May 29, 2013

KUFUATIA GAZETI LA NIPASHE KOTOA HABARI HII YA KUMUHUSISHA NA UASI MAKAMBA AJIBU

Gazeti la leo la Nipashe, katika ukurasa wa mbele, lina picha yangu na kichwa cha habari kinachosema "Waziri Adaiwa Kuchochea Uasi: wananchi wavamia kiwanda; aahidi kuwawekea wakili dhidi ya mwekezaji". Habari hii ina nusu ukweli.

Ni kweli wana Bumbuli tumechoshwa na mbia/mwekezaji katika kiwanda chetu cha chai na uongozi wa Chama cha Wakulima wa Chai. Hali hii ilidhihirika wazi kwenye mkutano wangu na wakulima wa chai siku ya Jumapili. Kwa miaka tisa sasa, wananchi wamekuwa wanalalamika kuhusu kudhulumiwa, kunyanyaswa na kuonewa na kutonufaika na zao lao la Chai. Nimefanya juhudi mbalimbali za kumaliza tatizo hili, ikiwa ni pamoja na vikao zaidi ya vitatu kati yangu, mwekezaji, viongozi wa wakulima, pamoja na Bodi ya Chai. Mwaka juzi, niliongoza kikao cha wadau wa Chai Kanda ya Kaskazini na kupigania kupandishwa bei ya chai kutoka shilingi 110 hadi 206. Hata hivyo, malipo kwa wakulima yamekuwa yanacheleweshwa na taarifa za mapato na matumizi zimekuwa hazitolewi na mbia/mwekezaji.

Pia wapo viongozi wanaonufaika na dhuluma hizi, ikiwa ni pamoja na kulipwa mshahara na mbia kila Mwezi pasipo kufanya shughuli yoyote.

Wakulima, ambao ni wamiliki wa kiwanda, sasa wamechoka. Wamechoshwa na mbia wao na wamechoshwa na viongozi wao. Nami niko nao na nawaunga mkono. Kama kuwaunga mkono watu wangu ni uasi, naikubali label hiyo. Tutapigana hadi tupate haki yetu. Nitaweka wakili ili tutafute haki yetu kisheria.

Niweke baadhi ya mambo sahihi:

1. Hakujatokea vurugu wala machafuko yoyote. Wananchi wameamua wenyewe kwenda kukaa nje ya kiwanda kulinda mali yao.

2. Tofauti na ilivyoripotiwa, hakuna uharibifu wowote wa mali uliofanyika. Polisi wameenda kuangalia na kukuta kila kitu salama na kuondoka.

3. Tunafanya jitihada mbalimbali kwa kushirikiana na Bodi ya Chai ili wakulima wapate sehemu nyingine ya kuuza chai yao wakati tunatafuta suluhu.

4. Wapo wanasiasa uchwara wanaodai tuwe na amani na tukubali unyonyaji kisa tu kwamba siku zote tumekuwa wapole tangu enzi za mababu. Watuache tudai haki yetu.

5. Uamuzi huu ni wa wakulima wenyewe. Kusema eti wanachochewa ni kuwatukana, kana kwamba ni wajinga ambao hawajui kipi sawa na kipi si sawa.

0 Weka maoni yako hapa:

Post a Comment

COMMENT HAPA