JUMA KASEJA
VIGOGO wa Yanga walikuwa wanabishana kuhusu nani wamsainishe kati ya kipa Deo Munishi ‘Dida’ na Juma Kaseja, wakashindwa kufikia muafaka. Ngoma ikalala.
Wakaamka asubuhi, wakakaa tena, wakafikiria weee,
hawakufikia muafaka, baadaye wakapata jibu. Wakamkabidhi kipa wao namba
moja, Ally Mustapha ‘Barthez’ rungu afanye uamuzi kati ya Kaseja na Dida
nani anataka afanye naye kazi Jangwani.
Unajua alichofanya Barthez akawaambia: “Nileteeni
Dida.” Mwenyekiti wa Usajili wa Yanga, Abdallah Bin Kleb akampigia simu
Dida akakutana naye chemba juzi Alhamisi jioni jijini Dar es Salaam na
bila ajizi akamsainisha mkataba wa miaka miwili, biashara ikawa imeisha.
Kwa maana hiyo mkataba wa Kaseja ukawa kama
umechanwa Jangwani, lakini mkataba wa Dida ukapigwa muhuri, sahihi na
dole gumba kijana akale chake akaondoka.
Simba imetangaza kumtema Kaseja na kwa sasa anahaha kusaka klabu mpya.
Bin Kleb aliliambia Mwanaspoti kuwa walifikiria
kwanza kumsajili Kaseja wakakutana na kukuna vichwa sana kabla ya kuamua
kuachana na kipa huyo ambaye ni nahodha wa Taifa Stars baada ya kupata
pia uamuzi wa Barthez.
“Tulianza kukusanya maoni kuhusiana na suala la
kipa, kuna wadau wa Yanga walisema tunaweza kumsajili Kaseja huku
wengine wakisema tuachane naye kwani aliwahi kudumu Yanga kwa msimu
mmoja tu pamoja na kusajiliwa kwa pesa nyingi,” alisema Bin Kleb.
“Kwa kifupi Barthez ndiye aliyepiga kura ya veto
kwa Dida na kusisitiza kuwa lazima asajiliwe kipa huyo ambaye aliwahi
kusota naye benchi katika klabu ya Simba huku Kaseja akitawala. Hakukuwa
na pingamizi zaidi ya kuanza mazungumzo naye Dida,” alisema.
Bin Kleb alisema pamoja na Dida kukumbwa na kashfa
ya rushwa iliyohusisha klabu ya Simba, msukumo mwingine walioupata ni
uamuzi wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) ambayo
ilimsafisha kipa huyo na wenzake watatu.
“Naomba wana Yanga wampe sapoti kubwa kama
wachezaji wengine, ambao waliwahi kuichezea Simba kwa kipindi fulani,”
alisema kiongozi huyo huku Dida akiomba sapoti ya wachezaji wenzake.
“Naomba mniamini kama ilivyokuwa kwa Kaseja ambaye
alicheza Yanga huku akiwa ametokea Simba ambako alikuwa amecheza zaidi
ya miaka saba. Naomba wanachama, wazee wa Yanga, wadau, mashabiki
waniamini kama ulivyofanya uongozi nitafanya kazi nzuri.”
Dida, Barthez na Kaseja wote wamekuwa kucheza pamoja Simba.
chanzo http://www.mwanaspoti.co.tz
chanzo http://www.mwanaspoti.co.tz
0 Weka maoni yako hapa:
Post a Comment
COMMENT HAPA