Baada ya gazeti la Tanzania Daima kutoa habari leo hii Hamisi Andrea Kigwangalla, atoa ufafanuzi juu yake
Mbunge wa Jimbo la Nzega,
Taarifa kwa vyombo vya habari
Bungeni, Dodoma, Mei 1, 2013.
Nawasalimu kwa heshima na taadhima.
Napenda kutumia fursa hii kutoa taarifa kwa wanahabari na umma kwa
ujumla kufuatia habari iliyotoka leo mapema asubuhi kwenye gazeti la
Sauti ya watu Tanzania Daima, toleo Na.3071 na kuzua mjadala mkubwa na
mzito kwenye jamii pamoja na kwenye mitandao ya kijamii kuhusiana na hadhi,
heshima na uadilifu wangu kwenye jamii nikiwa kama kiongozi wa umma.
Niwape pole wale wote walioguswa na kushughulishwa na jambo hili, haswa
familia yangu, ndugu, marafiki na wananchi wa Nzega; ambao siku zote
wanaamini sana katika uadilifu wangu na namna ninavyosimamia misingi ya
haki, sheria na uzalendo.
Nimesikitishwa sana na habari hii
hususan kwa kuwa ilichapishwa bila kunipa fursa ya kueleza kwa mapana
uhusika wangu. Niwapongeze gazeti la Nipashe kwa kupuuza uzushi huu mara
baada ya kunipigia na kueleza upande wangu wa hadithi.
Kumekuwa na wimbi kubwa la baadhi ya watu kwenye baadhi ya vyombo vya
habari kuandika habari za uongo kwa maslahi maovu ya kuwachafua
wanasiasa na watu wengine. Watanzania sote tubadilike na tukatae tabia
za kutumika vibaya namna hii, maana ni hatari kwa ustawi wa weledi, na
kwa umoja na mshkamano wa kitaifa. Ukishaandika jambo ambalo litamchafua
mwenziyo, hata kama utamsafisha kiasi gani ni wazi hautokuwa na uhakika
kuwa utawafikia wale wale waliosoma zile za jana za kumchafua – hivyo
ni jambo la kawaida kabisa kuanza kwanza kwa kuwa na uhakika kabisa na
habari kabla ya kuiandika.
Mfano mwaka 2010 tu mara baada ya
kuteuliwa nilizushiwa kashfa ya uongo kabisa inayohusiana na Uraia wangu
na gazeti moja maarufu la kila siku na mengine yakaweka kwenye ukurasa
wa mbele kabisa kwamba Kigwangalla ni Mrundi; hawakusema ni mrundi wa
wapi, toka lini ama kivipi, walisema ni mrundi tu! Basi hata kusema
shaka yao inaanzia wapi hawakusema. Kwa kuwa vyombo vya dola
vilinisafisha na kupelekea kushinda mapingamizi yote yaliyowekwa na
washindani wangu kisiasa, niliamua kudharau na kusema yatapita tu na
yatasahaulika.
Pia gazeti lingine likaandika kwamba kampuni ya
Kigwangalla ni miongoni mwa makampuni yaliyowahi kufaidika na ‘stimulus
package’ baada ya mdororo wa uchumi mwaka 2008. Gazeti hata halikutaja
kampuni ya Kigwangalla ni ipi, inaitwaje, Kigwangalla ana hisa kiasi
gani, anaendesha kampuni hiyo ama la, na kampuni hiyo imepewa sh ngapi
kutoka benki kuu, na je imepewa pesa hizo kwa nyaraka zipi na zenye
namba gani? Na je pesa hizo imepewa kihalali ama imepitia mlango wa
nyuma? Kama imezipata pesa hizo kinyume na utaratibu, basi kuna ushahidi
gani! Kwa kuwa yalikuwa mambo ya uongo na uzushi niliamua kudharau na
kuacha kama ilivyo.
Gazeti lingine la kila siku liliwahi tena
kuandika ‘Kigwangalla atajwa kufadhili mgomo wa madaktari’ na liliweka
hadithi hii kwenye ukurasa wake wa mbele kabisa. Halikusema amefadhili
sh ngapi? Amempa nani? Zimeenda kufanya nini fedha hizo? Kwa kuwa
lilikuwa ni jambo la uongo, pia nilidharau na kuacha lipite. Mwaka jana
Novemba pia gazeti lingine liliandika habari na kuweka picha yangu na ya
Ndg. Hussein Bashe, na katikati yetu picha ya bastola, na kusema
‘Kigwangalla na Bashe na vita ya bastola Nzega’, na humo ndani kueleza
kuwa Kigwangalla na Bashe wanyoosheana bastola wakati wakirudisha fomu
za kugombea ujumbe wa NEC. Na
kuna mengine mengi: yale ya rushwa ya vitumbua n.k.
