Mar 11, 2014

SOMA TAARIFA KUTOKA CUF KUHUSU ZANZIBA NA MJADARA WA KATIBA

THE CIVIC UNITED FRONT
(CUF- Chama Cha Wananchi)
Office of the Secretary General

Our Ref: CU/HQ/KR/HUM/181 Date: 11/03/2014


       TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI


Ukweli utaendelea kubaki ulimwenguni kwamba Zanzibar ni Nchi iliyokuwa huru tangu asili na zama, ambayo ikitegemea raslimali zake za ndani kwa kujiendesha katika nyanja zote za kimaisha.


Ukweli huu katu hauwezi kuondoshwa na uoni au uelewa finyu wa watu, ambao baadhi yao wanajiita wasomi, kwa sababu ya kuchunga utashi binafsi, maslahi, itikadi, ubabaishaji, upotoshaji wa makusudi na matakwa ya taasisi wanazozitumikia.


Si sahihi hata kidogo na pia ni upotofu uliodhahiri kudai ati Uchumi wa Zanzibar unategemea Bara na kwamba mchango wake katika Muungano ni sawa na hakuna au pia uwezo wake wa kulipa madeni ya mikopo ni shaka tupu.


Huo ni upotofu na upotoshaji wa makusudi unaolenga kuwababaisha wananchi, hasa wa Visiwa vya Unguja na Pemba, ambao sasa wanaelewa nini wanachokihitaji; ni azma pia ya kuwazuga Wajumbe wa Bunge Maalum la Katiba, hasa wale waliodhamiria kupigania Muungano wenye maslahi kwa pande zote za Jamhuri za Tanzania.


La msingi ni kwamba wasiibuke watu wakajaribu kuwalisha maneno au kuwapumbaza Wazanzibari waliokwishajifunza vyema na kuikubali Historia kubwa ya Dola yao Huru yenye utajiri na iliyoheshimika Duniani, ambayo hatimaye imefikia pabaya kwa kile ambacho hadi sasa wanahoji iwapo huo unaoitwa Muungano wa Mwaka 1964 ulikuja kwa azma ya kuinufaisha au kuidhoofisha Zanzibar.


Lazima ieleweke kwamba kinachojadiliwa hapa siyo haja ya kuwa au kutokuwa na Muungano, bali la msingi ni kuwepo fungamano lenye kuheshimu na kuthamini nafasi za kila muhusika, iwe Jamhuri Huru ya Tanganyika na pia Jamhuri Huru ya Zanzibar, zilizodhihiri pasi na ghilba wala jinamizi au azma mbaya zilizofichikana; na hapo ndipo waliposimama Wazanzibari waliowengi katika kuelekea Mabadiliko ya Katiba, na siyo ubabaishaji wa watu wanaojiita wasomi wa kuwaziba macho watu wa Nchi hii.


Hapa hoja ni jee Zanzibar ilimtegemea nani kabla ya kuungana na Tanganyika; au ilishindwa kwa kiasi gani kulipia Uwanachama wake wa Jumuiya mbali mbali za Kimataifa, mathalan Kiti Chake cha Umoja wa Mataifa na Jumuiya ya Madola; au ilidaiwa na nani deni lisilolipika?


Katika kuepusha uzandiki na pia kujaribu kurejesha heshima ya Nchi hii, ambayo kwa kiasi kikubwa ilipotelea ndani ya kile kinachopewa kila aina ya majina, mara kero za Muungano mara jinamizi mara kiini macho au vyenginevyo, Serikali za Awamu zote zilizopita za Uongozi wa Zanzibar ziliwahi kuwasilisha Waraka zilizojaa mapendekezo ya kujivua kutokana na pingu hizo za kudhoofisha.


Miongoni mwa mapendekezo hayo ni kuyaondoa Mambo yote yaliyowekwa kinyemela baadhi yao, katika hiyo inayodaiwa kuwa Orodha ya Mambo ya Muungano, ambayo ni pamoja na Mafuta na Gesi Asilia, Elimu ya Juu, Posta, Mawasiliano ya Simu, Kodi ya Mapato, Biashara 


ya Nje, Ushuru wa Bidhaa (Excise Duty), Usafiri wa Anga, Takwimu, Tafiti, Ushirikiano wa Kimataifa, Mambo ya Nje, Leseni za Viwanda, Polisi na Usalama.


Tena kwa azma njema, Waraka hizo zote kutoka Serikali ya Zanzibar ya Awamu tofauti, zilisisitiza mambo muhimu ya kuulinda Muungano, yakiwemo Masuala ya Muungano kulindwa kwa Misingi ya Katiba na Sheria badala ya ‘sumu’ ya siasa na maelewano (good will); Muungano kuwa na maeneo machache yanayoweza kusimamiwa na kutekelezwa kwa urahisi kisheria;


Muungano kuainisha wazi wazi washirika wake wakuu, mipaka na haki zao; Muungano kutoa fursa sawa za kiuchumi kwa pande zote mbili (Tanganyika na Zanzibar); na pia ulazima wa kuwa na 
Muungano unaoweza kuhimili mabadiliko ya kisiasa na kiuchumi.

Suala hapa ni jee ugumu ulikuwepo wapi wa kutekeleza mapendekezo hayo yaliyokuwa na azma njema ya kujenga


 Muungano wa dhati wenye heshima; au kilichosubiriwa ni hiki kisingizio cha sasa cha watu wanaojiita wasomi na ambao wangeliweza kuwa tegemeo la Taifa, wakidai ati Zanzibar haina uwezo wa kujitegemea au kulipa madeni; ni nini hicho kama si kupotoka au kupotosha kwa makusudi?

Kinachohitajika hapa siyo kuwasilisha tena data za namna ambavyo Zanzibar imekuwa ikidhoofika siku hadi siku kutokana na mfumo usiofaa au azma iliyofichikana ndani ya Muungano; Waswahili wanasema “mwenye macho haambiwi tazama”, na kwa msomi mwenye uoni hasa, ataamini namna Wazanzibari walivyodhoofika kwa kubebeshwa mazigo ya madeni na mikopo isiyokuwa na tija, tena ambayo sehemu kubwa inaangukia mikononi mwa mafisadi.


Chama cha Wananchi, CUF, na kama ilivyo kwa Wazanzibari wengi, au hata Watanzania waungwana kwa ujumla, hakiamini na katu hakitoamini kwamba ati “Serikali Mbili haziepukiki”.


Chama cha Wananchi, CUF, kinatoa wito kwa waungwana na wapenda haki, sambamba na Wajumbe wote wa Bunge la Katiba, kusimama juu ya hoja ya kudai Katiba yenye maslahi na Muungano wenye heshima, inayozingatia maoni, mapendekezo na mahitaji ya umma wote, pasi na kukubali kubabaishwa au kupotoshwa kwamba ati Zanzibar haina uwezo wa kujitegemea.


HAKI SAWA KWA WOTE
……………………………………………
Salim Bimani,


Mkurugenzi wa H/B, Habari, Uenezi na Mahusiano na Umma

Headquaters: P.O.Box 3637, Zanzibar, Tanzania. Tel.: 024 22 37446 Fax.: 024 22 37445


Main Office: PO. Box 10979, Dar-es-Salaam, Tanzania. Tel. 022 861009 Fax.: 022 861010

0 Weka maoni yako hapa:

Post a Comment

COMMENT HAPA