LIPUMBA ASHAURI TANZANIA TUJIPANGE KUIMARISHA UCHUMI WETU NDANI YA JUMUIYA YA AFRIKA MSHARIKI.
THE CIVIC UNITED FRONT - CUF,
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI - Na. Prof Ibrahim Lipumba,
TAREHE 10/11/2013
TANZANIA TUJIPANGE KUIMARISHA UCHUMI WETU NDANI YA JUMUIYA YA AFRIKA MSHARIKI.
Tarehe 7 Novemba 2013 Rais Kikwete alilihutubia Bunge la Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania. Madhumuni makubwa ya hotuba hiyo ilikuwa kuelezea
msimamo wa Tanzania kuhusu Jumuiya ya Afrika Mashariki baada ya Kenya,
Uganda na Rwanda kukutana mara tatu bila kuihusisha Tanzania. Katika
mikutano ya viongozi wakuu wa nchi hizo ambayo iliishirikisha Sudan ya
Kusini walijadili na kufikia maazimio kuhusu mambo ambayo kimsingi na
kiitifaki yanapaswa kujadiliwa katika vikao vya Jumuiya ya Afrika
Mashariki.
CUF – Chama Cha Wananchi kinaunga mkono msimamo wa
Rais Kikwete kuwa pamoja na vitimbi vilivyofanywa na Kenya, Uganda na
Rwanda dhidi ya Tanzania na Burundi, Tanzania haitajitoa na wala
haitakuwa chanzo cha kuvunjika kwa Jumuiya ya Afrika Mashariki. CUF
inalaani vikali vitimbi vya kuitenga Tanzania vilivyofanywa na Kenya,
Uganda na Rwanda. Tunatoa wito kwa Watanzania wote kushikamana kwa
dhati, kujenga umoja wa kitaifa, kujenga na kuimarisha miundombinu ya
nchi yetu na kuongeza ushindani wetu wa kiuchumi ndani ya Jumuiya ya
Afrika Mashariki na Ulimwengu kwa ujumla.
Tarehe 24-25 Juni
2013, siku chache kabla Rais Obama hajatua Dar es Salaam, Marais wa
Kenya, Rwanda na Uganda walikutana kuimarisha uhusiano wao wa kibiashara
na kurahisisha usafiri baina ya nchi hizo tatu. Kwa kawaida masuala
haya ya kuimarisha biashara na usafiri baina ya nchi za Jumuiya ya
Afrika Mashariki huzungumzwa kwa pamoja na nchi zote wanachama wa
Jumuiya hii. Inaelekea Kenya, Rwanda na Uganda wameamua kuwaacha kando
Tanzania na Burundi.
Mimi nilidhani ziara ya Rais Obama
Tanzania ilielekea kutowafurahisha baadhi ya jirani zetu ambao
wangependa Rais Obama atembelee nchi zao badala ya Tanzania. Kenya
walisusia Mkutano wa Rais Obama na Wafanyabiashara wa Africa (Business
Leaders Forum) ambao uliandaliwa na Corporate Council on Africa.
Uhusiano kati ya Rwanda na Tanzania umezorota baada ya Rais Kikwete
kuwapa ushauri viongozi wenzake katika kikao cha Umoja wa Afrika, Addis
Ababa kuwa njia muhimu ya kumaliza migogoro ya kisiasa na kiusalama na
kuleta amani katika Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo ni kwa nchi jirani
za Kongo, ikiwemo Rwanda na Uganda ni kuzungumza na kufikia muafaka wa
kisiasa na mahasimu na waasi wao waliokimbilia Kongo. Ushauri wa Rais
Kikwete umetafsiriwa visivyo nchini Rwanda na kusababisha kuzorota kwa
uhusiano kati ya nchi zetu mbili.
Wachambuzi wa mambo ya
uhusiano wa kimataifa wanaamini ushauri wa Rais Kikwete umechukuliwa
kama kisingiziyo. Tatizo kubwa ni Tanzania kukubali kupeleka wanajeshi
wake Kongo kama sehemu ya Jeshi la Umoja wa Mataifa la kuleta amani
Mashariki ya Kongo. Wanajeshi wetu ndani ya Brigedi Maalum ya Jeshi la
Umoja wa Mataifa Kongo (MONUSCO) inayoongozwa na Brigedia Jenerali James
Aloisi Mwakibolwa wa JWTZ imefanya kazi nzuri na kufanikisha kulisaidia
Jeshi la Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo kulisambaratisha jeshi la
waasi la M23 ambao viongozi wake wa juu wamekimbilia Uganda.
