Dr. Kitila Mkumbo( Mjumbe kamati kuu chadema) atoa Tamko
Kufuatia
taarifa zinazosambazwa kwenye mitandao ya kijamii kuhusu kuhongwa kwa
Zitto naye kuhonga watu wengine, nikiwemo mimi, ili kutoa siri za chama
chetu (CHADEMA) kwa lengo ya kukivuraga watu, wengi sana wameniandikia
email, sms na hapa fb ili nitoe ufafanuzi kuhusu ukweli wa mimi kuhongwa
na Zitto na mahusiano yangu na mwanasiasa huyu nguli. Mwanzoni
nilipuuzia na sikutaka kabisa nitoe maoni kuhusu jambo hili kutokana na
kiwango cha ujinga kilichomo ndani ya waraka huo unaosambazwa. Hata
hivyo kwa kuwa watu wengi wamenitaka nitoe ufafanuzi, napenda kueleza
haya yafuatayo:
i)
Mimi Kitila Mkumbo, pamoja na umaskini wangu, sijawahi kuhongwa popote
na sitarajii kuhongwa. Taarifa zinazosambazwa juu yangu ni za uwongo wa
kijinga na uzushi wa kitoto kwa malengo ya siasa nyepesi. Ni wazi kwamba
wanaosambaza habari chafu juu yangu hawanijui na ndiyo maana wanaweza
kudiriki kuzusha kwamba mie Kitila Mkumbo naweza kuhongwa sh. 200,000/=.
Hakuna namna nyingine ya kuthibitisha kwamba waraka huu na maudhui yake
ni mambo ya kutunga zaidi ya hilo la kuzusha kwamba nami ni miongoni
mwa watu waliohongwa.
ii)
Kuhusu mahusiano yangu na Zitto ni kwamba kijana huyu ni rafiki yangu
wa miaka mingi tuliyejuana na kuanza urafiki kabla ya hata mie kuijua
CHADEMA. Urafiki wetu ulikuwepo, upo na utaendelea kuwepo ndani na/au
nje ya siasa. Wasiopenda hili poleni sana. Mie ni mtu mzima na hakuna
mtu yeyote mwenye uwezo wa kunichagulia marafiki na/au maadui.
iii)
Wanaosambaza waraka huu ni watu woga wa demokrasia na wasioijua
CHADEMA. Chama hiki kimejipambanua kwa miaka mingi kwamba ni chama
kinachopigania demokrasia ndani na nje ya chama. Matatizo yetu
hushughulikiwa kikamilifu ndani ya vikao ambapo huwa tunajadili mambo
kwa upana. Watu wenye makosa husutwa, huonywa na ikibidi huadhibiwa.
Kama kweli haya yanayosambazwa yangekuwa na hata chembe ya ukweli, na
kama kweli waraka huu umetoka makao makuu ya chama, sioni ni kwa nini
jambo hili zito kiasi hiki haliletwi kwenye vikao vya chama na sisi
tunaotuhumiwa kukivuruga chama tushughulikiwe kwa mujibu wa taratibu
kama ambavyo watu wengi wamewahi kushughulikiwa ndani ya chama chetu kwa
makosa waliyotenda.
iv)
Ni vizuri tukajenga utamaduni wa kuhoji mambo badala ya kuyameza kana
kwamba tunasoma msaafu. Hivi huyo mtu anayemhonga Zitto bilioni mbili
(2,000,000,000) ili atoe siri za chama, ni siri gani hizo ambacho chama
cha siasa kinazo ambazo ni za hatari hata itolewe hongo kama hiyo?
v)
Ninasikitishwa na idara ya uenezi wa chama chetu kukaa kimya bila kutoa
maelezo juu ya jambo hili, hasa pale ambapo tumeambiwa waraka huu
umetoka makao makuu. Hii si kawaida kwa idara yetu hii nyeti
iliyosheheni watu mahiri. Mara zote huwa wepesi kabisa kwa vijana wetu
katika idara hii kutoa ufafanuzi, tena kwa mambo mepesi kabisa
yanayokigusa chama, vipi makamanda kwenye jambo hili imekuwaje?
v)
Mwisho kama kuna watu walidhani kwamba kwa uzushi huu watanikatisha
tamaa na kunirudisha nyuma katika kutoa mchango wangu wa kuimarisha
siasa ya vyama vingi hapa nchini, na kuijenga CHADEMA kama chama mbadala
imara wamekosea. Nipo imara na nitaendelea kutoa mchango wangu
kikamilifu. Poleni sana wote mliokwazwa na jambo na ufafanuzi wangu ndio
huo.
0 Weka maoni yako hapa:
Post a Comment
COMMENT HAPA