Aug 14, 2013

CCM YATOA UFAFANUZI KUHUSIANA NA TAARIFA YA KUVULIWA UANACHAMA MADIWANI WAKE 8

Chama Cha Mapinduzi
   TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI.

Halmashauri Kuu ya CCM Mkoa wa Kagera jana tarehe 13/08/2013 katika kikao chake cha siku moja kilichofanyika mjini Bukoba imetangaza uamuzi wake wa kuwafutia dhamana ya CCM hivyo kuwavua Udiwani Madiwani wanane wa Manispaa ya Bukoba waliotokana na CCM.

Kwa mujibu wa utaratibu wa kutoa adhabu kwa viongozi wa CCM walio kwenye vyombo vya dola hasa Wabunge na Madiwani uamuzi wa Halmashauri Kuu ya Mkoa sio wa mwisho. Uamuzi huo unapaswa kupata Baraka za Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa ndipo utekelezwe.

Hivyo basi, mpaka sasa Madiwani hao wanane waliosimamishwa wanapaswa kuendelea na kazi zao kama kawaida wakisubiri kikao cha Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa kitakachoketi tarehe 23 Agosti, 2013 mjini Dodoma ambacho pamoja na mambo mengine kitapitia uamuzi huo wa Halmashauri Kuu ya Mkoa wa Kagera.

Pamoja na hilo, tumepokea barua za Madiwani hao za kukata rufaa kupinga uamuzi huo wa Halmashauri Kuu ya Mkoa kwa msingi wa madai ya kukiukwa kwa utaratibu katika kufikia uamuzi huo.

Tunawasihi wananchi wa Bukoba na Kata husika, wanachama na viongozi wote kuwa watulivu katika kipindi hiki ambapo suala hili linashughulikiwa na vikao vya Kitaifa.

Imetolewa na:-

Nape M. Nnauye,
KATIBU WA HALMASHAURI KUU YA TAIFA
ITIKADI NA UENEZI
14/08/2013

0 Weka maoni yako hapa:

Post a Comment

COMMENT HAPA