanganyiro cha Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania bara, imefikisha jumla ya pointi 23 sawa na Simba SC ambao wanaongoza ligi kwa tofauti ya mabao ya kufunga na kufungwa.
 
Yanga ilianza mbio za kusaka point 3 muhimu na katika sekunde ya 15 ya mchezo, Mshambuliaji Saimon Msuva alikosa bao la wazi baada ya kupewa pasi nzuri na Haruna Niyonzima, lakini Msuva alishindwa kuukwamisha mpira huo wavuni.

Dakika ya 2 ya mchezo, Nadri Haroub 'Cannavaro' aliipatia Yanga bao la kwanza kwa kichwa, akiunganisha mpira wa faulo uliopigwa na Athuman Idd baada ya mshambuliaji Didier Kavumbagu kuchezewa ndivyo sivyo nje kidogo ya eneo la hatari.
 
Saimon Msuva, Hamis Kiiza na Haruna Niyonzima walikosa mabao mengi ya wazi katika kipindi cha kwanza kutokana na kutokua makini katika umaliziaji hali iliyopelekea mpaka dakika  30 za mchezo Yanga kuendelea kuwa mbele kwa bao 1 tu.
 
Didier Kavumbagu aliipatia Yanga bao la pili katika dakika ya 39 baada ya kumalizia pasi nzuri iliyopigwa na mshambuliaji Hamis Kiiza na kumkuta mfungaji ambaye hakufanya ajizi na kuukwamisha mpira huo wavuni na kuhesabu bao lake la tano.
 
Wachezaji wa timu ya Yanga waliendelea kuutawala mchezo kwa dakika zote za kipindi cha kwanza na kama umaliziaji ungekuwa makini basi Yanga ingeibuka na ushindi mkubwa zaidi katika dakika 45 za kipindi cha kwanza. 

Mpaka dakika 45 za kipindi cha kwanza Young Africans 2-0 Mgambo JKT.

Kipindi cha pili kilianza kwa Yanga kufanya mabadiliko kwa kumuingiza Kelvin Yondani aliyekuwa majeruhi kwa mda mrefu kuchukua nafasi ya Shadrack Nsajigwa.
 
Mabadiliko hayo yalileta uhai kwa vijana wa Jangwani kwani Mbuyu Twite ambaye alirudi kucheza nafasi ya mlinzi wa kulia, alipata nafasi ya kupanda mbele kuongeza nguvu mashambulizi hali iliyopelekea walinzi wa Mgambo JKT kumchezea faulo nyingi sana.
 
Jeryson Tegete ambaye aliingia kuchukua nafasi ya Didier Kavumbagu aliipatia Yanga bao la tatu baada ya kumalizia krosi safi iliyopigwa na Oscar Joshua aliyepanda kuongeza nguvu mashambulizi na kumkuta Tegete alifunga kwa kupiga shuti kali na mpira kuingia sehemu ya nyavu ndogo za juu.
 
Kama washambuliaji wa Yanga wangekuwa makini wangeweza kufunga mabao mengi zaidi, lakini kutokua kwao makini katika umaliziaji wa Saimon Msuva, Hamis Kiiza na Haruna Niyonzima uliwafanya wasiweze kupata mabao mengine ya ziada kwani nafasi walizozipata zingeweza kuifanya Yanga iondoke na ushindi mnono.

Mpaka dakika 90 za mchezo za mwamuzi Martin Sanya zinamalizika, Yanga iliibuka na ushindi wa mabao 3-0 Mgambo JKT

Yanga inajiandaa na mchezo wake dhidi ya Azam Fc siku jumapili, pambano ambalo litafanyika katika Uwanja wa Taifa jijini Dar es salaam.

Yanga: 1.Ally Mustapha, 2.Shadrack Nsajigwa/Klevin Yondani, 3.Oscar Joshua, 4.Nadir Haroub, 5.Mbuyu Twite, 6.Athuman Idd, 7.Saimon Msuva, 8.Frank Domayo/Nurdin Bakari 9.Didier Kavumbagu/Jeryson Tegete, 10.Hamis Kiiza, 11.Haruna Niyonzima

0 Weka maoni yako hapa:

Post a Comment

COMMENT HAPA