KATIBU Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Dk.
Willibrod Slaa amefufua upya tuhuma za ufisadi ndani ya Benki Kuu ya
Tanzania (BoT) kupitia Akaunti ya Madeni ya Nje (EPA), huku akiwalaumu
Rais Jakaya Kikwete na Rais Mstaafu, Benjamin Mkapa kuwa chanzo cha
kutochukuliwa hatua mafisadi.
Dk. Slaa mbali ya kuwashutumu
Kikwete na Mkapa, alielekeza shutuma pia kwa Gavana wa Benki Kuu ya
Tanzania (BoT), Beno Ndulu, akisema kuwa chanzo kikubwa cha Watanzania
wengi kuwa masikini wa kutupwa, huku mafisadi wakiachwa wakimiliki
uchumi mkubwa na kujenga majumba nje ya nchi.
Katibu
Mkuu huyo wa Chadema ambaye alikua mgombea Urais wa chama hicho mwaka
2010, ameshutumu vyombo vya dola na Mkurugenzi wa Mashtaka nchini
(DPP), Dk. Elieza Feleshi akivituhumu kwa kushindwa kumkamata na
kumfikisha mahakamani, Mbunge wa Bariadi Magharibi, Adrew Chenge,
aliyehusishwa na tuhuma za rushwa iliyotokana na ununuzi wa rada nchini
Uingereza hasa baada ya kukutwa na mamilioni ya fedha katika benki za
nje ya nchi.
Dk. Slaa ametoa kauli hiyo Jumapili Machi 17, 2012,
alipozungumza kwenye kongamano la wanafunzi wa Chuo cha Mtakatifu
Augustine (SAUT), lililofanyika katika maeneo chuo hicho Nyegezi,
Mwanza.
Akizungumza kwa kujiamini, Dk. Slaa amesema Rais Kikwete
na Serikali yake ameshindwa kuwasaidia wananchi wake katika kudhibiti
mifumuko ya bei, pamoja na kushuka kwa uchumi wa nchi.
“Kwa sasa
nchi ipo pabaya sana, uchumi wa nchi umeshuka sana duniani. Ukiangalia
Tanzania tulianza pamoja kiuchumi na nchi za Singapore na
Malaysia….lakini kwa sasa nchi hizi zimetuacha mbali kiuchumi.
“Tanzania kwa sasa inashikilia nafasi ya tatu kwa umasikini duniani. Na
ndiyo inayoongoza kwa wananchi wake kuwa masikini katika nchi za Kusini
mwa Jangwa la Sahara (SADC). Tunataka mabadiliko, na mwaka 2015 Chadema
imejipanga vema kushika dola,” alisema Dk. Slaa.
Alisema, Rais
Kikwete ameshindwa kutekeleza ahadi ya Serikali yake ya kutoa fedha za
kutosha kwa kila mwanafunzi na kwamba fedha nyingi zimekuwa zikiishia
kwenye safari za Rais. Alisema hadi sasa amefikisha safari 325 tangu
achaguliwe mwaka 2005.
Mbali na hayo, Dk. Slaa alimtaka Rais Kikwete
kujitokeza hadharani kueleza fedha za EPA zilizopelekwa, kwani hakuna
akaunti ya fedha hizo iliyofunguliwa na kuwekwa kwa fedha hizo, wala
Mdhibiti na Mkaguzi wa Hesabu za Serikali (CAG), na Bunge hawajui
zilipo.
“Rais
alilitangazia taifa kwamba mafisadi wa EPA wamerudisha fedha
walizokwapua. Fedha hizi hakuna akaunti zilipofunguliwa, CAG hajui na
hata Bunge na wabunge wake hawajui hizo fedha zipo wapi,” alihoji.
Katika hatua nyingine, aliishutumu Serikali ya Rais Kikwete kuwadanganya
Watanzania juu ya mradi wa Kilimo Kwanza, akisema mradi huo umeasisiwa
na watu fulani kwa maslahi yao, na alimuomba kiongozi huyo wa nchi
ajitokeze aueleze umma iwapo Serikali yake ilikaa kuandaa mradi huo na
nani waliokaa na tarehe gani.
Hata hivyo, alimtuhumu Rais Kikwete
kutumia Baraza la Mawaziri kuligeuza kama sehemu ya ‘ulaji wa siasa’,
kwani alisharuhusu Gavana BoT, Beno Ndulu kushiriki vikao vya Baraza
hilo, wakati Gavana huyo haruhusiwi kuingia Baraza la Mawaziri kwa
mujibu wa sheria.
