ALICHOFANYIWA MKURUGENZI WA CUF MH.MKETO HUKO MTWARA
ALICHOFANYIWA MKURUGENZI WA CUF MH.MKETO HUKO MTWARA..huu ni zaidi ys Unyama.
MATESO NA UKATILI MKUBWA ALIOFANYIWA NAIBU MKURUGENZI WA OGANAIZESHENI
UCHAGUZI NA BUNGE WA CUF TAIFA MHE. SHAWEJI MKETO NA VIONGOZI WENGINE WA
CUF MKOANI MTWARA.
A. Muhtasari
Jeshi la Wananchi wa Tanzania
katika kambi yao ya Naliendele yamewafanyia mateso makubwa viongozi wa
CUF akiwemo Mheshimiwa Shaweji Mketo, Naibu Mkurugenzi wa Oganaizeshani,
Uchaguzi na Bunge ambaye alipigwa mpaka akazimia na kuchomwa sindano na
kemuwekea drip 3 kabla hajazinduka saa 10 alfajiri. Rais Kikwete
asitishe mara moja vitendo vya uvunjaji wa haki za binadamu unaofanywa
na askari Mkoani Mtwara. Taarifa ninayoitoa inatokana na maelezo na
utafiti uliofanywa na Naibu Katibu Mkuu, Julius Mtatiro niliyemtuma
kwenda Mtwara kufuatilia kukamatwa kwa Mketo na wenzake.
B. Shughuli halisi alizofanya Mhe. Mketo alipofika Mtwara Mjini;
Jumatano tarehe 26 Juni 2013 Mkurugenzi wetu wa Oganaizesheni Uchaguzi
na Bunge Mhe. Shaweji Mketo alitumwa na Chama chetu kuhudhuria kesi
inayowakabili viongozi mbalimbali wa CUF katika mahakama ya Mtwara Mjini
(Kesi inayomkabili MHE.KATANI AHMAD KATANI na wenzake).
Mhe. Mketo
alipotoka mahakamani alifanya kikao na wanachama wa CUF Mtwara mjini
ambao walimueleza unyanyasaji na ukatili mkubwa ambao wanajeshi na
polisi wanawafanyia wananchi wa Mtwara. Palitolewa taarifai ya mwanamke
mmoja aliyenajisiwa na ambaye aliripoti tukio husika katika kituo cha
polisi cha Msimbati kilichoko Mtwara na alipeleka polisi hadi ushahidi
wa mipira ya kiume iliyotumika kumfanyia unyama huo lakini polisi
hawakuchukua hatua yoyote hadi leo.
Mhe. Mketo na viongozi wengine
waandamizi watano walielekea maeneo ya kijiji cha Msimbati ambako
mwanamke huyo amesitiriwa baada ya unyama huo. Mzazi wa binti aliyebakwa
anajulikana kwa jina la SELEMANI BIN OMARI. Mhe. Mketo na viongozi
aliokuwa nao walifika kijiji cha Msimbati na kukutana na mwanamke
aliyebakwa mbele ya familia yake, waliongea naye kwa kina na mwanamke
huyo alieleza kila kilichojiri;
C. Maelezo ya mwanamke aliyebakwa yaliyotolewa na mwanamke husika mbele Mkurugenzi Mketo tarehe 27 Juni 2013;
Siku ya tukio mwanamama huyo ambaye ameeleza ana umri wa zaidi ya miaka
40 lakini kimaumbile anaonekana kama ana miaka 20 - 25 alikuwa anawasha
moto nyuma ya nyumba yao huku mama yake mzazi akisuka mkeka sehemu ya
mbele ya nyumba yao. Ghafla akaona wanajeshi watatu wameingia nyumbani
kwao. Mwanajeshi mmoja akamuuliza anawasha moto wa nini, akawajibu
anataka kupika. Yule mwanajeshi akamwambia “twende kwanza ndani” na
akamshika na kumvutia ndani. Askari Yule akamuingiza katika mojawapo ya
vyumba na kumrusha kitandani kwa nguvu.
