Jun 9, 2012

Yanga waipiga Simba bao la tatu




MICHAEL MOMBURI
USAJILI wa Ligi Kuu ndio kwanza umeanza kunoga lakini matajiri wa Yanga wameshaipiga Simba mabao matatu ya haraka haraka na yamebaki mawili tu kuchomoa kipigo cha mabao 5-0 ilichokipata uwanjani kwenye mechi ya Ligi Kuu Bara msimu uliopita.

Bao la kwanza ambalo Yanga walilifunga ni usajili wa kiungo Nizar Khalfan. Simba ilitangaza kumsajili mchezaji huyo, lakini Yanga ikafanya umafia ikamuwekea noti mezani akamwaga wino na kumtaka rasmi kwamba yeye ni mali ya Yanga. Hilo likapita kila mtu akauchuna.

Kama masihara, Mwanaspoti ikafichua kwa mara ya kwanza kuwa beki Kelvin Yondani amesaini Yanga na Simba.

Simba walikanusha habari hizo kwa nguvu zote, lakini Yanga wakatoa uthibitisho wa picha na maandishi bado Simba wakasisitiza wana mkataba naye. Yondani akaibuka Alhamisi usiku na kutamka kwa mdomo wake; "Nimesaini Yanga na naomba ushirikiano wa kila hali, naishukuru Simba kwa kunifikisha hapo nilipo nawataki kila la kheri."

Kabla hilo halijapoa hapa kuna jingine kali ambalo ni bao la tatu. Yanga imethibitisha kumsajili kipa wa Simba, Ally Mustapha 'Barthez' kwa thamani ya Sh 18 milioni lengo ikiwa ni kuikimbia nafasi yake maalum aliyowekea kwenye benchi la Simba kuanzia dakika ya kwanza mpaka ya mwisho wa mechi zote kila msimu.

Habari za kuaminika ambazo Mwanaspoti inazo ni kwamba Barthez alisainishwa na Seif Ahmed 'Magari' sambamba na Abdallah Bin Kleb ambaye anagombea nafasi ya ujumbe kwenye uchaguzi ujao wa Yanga. Matajiri hao wawili ndio wanaoongoza jopo la vibosile wengine wanaowezesha usajili wa Yanga kwa ajili ya msimu ujao.

"Barthez ameshasaini kila kitu wiki hii na fedha zake amechukua, ni kipa mzuri sana na atacheza sana akiwa na Yanga.

Tutakachofanya tutawapa Mtibwa Shabaan Kado na wao watupe mchezaji mmoja wa ndani kwavile Kado bado tuna mkataba naye,"mmoja wa viongozi wa usajili aliithibitishia Mwanaspoti.

"Tutabaki na Barthez na Said Mohammed, suala la Yaw Berko bado halijafikiwa muafaka wa moja kwa moja bado tunajadiliana lakini muda mfupi ujao kila kitu kitakuwa wazi, Berko tatizo lake la majeruhi ya mara kwa mara ndio inatupa wasiwasi,"aliongeza kiongozi huyo aliyekiri kwamba wamemkosa kiraka wa Uganda, Owen Kasule aliyesajiliwa El Merreikh.

"Tupo kwenye mazungumzo na Danny Mrwanda na Mussa Mgosi lakini kama tukifanikisha kumalizana na Mrwanda kwa wakati hatutamsajili Mgosi,"kilisema chanzo chetu.

Mwanaspoti linajua kwamba Bin Kleb aliyewezesha na kumsajili Haruna Niyonzima 'Fabregas' msimu uliopita, amepania kushusha wachezaji kadhaa wenye majina makubwa Yanga na jana Ijumaa jioni kulikuwa na kikao kizito jijini Dar es Salaam kukamilisha suala hilo.

Wachezaji wengine waliothibitishwa kusaini Yanga ni beki Juma Abdul wa Mtibwa, Barthez na Kelvin Yondani wote Simba, Nizar Khalfan(huru) na David Luhende wa Kagera.

Wachezaji walioko kwenye orodha ya kuachwa Yanga ni Shadrack Nsajigwa, Kiggi Makassi, Godfrey Bonny, Abuu na Zubeir Ubwa, Bakar Mbegu, Chacha Marwa, Davies Mwape wa Zambia na Kenneth Asamoah wa Ghana.

chanzo na mwanaspoti

0 Weka maoni yako hapa:

Post a Comment

COMMENT HAPA