TAARIFA KUTOKA SHIRIKA LA NYUMBA
Utangulizi: Jumatatu na Jumanne ya wiki hii, kumekuwa na taarifa
zilizochapishwa kwenye moja ya gazeti la kila siku zikieleza kuwa
Mkurugenzi Mkuu wa NHC, Bw. Nehemia Kyando Mchechu ameundiwa zengwe na
Bodi ya Wakurugenzi ya NHC kwa nia ya kuhakikisha kuwa harejeshwi tena
katika wadhifa huo, hasa baada ya Bw. Mchechu kumaliza muda wake wa
kuliongoza Shirika hili. Aidha, gazeti hilo liliwaaminisha umma wa
watanzania kuwa mizengwe hiyo inaungwa mkono na vigogo wa Serikali
wakiwemo Wabunge ambao kuwepo kwa Bw. Mchechu katika Shirika kumewanyima
ulaji ikiwemo kupangishwa nyumba za Shirika. Gazeti lililienda mbali
zaidi likidai kuwa Bw. Mchechu amewekewa masharti magumu na Bodi hiyo ya
kumtaka apunguze idadi ya Wakurugenzi wa Menejimenti ya sasa ya
Shirika.
Kwa kuwa habari hizo zimeleta mtafaruku katika Shirika
na zimesababisha umma kuwa na mijadala mbalimbali juu ya jambo hili,
tungependa kuwataarifu umma kuwa taarifa hizo hazina ukweli wowote, na
Shirika la Nyumba la Taifa linapenda kutoa ufafanuzi kama ifuatavyo:-
1. Kwanza, ifahamike kuwa Bodi ya Wakurugenzi ya NHC ina miezi miwili
tu tangu iteuliwe na Mamlaka husika na haijawahi kukaa katika kikao
chochote kujadili suala la kumuondoa Mkurugenzi Mkuu na kupunguza
Menejimenti ya Shirika iliyopo sasa.
2. Tunapenda kuwafahamisha
kuwa Mkurugenzi Mkuu na Menejimenti ya Shirika bado wana mikataba halali
ambayo haijamalizika muda wake, hivyo hoja ya kuwa Bwana Mchechu na
Menejimenti yake wanaundiwa zengwe baada ya kumaliza muda wao haina
ukweli wowote.
3. Kwamba kutokuwepo kwa Mkurugenzi Mkuu kwenye
ufunguzi wa miradi hakukutokana na kuwepo mizengwe kama ilivyoripotiwa
na Gazeti hili. Bw. Mchechu alikuwa katika likizo yake ya mwaka
iliyooanza tarehe 30 Juni na kumalizika Julai 18, 2014. Likizo hii ni
stahili halali ya Bw. Mchechu kama walivyo watumishi wengine wa umma, na
hakuichukua likizo hii kutokana na kuwepo mizengwe ya kumuondoa kama
ilivyoripotiwa na Gazeti hili. Kuanzia tarehe 21 Julai, 2014 Bw. Mchechu
yupo kikazi nje ya nchi na anatarajiwa kuwa ofisini kwake tarehe 28
Julai, 2014.
4. Mwisho, tunapenda kuwatanabaisha wanahabari
kuwa kama ilivyo kawaida yetu, NHC imekuwa na itaendelea kuwa mstari wa
mbele kutoa habari makini kwa vyombo/chombo chochote cha habari bila
kuficha jambo lolote. Hivyo, tunawaomba muendelee kuitumia vyema fursa
hii kupata habari zenye ukweli na zilizo sahihi kwa jambo lolote
mnalohitaji kuufahamisha umma wa watanzania. Kwa kufanya hivyo,
tutaendelea kuwa washirika wakubwa wa vyombo vya habari, tukizingatia
kuwa vyombo vya habari vina dhima na dhamana kubwa katika kuleta tija
kubwa kwa Shirika na Taifa letu. Aidha, tunawafahamisha wateja wetu kuwa
hakuna mtafaruku wowote uliyopo ndani ya Shirika la Nyumba la Taifa na
kwamba tunaendelea kuwapa huduma zetu zilizo bora katika sekta ya nyumba
tuliyoaminiwa na Taifa kuisimamia.
IMETOLEWA NA:
BW. DAVID SHAMBWE,
KAIMU MKURUGENZI MKUU,
0 Weka maoni yako hapa:
Post a Comment
COMMENT HAPA