Wale askari wengine wawili,
mmoja akalinda upande aliokuwepo mama yake mzazi akisuka mkeka na
mwingine akalinda mlango wa upande ambako mwanamke huyu alikuwa anawasha
moto. Mule chumbani, askari Yule alimlazimisha kufanya mapenzi na
juhudi zake za kupinga hazikusaidia kwani alitishiwa kuwa akipiga kelele
atapigwa sana. Askari Yule alisisitiza kuwa baada ya kumridhisha atampa
shilingi elfu tatu 3,000/-. Kwa sababu ya kumzidia nguvu na kumtishia
kumuua, askari husika alifanikiwa kutoa pakiti ya mpira wa kiume na
kuuvaa na kumuingilia kwa nguvu. Baada ya kitendo kile askari Yule
alivaa nguo akaungana na wenzie waliokuwa wakilinda milango yote miwili
wakaondoka huku mbakaji akiacha pakiti ya mipira ya kiume ene la tukio.
Baadaye familia ya mwanamke huyu ilitoa taarifa kwa mwenyekiti wa
Kitongoji chao anayetokana na Chama Cha Wananchi CUF na mwenyekiti
akawataka waende wakaripoti polisi. Waliripoti kituo cha Polisi Msimbati
wakapewa nyaraka ili waelekee hospitali. Walipokwenda hospitali,
daktari alifanya vipimo na kuwajulisha polisi na ndugu kuwa mwanamama
Yule amebakwa na kwamba kuna michubuko ya wazi katika sehemu zake. Baada
ya ripoti hiyo kutolewa, polisi waliichukua na hadi leo haijulikani iko
wapi.
D. Kutishiwa familia ya mwanamke aliyebakwa, kutekwa na kuteswa kwa daktari aliyempima na kuthibisha kitendo alichofanyiwa;
Mwanamke husika na familia yake wameendelea kutishiwa sana na askari
jeshi. Mwenyekiti wa Kitongoji wa CUF amehojiwa mara kadhaa na wanajeshi
na daktari aliyefanya uchunguzi ule alivamiwa nyumbani kwake na
wanajeshi usiku wa kuamkia tarehe 27 Juni 2013 akakamatwa na kupelekwa
kwenye kambi ya jeshi ya Naliendele na kuteswa hadi majira ya alfajiri.
Alikuwa anateswa ili asijihusishe tena na namna yoyote ya kutoa ushahidi
kwa mtu yeyote kuhusu uthibitisho wa tukio la ubakaji uliofanywa na
askari wa jeshi.
E. Safari ya Mhe. Mketo na Viongozi waandamizi kutoka Msimbati kurudi Mtwara Mjini na kutekwa na wanajeshi kulivyotokea;
Kati ya saa 11.30 – 12.00 jioni walifika eneo la kilometa tatu kabla ya
kuingia mjini (Eneo la njia pacha). Magari mawili ya kijeshi moja
likiwa aina ya TATA na lingine likiwa DEFENDER ya jeshi yaliziba
barabara. Ilibidi gari ya mhe. Mketo iliyokuwa ikipeperusha bendera ya
chama chetu isimame (Gari hii ni aina ya NISSAN PATROL yenye namba T 866
BGW – Mali ya Chama Cha Wananchi CUF). Askari jeshi zaidi ya 50
waliivamia gari aliyokuwemo Mhe. Mketo na viongozi waandamizi na kuanza
kuwapiga bila sababu na kisha kuwarusha kwenye karandinga la jeshi.
Viongozi waliotekwa kwa kushtukizwa walikuwa ni;
1. Shaweji Mketo – Naibu Mkurugenzi wa Oganaizesheni Uchaguzi na Bunge,
2. Salum Hamis Mohamed – Mwenyekiti CUF Mtwara Mjini,
3. Ismail Hamis Jamal – Mwenyekiti CUF Mtwara Vijijini,
4. Ismail Bakari Njalu – Mwenyekiti wa vijana(JUVICUF) Mtwara Mjini,
5. Said Issa Kulaga – Katibu CUF Mtwara Mjini,
6. Kashindye Kalungwana – Dereve wa CUF Ofisi Kuu.
Baada ya kuwateka waliwapeleka katika kambi ya jeshi ya NALIENDELE
ambako walishikiliwa kwa jioni, usiku mzima na asubuhi ya tarehe 28 Juni
2013. Baada shinikizo la kuwaachia nililolitoa, wanajeshi waliwaachia
viongozi wote majira ya saa 5 asubuhi kwa kuwakabidhi kwa RPC wa Mkoa wa
Mtwara ambaye hadi anakabidhiwa viongozi hao alikataa kabisa kutoa
ushirikiano kwa chama, kila alipopigiwa simu alijibu yuko vikaoni na
kuwa hawezi kuongea. Majira hayohayo, RPC aliondoka na viongozi wote 6
hadi makao makuu ya jeshi la polisi Mtwara na kisha wakaanza kuhojiwa na
kisha wakapelekwa mahakamani.