Yote haya kwa ujumla wake yalikuwa ni mambo ya uongo na yasiyo na
chembe ya ukweli hata kidogo. Mara zote nimekuwa nikiyadharau na kuongea
na wahariri wa vyombo husika vya habari kwa namna inayoashiria urafiki
na weledi wa kushirikiana na kufanya kazi pamoja na si vinginevyo;
ushauri ambao niliupata mwaka 2009 kutoka kwa moja ya wanasheria wa
kampuni yangu (wa kampuni ya Marando, Mnyele & Co. Advocates),
wakili nguli Mzee Mabere Nyaucho Marando, ambaye alisema ‘wasamehe tu
hawa gazeti la Sauti Huru maana ni vema kujenga marafiki wengi zaidi na
media kwa kuwa wewe ni kijana, kuliko kujenga maadui – na niliwasamehe
bila gharama yoyote ile’. Mzee Marando hakukosea, ila ukweli ni kwamba
ukifanya hivyo utaona patatulia kwa muda na baada ya hapo pataibuka tena
jambo lingine la ukurasa wa mbele linaloandikwa bila ukweli wowote ule!
Imekuwa wimbo wa kawaida kwenye baadhi ya media houses! Kufanya kazi
kwa maslahi ya watu fulani ama chama fulani, misingi ya weledi ya
uandishi haipo! Cha muhimu ni maelekezo ama utashi wa anayetoa chochote.
Jambo moja kubwa nililojifunza kutokana na yote haya ni
kwamba, jambo likiishaandikwa kwenye media halifutiki kwenye bongo za
watu, hata muda ukipita namna gani! Leo hii kila siku haya mambo
yamekuwa yakirudiwa rudiwa kwenye mitandao ya kijamii hata baada ya
kuyatolea ufafanuzi wa kina. Nimefika mahali nimeona niachane na passive
ways za kushughulika na media ili kuweka sawa kumbukumbu zangu mbele ya
umma wa watanzania.
Ya ukweli: ni kweli kwamba ninamiliki hisa
kwenye kampuni ya Emergent Africa Ltd. Nina hisa 40% na mke wangu Dr.
Bayoum Kigwangalla anamiliki hisa 11%. Sijihusishi na kuendesha biashara
hii kama mtendaji wa kila siku – kampuni ina watumishi wake sehemu
mbalimbali. Ni kweli kwamba kampuni ina mradi wa kujenga chuo cha afya
Nzega (International Institute for Health Tabora), eneo la uchama, na ni
kweli imepewa orodha ndefu ya vitu ilivyosamehewa kodi na serikali kwa
kuwa ni vitu/vifaa vya mtaji (deemed capital goods). Ni kweli kwamba
kampuni imewahi kuingiza nchini kontena moja lenye vifaa vichache sana
katika vinavyotajwa kwenye habari ile, na vingi kati ya hivyo vipo aidha
kwenye stoo ya kampuni iliyopo Nzega ama ya Dar es salaam, Kigamboni.
Kwa kuwa vipo, wanahabari wanakaribishwa kwenda kuvitazama vitu hivi
kama wanapenda.
Ya uongo: Si kweli kwamba nina hisa 78% na mke
wangu Dr. Bayoum Kigwangalla ana hisa 22% - ni uongo. Si kweli kwamba
kampuni imeagiza vitu na kuvipitisha bandarini na forodhani kwa msamaha
kwa nia ya kuuza na hivyo kuiibia serikali kwa njia ya kukwepa kodi. Si
kweli kwamba kampuni ya Emergent Africa Ltd imeingiza vifaa vyote
ambavyo imepewa msamaha, kama habari inavyotaka kuwaaminisha waTanzania.
Sijawahi kuuza bidhaa zozote zile za kampuni hii zilizoingizwa nchini
kwa njia ya msamaha wa kodi. Kampuni ya Emergent Africa Ltd haina mradi
wa kuuza tiles na hivyo haijawahi kufanya biashara hiyo.
