TAMKO LA JUMUIYA YA VIJANA KUUNGA MKONO KAZI YA SEKRETARIETI YA CHAMA CHA MAPINDUZI CHINI YA KATIBU MKUU NDUGU ABDULRAHAMAN KINANA.
“..Chama
Cha Siasa chochote duniani hubomoka kutokana na migongano iliyokithiri
ya muda mrefu. Uzoefu wa vyama vikubwa vilivyoporomoka umeonyesha
hivyo! Chama lazima kidhibiti uchu wa madaraka wa baadhi ya viongozi
wake na ndani ya serikali yake...” – Dr Eginald P. Mihanjo
“..Chama cha siasa ni itikadi. Chama cha siasa ni siasa kwa maana halisi
ya neno lenyewe siasa –“siasa”. Ni mahali ambapo watu wenye madhumuni
mamoja yaliyoainishwa waziwazi hukutana na kuwa kitu kimoja. Chama cha
siasa sio mkusanyiko wa “majini dume yenye tamaa”, - majini ambayo
yametanguliza mbele tamaa kufa na kupona-tamaa ya kutengeneza pesa au
kupata vyeo kwa gharama yoyote! – Dr Bashir Ally
“..hakika
Chama ni watu na uhai wa Chama chochote cha siasa duniani unategemea
mchango wa fikra za wanachama wake waaminifu. Chama kinachokosa
changamoto ya wanachama wanaofikiri ni chama cha wafu...”-- Makwaia wa
kuhenga.
UTANGULIZI:
Hili ni tamko la vijana makini wa
jumuiya ya umoja wa vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM) kuunga mkono
juhudi na utendaji wa sekretarieti ya halmashauri kuu ya Chama Cha
Mapinduzi ikiongozwa na Katibu Mkuu Komredi Abdulrahaman Kinana.
Maneno ya utangulizi yamebeba dhima ya tamko hili, kufuatia taarifa
zilizoripotiwa kwenye baadhi ya vyombo vya habari vikiwanukuu baadhi ya
wanachama wa Chama Cha Mapinduzi, Ndugu Guninita akiwatuhumu Viongozi wa
Sekretarieti ya Halmashauri Kuu ya CCM, Katibu Mkuu Ndugu Abdulrahaman
Kinana na Katibu wa Itikadi na Uenezi Ndugu Nape Moses Nnauye.
Sisi Vijana tunatambua kuwa tuhuma hizo na maneno hayo ya hovyo
yametolewa kwa nia ovu yenye kulenga kuwakatisha tamaa Viongozi hao wa
Chama. Tunafahamu kuwa upo mkakati wa kiuhaini ulioandaliwa na
kuratibiwa na “mtandao” ndani ya Chama ambao umejipanga kuendesha uhaini
huo.
Sisi vijana wa UVCCM tunatambua na kuthamini juhudi za Katibu
Mkuu na Sekretarieti yake katika kukijenga na kukiimarisha Chama kwa
kuisimamia barabara misingi na shabaha ya kuundwa kwake, katika umri
wetu hatukuwahi kuona Chama kikiwa karibu na wananchi kwa kufuatilia,
kusikiliza na kushiriki katika utatuzi wa kero, shida na changamoto zao
kama ilivyo katika kipindi hiki chini ya Comrade Kinana na timu yake.
Juhudi hizi ni za kuungwa mkono na kamwe si za kubezwa na mwanaCCM
muadilifu, muaminifu na mwenye mapenzi ya kweli kwa Chama.
Juhudi za
kukiimarisha Chama kutoka ngazi za chini, kwa mabalozi ni mkakati bora
kuwahi kutekelezwa na Chama, kukirudisha Chama kwa wanachama ni kutimiza
lengo la kuundwa kwa Chama hiki, Chama hiki ni cha wanyonge, masikini
wa Taifa hili,
HAIWEZEKANI matajiri watake kukihodhi na waratibu
mikakati ya kukihujumu kwa pesa zao hali sisi vijana tukitazama,
tunasema tutakilinda Chama chetu na tutawalinda viongozi wetu waadilifu.
Ni hawa ambao wanabezwa leo ndio wameweza kurudisha Imani ya
wananchi kwa Chama, Imani na matumaini ambayo tayari yalishaanza kupotea
na Chama kuonekana si tena cha wanyonge, wakulima na wafanyakazi wa
nchi hii.
Ni Comrade Kinana na timu yake ndio waliozunguka kwenda
kukutana na wakulima wa Pamba kule mikoa ya Kanda ya ziwa na kumpeleka
balozi wa China na kumshawishi kujenga viwanda ili kuboresha manufaa kwa
wakulima.
Ni Comrade Kinana na timu yake ndio waliokwenda Kusini
kukutana na wakulima wa Korosho na kushirikiana nao pamoja na bodi
kutatua tatizo la Korosho.
Ni Comrade Kinana na timu yake ndio
walioibua hoja na kero za wafugaji, walimu na wananchi kwa ujumla, na
kuwataka viongozi wa Serikali kuhakikisha wanawajibika kwa wananchi
walipa kodi wa Taifa hili.
Kupinga mafanikio ya Ziara hizo ni kupinga utetezi wa wanyonge.
Mtu anayebeza ziara hizo na kuwaita Viongozi waliozifanya waropokaji na
wahuni wahuni ni mtu mjinga, mtu wa hovyo,hana maadili, asiyekipenda
Chama, mhaini na mzandiki anayepaswa kuchukuliwa hatua kali za kinidhamu
ili iwe fundisho kwa wengine.
TAMKO hili limezingatia wosia wa Baba
wa Taifa, muasisi wa Chama Cha Mapinduzi Mwl Julius Kambarage Nyerere
katika kitabu Chake TUJISAHIHISHE.
“Inapofikia wasimamizi wa
Kanuni za Chama wanapigwa vita ya wazi kwa uamuzi wao wa kukisimamia
Chama, tafsir yake ni moja tu watu wanaowapiga vita hawakitakii mema
chama chetu.”
Imetolewa na Paul Makonda.
Katibu wa Hamasa na Chipukizi.
0 Weka maoni yako hapa:
Post a Comment
COMMENT HAPA