Ndugu Wananchi;
Namshukuru Mwenyezi Mungu, mwingi wa rehma, kwa kutujaalia uzima na kutuwezesha
kumaliza mwezi Septemba salama na kuwasiliana kwa kutumia utaratibu wetu huu
mzuri. Naomba radhi kuzungumza nanyi siku ya leo kwa sababu nilikuwa
safari na nilirejea jioni ya tarehe 30 Septemba, 2013. Awali
nilifikiria nisiseme, nisubiri mwisho wa mwezi wa Oktoba. Lakini, baada
ya kupata taarifa ya yaliyojiri, nimeshauriwa na nimekubali angalau niyasemee
baadhi ya mambo huenda itasaidia. Niwieni radhi nisipoyasemea baadhi ya
mambo siyo kwa kuyapuuza, bali kwa kuepuka hotuba kuwa ndefu mno.
Nitayatafutia mahali pengine pa kuyasemea.
Uhusiano na Rwanda
Ndugu Wananchi;
Katika hotuba yangu ya mwisho wa mwezi wa Julai, nilizungumzia hali ya uhusiano
wetu na Rwanda kutokuwa mzuri na tatizo la ujambazi na wahamiaji haramu katika
Mikoa ya Kigoma, Geita na Kagera. Nafurahi kusema kuwa kwa yote mawili
kuna maendeleo ya kutia moyo.
Tarehe 5 Septemba, 2013, nilikutana na kuzungumza na Mheshimiwa Rais Paul
Kagame wa Rwanda mjini Kampala. Tuliitumia fursa ya ushiriki wetu katika Mkutano
wa Nchi za Maziwa Makuu kuzungumzia uhusiano baina yetu na nchi zetu.
Mazungumzo yalikuwa mazuri na sote tulikubaliana kuwa yaliyopita si ndwele
tugange yajayo. Kwa sababu hiyo tulielewana kuwa tutengeneze mazingira
yatakayosaidia kutuliza hali na kurudisha nchi zetu katika uhusiano mwema kama
ilivyokuwa siku zote. Nawaomba ndugu zangu hususan wanasiasa, watumishi
wa umma, wanahabari na wenye mitandao ya kijamii na blog na wananchi kwa ujumla
tusaidie kuimarisha uhusiano mwema baina ya Rwanda na Tanzania na watu wake.
Majambazi na
Wahamiaji Haramu
Ndugu Wananchi;
Katika
hotuba hiyo pia nilisema kuwa tutachukua hatua thabiti dhidi ya majambazi na
wageni wanaoishi nchini bila ya kuzingatia taratibu zinazohusika.
Niliwataka majambazi wajisalimishe wao na silaha zao kwa hiari. Wale
wanaoishi nchini bila ya kuwa na kibali halali wahalalishe ukaazi wao au
warejee makwao. Nilitoa siku 14 kuanzia tarehe 29
Agosti, 2013 wafanye hivyo kwani baada ya hapo tungeanzisha operesheni maalum
ya kushughulika na watu wa makundi yote mawili.
Ndugu Wananchi;
Kumekuwepo na mafanikio ya kutia moyo. Kwa upande wa wahamiaji wanaoishi
nchini kinyume cha sheria watu wapatao 21,254 waliondoka kwa
hiari. Hali kadhalika zaidi ya ng’ombe 8,000 waliondolewa na silaha
102 zilisalimishwa. Baada ya
operesheni kuanza tarehe 6 Septemba, 2013 na kumalizika tarehe 20 Septemba,
2013, wahamiaji haramu 12,828 walirejeshwa makwao
na watuhumiwa 279 wa unyang’anyi wa kutumia silaha
walikamatwa. Aidha, mabomu 10 ya kutupa kwa mkono
(offensive hand grenades), silaha 80, risasi
780
na mitambo 2 ya kutengeneza magobole
vilikamatwa. Pia, ng’ombe 8,226 walikamatwa
wakichungwa katika mapori ya hifadhi. Kwa upande wa mazao ya misitu, mbao
2,105 zilikamatwa pamoja na nyara mbalimbali
za Serikali.
Ndugu Wananchi;
Agizo la kuwataka watu wanaoishi nchini isivyo halali wahalalishe ukaazi wao au
waondoke kwa hiari au wataondolewa lilipotoshwa hasa na vyombo vya habari vya
nje ya Tanzania. Walikuwa wanadai eti Tanzania ilikuwa inafukuza
wakimbizi. Madai hayo si ya kweli hata kidogo. Hadi kufikia
tarehe 30 Septemba, 2013 wakimbizi 68,711 walikuwepo kwenye
Kambi ya Nyarugusu, Mkoani Kigoma. Hakuna mkimbizi ye yote aliyetakiwa
kuondoka. Ukweli ni kwamba hakuna mtu ye yote kati ya wale watu
walioondoka kwa hiari au kusaidiwa kuondoka wakati wa operesheni ambaye ni
mkimbizi. Kama ingekuwa hivyo, wa kwanza kulalamika wangekuwa wenzetu wa
Shirika la Wakimbizi la Umoja wa Mataifa. Bahati nzuri jambo hilo
halikutokea.