Ingekuwa ni dhambi kubwa kama kweli ningekuwa naviuza vifaa hivi bila
kuvilipia kodi. Na kama ningekuwa sina mradi genuine wa ujenzi wa chuo
na labda nimetumia vibaya nafasi yangu ya ubunge kujipatia msamaha ili
kurahisisha biashara zangu basi ningeanza kwa kuuza cement (ambayo ni
bidhaa inayokimbia sana sokoni na kampuni yangu imepewa msamaha wa
karibu tani 5000 – lakini sijawahi kuutumia msamaha huu kununua hata
mfuko mmoja wa cement!). Ama ningeingiza mabati/vigae vya kuezekea
(ambavyo pia vinakimbia sana sokoni kwa kuwa watu wengi wanajenga –
lakini sijaingiza hata kigae kimoja!), ama ningeingiza malori 4, Nissan
Navara pick up 4, Mitsubishi Canter 2, Landcruiser Hardtop 4( ambazo
zinatumika sana kwenye utalii na hata kwenye barabara za vumbi) kwa
msamaha – lakini sijaingiza hata gari moja kati ya haya, kinyume na
habari hii ya Tanzania Daima inavyotaka kuuaminisha umma! Kuonesha
uadilifu nitaeleza hapa mfano mmoja kwamba mnamo Novemba mwaka jana
nilinunua gari moja SUV aina ya Nissan Patrol (T934 CDB) na nimeilipia
kodi zote bila msamaha japokuwa ningeweza kutumia msamaha wa kodi
kununua na kuingiza moja ya magari yaliyopo kwenye msamaha huu wa
kampuni ambayo mimi ni major shareholder. Pia nina ujenzi wa nyumba ya
kuishi Nzega, Tabora na Dar es salaam katika hatua mbalimbali: ningeweza
kutumia msamaha huu wa kodi wa kampuni yangu ili kujipatia unafuu
kwenye manunuzi ya vifaa mbalimbali vya ujenzi kama cement, vigae ama
mabati, lakini sijawahi kufanya hivyo hata siku moja!
Kuwa na
hisa kwenye kampuni inayofanya biashara halali siyo dhambi. Kupata
msamaha wa kodi siyo dhambi. Dhambi ingekuwa kuviuza baada ya kupata
msamaha. Kama kuna mtu anaamini kuwa kuna vifaa vimeuzwa na kampuni
yangu, kati ya hivi vilivyoingizwa nchini kwa msamaha, anakaribishwa
kuleta uthibitisho wa nyaraka za mauzo (cash sale receipts, tax invoice
ya mauzo, pay-in slip ya benki ya malipo, delivery note, ama receipt
yoyote ile ya kampuni hii inayoashiria kuwa mauzo yamefanyika) ili
niweze kufuatilia kujua ni nani aliyeuza na kwa nini alifanya hivyo ili
niweze kuchukua hatua za kinidhamu dhidi yake ikiwa ni pamoja na
kumpeleka mbele ya vyombo vya sheria.
Msamaha wa vifaa hivi ni
kwa ajili ya Ujenzi wa Chuo Cha Afya Nzega (kitakachoitwa International
Institute for Health Tabora), ambacho nilikianza kwa fedha zangu mpaka
pale kilipofikia na sasa tunasubiria majibu ya benki ya maombi yetu ya
mkopo ndipo tuendelee. Na msamaha huo upo na hautotumika kwa mambo
mengine ya binafsi kama nilivyoeleza hapo juu kwenye ununuzi wa gari
langu binafsi la kutembelea na ujenzi wa nyumba yangu binafsi ya kuishi
Nzega, Tabora ama Dar es salaam (ambako ninajenga).
Watanzania
tuache kushabikia uongo. Kufanya hivyo kunaziba mianya ya ukweli
kutamalaki. Tuache kutazama mambo kwa macho ya wivu, husda na majungu.
Tusimame kwenye misingi ya ukweli daima. Nchi hii itaendelezwa na watu
wenye kuchukua maamuzi thabiti na hatua za maksudi za kuleta mabadiliko –
kama miradi ya namna hii (ya chuo cha afya Nzega kule!).
Nchi
yetu bado ina watu waaminifu na waadilifu na tunaamini tutafanikiwa
kuwadhibiti walio waovu. Hata siku moja kweli haijawahi kushindwa vita
na uongo. Si kila mtu aliyeko kwenye uongozi ndani ya CCM basi ni
fisadi, watu wazuri na wasafi wapo pia. Tusimuangalie kila mtu kwa sura
ya ‘ufisadi’ na ‘ubadhirifu’ tu! Tuaminiane jamani. Tusifedheheshane na
kukatishana tamaa. Safari kuelekea mapinduzi ya maisha ya watanzania
kiuchumi na kijamii bado ni ndefu lakini tutafika. Tufanyeni kazi.
Taarifa hii nimeiandika na kuitoa mimi mwenyewe, Hamisi Andrea
Kigwangalla, M.D., Mbunge, Jimbo la Nzega. (simu yangu ya kiganjani ni
0782636963 na email yangu ni hkigwangalla@gmail.com, website: www.hamisikigwangalla.com )
0 Weka maoni yako hapa:
Post a Comment
COMMENT HAPA