Oct 6, 2013

MAREKANI YAISHAMBULIA AL SHABAB, YAMKAMATA KIONGOZI WA AL QAIDA LIBYA



Kundi la askari wa Jeshi la Majini la Marekani limefanya shambulizi katika pwani ya mji wa kusini mwa Somalia dhidi ya wapiganaji wa Al Shabab jana.

Shambulizi hilo limelenga kamanda wa ngazi za juu wa wanamgambo wa kundi hilo la Al Shabab aliyetajwa kwa jina la Abu Siyad katika mji wa Baraawe. Afisa mmoja wa jeshi la Marekani amesema kundi hilo la wanamaji wa Marekani halikufanikiwa katika shambulizi hilo.

Maafisa wa Marekani wamesema kuwa shambulizi hilo lilipangwa wiki moja na nusu iliyopita na kwamba lilichochewa na hujuma iliyofanywa na wanamgambo wa Al Shabab dhidi ya jengo lenye maduka la Wastgate jijini Nairobi mwezi uliopita.

Msemaji wa kundi la al Shabab Abdulaziz Abu Musab amesema makomando wa kigeni wamevamia pwani ya mji wa Baraawe kwa kutumia boti mbili za kasi kubwa na kwamba hawakufanikiwa kufikia malengo yao. Amesema askari wa Marekani walilazimika kukimbia baada ya kukabiliwa na mashambulizi makali ya al Shabab.


Habari zinasema mji huo  unaolindwa na wapiganaji wa al-Shabaab ulishambuliwa kutoka baharini katika mapambano yaliyodumu zaidi ya saa moja. Radio ya Mogadishu imesema shambulizi hilo lilitekelezwa jana usiku kwa ndege za kigeni. 

Mji wa Barawe ambao uko kilomita 250 kusini mwa mji wa Mogadishu, umekuwa ukidhibitiwa na wapiganaji wa al-Shabaab kwa miaka kadhaa na umekuwa ukishuhudia mashambulizi ya mara kwa mara kutoka kwa vikosi vya kigeni.

Marekani imepanga kufanya mashambulizi katika pwani ya Afrika mashariki na Libya kwa madai ya kuwatafuta vinara wa ugaidi.Wakati huo huo taarifa zinasema shambulizi la Libya wamefanikiwa kumkamata kiongozi wa Al qaida nchini humo Abu Anas al Liby (أبو أنس الليبي) ambaye alikuwa akitafutwa kwa muda mrefu kwa tuhuma za kuhusika na ulipuaji wa mabomu mwaka 1998 katika nchi za Tanzania na Kenya ambapo watu 224 walikufa.

Marekani iliweka zawadi ya dola milioni 5 kwa mtu yeyote atakayetoa taarifa za kukamatwa kwake.

                   
chanzo na  http://ahbaabur.blogspot.com  

0 Weka maoni yako hapa:

Post a Comment

COMMENT HAPA