Feb 21, 2014

VIONGOZI WANAPAMBANA KUONGEZANA POSHO, WANANCHI WANATESEKA NA UMASIKINI.,'' MTATIRO''



Masuala ya ajabu na aibu kama haya ya kuongezana posho wakati mamilioni ya watanzania wanakufa na njaa, maradhi, huduma mbovu na kukataa tamaa, hayakubaliki.

Wananchi masikini lazima waamke na kupinga kwa nguvu masuala haya. Kama ikitokea wananchi wakaandamana kupinga jambo hili ntawaunga mkono kwa asilimia mia moja.

Binafsi nitatimiza wajibu wangu bila woga, nitalipinga jambo hili hadharani ndani ya bunge, na nitakataa nyongeza ya posho. Nitafanya lile niwezalo.

Mtume Muhammad(SAW) aliwahi kusema, ukiona mtu anatenda maovu jaribu kuzuia, ukishindwa kemea na ukishindwa basi chukia jambo hilo.

Nimeanza mchakato wa kuwasiliana na wabunge wote wanaopinga ongezeko la posho, natambua watakuwa wachache lakini sauti zetu zitasikika, hata kama wengi wataka posho watatushinda, ukweli kuwa msimamo wetu utaiamsha jamii, hata kama tutachekwa, ukweli ni kuwa taifa linahitaji viongozi wathubutu na ambao haataona aibu kusema this is wrong hata kama watachekwa na kudhihakiwa.

Hivi sasa taifa letu limefikia mahali pabaya mno. Deni la taifa ni trilioni 27, hali ya uchumi ni mbovu, mishahara ya wafanyakazi ni kiduchu, watoto wanakufa kwa utapiamlo, wanawake wanajifungulia sakafuni, watoto wadogo wanakaa kwenye mavumbi ili wasome, maji safi na salama hakuna, barabara ni mbovu hazipitiki, wakulima hawana pembejeo, wazee wenye umri mkubwa na watoto hawana matibabu ya uhakika.

Pamoja na yote hayo, viongozi wanakutana na kuanzisha mjadala wa kuongezana posho. Posho ya shs laki tatu inatosha sana na nmesema inabakia. Mjadala wa kuongezana POSHO ni upuuzi na ninaupinga ndani na nje ya nafsi yangu, nitaupinga kwa maneno na vitendo.

Kuna wabunge wa chama kimoja cha upinzani walinifuata wakiwa kundi, wakaanza kunihoji na kunicheka, ati napigana vita ambayo Zitto Kabwe alishindwa, nikasikitika sana. Hoja zao ni kwamba hizo posho hata zikipingwa zitaliwa na CCM hivyo ni bora ziliwe na sisi. Mie nikawaambia CHANGE STARTS FROM YOU AND ME! Na nikawaambia SHAME IN YOU AND YOUR GRAVES!

Vyama vyetu vikianza kuiga tabia za CCM au kujaribu kuziishi, vitapoteza uhalali wa kuwakomboa watanzania. Vyama vyetu lazima viwe mstari wa mbele kupinga matumizi makubwa yasiyo muhimu.

Watu wachache wanaweza kufikiri hii ni vita ndogo. Nawaambia kuwa hii ni vita ya MAMILIONI YA WANANCHI dhidi ya VIONGOZI WACHACHE WALAFI ambao matumbo yao hayatosheki. Vita hii itakwisha kwa wananchi kuwaondoa madarakani viongozi WAFIKIRI KULA, WALAFI na WABADHIRIFU.

0 Weka maoni yako hapa:

Post a Comment

COMMENT HAPA