Tarehe 28 Agosti, 2013 viongozi wa Kenya, Uganda na Rwanda walikutana
mjini Mombasa, Kenya ambapo walishiriki katika sherehe maalum ya Rais
Kenyatta kuzindua gati jipya la kuegesha meli ili ziweze kupakuliwa kwa
haraka na kuongeza ufanisi. Lengo la Mamlaka ya Bandari ya Kenya ni
kuifanya Mombasa kuwa bandari inayoongoza kwa kuhudumia siyo tu Kenya,
bali Tanzania ya Kaskazini, Uganda, Rwanda, Burundi, Kongo, Sudan ya
Kusini, Ethiopia na Somalia.
Mkutano wa tatu wa Marais wa
Kenya, Uganda na Rwanda ulifanyika tarehe 28 Oktoba, 2013 mjini Kigali,
Rwanda. Rais Kikwete ameeleza kuwa Mambo yapatayo manane ya msingi
yaliyoamuliwa kufanywa na nchi hizo;
(1) Kujenga reli ya kisasa kutoka Mombasa hadi Kampala, Kigali na Bujumbura.
(2) Ujenzi wa Bomba la Mafuta la kutoka Kenya hadi Uganda na Sudani ya Kusini.
(3) Kujenga Kiwanda cha kusafisha mafuta nchini Uganda.
(4) Kuanzisha Himaya Moja ya Ushuru wa Forodha wa Jumuiya ya Afrika Mashariki na kutekeleza vipengele vyote;
(5) Kuharakisha Shirikisho la Afrika Mashariki na kwamba itaundwa Kamati ya kuandaa rasimu ya Katiba ya Shirikisho.
(6) Kuharakisha uanzishwaji wa Visa ya pamoja ya Utalii ya Jumuiya ya
Afrika Mashariki (Single East African Community Tourist Visa);
(7) Kuandaa utaratibu wa kutumia vitambulisho vya taifa kama hati ya kusafiria katika nchi zao; na
(8) Kuongeza uzalishaji na usambazaji wa umeme.
Katika mambo haya manane, manne yanatawaliwa na itifaki ya Jumuiya ya Afrika Mashariki.
Mambo hayo manne ni Kuanzisha Himaya Moja ya Ushuru wa Forodha wa
Jumuiya ya Afrika Mashariki na kutekeleza vipengele vyote, Kuharakisha
Shirikisho la Afrika Mashariki, Kuharakisha uanzishwaji wa Visa ya
pamoja ya Utalii ya Jumuiya ya Afrika Mashariki, Kuandaa utaratibu wa
kutumia vitambulisho vya taifa kama hati ya kusafiria.
Katika
haya manne Rais alieleza kuwa mawili yalifanyiwa uamuzi wa pamoja na
hana matatizo nayo. “Mambo hayo ni matumizi ya vitambulisho vya taifa
kama hati ya kusafiria na Visa ya Pamoja ya Utalii kwani tuliamua kwa
pamoja kuwa nchi wanachama zilizokuwa tayari waanze.”
Katika
masuala ya kuanzishwa kwa Himaya Moja ya Ushuru wa Forodha (Single
Customs Territory) na Shirikisho la Afrika Mashariki Kenya, Uganda na
Rwanda wamekiuka uamuzi wa pamoja wa Jumuiya ya Afrika Mashariki.
Rais alieleza “Katika Mkutano Maalum wa 11 wa Wakuu wa Nchi wanachama
uliofanyika tarehe 28 Aprili, 2012 Jijini Arusha, tulipokea na kuridhia
mapendekezo ya kuanzisha Himaya Moja ya Ushuru wa Forodha (Single
Customs Territory).
Kwa mujibu wa mapendekezo hayo kila nchi
mwanachama itasimamia shughuli zake za kiforodha na kukusanya mapato
yake kama ilivyo sasa. Hata hivyo, kwa bidhaa zinazopitia nchi moja
kwenda nchi nyingine mwanachama, ukaguzi na ukusanyaji wa mapato
utafanyika katika kituo cha kwanza bidhaa hizo zinapoingilia.
