SMZ yaruhusu Sheikh Azzan kutibiwa nje
Zanzibar. Wizara ya Afya Zanzibar imeruhusu mshtakiwa wa nne, Kiongozi
Mwandamizi wa Jumuiya ya Uamsho na Mihadhara ya Kiislam (Jumiki), Sheikh
Azzan Khalid Hamdani (56), kupelekwa nje kutibiwa baada ya kukosekana
tiba ya maradhi yanayomsumbua visiwani hapa.
Sheikh Azzan
alilazwa Hospitali ya Rufani ya Mnazi Mmoja kuanzia Septemba Mosi, mwaka
huu baada ya kupoteza nguvu akiwa Gereza la Kiinua Miguu na imebainika
anasumbuliwa na vijiwe kwenye figo.
Kuruhusiwa kwa Sheikh Azzan kupata tiba nje, kumethibitishwa na wakili
wake, Salum Towfiq mbele ya Naibu Mrajisi wa Mahakama Kuu Zanzibar,
Yesaya Kayange.
Wakili Towfiq alisema mteja wake hali yake siyo
nzuri, amepata barua ya Wizara ya Afya Zanzibar kwamba maradhi
yanayomsumbua hayatibiki Zanzibar na kutaka mwongozo.
Licha ya
ombi hilo, Wakili Tawfiq aliwasilisha malalamiko kuwa wateja wake
wananyanyaswa, ikiwamo kutopata nafasi ya kuwasiliana na familia zao
kupitia simu na wanapokuwa kwenye mazingira ya Mahakama.
Alidai
Chuo cha Mafunzo Zanzibar (Magereza) kimewawekea utaratibu wa kukutana
na familia zao mara mbili kwa mwezi, huku akiomba Mahakama itoe
mwongozo.
Pia, alidai hata wanafamilia wanapotaka kwenda
mahakamani kusikiliza mwenendo wa kesi hukumbana na misukosuko na
kushindwa kuingia ukumbini kutokana na kuimarishwa ulinzi na kuzuia njia
za kuingia na kutoka.
Hata hivyo, Kayange alisema ombi la
kwanza la matibabu ya mshtakiwa liko nje ya uwezo wake na kutaka
liwasilishwe Mahakama Kuu. Pia, katika ombi la pili alikitaka Chuo cha
Mafunzo Zanzibar kuwatendea haki washtakiwa kwa mujibu wa taratibu na
sheria. Kayange aliahirisha kesi hiyo hadi Oktoba 7
0 Weka maoni yako hapa:
Post a Comment
COMMENT HAPA