Dec 16, 2013

KUFUATIA KATIBA YA NZANZIBAR KUKINZANA NA KATIBA YA JAMHURI HII NDIO TAARIFA KUTOKA CUF KUHUSU MCHAKATO WA KATIBA MPYA

  PROFESA IBRAHIMU HARUNA LIPUMBA
THE CIVIC UNITED FRONT - CUF,
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI.

Imetolewa na Mwenyekiti wa CUF - Taifa, Prof. Ibrahim Haruna Lipumba.

Tanzania iko mbioni kukabiliwa na mgogoro mkubwa wa kikatiba. Tayari mabadiliko ya katiba ya Zanzibar yanakinzana na Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya 1977 lakini hayakinzani na sheria mama ambayo ni makubaliano ya Muungano (Articles of the Union).

Ili kukabiliana na changamoto ya kupata katiba mpya, kuwa na daftari safi la wapiga kura, kuunda Tume huru ya uchaguzi, na kuwa na uchaguzi ulio huru na wa haki 2015, Rais Kikwete baada ya kushauriana na wadau mbalimbali aunde serikali ya umoja wa kitaifa.

Serikali ya Umoja wa Kitaifa pia iimarishe uwajibikaji wa vyombo vya dola na viongozi, ishughulikie kadhia ya matumizi mabaya ya fedha za umma na iimarishe ukusanyaji wa mapato serikali ili miradi ya maendeleo kama vile ujenzi wa barabara na ufuaji wa umeme iweze kukamilishwa.

Mchakato wa Katiba mpya unapaswa kuwapa wananchi matumaini ya kujenga Tanzania mpya yenye haki sawa kwa wote na itakayojenga uchumi ambao hatua kwa hatua, utaleta neema kwa wananchi wote. Katiba itamke wazi rasilimali na maliasili ya nchi itatumiwa kwa manufaa ya wananchi wote na vizazi vijavyo. Uandikaji wa katiba mpya ni fursa adhimu ya kujenga muafaka wa kitaifa unaowapa imani na matumaini wananchi kuwa mfumo wa utawala, siasa na uchumi unaowekwa na katiba unalinda maslahi yao na utawaletea maendeleo wayatakayo.

Mchakato wa kupata katiba mpya kabla ya 2015 una vikwazo vingi. Ni wazi Katiba Mpya haiwezi kapatikani ifikapo tarehe 26 Aprili 2014 wakati tunasheherekea miaka 50 ya Muungano. Rasimu ya mwisho ya Tume ya Katiba itapatikana mwezi huu. Rais anawajibika kukamilisha uundaji wa Bunge la Katiba kwa kuteua wabunge 201 baada ya kupata mapendekezo toka wadau mbali mbali vikiwemo vyama vya siasa, vyama vya wafanyakazi, vyama vya wakulima, taasisi za dini na kadhalika. Itakuwa bahati kama Bunge la katiba litaweza kuanza shughuli zake katika ya kumi la mwisho la mwezi wa Januari.

Tume ya Jaji Warioba imefanya kazi kubwa ya kuratibu maoni na kuja na mapendekezo ya katiba mpya ambayo hayakushinikizwa na matakwa ya Chama tawala cha CCM. Mwanazuoni na mchambuzi wa mambo ya katiba na sheria Prof. Chris Maina Peter amediriki kuita Rasimu ya Katiba kuwa Mapinduzi ya kimya kimya. Tume imeonyesha ujasiri mkubwa na uhuru wake hasa ukizingatia pendekezo kuu la Rasimu ya Katiba ni mfumo wa serikali tatu (Sura ya sita ibara ya 57 – 66) ambao unakinzana na msimamo rasmi wa Chama tawala cha CCM na wosia wa hayati Mwalimu Nyerere kuhusu mfumo wa Muungano.

Rasimu ya Katiba ina mabadiliko makubwa ya msingi ikiwa ni pamoja na mfumo wa Muungano wa serikali tatu, kupunguza mambo ya muungano kutoka 22 na kuwa saba, kuruhusiwa mgombea binafsi, Rais kutangazwa kushinda akipata zaidi ya asilimia 50 ya kura zote zilizopigwa la sivyo uchaguzi urudiwe kwa wale wawili walio ongoza kwa kura, haki ya wananchi kumuondoa Mbunge wao madarakani, Ukomo wa vipindi vitatu vya mtu mmoja kuwa mbunge, Tume huru ya uchaguzi, Mawaziri kutokuwa wabunge, Spika kutokuwa mbunge, haki za watu wenye ulemavu, kupanuliwa kwa haki za binadamu, kuondolewa kwa viti maalum vya wanawake na badala yake kila jimbo kuwa na mbunge mwanamke na mbunge mwanaume,

Kuanzishwa kwa Mahakama ya Juu (Supreme Court), haki ya kumiliki mali na hifadhi ya mali haitahusu mali iliyothibitishwa kwamba haikupatikana kwa njia halali na mengine mengi.
Hata hivyo mambo mengi muhimu kama vile umilikaji wa ardhi, maliasili na rasilimali za nchi kutumiwa kwa manufaa ya wananchi wote, elimu, afya, mazingira ya kukuza uchumi unaoleta neema kwa wananchi wote, wajibu, uwezo na uhuru wa serikali za mitaa hayajaingizwa ndani ya katiba kikamilifu kwani rasimu ya katiba imeshughulikia mambo ya muungano. Hoja ya Tume ya Jaji Warioba ni kuwa mambo haya yataingizwa kikamilifu katika katiba ya washiriki wa Muungano – Tanzania Bara na Zanzibar.

