Mar 6, 2014

UKISTAAJABU YA MUSSA UTAONA YA FARAUNI AJABU AL AHLY HAWAJUI MECHI ITACHEZWA WAPI

      
Katika hali ya kushangaza wenyeji timu ya Al Ahly mpaka sasa wameshindwa kuwadhibitishia viongozi wa Young Africans pamoja na Ubalozi wa Tanzania nchini Misri juu ya Uwanja utakaotumika kwa ajili ya mchezo wa marudiano Klabu Bingwa Barani Afrika siku ya jumapili.

Sheria za mashindano ya CAF zipo wazi na zinaelekeza timu mwenyeji wanapaswa kuwajulisha wageni uwanja utakaotumika kwa mchezo takribani siku 10 kabla ya mchezo, huku mpaka leo siku ya jumatano takribani siku nne kabla ya mchezo wakishindwa kutabanaisha mchezo utakapofanyika.

Mapema jana mchana Afisa Ubalozi wa Tanzania nchini Misri Bw Idrisa Juma alifika makao makuu ya Al Ahly kuweza kujua taratibu za mchezo huo lakini hakufanikiwa kupata majibu kamili zaidi ya kuahidiwa kufikia leo mchana kwamba watakua wameshapata majibu juu ya ni sehemu gani mchezo utafanyika.

Afisa Habari wa Young Africans Bw Baraka Kizuguto leo asubuhi aliambatana na maofisa Ubalozi mpaka makao makuu ya klabu ya Al Ahly na kukutana na meneja Said Abdoulaziz na meneja usalama Morgan na katika mazungumzo hayo walisema mpaka muda huo walikuwa hawajapata maamuzi ya serikali juu ya uwanja utakaotumika kwa mchezo.

"Tumeomba mchezo ufanyike kati ya Uwanja wa Cairo au mji wa Alexandria lakini Serikali imekataa kutoa Viwanja yake pamoja na ulinzi katika mchezo wetu kutokana na washabiki wetu kufanya vurugu kwenye mchezo wa Super Cup dhidi ya CS Sfaxien ya Tunisia" alisema Said.

Katika kikao hicho kilichofanyika kwa zaidi ya masaa mawili Uongozi wa Young Africans uliomba mchezo wake ufanyike jijini Cairo kwani ndo sehemu waliyojiandaa kwa mchezo kufuatia taarifa ya Al Ahly walipokuja Tanzania kwenye mchezo wa awali.

Mara baada ya mazungumzo hayo waliahidi kuongea na waziri mwenye dhamana ya michezo kuruhusu mchezo ufanyike jijini Cairo na kwamba mchezo huo kama iliyoamuriwa tangu awali na mamlaka husika ya ulinzi na usalama hautakua na washabiki wowote kwa uwanja wowote utakaochezewa.

Akiongea na mtandano rasmi wa klabu ya Young Africans Kizuguto amesema wamekaa kusubiria majibu ya Uwanja utakaotumika kwa mchezo zaidi ya masaa 6 bila majibu huku viongozi hao wa Al Ahly wakipigiwa simu na kutopokea.

"Tuliwaambia jiji la Cairol lina Viwanja zaidi ya 10 vyote vyenye hadhi ya kimataifa sio lazima tucheze Cairo International, wajaribu kuomba viwanja vingine lakini walionekana kutokua tayari na zaidi kusisitiza watamuomba waziri wa michezo aruhusu mchezo ufanyike Cairo bila washabiki" alisema Kizuguto
Kutokana na mazingira hayo ya ucheleweshwaji kutangaza sehemu utakaofanyika mchezo Ubalozi wa Tanzania nchini Misri kupitia Balozi wake Bw Mohamed Hamza na maafisa wake na uongozi wa Young Africans umeendelea kufanya maandalizi kwa njia zote kuhakikisha timu inafika salama na kupata huduma zote muhimu ikiwa ni pamoja na malazi, chakula, uwanja wa mazoezi na ulinzi kwa kipindi chote timu itakapokuwa nchini Misri.

Msafara wa watu 30 unatarajiwa kuwasili kesho alfajiri jijini Cairo kwa shirika la Ndege la Egypt Air na kupokelewa Uwanja wa Ndege na Balozi Hamza, pamoja na maafisa Ubalozi kisha kuelekea sehemu maalumu ambayo timu ndipo itakapokua imeweka kambi mpaka siku ya mchezo.

0 Weka maoni yako hapa:

Post a Comment

COMMENT HAPA