Ndugu Wananchi;
Yalikuwepo pia madai kwamba tunawaonea na kuwatesa watu walioishi nchini miaka
mingi. Ati iweje sasa ndiyo waambiwe kuwa siyo raia. Siku zote
Serikali ilikuwa wapi? Uraia haupatikani kwa kuishi nchi ya kigeni kwa miaka
mingi. Unapatikana kwa kutimiza masharti ya kuomba na kupewa uraia.
Kama mtu hakufanya hivyo anabaki kuwa raia wa nchi aliyotoka au walikotoka
wazazi wake. Ipo mifano ya watu mashuhuri ambao walilazimika kuachia
nyadhifa zao baada ya kugundulika kuwa siyo raia. Hawakuwa wanaonewa,
ndiyo matakwa ya Katiba na Sheria za nchi yetu.
Ndugu Wananchi;
Katika kutekeleza operesheni hii niliagiza kuwa wale watu ambao wameishi hapa
nchini miaka mingi ambao wana nyumba, mashamba au mali mbalimbali au wameoa au
kuolewa na wana watoto au hata wajukuu waelekezwe kuhalalisha ukaazi wao.
Iwapo watakataa kufanya hivyo basi wasaidiwe kurejea kwao. Pia niliagiza
watu wasiporwe mali zao wala kudhulumiwa. Sijapata taarifa ya kufanyika
kinyume na maelekezo yangu. Lakini kama wapo watu waliotendewa tofauti,
taarifa itolewe kwa Wakuu wa Wilaya na Mikoa au hata Ofisi ya Rais ili hatua
zipasazo zichukuliwe. Hatutaki watu wadhulumiwe au kuonewa.
Napenda kutumia nafasi hii kumpongeza Waziri wa Ulinzi na JKT, Mheshimiwa Shamsi
Vuai Nahodha na Waziri wa Mambo ya Ndani, Mheshimiwa Emmanuel Nchimbi kwa
uongozi wao mzuri katika zoezi hili. Pia, nawapongeza Makamanda na askari
wa JWTZ na Polisi pamoja na maafisa wa Idara ya Uhamiaji, Idara ya Mifugo,
Idara ya Wanyamapori, Idara ya Misitu na Idara nyinginezo za Serikali kwa kazi
kubwa na nzuri waliyofanya. Najua awamu ya kwanza imeisha tarehe 20
Septemba, 2013 na kama nilivyosema kuwa safari hii operesheni itakuwa endelevu,
muda si mrefu awamu ya pili itafuata. Nawaomba waendelee kuchapa kazi kwa
bidii, maarifa na nidhamu ya hali ya juu.
Ziara ya Canada na
Marekani
Ndugu Wananchi;
Kati
ya tarehe 17 na 28 Septemba, 2013 nilifanya ziara ya kikazi katika nchi za
Canada na Marekani. Nchini Canada nilitembelea Chuo Kikuu cha Guelph
ambapo nilitunukiwa Shahada ya Heshima ya Uzamivu kwa kutambua jitihada zetu
tuzifanyazo kujiletea maendeleo na mafanikio ya kutia moyo tunayoendelea kupata
licha ya changamoto zinazotukabili. Katika mazungumzo yangu na uongozi wa
chuo hicho wamekubali kuwa na ushirikiano wa karibu na Wizara zinazohusika na
Elimu, Kilimo na Mifugo pamoja na Chuo Kikuu cha Kilimo cha Sokoine,
Morogoro na Chuo Kikuu cha Dodoma. Nimewataka Mawaziri wa Wizara hizo na
viongozi wa vyuo hivyo kuchangamkia fursa hiyo bila kuchelewa.
Ndugu Wananchi;
Nchini
Marekani nilikutana na kuzungumza na maafisa na viongozi mbalimbali wa Serikali
ya nchi hiyo wakiwemo Rais Barack Obama na baadhi ya Wabunge wa Bunge la
Marekani. Mazungumzo yetu yalilenga kuimarisha ushirikiano baina ya nchi
zetu na mambo yalienda vizuri. Wote walituhakikishia kuwa mambo
tuliyoyazungumza na kukubaliana na Rais Barack Obama wakati wa ziara yake
nchini yanaendelea kufanyiwa kazi. Miongoni mwa hayo maombi yetu ya
kupatiwa vitabu milioni 2.4 vya sayansi na hisabati
yamekubaliwa na utekelezaji umeanza. Upatikanaji wa vitabu hivyo
utamwezesha kila mwanafunzi wa sekondari kuwa na kitabu chake.
Ndugu Wananchi;
Jambo
lingine kubwa na la faraja kwetu ni kuwa mapendekezo yetu ya miradi ya umeme na
barabara za vijijini za kugharamiwa na Serikali ya Marekani kupitia Shirika lao
la Changamoto za Milenia yamepokelewa vizuri. Kinachosubiriwa ni miradi
ipi itakubaliwa na Bodi ya MCC na kiasi gani cha fedha kitatengwa na Bunge la
Marekani kwa ajili hiyo.
Tuzo ya Uhifadhi
Jambo
lingine muhimu katika safari yangu ya Marekani ni kutunukiwa tuzo na
“International Congressional Conservation Foundation” kwa kutambua juhudi zetu
katika kuhifadhi wanyama pori na mafanikio tuliyoyapata. Licha ya
changamoto mbalimbali tunazokabiliana nazo, tuzo hii imetupa moyo wa kuongeza
nguvu katika jitihada tunazozifanya sasa kupambana na ujangili na matatizo
mengine ya uhifadhi wa wanyama na misitu.
