CUF YATOA MAELEZO KUHUSU PESA ZA RUZUKU {CUF HAIHUSIKI KATIKA HOJA YA VYAMA KUTOWASILISHA HESABU ZAKE OFISI YA MKAGUZI MKUU WA SERIKALI.}
Chama
Cha Wananchi CUF kinapenda kuwajulisha watanzania kwa ujumla kuwa,
kimetekeleza sheria mbalimbali ambazo zinataka vyama vya siasa vipeleke
hesabu zake ili zikaguliwe na vyombo maalum vya serikali.
Kwa
mujibu wa sheria ya vyama vya siasa kifungu cha 14, vyama vilivyo na
usajili wa kudumu vinatakiwa kuwasilisha kwa msajili wa vyama vya siasa
hesabu za kila mwaka zilizokaguliwa na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za
serikali(CAG). Sheria hii ina maana kuwa kwa CAG vyama vinapita kama
PROCESS na kwamba kwa MSAJILI ndipo hasa vyama vinapaswa kupeleka ripoti
ya hesabu zilizokaguliwa na CAG.
Hiyo ina maana kuwa vyama
sasa vinawasilisha hesabu zisizokaguliwa kwa CAG na CAG ambaye ni ofisi
ya serikali ana jukumu la kufanya ukaguzi mpana zaidi mpaka ajiridhishe
na hiki ndicho CUF imekuwa ikitekeleza.
Hesabu za mwisho ambazo
CUF imeziwasilisha kwa MKAGUZI MKUU WA SERIKALI ni zinazoishia tarehe
31/12/2011 ambapo ziliwasilishwa tarehe 11/09/2012 kupitia barua yenye
kumbukumbu namba CUF/AK/DSM/KM/OO3/1A/2012/39 iliyosainiwa na MKURUGENZI
WA FEDHA WA CUF ndugu. Salim Mandari iliyokuwa na kichwa cha habari
“KUWASILISHA HESABU ZISIZOKAGULIWA KWAKO KWA AJILI YA UKAGUZI HESABU
ZINAZOISHIA 31/12/2011”.
Hatua hii ilitokana na kutekeleza
sheria pamoja na maelekezo ya barua ya msajili wa vyama vya siasa
iliyokuwa na kumbukumbu namba CDA.112/123/01A/37 ambayo ilimtaka Katibu
Mkuu wa chama chetu awasilishe hesabu zisizokaguliwa kwa Mkaguzi Mkuu wa
Hesabu za serikali kama hatua ya MSAJILI kukimbusha chama.
Tumesikitishwa na kauli tulizozisikia kupitia katika vyombo vya habari
kuwa chama chetu ni miongoni mwa vyama kadhaa ambavyo havijawasilisha
hesabu kwa mkaguzi mkuu wa serikali kwa kipindi cha miaka minne sasa.
Tunaomba watanzania wazipuuze taarifa hizo kutuhusu kwa sababu hazina
ukweli wowote.
Chama Cha Wananchi CUF pia kinapenda kuujulisha
umma kuwa hesabu zake ambazo hazijawasilishwa kwa Mkaguzi Mkuu wa hesabu
za serikali ni zile zinazoishia tarehe 31/12/2012 ambazo wakaguzi wa
ndani na wa nje wamemaliza kuzikagua mwezi Julai mwaka 2013 na
zitathibitishwa na kikao cha Kamati ya Utendaji ya Taifa cha mwezi
Oktoba 2013 na Baraza Kuu la Uongozi la Taifa litakalokaa mwezi Novemba
2013 na kisha zitawasilisha kwa CAG kabla ya mwezi Desemba 2013. Hii ina
maana kuwa hesabu ambazo hazijamfikia msajili ni za mwaka mmoja
uliopita na siyo miaka minne kama ambavyo kamati ya PAC imetangaza.
Chama chetu kimesikitishwa na kufadhaishwa na hatua ya kamati
kuvihukumu vyama vyote vya siasa wakati jambo hili ni la chama kimoja
kimoja. Na mbaya zaidi ni pale ambapo mwenyekiti wa kamati ya PAC mhe.
Zitto Kabwe amekuwa akishinda kwenye mitandao ya kijamii “akishupalia”
kuvichukulia hatua vyama – kikiwemo chama chetu huku hana taarifa za
kina za namna tulivyotekeleza wajibu wetu.
Ikiwa kamati ya
bunge inashinda kwenye mitandao ya kijamii ikihukumu na kutoa taarifa za
uongo kwa umma bila hata kuwasiliana na vyama vya siasa ni jambo la
kufedhehesha mno. Kamati makini ya bunge ni ile ambayo inapokea taarifa
kutoka pande zote muhimu, inakutana na wadau wote na kisha inajua tatizo
liko wapi na kuujulisha umma nani amesababisha uzembe.
Kwa
sababu kamati hii imeligeuza jambo hili kuwa mtaji wa kisiasa na
kukitangaza chama chetu kuwa hakikutambua wajibu wake jambo ambalo siyo
sahihi, Chama chetu kinatafakari hatua za kuchukua ikiwemo kumuandikia
Spika ili azifundishe kamati zake namna bora ya kufanya kazi zake kama
kamati za umma.
Chama chetu pia hadi leo hakijapokea barua
yoyote ya kuitwa na kamati ya bunge ya hesabu za serikali siku ya tarehe
25 Oktoba. Kwa hiyo, CUF haitahudhuria katika kikao hicho kwa habari za
kuitiwa kupitia kwenye FACEBOOK, TWITTER, WHATS UP n.k.
Kama
kamati inatuhitaji twende kuifafanulia taarifa za upande wa pili baada
ya kumaliza kazi yake ya kutuchafua, na ituandikie barua rasmi ya
kutuita tarehe 25, tukipata barua tutakwenda. Ikiwa hatuitwi tarehe hiyo
kwa barua rasmi hatutakwenda na kamati ya PAC haitakuwa na "LOCUS
STAND" ya kutuhoji mahali popote pale.
Tunapenda watanzania
waelewe kuwa chama chetu kimekuwa pekee ambacho kimepata hati safi za
ukaguzi wa fedha kila mara tangu kuanzishwa kwa mfumo wa vyama vingi na
hatukuwahi kupata doa wala kashfa katika masuala ya fedha.
Mungu Ibariki Tanzania!
“HAKI SAWA KWA WOTE”
Julius Mtatiro,
Naibu Katibu Mkuu,
Chama Cha Wananchi CUF – Tanzania Bara.
0 Weka maoni yako hapa:
Post a Comment
COMMENT HAPA