Mapato hayo yatawasilishwa kwa nchi husika baada ya kuthibitisha kuwa
bidhaa zilivuka mpaka. Wakuu wa Nchi waliagiza Baraza la Mawaziri kuunda
Kikosi Kazi cha kujadiliana na kuandaa utaratibu wa utekelezaji wa
mfumo huo.
Taarifa ya kikosi kazi inatakiwa kutolewa katika
Mkutano wa 15 wa Wakuu wa Nchi utakaofanyika Kampala, Uganda tarehe 30
Novemba, 2013. Kabla hata ya kupokea taarifa ya kikosi kazi, Kenya,
Uganda na Rwanda wameamua kutekeleza Single Customs Territory nje ya
taratibu za Jumuiya ya Afrika Mashariki.
Mwezi Agosti Chama cha
Wasafirishaji wa Mafuta Tanzania (Tatoa) kilitoa taarifa kwenye Kamati
ya Kudumu ya Bunge inayosimamia mambo ya Bajeti kuwa ifikapo Septemba
mwaka huu Rwanda na Uganda watasitisha kutumia bandari ya Dar es Salaam
kupitisha mizigo yao. Serikali ilikanusha taarifa lakini inaonekana kuwa
Rwanda na Uganda wameamua kuwa watasita kutumia bandari ya Dar es
Salaam na kwa hiyo wanaweza kuanzisha taratibu za Single Customs
Territory na Kenya bila kuishirikisha Tanzania.
Taarifa kuhusu
Rwanda na Uganda, kutotumia Bandari ya Dar es Salaam lisitazamwe
kisiasa. Bandari ya Dar es Salaam ina udhaifu mkubwa unaolalamikiwa na
wafanyabiashara wa ndani na nje ya nchi. Siyo Rwanda na Uganda tu ndiyo
wanaoilalamikia bandari ya Dar es Salaam, bali Kongo, Zambia na Malawi
pia wanalalamika.
Bandari ya Dar es Salaam ina sifa ya
ucheleweshaji wa kupakua shehena za mizigo toka kwenye meli, wizi wa
mizigo, yakiwamo makontena na vifaa vya magari kama vile taa na redio;
uchakachuaji wa mafuta; urasimu na ucheleweshaji wa mizigo kutoka
bandarini; ukubwa wa tozo za bandari na barabara; na ugumu wa magari ya
mizigo kufika na kutoka bandarini, taratibu za kutoaa mizigo
zisizotabirika na rushwa bandarini na barabarani.
Asilimia 90 ya biashara yote ya Tanzania na nchi za nje inapita katika bandari ya Dar es Salaam.
Nchi sita za jirani – Malawi, Zambia, Kongo, Burundi, Rwanda na Uganda
ambazo hazina bandari zinaitumia bandari ya Dar es Salaam. Hata hivyo
bandari ya Dar es Salaam inakabiriwa na ushindani mkubwa kutoka bandari
ya Mombasa inayofanya kazi kwa ufanisi mzuri zaidi. Bandari ya Beira
Msumbiji ina ushindani mkubwa kwa mizigo inayoenda Malawi, Zambia na
hata Kongo.
Bandari ya Dar es Salaam haifanyi kazi kwa ufanisi.
Utafiti wa Benki ya Dunia unaonyesha kuwa, ikiwa bandari ya Dar es
Salaam itafanya kazi kwa ufanisi kama bandari ya Mombasa, pato la taifa
la Tanzania litaongezeka kwa dola bilioni 1.8 kila mwaka sawa na
asilimia 7 ya pato la taifa la sasa. Nchi jirani zinazotumia bandari ya
Dar es Salaam zitaongeza mapato yao kwa dola milioni 800. Utendaji mbovu
wa bandari zetu unatokana na ombwe la uongozi, ufisadi na menejimenti
mbovu.
Tanzania inaweza kukuza uchumi wake kwa asilimia 10 kila
mwaka na kuongeza ajira kwa wingi ikiwa itatumia fursa za jiografia
zikiwemo bandari zake kuwa kituo cha usafirishaji, viwanda na biashara
kwa nchi sita zinazopakana na Tanzania na ambazo hazina bandari.