Ndugu Wananchi;
Kilichotupa
moyo zaidi ni kauli za utayari wa kutusaidia katika mapambano hayo zilizotolewa
wakati wa kupewa tuzo na katika mkutano wa mfuko wa Maendeleo wa Clinton na
katika mkutano maalum wa kupambana na ujangili na biashara ya meno ya tembo
duniani.
Baraza Kuu la Umoja
wa Mataifa
Ndugu Wananchi;
Shabaha
kuu ya safari yangu ya Marekani ilikuwa kuhudhuria Mkutano wa 68 wa Umoja wa
Mataifa unaoendelea jijini New York mpaka Desemba, 2013. Mada kuu ya
mkutano wa mwaka huu ni kuandaa agenda ya maendeleo baada ya mwaka 2015 yaani: Post
2015 Development Agenda: Setting the Stage. Kama
mtakavyokumbuka Malengo ya Milenia yaliyoamuliwa na Baraza Kuu la Umoja wa
Mataifa mwaka 2000, yanafikia ukomo wa utekelezaji wake mwaka 2015.
Katika
Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa mwaka huu mjadala umehusu nini kifanyike baada
ya mwaka 2015. Hata hivyo, mjadala huo unaanza kwa kufanya tathmini ya
utekelezaji wa yale Malengo Manane ya Milenia ya mwaka 2000 umefikia wapi mpaka
sasa na utafikia wapi mwaka 2015 kwa kila nchi na kwa dunia kwa ujumla.
Tathmini ya jumla inaonesha kuwa kumekuwepo na jitihada kubwa ya kutekeleza
malengo haya katika kila nchi. Yapo malengo ambayo utekelezaji wake
umefikia shabaha hivi sasa na yapo ambayo upo uwezekano wa shabaha kufikiwa
ifikapo mwaka 2015. Vile vile yapo ambayo shabaha haitafikiwa.
Ndugu Wananchi;
Kwa
upande wetu, Tanzania, tumefikia shabaha katika mambo yafuatayo:
- Lengo la Milenia namba 2 kuhusu uandikishaji wa watoto wenye umri wa kwenda shule ya msingi;
- Lengo la Milenia namba 3 hasa kuhusu usawa wa kijinsia katika Shule za Msingi na Sekondari. Ukweli ni kwamba, wasichana wanaanza kuwa wengi kuliko wavulana. Hatujafikia shabaha kwa upande wa usawa wa kijinsia katika elimu ya juu na ni vigumu kulifikia ifikapo 2015. Pia hatujafikia lengo kwa upande wa usawa wa Wabunge wanawake na wanaume. Hata hivyo, kwa kutumia mchakato wa Katiba unaoendelea sasa tunaweza kufikia lengo katika uchaguzi wa 2015 iwapo tutaamua iwe hivyo;
- Lengo la Milenia namba 4 kuhusu kupunguza idadi ya vifo vya watoto wachanga na wale wenye umri chini ya miaka mitano;
- Tumefikia shabaha kwa Lengo la Milenia Namba 6 kuhusu kupunguza maambukizi ya UKIMWI; na
- Kwa upande wa lengo namba 7 kuhusu mazingira, tumefikia shabaha kwa upande wa upatikanaji wa maji mijini. Bado tuko nyuma kwa maji vijijini ingawaje tunaweza kufikia lengo ifikapo mwaka 2015 kama tutaendeleza uwekezaji tulioamua kufanya katika bajeti ya mwaka huu. Lakini, hatutaweza kufikia shabaha kwa upande wa usafi wa mazingira mijini na vijijini ifikapo mwaka 2015. Safari bado ndefu sana.
Ndugu Wananchi;
Malengo
ya Milenia namba 1 na namba 5 ambayo bado tuko nyuma sana ya shabaha
hatutafikia lengo ifikapo 2015. Tumeendelea kutekeleza lengo la Milenia namba
1
kuhusu kupunguza umaskini na njaa kwa zaidi ya nusu kutoka kiwango cha mwaka
2000. Hatua tunazochukua kuleta mageuzi katika kilimo zina lengo la
kuhakikisha usalama wa chakula na kuongeza mapato ya wakulima. Mafanikio
yanaanza kuonekana lakini si ya kiwango cha kutufikisha kwenye lengo ifikapo
mwaka 2015. Tunao, pia, mpango wa kupanua programu ya TASAF ya Conditional
Cash Transfer
ili tuwafikie watu wengi maskini. Hata kama tutafanikiwa
kuutekeleza mapema mpango huu utatusogeza sana mbele lakini bado tutakuwa chini
ya lengo kwa upande wa kupunguza umaskini ifikapo 2015.
Ndugu Wananchi;
Kwa
upande wa Lengo la Milenia namba 5, kuhusu afya ya kina mama wajawazito
bado tuko nyuma katika kupunguza vifo vya kina mama wajawazito na kuongeza
idadi ya wajawazito wanaojifungua chini ya uangalizi wa wataalamu wa
afya. Hatutaweza kufikia shabaha ifikapo mwaka 2015. Mpango wa
Maendeleo ya Afya ya Msingi (2007 – 2017) una nia ya kukabiliana na matatizo
haya. Tumeongeza ujenzi wa zahanati, vituo vya afya na hospitali, tumeboresha
upatikanaji wa dawa na tumepanua sana mafunzo ya madaktari, wauguzi na wakunga
mambo ambayo yamesaidia kutufikisha hatua tuliyopiga mpaka sasa. Naamini juhudi
zetu tukiziendeleza zitatusogeza mbele zaidi ingawaje bado tutakuwa chini ya
lengo. Miaka michache ijayo, tatizo hili nalo litakuwa historia.
