Mar 7, 2014

Simba yalimwa faini kwa kuendekeza vitendo vinavyoashiria ushirikina



Bodi ya Ligi Kuu Tanzania (TPLB) imeipiga faini ya jumla ya sh. milioni moja klabu ya Simba kutokana na makosa mbalimbali ikiwemo vitendo vinavyoashiria ushirikina uwanjani.

Simba ilifanya vitendo hivyo katika mechi yake dhidi ya Mbeya City ambapo imepigwa faini ya sh. 500,000. Pia imepigwa faini nyingine ya sh. 500,000 kwa makocha wake Loga, Selemani Matola na Idd Pazi kuingia uwanjani na kumzonga mwamuzi kwenye mechi hiyo.

Naye mshambuliaji wa Simba, Amisi Tambwe amepigwa faini ya sh. 500,000 kwa kushangilia bao alilofunga kwenye mechi hiyo kwa kuonesha ishara ya matusi kwa kidole.

Mbeya City imepigwa faini ya sh. 300,000 kwa washabiki wake kuingia uwanjani kwenye mechi dhidi ya Kagera Sugar iliyochezwa mjini Bukoba. Klabu za Yanga na Coastal Union zimepigwa faini ya sh. 500,000 kila moja kwa washabiki wao kurusha chupa za maji uwanjani wakati timu hizo zilipopambana jijini Tanga.
Kiungo wa Mtibwa Sugar, Shabani Nditi amepigwa faini ya sh. 500,000 kwa kumpiga mchezaji wa Simba, wakati Salvatory Ntebe pia wa Mtibwa Sugar amepigwa faini ya sh. 500,000 kwa kumtukana refa kwenye mechi dhidi ya Mbeya City.

Pia mshambuliaji wa Mtibwa Sugar, Musa Mgosi amepigwa faini ya sh. 500,000 kwa kosa la kupiga uwanjani kwenye mechi dhidi ya Ashanti United ambapo vilevile atakosa mechi tatu za ligi. Coastal Union imepigwa faini ya sh. 500,000 kwa washabiki wake kumrushia chupa za maji kipa wa Mbeya City.
Nayo JKT Ruvu imepigwa faini ya sh. 300,000 kwa kuchelewa kufika uwanjani kwenye mechi dhidi ya Simba iliyochezwa Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Vilevile wamiliki wa Uwanja wa Mkwakwani jijini Tanga wameandikiwa barua ya kufanya marekebisho ya vyumba vya wachezaji, kwa vile havina hewa ya kutosha.

Kwa upande wa Ligi Daraja la Kwanza (FDL) klabu zilizopigwa faini kutokana na makosa mbalimbali ni Friends Rangers (sh. 200,000), Lipuli (sh. 200,000), Majimaji (sh. 400,000), Polisi Morogoro (sh. 400,000) na Transit Camp (sh. 200,000).

Kocha Msaidizi wa Polisi Morogoro, John Tamba atapelekwa kwenye Kamati ya Maadili kutokana na vitendo visivyo vya kimaadili katika mechi dhidi ya Burkina Faso.

Kiongozi wa Lipuli, Hamis Kiemba na wachezaji Boniface Sawaka, George Enock na Green Paul watapelekwa katika Kamati ya Nidhamu kutokana na utovu wa nidhamu waliofanya kwenye mechi dhidi ya Kimondo.

Naye mchezaji Sangalau Nyamoka wa JKT Kanembwa aliyelalamikiwa uhalali wake na Polisi Tabora suala lake linapelekwa Kamati ya Nidhamu.

chanzo na http://www.timesfm.co.tz/blog

0 Weka maoni yako hapa:

Post a Comment

COMMENT HAPA