F. Mashtaka waliyosomewa mahakamani;
Majira ya tarehe 28 Juni 2013 saa 10 jioni walifikishwa katika mahakama
ya wilaya ya Mtwara Mjini na kusomewa mashtaka matatu katika kesi ya
jinai namba 137 ya mwaka 2013;
1. Shtaka la kwanza ni Njama za
kutenda makosa kinyume na kifungu cha 384 cha Sheria ya Mwenendo wa
makosa ya jinai kama ilivyorekebishwa mwaka 2002 ambapo inadaiwa kwamba
tarehe 27 Juni 2013 katika eneo la barabara ya Msimbati ndani ya wilaya
ya Mtwara Mjini katika mkoa wa Mtwara wote kwa pamoja walipanga njama za
kutenda makosa.
2. Shtaka la pili ni Kusanyiko lisilo halali
kinyume na kifungu cha 74(1) na 75 cha Sheria ya Mwenendo wa makosa ya
jinai kama ilivyorekebishwa mwaka 2002 na kwamba shtaka hilo pia
linakwenda kinyume na kifungu cha 43,44 na 45 cha Sheria ya Polisi na
Polisi wasaidizi kama ilivyorekebishwa mwaka 2002 ambapo inadaiwa kwamba
tarehe 27 Juni 2013 katika eneo la barabara ya Msimbati ndani ya wilaya
ya Mtwara Mjini katika mkoa wa Mtwara wote kwa pamoja walifanya
kusanyiko ambalo si halali ambalo lilisababibsha kuvunjika kwa amani na
kuleta hofu kwa wananchi.
3. Shitaka la tatu ni kupanga na kuchochea
ufanyaji wa makosa kinyume na kifungu cha 390 cha Sheria ya Mwenendo wa
makosa ya jinai kama ilivyorekebishwa mwaka 2002 ambapo inadaiwa kwamba
tarehe 27 Juni 2013 katika eneo la barabara ya Msimbati ndani ya wilaya
ya Mtwara Mjini katika mkoa wa Mtwara wote kwa pamoja waliwachochea
wananchi wa Mtwara kutenda makosa.
Walipokana makosa hayo dhamana
iliwekwa wazi lakini kwa sharti la kila mshtakiwa kuwa na mdhamini mmoja
mwenye mali isiyohamishika na atakayewasilisha hati iliyothaminiwa ya
mali husika ambapo thamani ya mali atakayowasilisha iwe ni shilingi
milioni 20 na kuendelea.
G. Kushindwa kukamilisha masharti magumu ya dhamana na kukataliwa kupokelewa gerezani;
Kutokana na hali halisi kuwa Mtwara Mjini haina hati zilizothaminiwa
kwa wananchi wengi mawakili na wanachama wetu hawakuweza kufanikiwa
kukamilisha sharti hilo hivyo viongozi wetu walipelekwa gereza kuu la
Mtwara mjini hadi hapo masharti ya dhamana yatakapotekelezwa. Askari
magereza walipowakagua walikataa kuwapokea kwa sababu kwamba “magereza
haipokei wagonjwa” kwani magereza walithibitisha kupigwa na kuumizwa
kikatili kwa wahusika wote sita. Iliwapasa Askari polisi kuondoka nao
wote katika gari la polisi na kuwapeleka hospitali ya mkoa wa Mtwara
majira ya saa 12 jioni. Hospitalini madaktari walijionea kipigo kikubwa
walichopata maeneo mbalimbali ya miili yao, pamoja na hayo madaktari
walieleza kuwa hospitali ya Mkoa haina dawa kwa ajili ya matibabu.