Ndugu Wananchi;
Lengo
la Milenia namba 8 linazihusu nchi tajiri kuongeza michango yao kusaidia nchi
zinazoendelea kutekeleza Malengo ya Milenia. Bahati mbaya sana mataifa
tajiri hayajafikia viwango wanavyotarajiwa kutoa na hata vile wanavyoahidi
wenyewe kutoa katika majukwaa mbalimbali. Kama wangetimiza ahadi zao,
sura ya utekelezaji wa Malengo ya Milenia ingekuwa tofauti kabisa.
Ndugu Wananchi;
Hiyo
ndiyo hali ya utekelezaji wa Malengo ya Milenia hapa nchini. Hakuna nchi ye
yote duniani iliyofanikiwa kutekeleza shabaha za malengo yote kwa
ukamilifu. Ushauri wa viongozi wote waliozungumza ulitaka mataifa
yaliyoendelea yatimize ahadi zao za kuchangia utekelezaji wa Malengo ya
Milenia. Ilionekana suala la upatikanaji wa fedha halina budi kuangaliwa
kwa makini sasa na baada ya mwaka 2015. Bila ya hivyo ufanisi utakuwa
mdogo katika kuongeza kasi ya utekelezaji kwa pale paliposalia kufikia malengo
ya 2015 na hata kwa Malengo ya baada ya mwaka 2015.
Mashambulizi ya
Kigaidi ya Westgate, Nairobi
Ndugu Wananchi;
Wakati
nikiwa safarini, tarehe 21 Septemba, 2013 kulitokea shambulilizi la
kigaidi katika Jengo la Biashara la Westgate, huko Nairobi, Kenya. Watu 67
walipoteza
maisha na zaidi ya 200 walijeruhiwa. Nilituma salamu za
pole na rambirambi kwa Mheshimiwa Rais Uhuru Kenyatta na wananchi wa Kenya na
kuwahakikishia kuwa tupo pamoja nao katika wakati huu wa majonzi.
Nafahamu
kuwa baada ya tukio hilo watu wengi hapa nchini wameingiwa na hofu kuhusu
usalama wetu. Ni hofu ya msingi kwani tarehe 8 Agosti, 1998 Ubalozi wa
Marekani hapa nchini ulishambuliwa na magaidi na ndugu zetu 11 wasio na hatia
walipoteza maisha.
Ndugu Wananchi;
Napenda
kuwafahamisha kuwa tangu shambulio la mwaka 1998, Serikali imekuwa inajenga
uwezo wa vyombo vyetu vya ulinzi na usalama kupambana na ugaidi katika nyanja
mbalimbali. Tunaendelea kujiimarisha bila kusita siku hadi siku.
JWTZ, Polisi na Idara ya Usalama wa Taifa wamekuwa na ushirikiano wa karibu kwa
ajili hiyo. Juhudi zetu hizo ndizo zinazotufanya tuwe salama hadi sasa.
Baada
ya tukio la Kenya, vyombo vyetu vya ulinzi na usalama vimeimarisha mikakati yao
maradufu. Pamoja na kujizatiti kwetu huko hatuwezi kusema kuwa tukio la
kigaidi halitaweza kutokea nchini. Uhakika huo hatuna kwani hata mataifa
makubwa na tajiri yameshambuliwa. Kilicho muhimu ni kuendelea kuchukua
tahadhari na wananchi kusaidia ili vyombo vyetu vifanikiwe zaidi.
Hali
kadhalika, tumewataka watu wote wenye shughuli zinazokusanya watu wengi kama
vile maduka, maofisi, mahoteli, migahawa n.k. waweke kamera za ulinzi nje na
ndani ya maeneo yao. Pia waangalie uwezekano wa kuweka vifaa vya upekuzi
(metal detectors and x-rays). Najua watu wanaweza kulalamikia usumbufu au
gharama, lakini gharama na hasara ya kushambuliwa ni kubwa zaidi kuliko ya
usumbufu huo.
Ndugu Wananchi;
Nawaomba
muendelee kufanya shughuli zenu bila ya hofu ingawaje msiache kuwa makini na
kuchukua tahadhari. Watu watoe taarifa kwa vyombo vya usalama wanapoona
mtu au watu au kitu cha kutilia shaka. Ni muhimu kwa usalama wake, wa
kila mtu, jamii na taifa. Maafisa husika wa vyombo vya ulinzi na usalama
wataendelea kuelimisha umma kuhusu hatua mbalimbali za tahadhari za
kuchukua. Sisi Serikalini tumejipanga kuchukua hatua zaidi kuimarisha
ulinzi na usalama wa nchi yetu na watu wake.