Alisema kinachofanyika hivi sasa ni danganya toto
juu ya uchumi wa nchi, na kwamba takwimu zinazotolewa na benki Kuu hapa
nchini si sahihi, alihoji kwamba: “Kama Gavana wa benki kuu anaingia
kwenye baraza la mawaziri, anaenda kufanya nini kama si kupika takwimu
za kiuchumi?. Takwimu za uchumi kukua kwa asilimia 6 zinatoka wapi?”.
Hata
hivyo, alisema amekamata barua ya Rais Kikwete aliyoituma kwa Shirika
la Fedha Duniani (IMF), alilishukuru kwa kuisaidia Tanzania kifedha, na
alisema hali hiyo inadhihirisha kwamba Tanzania ilivyoshamiri kwa
kuombaomba.
Kuhusu Mkapa.
Dk. Slaa
alimtuhumu waziwazi Rais Mstaafu, Benjamin Mkapa kwa kile alichokiita
kwamba kaharibu mfumo mzima wa uchumi wa nchi, kutokana na sera zake za
ubinafsishaji ambapo baadaye alilazimika kujimilikisha mgodi wa mkaa ya
mawe wa Kiwira.
“Mkapa
alibinsfsisha mashirika, makampuni na baadaye aliamua kujimilikisha
Kiwira. Huyu Mkapa ni mmoja wa viongozi walioiharibu sana nchi yetu
hii,” alisema Katibu Mkuu huyo wa Chadema taifa.
Hata hivyo,
alisema Rais huyo mstaafu pamoja na Rais Kikwete wamevunja rekodi
duniani kwa kuruhusu makampuni ya kuchimba madini nchini kujenga viwanja
vya ndege katika maeneo ya migodi kwa ajili ya kusafirisha madini,
jambo alilosema kwamba ni kutoa njia ya kuruhusu kuibiwa kirahisi kwa
madini.
“Tembea dunia nzima huwezi kuona nchi inayoruhusu
mwekezaji kujenga viwanja vya ndege katika maeneo ya migodi yao. Kwa
hapa Tanzania wenye migodi wameruhusiwa kujenga viwanja vya ndege ili
wachukuwe kirahisi madini yetu na kuwaacha hoi Watanzania, hivi ni nchi
gani hii?” alisema Dk. Slaa.
Gavana Ndulu
Slaa alisema Gavana wa Benki Kuu ameshindwa kuwashughulikia watu wanaotengeneza noti bandia, na kwamba
Gavana
huyo alishakabidhiwa mtuhumiwa na mashine ya kutengeneza noti bandia,
lakini hadi sasa ameshindwa kulifanyia kazi suala hilo.
Kwa mujibu
wa Dk. Slaa, Gavana Ndulu na vyombo vya dola wakiwemo Makamanda wa
Polisi nchini na Mkuu wa jeshi hilo (IGP), wameonekana dhahiri kuruhusu
biashara ya kutengenezwa kwa noti bandia, hivyo kuharibu kabisa uchumi
wa taifa.
Kuhusu Chenge
Dk. Slaa alihoji
sababu ya Serikali ya CCM kushindwa kumkamata na kufikisha mahakamani,
Andrew Chenge kwa tuhuma nzito zinazomkabili za ufisadi wa mamilioni ya
fedha zilizokutwa katika akaunti huko nchini Uswisi.
“Chenge
alikutwa anamiliki fedha nyingi sana huko nje ya nchi. Ushahidi
ulishawasilishwa kwa DPP, lakini hadi sasa hakuna hatua zozote
zilizochukuliwa dhidi ya Chenge,” alisema Dk. Slaa huku akishangiliwa
kwa nguvu zote.
Habari hii imeandikwa na Sitta Tumma – Mwanza.
wa jamii forams
BONDE FC NI MABINGWA WAPYA WA BEIRA YOUTH CUP 2012
-
Timu ya Bonde fc jana iliibuka kuwa mabingwa wapya wa BEIRA YOUTH CUP
2012 ubingwa huo umepatikana baada ya kuibuka na ushindi wa gili 5-4 dhidi
ya New B...
12 years ago
0 Weka maoni yako hapa:
Post a Comment
COMMENT HAPA