Ilimpasa mhe. Mketo kutakiwa kutafuta fedha za matibabu kwa hivyo
alitafuta na kupata pesa za madawa na kuwapa madaktari ili watuhumiwa
wote wapate matibabu.
H. Maelezo ya jumla ya Mhe. Mketo juu ya
matukioa aliyohudhuria Mtwara siku ya kesi ya kina Katani aliyayoyatoa
mbele ya Mtatiro alipomtembelea gerezani 29 Juni 2013;
Naibu katibu
Mkuu wa CUF Mhe. Mtatiro na mawakili walifika Mtwara jumamosi tarehe 29
Juni 2013 na alifika gerezani na kuonana na mhe. Mketo na kufanya naye
mazungumzo chini ya ulinzi mkali. Mhe.Mketo alieleza kwa kina tukio zima
lilivyokuwa;
Alieleza kuwa wao walipofika Mtwara siku ya alhamisi
tarehe 27 Juni walihudhuria mahakamani katika kesi inayomkabili mhe.
KATANI AHMAD KATANI (Mwenyekiti wa JUVICUF taifa). KATANI na wenzie
kadhaa wakiwamo viongozi wa NCCR Mageuzi wanashtakiwa katika kesi moja
yenye mashtaka ya aina moja na nambari ya kesi moja. Cha ajabu katika
kesi hii iliyoitwa kwa kutajwa tu siku hiyo, hakimu wa mahakama ya
wilaya aliiahirisha hadi tarehe mbili tofauti wakati kesi ni moja na
washtakiwa walishtakiwa pamoja. Mhe. Katani aliambiwa atahudhuria
mahakamani tarehe 27 Julai 2013 huku wenzake kina Uledi wa NCCR Mageuzi
walitakiwa kuhudhuria mahakamani tarehe 29 Julai katika kesi ileile moja
na mashtaka yaleyale, hii ina maana kuwa mahakama imetangaza tarehe
mbili ambazo watuhumiwa katika kesi moja watahudhuria kila watuhumiwa
tarehe yao. Hatuelewi kwa nini mahakama imefanya hivi, mawakili wetu
wanashughulikia.
Baada ya ahirisho hilo Mhe. Mketo na viongozi
wengine walikusanyika ndani ya ofisi ya CUF wilaya ya mtwara mjini na
kufanya kikao kifupi na naada ya hapo walifunga safari ya kwenda kijiji
cha MSIMBATI ili kukutana na mwenyekiti wa CUF ambaye alipaswa
kuwapeleka kwa familia ya mwanamke aliyebakwa. Walipomaliza kuongea na
familia hiyo na mwanamke husika, walirekodi ushahidi na waliingia kwenye
gari kurudi Mtwara mjini.
I. Maelezo ya kuvamiwa, kuteswa, kutekwa
na wanajeshi hadi kukabidhiwa kwa polisi keshoye(Maelezo ya Mhe. Mketo
aliyoyatoa mbele ya Mtatiro):
Kilometa tatu kutoka mjini ndipo
walipokuta barabara imezibwa na magari ya jeshi huku wanajeshi zaidi ya
50 walio na silaha nzito zikiwemo bunduki za kijeshi wakiwasubiri.
Waliposimamisha gari tu milango yao ilifunguliwa kwa nguvu. Askari mmoja
mwenye bunduki alirusha ngumi ambayo mhe. Mketo aliipangua, kuona hivyo
askari Yule akahoji kwa nini Mketo amepangua ngumi yake, wakati anataka
kujibu askari mwingine alimpiga na kitako cha bunduki katika shavu la
kushoto. Katika sekunde chache ambazo walisimama wote walipigwa sana,
Mwenyekiti wa VIJANA Mtwara Mjini alipigwa na kuchanika sehemu za usoni.
Wote sta walibebwa juu juu na kutupwa katika karandinga la jeshi na
kuamriwa kulala chini kisha wakapelekwa kambi ya jeshi ya NALIENDELE.
Walipofikishwa NALIENDELE walianza kupigwa na kuteswa sana. Mketo
alishuhudia mateso ya kikatili mbayo hakuwahi kuyaona maishani.
Walivuliwa nguo zote na kulazwa kifudifudi na kumwagiwa maji ya baridi
na kupakwa chumvi kisha walianza kupigwa usiku kucha kwa kutumia mikanda
ya kijeshi, ngumi mateke na fimbo maalum za ngozi za wanyama na miti
maalum.