Mchakato wa Katiba
Mpya
Ndugu Wananchi;
Kama mtakavyokumbuka, Bunge lilitunga Sheria ya Mabadiliko ya Katiba Novemba,
2011. Sheria hii imeweka mchakato mzima wa kupata Katiba hiyo na kuunda
taasisi zake. Mwezi Mei, 2012, Tume ya Mabadiliko ya Katiba iliundwa na
imekamilisha hatua tatu muhimu katika mchakato huo. Hatua hizo ni kupokea
maoni ya wananchi, kutayarisha rasimu ya kwanza ya Katiba Mpya na kupokea maoni
ya Mabaraza ya Katiba ya Wilaya na ya taasisi. Hivi sasa Tume inaandaa
mapendekezo ya Rasimu ya Pili ya Katiba itakayopelekwa kwenye Bunge
Maalum. Baada ya tafakuri zake, Bunge Maalum litatoa rasimu ya mwisho ya
Katiba ambayo itapelekwa kwa wananchi kwa ajili ya uamuzi wa mwisho kupitia
kura ya maoni. Baada ya hatua hiyo, ndipo tutakapokuwa tumepata Katiba
Mpya.
Ndugu Wananchi;
Baada
ya Bunge la Novemba, 2011 kupitisha Sheria ya Mabadiliko ya Katiba, kulikuwepo
na madai ya kutaka sheria hiyo iboreshwe kutoka vyama vyote vya siasa vikiwemo
vyama vya upinzani na Chama tawala. Majadiliano yalifanyika baina ya
Serikali na vyama hivyo pamoja na shirikisho la asasi za kiraia.
Makubaliano yalifikiwa kuwa marekebisho yafanyike kwa awamu. Awamu ya
kwanza ihusishe Tume ya Mabadiliko ya Katiba kisha hapo yafanyike marekebisho
yanayohusu Bunge Maalum na mwisho Kura ya Maoni.
Kama
ilivyokuwa kwa mabadiliko yaliyohusu Tume ya Mabadiliko ya Katiba, safari hii
nayo vyama vya siasa vilitoa mapendekezo yao. Yalifanyika mazungumzo kati
yao na Serikali na maelewano kufikiwa kuhusu maeneo ya kufanyiwa marekebisho.
Serikali ilitayarisha rasimu ya Muswada na kuuwasilisha kwa wenzetu wa Serikali
ya Mapinduzi ya Zanzibar.
Ndugu Wananchi;
Serikali
ya Mapinduzi Zanzibar ilitoa mapendekezo yake na ushauri kwenye maeneo mawili.
Kwanza kwamba uteuzi wa wajumbe wa Bunge Maalum ufanywe na Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania kwa kushauriana na kuafikiana na Rais wa Zanzibar.
Pili walishauri kwamba kama Bunge Maalum litashindwa kufikia maamuzi ndani ya
siku 70 zilizopendekezwa, liweze kuongezwa
muda hadi kufikia siku 90. Maeneo mengine ya Muswada
waliafikiana nayo.
Ndugu Wananchi;
Kwa kuzingatia utaratibu wa kutunga Sheria, Serikali ilifikisha Muswada kwa
Spika wa Bunge ambaye nae aliuwasilisha kwenye Kamati ya Kudumu ya Katiba,
Sheria na Utawala. Kama ilivyo ada, Kamati hiyo ilifanya vikao na wadau
na kupokea maoni yao kuhusu Muswada. Nimeambiwa kulikuwa na mjadala wa
kina na mapendekezo mazuri yalitolewa na wadau. Kisha hapo Wajumbe wa
Kamati walikaa wenyewe kujadili Muswada walikuwepo pia Wabunge ambao si Wajumbe
wa Kamati walioshiriki kwa vile Kanuni zinaruhusu. Nimeambiwa pia kwamba
mjadala ulikuwa mpana na wa kina zaidi. Mapendekezo kadhaa yalitolewa na
Wajumbe kuhusu vifungu mbalimbali vya Muswada.
Ndugu Wananchi;
Nimefahamishwa
kuwa Wabunge wa vyama vyote walichangia na kwamba baadhi ya nyakati mambo
yalipokuwa ugumu mawazo mazuri ya baadhi ya Wabunge wa upinzani yalisaidia
kupata ufumbuzi. Nimeambiwa pia kwamba Wajumbe wa Kamati na upande wa
Serikali walikubaliana kwa maeneo mengi isipokuwa machache ambayo walikubaliana
kwa pamoja wayapeleke Bungeni ili Wabunge nao wayajadili na kuyapatia
ufumbuzi.
Ndugu Wananchi;
Baada ya Kamati kumaliza kazi yake, Waziri wa Katiba na Sheria, Mheshimiwa
Mathias Chikawe aliwasilisha Muswada Bungeni. Akafuatiwa na Mheshimiwa
Gosbert Blandes kwa niaba ya Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba,
Sheria na Utawala, kutoa maoni ya Kamati. Baadaye Msemaji wa Kambi ya Upinzani,
Mheshimiwa Tundu Lissu alitoa maoni yake.
Ndugu Zangu;
Baada
ya watu hao watatu kutoa maoni yao ilitarajiwa kuwa Wabunge wangeanza kujadili
Muswada. Naambiwa mambo hayakuwa hivyo. Badala yake kukazuka
malumbano baina ya Spika na baadhi ya Wabunge wa Upinzani wakitaka Muswada
usijadiliwe. Ilifikia wakati hoja hiyo ikabidi iamuliwe kwa kura ambapo
ilishindwa. Katika hali isiyotarajiwa, Wabunge wote wa upinzani wakatoka
nje ya Bunge isipokuwa wawili. Kitendo hicho kimewanyima Wabunge wengi wa
upinzani fursa ya kutetea hoja zao walizozitoa kupitia hotuba ya Msemaji wa
Kambi ya Upinzani. Pia wamejinyima nafasi ya kusema mambo mengine wakati
wa mjadala na Kamati ya Bunge zima.
