Apr 25, 2012

UKATILI WA JESHI LA POLISI DHIDI YA WANANCHI WA TANDAHIMBA


Baada ya maandamano ya amani ya wakulima wa korosho wa wilaya ya Tandahimba yaliyofanyika tarehe 11/04/2012 ambapo mkuu wa wilaya aliwajibu wakulima majibu yanayokatisha tamaa, yasiyo na chembe ya uongozi wala kutatua mustakabali wa madai yao; wakulima na baadhi ya wananchi waliweka magogo barabarani kama njia ya kupaza sauti yao. Katika mazingira hayo jeshi la polisi liliongeza vikosi vyake Tandahimba kwa hoja ya kulinda amani na kudhibiti hali ya mambo.

Badala ya kulinda amani na kuzuia vitendo vya uvunjifu wa amani- polisi waliishia kuanza kufanya ujambazi uliopindukia.

Mnamo tarehe 17/04/2012 majira ya saa 2 usiku ofisi ya OCD wa Tandahimba ambayo iko karibu na soko kuu na maduka ya mjini Tandahimba ilianza kuungua moto.

Walinzi wa soko na wananchi wote wananshuhudia kuwa wakati ofisi hiyo inaanza kushika moto waliokuwepo ndani na nje ya ofisi hiyo ni mapolisi wenyewe. Wananchi na watu wenye maduka walianza kusogea wakibeba maji na mchanga ili kuzima moto huo, walianza kuambulia kipigo cha kinyama. Polisi waliokuwepo katika ofisi hiyo na wale wa vikosi vingine walijazana na kuwapiga wananchi wakiwazuia wasizime moto huo.


Wananchi wa Tandahimba na hasa wafanya biashara wa eneo la sokoni wanaamini kwamba polisi walikuwa wanafahamu fika nini kimetokea, na bila kutia shaka walipanga mpango wa uchomaji wa ofisi ya OCD kwa maelekezo maalum ya kutengeneza mazingira ya uanzishwaji wa jambo Fulani. Hii ni kwa sababu baada ya kuungu ofisi ya OCD, hakuna hata majivu yaliyobakia kuonesha kuwa palikuwa na makaratasi n.k. Hali hiyo inapelekea wafanya biashara wa eneo hili kuamini kuwa vifaa vyote muhimu katika ofisi ya OCD viliondolewa kabla ya tukio hilo.


Baada ya tukio hilo polisi waliongezeka kwa wingi sana wakivalia sare rasmi na nguo za kawaida za askari kanzu. Walianza kupiga risasi za moto hovyo na mabomu ya machozi, walivamia maduka kadhaa ya bidhaa na simu na kuanza kupora huku magari ya polisi yakipakia bidhaa zilizoporwa na fedha na kuelekea njia ya Mtwara mjini au Newala.


Wakati uporaji unaendelea raia wote waliojitokeza kwenda kuzima moto walipigwa na kuumizwa sana(kwa ushahidi) na kufukuzwa kwa nguvu, wenye maduka iliwapasa kukimbia ili kuokoa maisha yao na wale wenye ujasiri walipojaribu kurudi walipigwa na kuumizwa mno.


Kwa ushahidi wa wananchi, polisi walivamia duka la kijana mmoja anayeuza mafuta ya taa, dizeli na petrol, walianza kuchukua mafuta waziwazi na kumwagia maduka kadhaa kwa kuchagua. Walimwagia duka hili na kuacha lile ilimradi walijua wanachofanya. Hapa inaonesha kuwa walielekezwa nini cha kufanya – jambo la ajabu sana ni kuwa maduka mengi kati ya yaliyomwagiwa mafuta na kuchomwa moto ni ya wafuasi wa Chama Cha Wananchi CUF ambacho kiliporwa ushindi jimboni humo katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2010. Maduka machache mno, kama 10% yalikuwa ya wafuasi wa CCM ambao walimuunga mkono mgombea wa CUF bwana KATANI. A. KATANI katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2010.


Katika kutoa ushahidi, polisi wanasema ofisi ya OCD ilichomwa na wananchi. Tunaweza kujiuliza maswali kama wananchi ndio waliichoma, kwa nini walipojitokeza kuzima moto ambao bado ulikuwa kidogo polisi walikuwa wanawapiga na kuwafukuza huku polisi ambao walikuwa wengi hawakufanya juhudi zozote za kuuzima moto huo? Kwa nini polisi walitazama ofisi ya OCD inaungua? Kuna nini kinafichwa hapa?