Serikali inaelewa wazi utendaji wa bandari ya Dar es Salaam ni mbovu na
hauridhishi. Hata hivyo, kwa sababu ya ombwe la uongozi, serikali
inasuasua kufanya mabadiliko yanayohitajika kuongeza tija na ufanisi wa
bandari ya Dar es Salaam.
Uzembe wa utendaji wa bandari ya Dar
es Salaam unasababisha msongamano wa meli zenye mizigo ya kushusha
bandarini. Ukisafiri kwa ndege kati ya Zanzibar na Dar es Salaam unaweza
kuhesabu meli zaidi ya ishirini zilizoweka nanga zikisubiri kupewa
ruhusa ya kwenda gatini kushusha mizigo. Katika mwaka 2012 muda wa meli
kusubiri kupata gati la kushushia mizigo bandari ya Dar es Salaam
ilikuwa siku 10 ukilinganisha na chini ya siku moja bandari ya Mombasa.
Hata baada ya makontena kupakuliwa inachukua muda mrefu – wastani wa
siku 10 au zaidi kushusha mizigo na kupata kibali cha kuisafirisha toka
bandarini.
Ukilinganisha na bandari ya Mombasa gharama za
bandari ya Dar es Salaam ni za juu kwa asilimia 22 kwa kila kontena.
Gharama za tozo na ushuru mbalimbali za bandari ya Dar es Salaam ni za
juu kwa asilimia 74 ukilinganisha na bandari ya Mombasa. Kwa kila dola
100 za gharama ya kushusha mizigo Mombasa, gharama ya kushusha mizigo
hiyo hiyo Dar es Salaam ni dola 174. Katika hali hii tusistaajabu nchi
jirani kuikimbia bandari ya Dar es Salaam.
Utendaji wa Shirika
la Reli umeporomoka sana. Shirika la Reli lilisafirisha mizigo ya tani
154,000 mwaka 2012 ukilinganisha na tani 1,446,000 mwaka 2002. Kuanguka
kwa shirika la reli pia kunachangia uharibifu mkubwa wa barabara kwani
mizigo mizito inayostahiki kusafirishwa kwa garimoshi inasafirishwa kwa
malori yenye uzito zaidi ya viwango vya barabara. Ikiwa reli ya kati
itafanya kazi kwa ufanisi na tija ya hali ya juu. Nchi za Kongo,
Burundi, Rwanda na Uganda wanaweza kutumia reli ya kati kusafirisha
mizigo yao kwenda na kutoka Dar es Salaam.
Reli ya TAZARA
haijatumiwa kwa kadri ya uwezo wake. TAZARA ilisafirisha mizigo ya tani
259,000 mwaka 2012 ukilinganisha na tani 677,000 mwaka 2002. Kwa kawaida
usafiri wa reli ni wa gharama za chini ukilinganisha na usafiri wa
barabara. Tuna wajibu wa kuimarisha utendaji wa Shirika la Reli na
TAZARA ili kuongeza ushindani wa kibiashara na kukuza uchumi wetu.
Kuhusu Shirikisho la Kisiasa la Afrika Mashariki Rais alieleza kuwa
“Katika Mkutano wa 14 wa Wakuu wa Nchi wanachama uliofanyika tarehe 30
Novemba, 2012, Nairobi, tulipokea taarifa ya hatua iliyofikiwa kuhusu
mchakato wa kutaka kuanzishwa kwa Shirikisho. Mkutano huo uliagiza
nchi wanachama kujadiliana zaidi kuhusu mpango kazi wa kufikia
Shirikisho la Kisiasa na mpango wa kutekeleza mapendekezo mengine
yaliyotolewa na Timu ya Wataalamu. Inategemewa kuwa Baraza la Mawaziri
litawasilisha mapendekezo ya majadiliano hayo katika Mkutano wa 15 wa
Wakuu wa Nchi mwezi Novemba, 2013. Iweje leo wenzetu hawa waamue
kuanzisha mchakato wao wa kuharakisha Shirikisho la Afrika Mashariki.”