Baadaye wanajeshi wale watesaji walianza kuwapiga mateke ya
nguvu maeneo ya usoni, tumboni na kichwani. Kwa bahati mbaya Mketo
alipigwa sana katika ubavu wake wa kulia ambapo amewahi kufanyiwa
oparesheni kubwa miezi kadhaa iliyopita. Alipoona anapigwa sana eneo
hilo akaona awaombe askari jeshi hao wampige maeneo mengine lakini eneo
hilo wamhurumie kwa sababu amefanyiwa oparesheni. Kusikia vile, askari
wale walimgeuza kwa nguvu na kuanza kumpiga mateke ya nguvu zaidi katika
eneo lile hadi alipoteza fahamu majira yale ya jioni. Baada ya kupoteza
fahamu askari wale walikuja na kuanza kumchoma sindano (ambazo
hazijulikani zilikuwa za nini), kisha walimtundikia dripu tatu za maji.
Mketo alizinduka majira ya saa 10 alfajiri ya ijumaa ya tarehe 28 Juni
2013 na alijikuta ana dripu, hakuelewa ni ya nini. Baadaye wanajeshi
walikuja na kuitoa, wanajeshi walipoondoka aliwauliza wenzie zile dripu
ni za nini, ndiyo wenzie wakamjulisha kuwa alitundikiwa dripu usiku
kucha.
Alfajiri hiyohiyo askari jeshi wale walirudi, wakamlaza
kifudifudi mhe. Mketo na kuanza kumpiga sana kwa fimbo katika miguu
yake, walimpiga kwa saa nzima hadi walipochoka na kuondoka. Baadaye
alianza kusikia maumivu makali maeneo yenye upasuaji (ubavuni na
tumboni), anasema anahisi kuna matone ya maji au vitu laini yanadondoka
ndani kwa ndani katika eneo alilofaniwa upasuaji mkubwa. Hali haikuishia
hapo tu, baadaye na hadi sasa anasema kila akienda msalani anajisaidia
choo chenye damu nyingi huku hana msaada wa matibabu zaidi ya yale
yasiyo na vipimo yanayoendelea gerezani.
Mketo anasema wenzake
watano ndio waliopigwa kuliko yeye, anasema kuwa “wenzake ndo wamepigwa
kipigo cha mbwa”, kwa sababu hawakupoteza fahamu usiku ule. Anaeleza
kuwa usiku kucha walipigwa kwa zamu na mafungu ya askari jeshi waliokuwa
wakiingia kwa zamu kwa idadi kadhaa. Wanawapiga viongozi wetu kwa nusu
saa hadi saa nzima kisha wanaondoka na kuja wengine. Askari wengi
waliowatesa walionekana kuwa walinyweshwa pombe ili waifanye kazi ile
bila huruma, Mketo anasema usingeongea na askari wale wakakuelewa
lolote. Kazi yao ilikuwa “ni kupiga tu, ukiweka kichwa wanapiga, ukiweka
tumbo wanapiga, ukiacha jicho wazi wanapiga tu”, kwa hiyo namna
ilokuwepo ilikuwa ni kulala kifudifudi na kuacha mwili upigwe
watakavyotaka.
Dereva Kashinde Kalungwana alipigwa na kuumizwa sana
ikiwemo eneo la mkono ambao anasema maeneo ya kiganya ni kama umekufa
ganzi hadi leo. Pamoja na sindano anazochomwa hadi sasa hauhisi mkono
wake, hivyo umefungwa kwa “crip bandeji” na ameubeba akikata tamaa.
Hospitalini hawakumjulisha lolote na hakupata matibabu yoyote ya maana,
alipewa madawa ya kumeza tu.