Baada ya uporaji ambao ulifanyika kwa wazi, bahati nzuri wafanyabiashara waliokuwa madukani waliwatambua baadhi ya askari wa Tandahimba ambao walikuwa pamoja na vikosi vya askari wengine katika uporaji huo na hata kamishna wa polisi PAUL CHAGONJA alipotumwa na IGP kwenda Tandahimba ameambiwa waziwazi ni askari gani walishiriki tena kwa majina na hasa ameelezwa walishiriki namna gani – wananchi wa Tandahimba wana kila namna ya ushahidi.


Maduka yalipoanza kuchomwa ndipo wananchi walishuhudia ukatili mkubwa. Wafanyabiashara walianza kuwapigia simu polisi wanaowafahamu, OCS, OCCID na OCD wakiomba wasaidiwe mali zao zisiungue lakini baadhi yao walijibiwa kuwa hali ile ni tete na kuwa polisi walitapaa kila eneo hivyo ni vigumu wao kupewa msaada wa kuokoa mali zao.


Kuna baadhi ya wafanyabiashara ambao waliruhusiwa aidha na OCCID au OCD wakaokoa mali zao lakini waliingizwa katika maeneo ya maduka yao chini ya ulinzi mkali wa polisi. Mmoja wa wafanyabiashara alipewa sharti na OCD kuwa atoe bidhaa zake alizookoa na kuzipeleka kwingineko na kwamba kukicha ziwe hazipo eneo la tukio. Mfanyabiashara huyo alifanikiwa kupata gari usiku huo na aliokoa asilimia tisini ya bidhaa zake.


Wakati uchomaji wa maduka unaendelea polisi pia walichoma gari moja aina ya ESCUDO lenye namba T323ADK huku mmiliki wake, Abdallah Abdallah akitazama kwa macho yake gari likimwagiwa petrol na kutiwa moto. Kabla hawajalichoma yeye alikuwa anaendesha kutoka nyumbani kwake kwenda kwenye duka lake sokoni baada ya kupata taarifa duka lake linaungua moto. Ghafla polisi walimsimamisha kwa ghadhabu na kumuamrisha azimishe taa.


Kati ya polisi waliomsimamisha anawatambua wawili, Afande Richard na Afande Venus. Alipotii amri yao na kusimama aliamrishwa kushuka ndani ya gari, wakati anajiandaa kushuka polisi walipiga risasi ambazo zilipasua tairi la nyuma la gari husika. Askari mwingine alivunja kioo cha gari kwa kukipiga na upanga. Alipoona hivyo alishuka na kukimbia na ndipo gari yake ikachomwa akiwa anatazama umbali wa mita 50-100 hivi. Duka lake la vyombo vya ndani limechomwa moto.


Kijana mwingine, Hamis Madisa, naye akiendesha pikipiki yake(namba hazikupatikana) alisimamishwa kwa mtindo huohuo. Bahati nzuri akamtambua askari mmoja anayeitwa Saleh kati ya waliomsimamisha na akamuomba amsaidie ili asidhuriwe na askari wenzie. 
 
Badala ya kumsaidia mwendesha pikipiki, askari yule alimjibu kuwa hali ni mbaya sana na kwamba akimbie haraka na aache pikipiki ili kuokoa maisha yake. Wakati anajiandaa kukimbia alipigwa sana, keshoye aliamini ataikuta pikipiki yake imetunzwa na askari anayemfahamu! Aliikuta pikipiki yake imechomwa moto. Anaamini polisi waliichoma moto japokuwa yeye hakushuhudia, kwani aliiacha chini ya ulinzi wao.

Unaweza kujiuliza inakuwaje ukatili mkubwa namna hii unafanyika, maduka yanaungua kutokea saa 3 usiku hadi alfajiri, yanaungua duka mojamoja huku polisi wanatazama na wanawafukuza wenye maduka wasiokoe chochote?


Kwa vyovyote vile huu ni ukatili mkubwa sana na usiomithilika ambao unafanywa na vyombo vya dola ili kuwanyamazisha wananchi wanaodai haki zao na hasa kwa kutumwa kulipiza visasi vya kisiasa, wananchi wa Tandahimba wameathiriwa sana, wamefanyiwa ukatili mkubwa na hili halivumiliki.