Bila kuwepo kwa rasimu ya katiba ya Tanzani Bara na Marekebisho ya katiba ya Zanzibar isikinzane na Katiba ya Muungano, zoezi la kupata dira na mwongozo wa kusimamia utawala, uchumi na siasa za Watanzania haujakamilika. Walau Zanzibar wana katiba lakini Tanganyika haina katiba wala mchakato wa kuipata katiba hiyo haujaanza.

Isitoshe rasimu ya Katiba ya Muungano ina mapungufu makubwa na kuna mambo mengi kama vile mfumo wa Muungano, Mambo ya Muungano, Ukuu wa Katiba ya Muungano, Mapato ya kugharamia Muungano yanahitaji mjadala wa kina ili kufikia Muafaka.

Bunge la Katiba litakuwa na kazi kubwa ya kupata muafaka kuhusu mambo haya muhimu. Hata wakifikia muafaka na kupata katiba mpya, mapendekezo yaliyomo katika Rasimu ya Katiba yatahitaji mabadiliko makubwa ya kisheria na kitaasisi ili kuweza kuitekeleza katiba mpya. Kenya ilikamilisha katiba yake na kuipitisha kwenye kura ya maoni Agosti 2010. “Hata hivyo, mabadiliko mbali mbali ya kisheria na kitaasisi kwa ajili ya utekelezaji wa Katiba hiyo yalichukua zaidi ya miaka miwili na nusu hadi Uchaguzi Mkuu wa mwezi Machi, 2013.”

Wengi wetu tungependa zoezi la kupata katiba mpya likamilike kabla ya uchaguzi mkuu wa 2015. Hali halisi ni wazi zoezi hilo haliwezi kukamilika kwa ufanisi kabla ya 2015. Sheria ya mabadiliko ya katiba inaeleza kuwa ikiwa katiba mpya haikupitishwa kwenye kura ya maoni, katiba ya sasa itaendelea kutumika.

Mchakato wa kupata katiba mpya, maoni yaliyotolewa na wananchi na rasimu ya katiba inayotokana na maoni hayo imebainisha wazi Watanzania hawaitaki katiba ya sasa. Kufanya uchaguzi kwa kutumia katiba ya sasa na Tume ya Uchaguzi iliyopo hakutakubalika na wananchi na kunaweza kuwa chanzo cha mgogoro mkubwa wa kisiasa.

Kura ya maoni inakabiliwa na kikwazo kikubwa cha kutokuwepo kwa daftari la kudumu la wapiga kura lililoandikisha wapiga kura wote. Daftari la wapiga kura halijaboreshwa na kuandikisha wapiga kura wapya baada ya uchaguzi mkuu wa 2010.

Mwezi Februari Rais Kikwete alitangaza kuwa vitambulisho vya kitaifa ambavyo vinatumia alama ya mwili ndivyo vitakavyotumiwa kwa kupigia kura ya maoni na uchaguzi mkuu. Alieleza mamlaka ya vitambulisho vya taifa itashirikiana na Tume ya Uchaguzi katika utoaji wa vitambulisho vya kitaifa ambavyo pia vitakuwa vitambulisho vya kupigia kura.

Zoezi la kuwapa wananchi vitambulisho vya kitaifa linaenda taratibu sana. NIDA haijakamilisha kutoa vitambulisho hivyo hata kwa wilaya za Dar es Salaam. Kwa kasi hii ya uandikishaji na utoaji wa vitambulisho vya kitaifa, zoezi hili halitakamilika katika miaka miwili inayokuja. Itafika 2015 na wananchi wengi wenye umri wa miaka 18 watakuwa hawajapata vitambulisho vya taifa.

Vitambulisho vya NEC havikidhi mahitaji. Vitambulisho hivyo vinaghushiwa kwa urahisi sana. Wadau wengi hawana imani na daftari la NEC. Ni vyema vitambulisho vya NIDA vyenye alama za mwili ndivyo vitumiwe kama vitambulisho vya kupigia kura.

Kura ya maoni kuhusu katiba haiwezi kuendeshwa kwa ufanisi bila kuwa na daftari la wapiga kura linaloaminika. Kura ya maoni inabidi ipigwe na wananchi wa pande mbili za Muungano. Tume ya Uchaguzi ya Taifa inatumia Tume ya Zanzibar kuwa wakala na daftari la ZEC kubaini wapiga kura wa Zanzibar. Daftari la ZEC linawanyima wananchi wengi wa Zanzibar kuandikishwa kupiga kura kwa madai kuwa hawana vitambulisho vya ukaazi.

Tume ya Taifa itawajibika kuwaandikisha Wazanzibari hawa wapate haki ya kupiga kura ya maoni kuhusu katiba.
Ili kusimamia vizuri mchakato wa kupata katiba mpya na kuhakikisha kuwepo kwa maridhiano na mshikamano wa kitaifa katika kipindi hiki nyeti ninamshauri Rais Kikwete aunde serikali ya umoja wa kitaifa.

Jukumu kubwa la serikali hiyo iwe kukamilisha mchakato wa kupata katiba mpya, kuunda Tume Huru ya Uchaguzi, kuandikisha wananchi wote wanaostahili kupiga kura wapewe vitambulisho vinavyotumia alama ya mwili ili kuhakikisha uchaguzi wa 2015 unakuwa huru na wa haki.

Serikali ya umoja wa kitaifa pia iimarishe utendaji wa serikali, ipambane na ubadhirifu ulioainishwa na Mdhibiti na Mkaguzi wa Hesabu za Serikali na Kamati za Bunge, ianzae kujenga utamaduni wa uwajibikaji na kutumia vizuri fedha za umma kwa maendeleo ya wananchi.

Ibrahim Haruna Lipumba
Mwenyekiti,
Jumapili, 15 Disemba 2013.

0 Weka maoni yako hapa:

Post a Comment

COMMENT HAPA