Kulipoanza kucha ndipo mhe. Mketo na
wenzake waliacha kupigwa. Baadaye waliingia wakubwa wa jeshi kutoka
kwenye kambi ile na kuwasalimu na kuwapa pole na kuwajulia hali. Baadaye
majira ya asubuhi alikuja Kamanda wa jeshi la Polisi Mkoa wa Mtwara
(RPC) na Mkuu wa Upelelezi wa Mkoa (RCO) . Kina Mketo walichukuliwa na
kupelekwa katika chuma maalum na kuwakuta viongozi wa jeshi la Ulinzi wa
kambi ile na Mkoa wa Mtwara wakiwa pamoja na RPC na RCO. Walihojiwa kwa
muda katika kikao hicho kisha wanajeshi wakawakabidhi kwa polisi wale
majira ya saa 5 asubuhi na wakapelekwa polisi chini ya ulinzi mkali wa
polisi na kuhojiwa na kisha tena kufikishwa mahakami na kusomewa
mashtaka hayo hapo juu na kurudishwa gerezani.
Pesa zao mbalimbali,
laptop, simu na viatu hadi sasa havijulikani vilipo. Vilichukuliwa
wakati wa kipigo kile cha askari jeshi na hata wakati Mketo anaondoka
pale kambi ya jeshi alipewa viatu viwili tofauti kwa kila mguu kwani
viatu vyake halisi havijulikani viko wapi. Anakumbuka kuwa viatu vyake
vilivuliwa kwa nguvu na mmoja wa askari wakati wamelazwa kifudifudi.
Pamoja na hali hiyo, Askari magereza wana maelekezo kuwa mtu yeyote
asiwaone kina Mketo na wasipelekwe mahali popte kwa ajili ya jambo
lolote nje ya Magereza kwa sababu maalum. Kuwaona lazima kupatikane
kibali maalum, haya ndo maelekezo aliyopewa mkuu wa gereza kutoka kwa
mwenyekiti wa kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa ambaye ni mkuu wa
mkoa, sababu inayotolewa ni kuwa Mketo na wenzie ni watu hatari sana na
kwamba ati “upelelezi utaharibiwa ikiwa watatembelewa mara kwa mara na
watu mbalimbali”.
J. Maelezo ya Jeshi la Polisi Mtwara na Hali halisi ya mambo;
Mtatiro alipofika Mtwara alimtafuta RPC wa Mtwara bila mafanikio.
Alibahatika kumpata RCO na kuongea naye siku ya jumamosi 29 Juni 2013.
RCO alidai kuwa viongozi wa CUF hawakupigwa na kwamba wako salama. RCO
alikiri kuwepo kwa tukio na taarifa za kubakwa au kunyanyaswa kijinsia
na wanajeshi (hana uhakika) lakini anasisitiza kuwa “mwanamke aliyebakwa
ndiye hataki kuendelea na mashtaka na kwamba polisi walipoongea naye
pamoja na kutotaka kuendeleza mashtaka dhidi ya wabakaji wake, ati
mwanamke huyo aliwajulisha polisi kuwa hajabakwa!”
Ukiangalia
mwenendo wa matukio yote hayo kuanzia “kuvamiwa na kutekwa kwa nguvu na
wanajeshi, kupelekwa kambi ya jeshi badala ya polisi, kuteswa kinyama
usiku kucha, kuja kusalimiwa na wakuu wa kambi ya jeshi asubuhi, kuja
kwa RPC na RCO asubuhi husika na kukubali kwao kuwapokea watu waliopigwa
kiasi kile, RPC na RCO kukubali kupika mashtaka ya kusadikika na
kuwabambikizia viongozi ambao hawakufanya mkutano wowote Mtwara, wala
kuchochea jambo lolote Mtwara, wala kuvunja amani yoyote Mtwara, kukiri
kwa RCO juu ya kuwepo tukio na taarifa za ubakaji wa mwanamke
Msimbati(pamoja na RPC kukubali na kukana kwa wakati), yote haya ni
kielelezo cha uvunjifu mkubwa wa katiba ya nchi, uvunjifu mkubwa sheria
zinazoongoza ukamataji wa raia na kuwashtaki, uvunjifu mkubwa wa
protokali za kijeshi na majukumu ya jeshi la ulinzi na polisi, uvunjifu
mkubwa wa haki za raia na ni ushenzi na unyama usiomithilika ambao sasa
majeshi yetu kwa Baraka za serikali, wakuu wa vikosi vya ulinzi na
usalama, wakuu wa mikoa na mamlaka zao, na wakuu wailaya na mamlaka zao
wamekubali haya yatendeke na yaendelee kutendeka. Kutekwa, kuteswa na
kubambikiziwa kesi kwa viongozi wetu na wananchi wa Mtwara ni mipango
iliyo wazi ya vyombo vya dola na mamlaka za serikali na wala si jambo la
bahati mbaya”.