Bila shaka yoyote, polisi walisimamia zoezi hili la uchomaji kwa maelekezo maalum na kuna ushahidi wa kutosha wa picha za matukio haya,sauti zilizorekodiwa na video za ushahidi wa wananchi walioporwa, waliopigwa risasi na ambao maduka yao yalichomwa pamoja na wale walioshuhudia kila aina ya matukio. Kamishna Paul Chagonja ameelezwa yote haya.


Zaidi ya maduka 55 yameteketezwa katika oparesheni hii ya polisi. Gari moja na pikipiki moja vimeteketezwa. Polisi walifanikiwa pia kuwakamata vijana zaidi ya 50 na kuanza mpango wa kuwabambikizia kesi za uporaji, wizi n.k. Baadhi ya vijana hawa huenda watafikishwa mahakamani na kubambikiziwa masuala ambayo yalifanywa na polisi.


Katika hali ya kushangaza, baada ya mimi na msafara wangu kuondoka Tandahimba na kujionea hali halisi ikiwa ni pamoja na kukusanya ushahidi na vielelezo mbalimbali vya ukatili wa jeshi la polisi, tulipanga kushiriki mkutano wa hadhara Mtwara mjini kuwajulisha wananchi juu ya madhila yanayowakumba wakulima wa Tanzania hususani wakulima wa korosho wa mikoa ya kusini pamoja na malipo ya kipigo na ukatili wanayolipwa na serikali ya Chama Cha Mapinduzi.


Mkutano wetu uliandaliwa ipasavyo na polisi walijulishwa kwa barua siku ya tarehe 20/04/2012 na walijulishwa kuwa mkutano ungefanyika siku mbili baadaye, yaani tarehe 22/04/2012. Viongozi wa Mtwara mjini walifanya matangazo kwa gharama kubwa yakiwemo matangazo ya redio na umma wa Mtwara mjini ulikuwa tayari kusikiliza Chama cha Wananchi CUF kingekuja na maelekezo gani juu ya manyanyaso wanayopewa wakulima ambao wanadai haki zao.


Polisi walitumia mbinu zilezile za hujuma za wazi na kuzuia mkutano wetu. Sababu ya kuzuia mkutano ni kuwa eti hali ya usalama mkoani Mtwara ni mbaya sana. Unaweza kujiuliza kama hali ya Usalama ni mbaya Tandahimba, kwa nini polisi wanazuia shughuli za kisiasa kwa chama chetu Mtwara mjini? Ukweli unabakia kuwa POLISI na SERIKALI waliogopa tusiwajulishe watu wa Mtwara Mjini na watu wa mikoa ya kusini na Watanzania kwa ujumla namna haki zao zinavyoporwa kwa mtutu wa bunduki. Polisi waliogopa tusiwaeleze wananchi ukweli na dunia ifahamu kuwa Tanzania ya leo ina jeshi la polisi ambalo linafanya ukatili mkubwa kuliko jeshi la polisi la wakoloni.


MASWALI YA KUJIULIZA;

 
A.JUU YA CHANZO CHA MOTO NA KUUNGUA OFISI YA OCD. 
1. Kama wananchi ndio walichoma moto ofisi ya OCD askari waliokuwa wakilinda ofisi hiyo walikuwa wapi?
 
2. Kama wananchi ndio waliochoma ofisi ya OCD kwa nini wananchi hao hao ndio walikuwa mstari wa mbele kutafuta maji na mchanga kuzima moto huo kabla haujawa mkubwa?
 
3. Kwa nini polisi wawazuie kwa nguvu wananchi wasije kuzima moto huo? 
4. Kwa nini polisi wasiuzime moto unaounguza ofisi ya OCD wakati wakikataa wananchi wasiuzime? 
5. Kwa nini polisi wanaangalia ofisi ya OCD ikiungua bila kuchukua hatua yoyote?