Wabunge
waliokuwepo waliendelea kuujadili Muswada na kutoa hoja na mapendekezo ya
kuuboresha. Walifanya hivyo wakati wa mjadala na wakati wa kupitia
kifungu kwa kifungu. Baadhi ya hoja na mapendekezo yalikubaliwa na
mengine yalikataliwa. Miongoni mwa yaliyokubaliwa na Wabunge, kwa mfano,
ni kuhusu elimu ya mtu atakayekuwa Mwenyekiti wa Bunge Maalum na lile la ukomo
wa uhai wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba.
Ndugu Wananchi;
Kwa
maoni yangu madai ya Kambi ya Upinzani yanazungumzika na hata baadhi yangeweza
kukubalika kama Wabunge wake wangekuwepo Bungeni na kushiriki mchakato wote wa
kujadili na kupitisha Miswada Bungeni. Bahati mbaya hawakuwepo, hivyo
hapakuwepo na mtu wa kusema mawazo yao. Baada ya kupoteza fursa yao
halali, kutaka kupata ufumbuzi nje ya Bunge ni jambo lisilowezekana. Haya
ni masuala yanayohusu Bunge ambayo hujadiliwa na kuamuliwa Bungeni na si
vinginevyo. Kuandamana nchi nzima au kuchukua hatua za kutotii sheria kama
Mwenyekiti wa CHADEMA, Mheshimiwa Freeman Mbowe anavyotaka, hakutaleta
mabadiliko wanayoyataka katika sheria hii. Naamini na wao wanautambua ukweli
huo.
Ndugu Wananchi;
Kuna
msemo wa wahenga kuwa “historia hujirudia”. Naomba hekima ziwaongoze
viongozi wa CHADEMA, CUF na NCCR-Mageuzi na zituongoze sote kutumia utaratibu
tulioutumia mwaka 2012. Kulipotokea mazingira kama haya pande zote
zilikaa pamoja na kuzungumzia hoja moja baada ya nyingine na kukubaliana nini
kifanyike na kifanyike vipi. Baada ya kuridhiana hatua zipasazo za
kisheria na kanuni zilichukuliwa na kumaliza mzozo.
Ndugu Wananchi;
Kufanya
kinyume cha hayo hakutaleta ufumbuzi wa mzozo huu. Tutaliingiza taifa
kwenye matatizo yasiyokuwa ya lazima. Tukikataa kufanya hayo Watanzania wanayo
kila sababu ya kuhoji dhamira zetu na kutilia shaka nia zetu. Watakuwa na
haki ya kuuliza nia ni hii yetu sote ya kupata Katiba Mpya kwa kutumia njia za
kikatiba na kisheria au tuna dhamira nyingine iliyojifisha?
Kama
dhamira yetu ni kutaka kupata Katiba mpya kwa mujibu wa Katiba na Sheria,
ushauri wangu na rai kwa ndugu zetu wa CHADEMA, CUF na NCCR-Maguezi ni kuwa
waachane na mipango ya maandamano na kufanya ghasia. Badala yake watumie
njia halali zinazotambulika kikatiba na kisheria kujenga hoja za kufanya
marekebisho wanayoyaona wao yanafaa kuboresha Sheria ya Marekebisho ya Sheria
ya Mabadiliko ya Katiba. Tukifanya hivyo tutakuwa tunajenga badala ya
kubomoa. Tutaliponya taifa. Sisi katika Serikali tuko tayari.
Ndugu Wananchi;
Napenda
pia kuzisemea baadhi ya hoja zilizotolewa na Kambi ya Upinzani.
Kwanza kabisa nasema kuwa nimesikitishwa sana na madai na tuhuma za uongo
eti katika uteuzi wa Tume ya Katiba sikuheshimu mapendekezo ya TEC, CCT na
walemavu.
Ndugu Zangu, Watanzania Wenzangu;
Siyo
tu kauli hiyo ya Mheshimiwa Tundu Lissu ni uzushi na uongo mtupu bali pia ni ya
unafiki, fitina na uzandiki wa hali ya juu. Nasema hivyo kwa sababu,
sipendi kuamini kuwa Mheshimiwa Mbunge amesema yale kwa kutokufahamu ukweli au
kwa bahati mbaya. Amesema yale kwa makusudi mazima ya kupotosha ukweli
ili pengine isaidie kujenga hoja yake ya kutaka Rais asiteue wale Wajumbe
166
wa Bunge Maalum.