Rais Museveni amekuwa mstari wa mbele kuharakisha kufikia Shirikisho la
Kisiasa. Wachambuzi wa siasa za Uganda wanaamini ana lengo la kuwa Rais
wa kwanza wa Shirikisho la Afrika Mashariki. Tanzania imekuwa kikwazo
kwani Watanzania wengi wanaamini haraka haraka haina baraka. Wanataka
ushirikiano wa Afrika Mashariki ufuate hatua zilizoanishwa katika
Mkataba ulioanzisha Jumuiya ambazo ni Umoja wa Forodha, Soko la Pamoja,
Umoja wa Sarafu na Fedha, na hatimaye Shirikisho la kisiasa
litakalopigiwa kura ya maoni na kila nchi.
Katika suala la soko
la pamoja Tanzania imesita kuruhusu masuala ya ardhi, ajira na uhamiaji
yaingizwe mara moja katika soko la pamoja la Afrika Mashariki. Nchini
Kenya suala la ardhi linaendelea kuleta mvutano mkali. Ni muhimu kwa
serikali kuwa makini sana katika sera ya ardhi, wananchi wasiporwe ardhi
yao.
Hata hivyo tusiwe na wasiwasi. Shirikisho la Kisiasa la
Kenya, Uganda na Rwanda ni ndoto ya mchana. Katika karne ya 21,
shirikisho la kisiasa lazima lijikite katika mfumo wa demokrasia. Kenya
imepiga hatua kubwa katika ujenzi wa demokrasia lakini bado
hawajafanikiwa kujenga umoja wa kitaifa. Baada ya uchaguzi mkuu wa mwaka
2007 kulitokea machafuko makubwa. Zaidi ya watu elfu moja walipoteza
maisha. Maelfu walikuwa wakimbizi wa ndani. Rais Kikwete na Rais Mstaafu
Mkapa walishiriki katika kuwasuluhisha Wakenya na hatimaye kupata
serikali ya umoja wa kitaifa. Baada ya uchaguzi wa mwaka huu Uhuru
Kenyatta aliibuka kuwa mshindi wa Urais. Mpaka hivi sasa Rais Kenyatta
anasuasua kufanya ziara kamili Kenya ya magharibi.
Rwanda na
Uganda ni utawala wa kidikteta. Rais Museveni alibadilisha katiba na
kuondoa kipengere cha ukomo wa mtu mmoja kuchaguliwa kuwa Rais. Kipindi
cha mwisho cha Rais Kagame kinamalizika mwaka 2017 na tayari kuna kauli
kuwa wananchi wa Rwanda wanataka aendelee kuwa Rais baada ya 2017.
Kitendo cha kuvunja taratibu na itifaki ya Jumuiya ya Afrika Mashariki
kinaonesha wazi kuwa viongozi hawa hawaaminiki. Ikiwa hawakuheshimu
makubaliano ndani ya Jumuiya ya Afrika Mashariki wanaweza pia baadhi yao
wasiheshimu makubaliano baina yao.
CHANGAMOTO KWA TANZANIA
1. Tujenge umoja wa kitaifa wa dhati unaojikita katika kuheshimu hakimu
na kujenga misingi imara ya demokrasia. Tuendelee kuhakikisha mchakato
wa kupata katiba mpya unakuwa shirikishi.
2. Tuimarishe miundombinu na ushindani wa kiuchumi wa Tanzania
3. Tujenge uchumi unaotumia vizuri raslimali za nchi na ukuaji wa uchumi unaongeza ajira na kuwanufaisha wananchi wote.
5. Tuimarishe vyombo vyetu vya ulinzi na usalama viwe na maadili ya juu
na vifanye kazi kwa weledi. Tusipuuze uwezekano wa jirani zetu kula
njama kutuhujumu
6. Katika kikao cha Viongozi Wakuu wa Afrika
Mashariki, Rais Kikwete awaondolee uvivu wenzake na kuwaeleza bayana
mambo wanayofanya hayakubaliki na yanadhoofisha Jumuiya ya Afrika
Mashariki
Ibrahim Haruna Lipumba
Mwenyekiti,
Jumapili, 10 Novemba 2013.
Dar Es Salaam.
0 Weka maoni yako hapa:
Post a Comment
COMMENT HAPA