 
B. CHANZO CHA MOTO NA KUUNGUA MADUKA ZAIDI YA 55
 
1. Kama polisi wanajenga hoja kuwa moto uliounguza ofisi ya OCD ndio ulisambaa na kuunguza maduka, vibanda vyote, soko, gari lililokuwa mbali na na soko na pikipiki iliyokuwa mbali na soko; kwa nini moto huo umeunguza maduka kwa kurukaruka? Kwa nini moto uunguze duka “A” na kurukia duka “C” na kisha kwenda duka “F”? 
2. Je moto huu ulikuwa na maelekezo maalum ya namna ya kuunguza? 
3. Kwa nini moto huu unaunguza maduka ya wafanyabiashara na kuyaacha maduka ya makada nguli wa CCM na kuacha duka la OCS wa Tandahimba? 
4. Kwa nini polisi wanawaruhusu baadhi ya makada wa CCM kuingia sokoni kuokoa mali za maduka yao wakati soko linateketea na wakati huohuo polisi haohao wanawazuia wafanyabiashara wengi wasiokoe mali zao?
 
5. Kama Polisi walikwenda Tandahimba kulinda amani kwa nini wabomoe maduka na kupora waziwazi huku wengine wakifahamika kwa majina na kwa sura na tena wengine wakiwaongelesha wenye maduka na kuwaomba wakimbie ati kwa sababu hali ni mbaya na kuwa wao(mapolisi hao wenyeji) hawana msaada kwa muda huo. 
6. Kwa nini OCS,OCCID na OCD wa Tandahimba wanapigiwa simu na wafanyabiashara kuombwa msaada wa kuokoa maduka yao yanayoteketea sokoni lakini wao wanajibu kuwa hali ni tete na wanawaambia wafanyabiashara ati “hali ni mbaya” na kuwa masuala ya operesheni hiyo ya choma maduka na piga watu “haiko chini ya uwezo wa OCD”? 
7. Kama OCD alifahamu maduka yanaungua kwa zaidi ya saa 7 na watu wakipigwa na risasi zikilia kila kona ya Tandahimba, yeye kama mkuu wa ulinzi kwa upande wa polisi kwa ngazi ya wilaya alichukua hatua gani? Na je anamjua kiongozi wa polisi aliyeamrisha ukatili huo ufanyike?
Kwa kweli kuna maswalimengi sana ya kujiuliza!!!

C.MSIMAMO WA CHAMA.

 
1. Serikali haitakwepa kuwajibika kwa hasara zilizojitokeza na watu walioumizwa katika tukio hilo. 
2. Serikali iwalipe wafanyabiashara wote kwa mali walizopoteza na majengo yaliyoharibiwa. 
3. Serikali iwalipe fidia watu wote walioumizwa kwa risasi au vipigo vya polisi katika operesheni hiyo ya kikatili ya polisi dhidi ya wananchi. 
4. Serikali iwafute kazi na iwafikishe mahakamani viongozi wote wa polisi na askari waliohusika na matukio hayo. 
5. Serikali imfukuze kazi mkuu wa wilaya ya Tandahimba ambaye ndiye mwenyekiti wa kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya kwa kushindwa kuongoza na kuwaeleza wananchi wa Tandahimba namna serikali inavyoshughulikia tatizo la malipo yao ya pili ya korosho. 
6. Vitendo walivyofanya polisi Tandahimba vinajenga uhasama mkubwa kati ya raia na jeshi la polisi. Serikali iunde tume huru maalum ya uchunguzi na ambayo haitawahusisha polisi ili ikafanye uchunguzi wa kina na wa wazi na kisha tume hiyo itangaze hadharani mambo iliyoyabaini na kuishauri serikali hatua za kuchukua ili kuondoa uwezekano wa vitendo hivyo vya kimakusudi na kikatili kujirudia mahali pengine ndani ya Tanzania. 
7. Tume ya Haki za binadamu ifanye uchunguzi wake kubaini uvunjifu wa haki za binadamu Tandahimba na kuwawajibisha wahusika na kupendekeza hatua za kuchukua hali hiyo isirudiwe Tandahimba na kokote Tanzania. 
8. Asasi za kiraia za haki za binadam na Msaada wa Kisheria wawape msaada wa kisheria wahanga na waathirika wa Tandahimba waweze kudai haki zao. 
9. Mtoto Wa Mtambokulima wapewe haki na uhuru wa kiuchumi wa kuuza korosho zao na mazao mengine kwa yeyote atakayewapa bei nzuri. Serikali iweke mazingira ya wafanya biashara kushindana kwa kuwapa bei nzuri wakulima wa korosho na mazao mengine.

 
Imetolewa;
Prof. Ibrahim Haruna Lipumba
Mwenyekiti wa CUF Taifa
24 Aprili 2012

0 Weka maoni yako hapa:

Post a Comment

COMMENT HAPA