Feb 18, 2014

MKWASA AWAFUATA AL AHLY CAIRO

 


Msaidizi wa timu ya Young Africans Charles Boniface Mkwasa mchana huu anaondoka kuelekea jijini Cairo nchini Misri kwenda kushuhudia mchezo wa Fainali ya (Super Cup) Mshindi wa Klabu Bingwa Afrika timu ya Al Ahly ya Misri dhidi ya Mabingwa wa Kombe la Washindi Afrika timu ya CS Sfaxien ya Tunisia mchezo utakaofanyika siku ya Alhamis katika dimba la Cairo International Stadium.                                       

Mkwasa anandoka kwa usafiri wa Shirika la Ndege la Ethiopia Airline ambapo atapitia jijini Adis Ababa kabla ya kuunganisha kuelekea Cairo ambapo atatua Uwanja wa Ndege majira ya saa 7 usiku na kupokelewa na wenyeji kutoka ofisi za Ubalozi wa Tanzania nchini Misri.

Kutokana na umuhimu wa mchezo huo Uongozi wa Young Africans kwa pamoja na Benchi la Ufundi walikaa na kukubaliana kuwa kocha msaidizi Mkwasa aende kushuhudia mchezo huo wa fainali ambao utaweza kusaidia kupata picha ya wapinzani Al Ahly ambao watacheza na Young Africans mwishoni mwa mwezi huu.

Lengo la safari ni kuweza kuwaona Al Ahly wanavyocheza katika mchezo huo wa fainali, pili ni kujua wanayocheza wakiwa katika uwanja wao wa nyumbani na tatu ni kuijua timu nzima kiufundi inachezaje.
Kwa upande wake Kocha Mkwasa amesema anaamini ataitumia vizuri nafasi hiyo ya kuutazama mchezo wa Super Cup kwa kuwasoma wapinzani na pindi atakaporejea atasaidiana na kocha mkuu kuwaandaa vijana tayari kwa mchezo huo.

Mkwasa mara baada ya kuutazama mchezo huo dhidi ya CS SFaxien siku ya Alhamis jioni saa 11 kamili kwa saa za Afrika Mashariki atarejea nchini siku ya ijumaa n akuungana na kikosi kwa ajili ya mchezo wa siku ya jumamosi dhidi ya timu ya Ruvu Shooting. 

Al Ahly Mabingwa watetezi wa klabu Bingwa Barani Afrika watacheza na Young Africans Tarehe 1 Machi 2014 katika mchezo wa kwanza wa kuwania kuingia katika 16 bora kisha kurudiana jijini Cairo wiki moja baadae.

0 Weka maoni yako hapa:

Post a Comment

COMMENT HAPA