Jul 27, 2012

TFF, Benki Zasaini Udhamini Wa BancABC Super 8

Benki ya ABC imesaini mkataba wa miaka mitatu na Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) kudhamini michuano ya BancABC Super 8 inayoshirikisha timu nane, nne kutoka Tanzania Bara na nyingine nne kutoka Zanzibar.

Hafla ya utiaji saini imefanyika leo (Julai 26 mwaka huu) kwenye ofisi za TFF, Dar es Salaam ambapo Katibu Mkuu Angetile Osiah amesaini kwa niaba ya shirikisho wakati kwa upande wa ABC, saini yake iliwekwa na Mkurugenzi Mtendaji wa benki hiyo kwa Tanzania, Boniface Nyoni.

Mashindano hayo yataanza Agosti 4-18 mwaka huu yakichezwa katika miji ya Dar es Salaam, Arusha, Mwanza na Zanzibar ambapo timu zote shiriki zitacheza katika vituo hivyo.

Uzinduzi rasmi wa mashindano hayo utafanywa Agosti 2 mwaka huu na Ofisa Mtendaji Mkuu (CEO) wa benki ya ABC yenye makao yake makuu nchini Botswana, na ina matawi katika nchi za Msumbiji, Zambia, Tanzania, Zimbabwe.

Katika uzinduzi huo, CEO ataelezea thamani ya mkataba huo ambapo utahusisha gharama za malazi, usafiri, vifaa na uendeshaji wa mashindano hayo.

Akizungumza baada ya kutia saini, Osiah amesema hatua hiyo ni sehemu ya mikakati ya TFF kuwa na mashindano mengi yatakayosaidia kuziandaa timu kabla ya kuanza Ligi Kuu.

Naye Nyoni amesema ABC imekubali kuingia kudhamini mpira wa miguu ikiwa ni lengo la kuchangia ustawi wa mchezo huo na kutoa sehemu ya faida wanayopata kwa kupitia michezo.

Timu zitakazoshiriki mashindano hayo ni zile zilizoshika nafasi tatu za juu katika Ligi Kuu ya Tanzania Bara na Ligi Kuu ya Zanzibar. Nyingine ni timu iliyoshika nafasi ya kwanza kwenye Ligi 

Daraja la Kwanza Tanzania Bara na Ligi Daraja la Kwanza ya Zanzibar ambazo nazo kwa kushika nafasi hizo zimeshaingia katika Ligi Kuu.






0 Weka maoni yako hapa:

Post a Comment

COMMENT HAPA