TAMKO rasmi la Ndugu Zitto Z. KABWE (MB) kuhusiana na kinachoitwa "Taarifa ya Siri ya Chadema"
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
TAMKO rasmi la Ndugu Zitto Z. KABWE (MB) kuhusiana na kinachoitwa "Taarifa ya Siri ya Chadema"
Ndugu Wanahabari,
NILIPOKUWA katika ziara ya bara la Ulaya kati ya Oktoba 21 mpaka
Novemba 2 mwaka huu (2013), nilipokea kwa njia ya barua pepe ripoti
inayoitwa "Taarifa ya Siri ya Chadema" ambayo pia ilikuwa imesambazwa
katika mitandao mbalimbali ya kijamii.
“Taarifa ya
Chadema inasema kwamba chama hicho (chama changu) kilikuwa kimechunguza
mwenendo wangu tangu mwaka 2008 hadi 2010 na kubaini kuwa mimi napokea
fedha kutoka Chama Cha Mapinduzi (CCM) ili kuivuruga Chadema.
Ripoti hiyo ilinihusisha pia na mwananchi raia wa Ujerumani, Andrea
Cordes ambaye, kwa mujibu wa ripoti hiyo, alinisaidia kupokea na
kuhifadhi kiasi cha dola 250,000 za Marekani kupitia kwenye akaunti yake
binafsi.
Taarifa hii ya kutunga na iliyojaa uongo wa kiwango cha kutisha, imenifadhaisha, kunisikitisha na kunikasirisha.
Taarifa hii iliibuliwa katika kipindi ambacho nilikuwa safarini kutetea
haki za Watanzania na Waafrika ambao utajiri wao wa rasilimali
unafaidiwa na watu wachache waliohifadhi mali katika nje za nje na pia
kupigania makampuni ya mataifa tajiri yalipe kodi stahiki katika nchi
zetu.
Pengine lengo la ripoti hiyo lilikuwa ni kutaka
kunipoteza kutoka katika nia na dhamira yangu ya dhati ya kutaka
Watanzania wafaidike na utajiri wao. Muda ambao watunzi wa ripoti hiyo
waliamua kutoa taarifa yao unazua maswali mengi kuliko majibu.
Nafahamu kwamba mimi ni mwanasiasa ambaye nimekuwa mlengwa (target) wa
mashambulizi kutoka kwa makundi mbalimbali ya wanasiasa na vikundi vyao.
Kama mwanasiasa, niko tayari kupokea changamoto zozote zinazokuja na
uanasiasa wangu.
Hata hivyo, ambacho sitakubali ni kwa watu
kutumia jina langu na uanasiasa wangu kunichafua mimi binafsi na watu
wengine wasiohusika kwa sababu ya kutaka kutimiza malengo yao ya
kidhalimu.
Raia huyo wa Kijerumani tayari amekana kuhifadhi
fedha zangu. Kwa maelezo yake kwa baadhi ya viongozi wa Chadema amekana
kuwa na akaunti inayotajwa na amekana pia kuwepo nchini Ujerumani katika
siku na wakati uliotajwa kwenye ripoti hiyo.
Ripoti hiyo
imemtaja pia mtu kama Dk. Charles Kimei, Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya
CRDB ikidai kwamba nilikutana naye na alishiriki kwenye igizo hilo la
kunipa fedha.
Niseme mapema kwamba tangu kuzaliwa kwangu
sijawahi hata mara moja kukutana na Dk. Kimei popote pale ndani au nje
ya nchi. Kumuingiza mtu ambaye amejenga jina lake kwenye taaluma ya
kibenki kwa sababu tu ya lengo ovu la kumchafua Zitto Zuberi Kabwe si
uungwana bali ni unyama.
Kutokana na uchafuzi huu wa wazi dhidi
ya taswira yangu binafsi na watu wengine walioingizwa kwenye mkumbo
huu, nimeandika rasmi kwa Katibu Mkuu wa Chadema, Dk.Wilbrod Slaa
kumwomba athibitishe kwamba kinachoitwa Taarifa ya Siri ya Chadema ni
kweli ni taarifa ya chama au kiikanushe ili niweze kuchukua hatua za
kisheria dhidi ya waandishi wa hekaya hiyo.
Cha ajabu,
nimepokea ujumbe wa kutishiwa maisha kutoka kwa mtu anayejiita Theo
Mutahaba na kuahidiwa KUPOTEZWA endapo nitaendelea na jitihada zangu za
kupambana na ufisadi na kutafuta haki kwa Watanzania wote pasipo kujali
tofauti zao za kiitikadi, kikanda, kikabila na kidini.
Natarajia kuchukua hatua kali za kisheria dhidi ya wote ambao wamehusika
na utungaji na uenezi wa taarifa hii. Nitahakikisha kwamba wahusika
wanatafutwa na kufunguliwa mashitaka stahiki ya upotoshaji na
kuchafuana.
Ni matarajio yangu kwamba wale wenye mapenzi mema
na Tanzania, mimi binafsi na utawala wa sheria, wataelewa nia yangu ya
kutafuta haki katika suala hili.
Nimeamua kujitolea maisha
yangu kwa ajili ya Watanzania na kama alivyopata kusema Rais Mstaafu wa
Afrika Kusini, Nelson Mandela; “Struggle Is My Life.”
Forward Ever, Backward Never- Kwame Nkrumah
Zitto Kabwe (Mb)
10/11/2013
0 Weka maoni yako hapa:
Post a Comment
COMMENT HAPA