PATRICK
Mutesa Mafisango (32), mchezaji tegemeo wa Simba SC amefariki dunia jijini Dar
es Salaam usiku wa kuamkia leo katika eneo la Keko jirani na Chuo cha VETA
jijini Dar es Salaam.
Mafisango
alikufa kutokana na ajali iliyotokea wakati gari alilokuwa akiendesha
lilipogonga mti ulio pembezoni mwa barabara ya Chang’ombe majira ya saa kumi
kasorobo alfajiri. Marehemu alifariki papo hapo.
Kwenye gari
aliyokuwamo Mafisango, kulikuwapo na abiria wengine wanne lakini ni Mafisango
pekee ndiye aliyefariki dunia.
Mwili wa
Marehemu umehifadhiwa katika Hospitali ya Taifa Muhimbili tayari kwa
kusafirishwa kwenda kwao Kinshasa, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC)
ambako atazikwa.
Ingawa
alikuwa na uraia wa Rwanda na akiichezea timu ya taifa ya nchi hiyo (Amavubi),
Mafisango alikuwa ni mzaliwa na raia wa DRC na uamuzi wa kuzikiwa huko ni wa
familia yake.
Msiba wa
Mafisango uko katika eneo la Keko Toroli jirani na kituo cha Chang’ombe Maduka
Mawili (Njia Panda Sigara).
Mwili wa
marehemu unatarajiwa kuagwa kesho Ijumaa saa nne asubuhi katika viwanja vya
Leaders, Kinondoni jijini Dar es Salaam kabla ya mwili wake kusafirishwa kwenda
Kinshasa majira ya saa kumi jioni.
Mafisango
alizaliwa Machi 30, 1980 huko Kinshasa Zaire wakati huo na ameacha mke na mtoto
mmoja wa kiume, Chris Paul, mwenye umri wa miaka mitano.
Mafisango
ameichezea Simba kwa msimu mmoja tu akitokea Azam ya Dar es Salaam lakini kabla
ya hapo alichezea pia TP Mazembe ya DRC, APR ya Rwanda na pia aliwahi kuwa
nahodha wa Amavubi kwa takribani miaka mitano.
Mwenyekiti
wa Simba, Ismail Aden Rage, Makamu wake, Geofrey Nyange Kaburu na wajumbe wa
kamati ya watendaji wameeleza kusikitishwa kwao na msiba huu mkubwa kwa klabu
na wamewataka wana Simba wote kuwa watulivu na kumwombea marehemu Mungu amlaze
mahali pema peponi.
Uongozi wa
Simba unaahidi kuwa utatoa taarifa nyingine zozote muhimu kwa wananchi ili
wafahamu kuhusu msiba huu pale itakapotokea.
Imetolewa
na
Ezekiel
Kamwaga
Ofisa
Habari
Simba SC
17/5/2012
0 Weka maoni yako hapa:
Post a Comment
COMMENT HAPA