Aidha tarehe 29 Juni 2013 Mtatiro ametembelea wakazi
kadhaa walioteswa katika kambi ya Naliendele wakiwemo watumishi wa
serikali ambao wanaugulia vidonda na maumivu makali vitandani. Wengi wao
wametishiwa kuwa wakienda hospitalini majeshi yatajua na kwamba
yatawafuata mahospitalini na kuwarudisha kwenye kambi ya mateso.
Kwa
bahati mbaya sana - vyombo vya habari, mashirika ya haki za binadamu na
asasi za kiraia havifuatilii kabisa matukio haya mabaya nay a kutisha
yanayoendelea Mtwara. Hii inakamilisha ule usemi kuwa “mikoa ya kusini
imetengwa na haipati huduma na haki za msingi ambazo binadamu
wanastahili”. Baadhi ya waandishi wa habari tulioongea nao Mtwara
wanaonesha kuwa na wao wanasakwa na wanajeshi ikiwa wataripoti matukio
haya. Tumewauliza mbona wakiwa Arusha hata kama ni katikati ya mabomu na
vipigo bado wanaripoti habari. Wanachojibu ni kuwa Arusha si Mtwara.
K. Hatua muhimu za kuchukua;
Tunatoa wito kwa Mahakama kuwapa dhamana mara moja viongozi wetu
waliopigwa na kubambikiziwa kesi ili wapate matibabu. Maisha ya viongozi
wetu yako hatarini. Mketo alifanyiwa operesheni kubwa mwaka jana na
inaonekana kuna damu inavuja ndani ya mwili wake (internal bleeding).
Wengine wamepigwa zaidi ya Mketo hatujui madhara makubwa waliyoyapata.
Tunawasiliana na Mawakili wetu na asasi za haki za binadamu kuelewa
hatua za kisheria tunazoweza kuchukua dhidi ya Jeshi la Wananchi
kuwateka nyara na kuwatesa viongozi wetu.
Vile vile tunawasiliana na
Mawakili kujua hatua za kisheria za kuchukua dhidi ya Jeshi la Polisi
la kushiriki katika kubambikizia kesi watu ambao wamekamatwa na kupigwa
na askari wa Jeshi la Wananchi.
Tunawasiliana na asasi za kiraia
zinashughulikia Haki za Binadamu na Haki za Wanawake kumsaidia mama
aliyebakwa kisaikolojia na kuhakikisha waliohusika wanafikishwa
mahakamani ili wanajeshi wanaobaka wajue kuwa hawako juu ya sheria.
Jeshi la Wananchi linajijengea uhasama mkubwa na raia wa kawaida mkoani
Mtwara. Hii ni hatari kwa usalama na amani ya kweli ya nchi yetu.
Utaratibu wa wanajeshi kukamata kupiga na kutesa wananchikwenye kambi ya
Naliendele usitishwe mara moja. Mkuu wa Mkoa ambaye ni afisa wa jeshi
mstaafu hana mahusiano mazuri. Anawadharau, kuwabeza na kuwaona ni
waswahili wasiokuwa na maana. Anajenga uhasama mkubwa kati ya wananchi
na serikali.
Tukio hili la utesaji la raia ndani ya Kambi ya Jeshi
la Wananchi ukiliunganisha na matukio mengine kama vile utesaji wa Dr.
Ulimboka, kutekwa nyara na kuteswa kwa Mwandishi wa Habari Absalom
Kibanda, kulipuliwa bomu katika mkutano wa hadhara wa CHADEMA katika
viwanja vya SOWETO, Arusha na matukio mengine kunadhihirisha hatua za
awali za kusambaratika kwa dola (Failed State). Rais Kikwete akiendelea
kuyafumbia macho mambo haya na kuruhusu vitendo vinavyofanywa na Jeshi
la Wananchi katika Kambi ya Naliendele taifa linaweza kusambaratika.
Ibrahim Haruna Lipumba
Mwenyekiti,
Jumapili, 30 Juni 2013
0 Weka maoni yako hapa:
Post a Comment
COMMENT HAPA