Napenda
ieleweke kuwa siishabikii kazi hiyo, lakini kwa kutimiza wajibu na maslahi ya
taifa nikiagizwa na Sheria za nchi nitafanya. Nasema hivyo kwa sababu
nafahamu ni kazi ngumu. Kama kazi ya uteuzi wa Wajumbe 30 wa Tume haikuwa
rahisi hata kidogo, hii ya uteuzi wa watu 166 itakuwa ngumu
zaidi. Ile ya Tume ilikuwa ngumu kwa namna mbili. Kwanza, kwamba taasisi
zilizoomba na waombaji walikuwa wengi mno kuliko nafasi za kujaza yaani 15 Zanzibar na 15 Bara. Zanzibar
ziliomba taasisi zaidi ya 60 na waombaji walikuwa zaidi ya 200 wakati Bara kulikuwa
na taasisi zaidi ya 170 zikiwa na waombaji zaidi ya 500. Kupata watu
30 kutoka orodha kubwa kiasi hicho si mtihani mdogo. Pili kwamba
tulitakiwa kuunda Tume inayoasili sura ya taifa, yaani watu wa nchi yetu kwa
maeneo, vyama vya siasa, dini, wanawake, vijana, walemavu, wafanyakazi, wasomi,
Wabunge, Wawakilishi, wanasheria, wafanyabiashara, wakulima, asasi za kiraia
n.k.
Ndugu Wananchi;
Pamoja
na changamoto hizo, lakini tulifanikiwa kuunda Tume iliyopokelewa vizuri na
jamii na kufanya watu wengi hata wale ambao hawakuteuliwa wahisi
kuwakilishwa. Tulifanyaje? Kwanza kabisa tulihakikisha kuwa tunapata
wawakilishi wa vyama vya siasa vyenye wawakilishi Bungeni na kwenye Baraza la
Wawakilishi na tunapata wawakilishi wa mashirika ya dini zetu kubwa yaani, TEC,
CCT na BAKWATA. Ndiyo maana nikasema kuwa kwa Mheshimiwa
Tundu Lisu kudai kuwa mapendekezo ya TEC na CCT hayakuheshimiwa ni uongo wa
mchana usiokuwa na kichwa wala miguu.
Baada
ya hapo ndipo tukaangalia waombaji wa makundi na taasisi nyingine.
Tulijitahidi sana kupata watu ambao wanawakilisha kundi zaidi ya
moja. Tulifikiria hivyo kwa sababu ni ukweli ulio wazi kuwa si kila
taasisi iliyoomba itapata mwakilishi kwani hata tungependa iwe hivyo nafasi
hazikuwepo. Kwa kutumia utaratibu huu makundi mengi yamepata uwakilishi
kutokana na watu waliopendekezwa na makundi mengi. Tumefanya kazi kubwa
sana ya kuwianisha mambo na makundi ya maslahi mbalimbali nchini.
Ndiyo maana naiona mantiki ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
akishirikiana na Rais wa Zanzibar wa kuwateua Wajumbe wa Bunge Maalum.
Dhana kuwa kila kikundi kiteue chenyewe watu ingefaa sana kama kungekuwepo na
nafasi za kutosha kila kundi nchini. Hilo haliwezekani, labda tuwe na
Bunge Maalum lisilokuwa na ukomo wa wajumbe.
Ndugu Wananchi;
Mimi
na Rais wa Zanzibar tumekuwa tunajiuliza baada ya kazi ngumu na nzuri
tuliyoifanya na iliyopongezwa na wengi ya kuteua Tume ya Mabadiliko ya Katiba
nini kilichoharibika sasa hata tuonekane hatuaminiki kuteua hawa 166? Kama ni kwa
sababu za Mheshimiwa Tundu Lissu, nimeshasema hazina ukweli wowote.
Ninapojiuliza kwa nini aseme uongo nashindwa kupata jibu linaloingia
akilini. Wakati mwingine nafikiria kuwa ni hiana. Lakini nadhani ni
hila za kisiasa zenye nia ya kutaka kupata watu wa kutetea maslahi ya chama
chake. Kama hiyo ndiyo shabaha basi amekosea sana.
Ndugu Zangu, Watanzania Wenzangu;
Hatutengenezi
Katiba ya Chama fulani bali Katiba ya nchi, Katiba ya watu wa vyama vyote na
wasiokuwa na vyama ambao ndiyo wengi kuliko wote. Lazima tuongozwe na
ukweli huo na tuwe na msimamo huo wakati wote. Lazima tukumbuke kuwa si
watu wote wanaostahili au kuwa na sifa ambao wataomba na kupata nafasi ya kuwa
Wajumbe, hivyo wale wachache watakao bahatika lazima wawasemee wote.
Wanatakiwa kusikiliza na kuwakilisha mawazo ya wote hata wale wasiokuwa wa
Chama chao au kundi lao.
Ndugu Wananchi;
Bahati
nzuri hii ndiyo sifa kubwa iliyooneshwa na Wajumbe wa Tume ya Mabadiliko ya
Katiba. Wamewasimamia na kuwasemea watu wote bila ya kubagua.
Natambua kuwepo kwa baadhi ya watu ambao hawafurahii msimamo huo na matokeo ya
kazi yao. Watu hao kuwalaumu Wajumbe wa Tume kwa ajili hiyo ni kuwaonea
na kutowatendea haki. Tunataka watakaokuwa Wajumbe wa Bunge Maalum nao
waige mfano huu mzuri. Wajali maslahi mapana ya taifa letu na watu wake
badala ya kujali yale ya taasisi zao au makundi yao.
Zanzibar
Kutokushirikishwa
Ndugu Wanachi;
Nimeambiwa
pia kuliwepo madai ya Zanzibar kutokushirikishwa ipasavyo. Nimeeleza kwa
kiasi gani Serikali ya Mapinduzi Zanzibar imeshirikishwa na kutoa maoni yake
yaliyojumuishwa katika Muswada. Hivyo basi napata tabu kuyaelewa madai
kwamba Serikali ya Mapinduzi Zanzibar haikushirikishwa msingi wake nini!
