VIONGOZI WA CUF TAIFA WATEKWA MTWARA
MH: PROFESA LIPUMBA
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
TAREHE 28/06/2012
KUTEKWA KWA NAIBU MKURUGENZI WA OGANAIZESHENI UCHAGUZI NA BUNGE WA
CHAMA CHA WANANCHI CUF TAIFA MHE. SHAWEJI MKETO NA VIONGOZI WENGINE WA
CUF MKOANI MTWARA.
Juzi Jumatano tarehe 26 Juni 2013 Mkurugenzi wetu
wa Oganaizesheni Uchaguzi na Bunge mhe. Shaweji Mketo alitumwa na chama
chetu kuhudhuria kesi inayowakabili viongozi mbalimbali wa CUF katika
mahakama ya Mtwara Mjini (Kesi inayomkabili MHE.KATANI AHMAD KATANI na
wenzake).
Mhe. Mketo alipotoka mahakamani alifanya kikao na
wanachama wa CUF Mtwara mjini ambao walimueleza unyanyasaji na ukatili
mkubwa ambao wanajeshi na polisi wanawafanyia wananchi wa Mtwara.
Palitolewa ushahidi wa binti mmoja aliyenajisiwa na binti huyo aliripoti
tukio husika katika kituo cha polisi cha Msimbati kilichoko Mtwara na
binti huyo alipeleka polisi hadi ushahidi wa wa mipira ya kiume
iliyotumika kumfanyia unyama huo lakini polisi hawakuchukua hatua yoyote
hadi leo.
Mhe. Mketo na viongozi wengine waandamizi watano
walielekea maeneo ya kijiji cha Msimbati ambako binti huyo amesitiriwa
baada ya unyama huo. Mzazi wa binti aliyebakwa anajulikana kwa jina la
SELEMANI BIN OMARI. Mhe. Mketo na viongozi aliokuwa nao walifika kijiji
cha Msimbati na kukusanya ushahidi walioufuata na kisha wakakutana na
wakakutana na mwenyekiti wa kijiji cha Msimbati ambaye anatoka Chama Cha
Wananchi CUF wakafanya naye kikao kifupi na kisha wakaondoka kurejea
Mtwara Mjini.
Kati ya saa 11.30 – 12.00 jioni walifika eneo la
kilometa tatu kabla ya kuingia mjini(Eneo la njia pacha). Magari mawili
ya kijeshi moja likiwa aina ya TATA na lingine likiwa DEFENDER ya jeshi
yaliziba barabara. Ilibidi gari ya mhe. Mketo iliyokuwa ikipeperusha
bendera ya chama chetu isimame(Gari hii ni aina ya NISSAN PATROL yenye
namba T 866 BGW – Mali ya Chama Cha Wananchi CUF). Askari jeshi zaidi ya
50 waliivamia gari yetu na kuanza kuwapiga mhe. Mketo na wenzie bila
kuwajulisha chochote na kisha kuwatupa katika karandinga la jeshi kama
vile wanatupa mizigo.
Baada ya kuwateka waliwapeleka katika kambi ya
jeshi ya NALIENDERO iliyoko maeneo ya jirani na Mtwara mjini na
kuwashikilia huko tangu jana jioni hadi leo mchana.
Mimi binafsi
nilifikishiwa taarifa hizo na Mhe. Mtatiro majira ya saa 2 usiku na
nilipopewa taarifa hizo nilipiga simu za mhe. Mketo (Naibu Mkurugenzi wa
Oganaizesheni Uchaguzi na Bunge CUF taifa) na Mhe. Kulaga(Katibu wa
Wilaya) na namba zao zilikuwa zinapokelewa na wanajeshi hao huku
wakijibu matusi. Taarifa tulizonazo ni kuwa Mh. Mketo na wenzie
wanateswa na ndiyo maana simu zao zikipigwa wanajeshi hao watesaji
wanajibu matusi.
Mhe. Mtatiro alimpigia RPC wa Mtwara na RPC akajibu
kuwa yeye hana taarifa na viongozi wetu kushikiliwa na hajui wako wapi.
