Sheikh Ponda Kuendelea Kusota Rumande Hadi Nov 21
KESI yenye mashtaka matatu inayomkabili Katibu wa Jumuiya na
Taasisi za Kiislamu nchini, Sheikh Ponda Issa Ponda, katika Mahakama ya
Hakimu Mkazi Mkoa wa Morogoro, imeshindwa kusikilizwa baada ya jalada
halisi la kesi hiyo kuitishwa katika Mahakama Kuu Kanda ya Dar es
Salaam kwa ajili ya kupitiwa upya.
Sheikh Ponda alifikishwa mahakamani hapo jana asubuhi kwa kutumia
usafiri wa basi maalumu la Magereza na safari hii kesi yake ilikuwa
mbele ya Hakimu Mkazi Mwandamizi, Mary Moyo, baada ya hakimu aliyekuwa
akisikiliza tangu awali, Richard Kabate, kuhamishiwa mkoani Dodoma.
Akitoa maelezo ya kesi hiyo, Hakimu Moyo alisema kuwa jalada halisi
la kesi hiyo limeitishwa Mahakama Kuu Dar es Salaam Oktoba 15, mwaka
huu, kwa ajili ya mapitio na kwamba Mahakama Kuu ina mamlaka ya
kisheria ya kuitisha jalada, hivyo kesi hiyo haitaweza kusikilizwa hadi
litakaporudi.
Hakimu Moyo alisema kuwa kwa sasa kesi hiyo itakuwa ikitajwa tu na
suala la mshitakiwa kuletwa ama kutoletwa mahakamani liko chini ya
Magereza, kwani dhamana ya mshitakiwa huyo imefungwa, hivyo ataendelea
kuwepo gerezani hadi Novemba 21, mwaka huu, itakapotajwa tena
mahakamani hapo.
Mapema baada ya kufikishwa mahakamani hapo, Hakimu Moyo alimuuliza
Sheikh Ponda kama ana taarifa zozote kuhusu kutokufika kwa mawakili
wake watatu ambao ni Batholomew Tarimo, Ignas Punge na Juma Nassor,
hata hivyo Sheikh Ponda alidai kuwa hana taarifa zozote.
Hata hivyo, upande wa mashtaka ukiongozwa na Wakili wa Serikali,
Sunday Hyela, umedai kuwa uko tayari kutoa ushahidi ambao ungeanza na
askari polisi mwenye namba F 4949 DC Kingazi wa Kituo Kikuu, lakini
hakuweza kutoa ushahidi wake kutokana na jalada halisi la kesi hiyo
kuitishwa na Mahakama Kuu kwa ajili ya mapitio.
0 Weka maoni yako hapa:
Post a Comment
COMMENT HAPA