Oct 29, 2013

MAALIM SEIF:CUF HATUNA IMANI NA MWENYEKITI WA TUME YA UCHAGUZI

Katibu Mkuu wa CUF Maalim Seif Sharif Hamad akihutubia mkutano wa hadhara katika viwanja vya Pwepweu jimbo la Tumbe Katibu Mkuu wa CUF Maalim Seif Sharif Hamad akihutubia mkutano wa hadhara katika viwanja vya Pwepweu jimbo la Tumbe

Chama Cha Wananchi (CUF) kimeanza kumtilia shaka Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC) Bw. Jecha Salim Jecha na kudai kuwa hana sifa za kuwa Mwenyekiti wa Tume hiyo.

Akizungumza na wanachama na wapenzi wa Chama hicho katika mkutano wa hadhara uliofanyika viwanja vya Pwepweu Tumbe, Katibu Mkuu Maalim Seif Sharif Hamad amesema Jecha ni mkereketwa wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), na kwamba kwa mazingira hayo hatoweza kutenda haki katika uchaguzi.

Akielezea zaidi kuhusu madai hayo Maalim Seif amedai kuwa katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2010, Jecha aliingia katika mchakato wa kugombania nafasi ya Ubunge katika Jimbo la Kwamtipura kupitia CCM, lakini hakuweza kupata nafasi baada ya kushindwa katika mbio za kugombea nafasi hiyo.

Maalim Seif ambaye pia ni Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar ameibua hoja hiyo baada ya kuwepo taarifa kuwa takwimu za wapiga kura wapya katika majimbo matano ya Unguja zimepotea kwenye Komputa, na kudai kuwa huo ni mkakati maalum ulioandaliwa na Chama Cha Mapinduzi kwa kushirikiana na Tume ya Uchaguzi Zanzibar.

Ameyataja majimbo yanayodaiwa kupoteza Takwimu zake za wapiga kura wapya kuwa ni Bumbwini, Donge, Kitope, Bububu na Mfenesini.

Maalim Seif ameenda mbali zaidi kwa kumtaka Mwenyekiti huyo ajiuzulu wadhifa huo na kama akishindwa basi Rais wa Zanzibar achukue jukumu la kumfuta kazi.

“Kwa kweli Mwenyekiti huyu hana sifa kabisa za kuwa Mwenyekiti wa ZEC kwa sababu ni mkereketwa wa CCM aliyegombea nafasi ya Ubunge katika uchaguzi mkuu wa 2010, hawezi kabisa kutenda haki katika uchaguzi”, alisema Maalim Seif na kuongeza

“Kwa hivyo namuomba sana Mwenyekiti huyu ajiuzulu, na kama akishindwa basi kwa heshima zote namuomba Rais Dokta Shein amuwajibishe kwa kumfuta kazi”, alisisitiza.

Katika hatua nyengine Maalim Seif amempongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Rais Jakaya Mrisho Kikwete kwa moyo wake wa kusimamia vyema mchakato wa mabadiliko ya katiba ya Tanzania.
Amesema kitendo cha kukubali kukutana na viongozi wa vyama vya upinzani ni hatua muhimu katika kuendeleza mchakato huo ambao ulionekana kuanza kuzorota baada ya vyama vya upinzani kuukataa muswada wa marekebisho ya sheria ya mabadiliko ya katiba.

Amewasisitiza wananchi wa Zanzibar kuacha tofauti zao katika kipindi hiki cha mchakato wa mabadiliko ya katiba, na badala yake washirikiane katika kupata katiba iliyo bora, yenye maslahi kwa Zanzibar na vizazi vijavyo.

Mapema akizungumza katika mkutano huo, Mwakilishi wa Tumbe Mhe. Rufai Said Rufai amesema atashirikiana na viongozi wengine wa Jimbo hilo pamoja na wa Wilaya ya Micheweni kuhakikisha kuwa vijana wote waliotimiza umri wa miaka 18 katika jimbo hilo wanapata vitambulisho vya Mzanzibari Mkaazi (ZAN ID).

Katika Mkutano huo Maalim Seif alikabidhi kadi 1536 kwa wanachama wapya waliojiunga na chama hicho wote wakitokea jimbo la Tumbe, ambapo miongoni mwao wametoka Chama Cha Mapinduzi.

 Wanachama wapya wa CUF katika Jimbo la Tumbe wakionyesha kadi zao baada ya kukabidhiwa na Katibu Mkuu wa Chama hicho Maalim Seif Sharif Hamad. Wanachama wapya wa CUF katika Jimbo la Tumbe wakionyesha kadi zao baada ya kukabidhiwa na Katibu Mkuu wa Chama hicho Maalim Seif Sharif Hamad.

0 Weka maoni yako hapa:

Post a Comment

COMMENT HAPA