Tumeendelea kuwajulisha viongozi mbalimbali wa jeshi la polisi na
ulinzi juu ya tukio hili. Hivyo, pamoja na mashuhuda kuona wakipelekwa
katika kambi hiyo ya jeshi bado kama chama hatujui hasa wako wapi kwani
simu zao zinapokelewa na watekaji na watesaji wao tu.
CUF – Chama
Cha Wananchi kimesikitishwa na kufadhaishwa na kitendo hiki cha utekaji
nyara viongozi na raia wasio na hatia yoyote. Tumeumizwa zaidi kaa chama
baada ya kuona kuwa jeshi la Ulinzi la Tanzania lenye mamlaka ya
kulinda mipaka ya nchi hivi sasa limeachiwa sasa kazi ya polisi ya
kukamata raia. Pamoja na Jeshi kuachiwa kazi za polisi(JAMBO AMBALO NI
KINYUME NA SHERIA), wanajeshi hao wanatumia mamlaka hayo batili kuteka
wananchi, kuwapeleka kwenye kambi za jeshi na kuwateka kwa siku
watakazotaka. Nchi yetu inaelekea wapi? Leo Tanzania mwananchi
anakamatwa na askari Jeshi badala ya polisi! Haya mamlaka askari jeshi
wamepewa na nani na wameyatoa wapi?
Kwa mujibu wa sheria hata
ikitokea mazingira ambayo hayakwepeki kwa askari wa jeshi au vikosi
vingine kumkamata raia, ni sharti la kwanza kuwa lazima wamkamate raia
huyo bila nguvu na wamkabidhi raia huyo kwa jeshi la polisi mara moja.
Sasa iweje Mketo na wenzie wakamatwe na wanajeshi (kinyume na sheria na
bila kufanya kosa lolote) saa 11 jioni eneo ambalo ni kilometa tatu tu
kutoka kituo kikuu cha polisi Mtwara mjini na badala yake wanapelekwa
kwenye kambi ya jeshi kuhojiwa kuteswa na kushikiliwa? Leo jeshi la
ulinzi ndiyo lina kazi ya kuhoji raia?
Tunataka serikali na jeshi
viwajibike haraka iwezeikanavyo. Jeshi la Ulinzi liache mara moja
vitendo vya kinyama vya kuteka na kutesa wananchi wa Mtwara na viongozi
wa CUF na tunataka wanajeshi wamuachie mhe. Mketo na viongozi wetu mara
moja na bila masharti yoyote.
Tayari tumewasiliana na wanasheria
wetu tokea jana usiku na timu yetu ya mawakili iko Mtwara Mjini tangu
asubuhi hii kufuatilia suala hili na kuhakikisha kuwa viongozi wetu
wanapata haki.
Tunaitaka serikali isiendeleze vitendo vya namna hii
kwani vinawavunja moyo wananchi na vinawakatisha tamaa na hali hii
ikiendelea wananchi watavichukia vyombo vya ulinzi na usalama, jambo
ambalo litakuwa na mustakabali mbaya.
Tunalitaka pia jeshi la polisi
lifanyie kazi ukatili aliotendewa binti ya Selemani Omari kwa kubakwa
na askari jeshi na askari husika afuatiliwe na sheria za nchi zichukue
mkondo wake. Sambamba na hilo ,asasi za kiraia, za kisheria na za
kutetea haki za wanawake zifanye juhudi kubwa kuhakikisha kuwa wanafika
Msimbati na kukutana na binti huyu aliyebakwa ili asaidiwe kisaikolojia
kwani kitendo alichofanyiwa ni kovu la kudumu kwa maisha yake. Chama Cha
Wananchi CUF kinatoa pole kwa binti aliyebakwa na familia yake, wawe
watulivu na wasaidiane na kila mdai haki kupigania haki yao.
Aidha
tunatoa wito kwa vyombo vya habari vifanye juhudi kubwa kuweka kambi
Mtwara ili kujionea ukatili wanaofanyiwa wananchi na kuuripoti kwa
watanzania wote, wananchi wa Mtwara wasitengwe na asasi zinazoweza
kutangaza ukatili wanaofanyiwa.
Imetolewa na :-
Prof. Ibrahim Lipumba
Mwenyekiti wa CUF-Chama cha wanachi, taifa
Mh.Prof.Ibrahim Lipumba
0 Weka maoni yako hapa:
Post a Comment
COMMENT HAPA