Labda kuna kitu sikuambiwa!
Nimeulizia
kuhusu hoja ya Kamati kutokufanya vikao Zanzibar kusikiliza maoni ya wadau wa
Zanzibar. Nimeambiwa kuwa Kanuni za Bunge hazina sharti hilo hivyo Kamati
haistahili kulaumiwa. Kama hivyo, nashauri kuwa suala hili lirudishwe
Bungeni ili Wabunge walizungumze na kulifanyia uamuzi muafaka. Vinginevyo watu
wataendelea kulauminiana isivyostahili. Hivyo basi, kuligeuza jambo hili
kuwa ni suala la kukataa Muswada au kususia vikao vya Bunge au kufanya
maandamano sidhani kama ni sawa.
Ndugu Wananchi;
Nimeambiwa
pia kuwa kulikuwa na hoja ya kutaka idadi ya Wajumbe wa kutoka Tanzania Bara na
Zanzibar iwe sawa kama ilivyo kwenye Tume ya Mabadiliko ya Katiba. Sababu
ya idadi ya Wajumbe wa Tume kuwa sawa inatokana na utaratibu wao wa kufikia
uamuzi. Ni kwa maelewano ya wote (consensus) na siyo kwa kupiga
kura. Ndiyo maana idadi imewekwa sawa ili sauti za pande zote zisikike
sawia. Bunge Maalum lina sharti la kufanya uamuzi kwa theluthi mbili ya
kura za kila upande kukubali. Bila ya hivyo hakuna uamuzi.
Hivyo
basi, katika Bunge Maalum nguvu si uwingi wa kura ambazo upande fulani unaweza
kupata bali ni ulinganifu sawa wa kura za kila upande peke yake. Huu
ndiyo msingi unaotumika katika Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania hivi
sasa kwa lengo la kulinda maslahi ya Zanzibar. Zanzibar ina Majimbo 50 ya uchaguzi na
Tanzania Bara ina Majimbo 189, hivyo ukiamua kwa wingi kila wakati
Wazanzibari watashindwa. Lakini, hapajakuwepo madai ya Zanzibar nao
kutaka kuwa na idadi sawa ya majimbo kama Bara au kupunguza majimbo ya Bara
yawe sawa na ya Zanzibar kwa sababu wingi si hoja. Msingi unaotumika ni kutoa
nguvu sawa za uamuzi kwa kila upande wa Muungano wakati wa kuamua masuala ya
Katiba. Hakuna mdogo wala mkubwa, wote wako sawa. Hakuna mdogo
kumezwa na mkubwa. Ndiyo msingi unaopendekezwa kutumika kwenye Bunge
Maalum hivyo hakuna kitakachoharibika kwa idadi ya Wajumbe
kutokukulingana. Nadhani inafaa ibaki ilivyo. Lakini kama Wabunge
wataamua waongeze idadi itakuwa kwa sababu nyingine siyo hii ya mfano wa Tume
ya Mabadiliko ya Katiba.
Ndugu Wananchi;
Katika orodha ya madai ya ndugu zetu wa upinzani lipo suala la uhai wa Tume ya
Katiba. Wanataka usiishe wanapokabidhi rasimu ya pili kwa Bunge Maalum
bali waendelee kuwepo mpaka mwisho wa mchakato. Nimeulizia
ilikuwaje? Nimeelezwa kuwa jambo hili halitokani na mapendekezo ya Serikali
wala ya Kamati ya Bunge ya Katiba, Sheria na Utawala. Limetokana na
pendekezo la Mbunge katika Bunge wakati wa kupitia vifungu na kuungwa mkono na
Wabunge wengi. Kwa hiyo kuilaumu Serikali si haki. Serikali inaweza
kuwa mshirika katika hoja hii.
Nami
naiona hoja ya Wajumbe wa Tume kuwa na wajibu wakati wa Bunge Maalum hasa wa
kusaidia kufafanua mapendekezo ya Tume. Je ushiriki huo uwe vipi? Je ni
Wajumbe wote au baadhi yao ni jambo linaloweza kujadiliwa.
Ndugu Wananchi;
Naomba
nimalizie kwa kuwasihi viongozi wa CHADEMA, CUF na NCCR-Mageuzi kuongozwa na
hekima iliyotumika wakati tulipokuwa na tatizo linalofana na hili kuhusu Sheria
ya Mabadiliko ya Katiba. Mimi naamini kama iliwezekana kufanikisha mambo wakati
ule inaweza kufanya hivyo hata safari hii. Itatufikisha pale tunapopataka
salama salimini bila maandamano, kushupaliana au uvunjifu wa amani.
Kupanga ni kuchagua, naomba sote, mmoja mmoja na kwa umoja wetu tuchague njia
ya mazungumzo na maelewano kwani itaihakikishia nchi yetu amani, usalama na
utulivu. Tukifanya hivyo historia itatuhukumu kwa wema.
Mungu
Ibariki Tanzania.
Nawashukuru
sana kwa kunisikiliza.
chanzo na jamii http://www.fikrapevu.com
0 Weka maoni yako hapa:
Post a Comment
COMMENT HAPA