Mar 26, 2012

MAJAMBAZI YAUA POLISI,YAPORA SMG MGODINI BARRICK GOLD

WATU wanaosadikiwa kuwa majambazi wenye silaha wamemuua polisi aliyekuwa akilinda mgodi wa dhahabu wa Tulawaka unaomilikiwa na Kampuni ya Barrick wilayani Biharamulo Mkoani Kagera na kutoweka na bunduki aina ya SMG yenye risasi 46 aliyokua akitumia polisi huyo.
Kamanda wa Polisi (RPC) Kagera,Henry Salewi
Habari zilizopatikana na kuthibitishwa na polisi, zimemtaja polisi aliyeuwawa kuwa ni PC Dickson mwenye namba G2626 ambaye aliyeuwawa Ijumaa Machi 23, 2012 akiwa katika lindo lake katika ukuta wa mgodi huo.
Kamanda wa Polisi mkoani Kagera, Henry Salewi amethibitishia FikraPevu kifo cha PC Dickson ambaye alikuwa lindoni na polisi wenzake wanne waliopelekwa katika mgodi huo kukabiliana na wahalifu wenye nia ya kuingia mgodini na kupora dhahabu na kuongeza kwamba mwili wa marehemu uligunduliwa na wenzake baada ya tukio hilo.
“Mwili wake uligundulika jioni na askali wenzake. Walikuta amepigwa na chuma cha kuchimbia madini kilichomtoboa kichwa mara nne,h awa walikuwa na nia ya kumuua na kuchukua bunduki,”alisema Kamanda Salewi
Pia alisema bunduki iliyoporwa ni SMG iliyokuwa na risasi 46 na kuwa polisi hao kila siku huenda kulinda ukuta wa mgodi huo asubuhi na kurudi jioni mbapo maeneo ya mgodi huo yamezungukwa na mapori makubwa ambayo hutumiwa na wahalifu.

Mwili wa polisi huyoi huyo aliyekuwa na umri wa miaka 29 utasafirishwa leo kwenda nyumbani kwao wilaya ya Sumbawanga mkoani Rukwa. Marehemu PC Dickson ameacha mke.

Kamanda Salewi amesema polisi wanaendelea na msako mkali wilayani humo ili kuwabaini wahalifu hao.

Mauaji hayo yametokea katika wiki ile ile ambayo wachimbaji wawili wa madini ya dhahabu wilayani Chato wakiuwawa kwa kuchomwa moto na wachimbaji wenzao baada ya kuwatuhumu kujihusisha na vitendo vya uhalifu.

Sehemu ya mgodi wa dhahabu wa Tulawaka unaomilikiwa na Barrick Gold

Wachimbaji wadogo katika machimbo ya Mataba katika tukio la Marchi 19, waliwateketeza kwa moto Jumanne William (35) na Juma Magesse (40)kwa tuhuma za uhalifu.

Akifafanua tukio hilo Salewi alisema kuwa wachimbaji hao walimkamata Jumanne baada ya kumuona amevaa koti alilodaiwa kupora katika tukio la uhalifu la Februari mwaka huu ambapo baadhi ya wachimbaji waliporwa madini.

Alisema baada ya kumshuku mtuhumiwa huyo walimkamata na kumhoji na kukiri kuhusika na tukio hilo ambapo aliwapeleka kwa mtuhumiwa mwingine Juma Magesse na baada ya kuwafikisha watuhumiwa wote walipigwa na kuuwawa kisha kuchomwa moto.
Aidha Kamanda Salewi alisema watuhumiwa wanne wanashiliwa kwa mahojiano ya tukio hilo, ambapo alikemea vitendo vya wananchi kujichukulia sheria mikononi dhidi ya wahalifu na kuwataka kuwafikisha wenye vyombo vya sheria.

Katika tukio jingine Kamanda Salewi alisema ya kuwa watu wawili wilayani Karagwe wanashikiliwa baada ya kukamatwa wakiwa na silaha aina ya bastola bila ya kuwa na kibali. Alisema watuhumiwa hao walikamatwa Machi 14, 2012 wakishukiwa kwenda kufanya uhalifu katika kituo cha mafuta.

Aliwataja watuhumiwa hao kuwa ni Apoliti John (33) na Mushabe Johnbosco wote wakazi wa kijiji cha Kibingo Wilayani humo ambao walikamatwa baada ya polisi kusimamisha na kulipekua gari walilokuwa wakisafiria.

Alisema hatua hiyo ilitokana na taarifa za raia wema ambapo hakuna polisi wanaendelea na uchunguzi na taarifa za awali zinadai kuwa walikuwa wanakwenda kupora katika kituo cha mafuta cha Omugakorongo.

Habari imeandikwa na Phinias Bashaya-Kagera

0 Weka maoni yako hapa:

Post a Comment

COMMENT HAPA