Kuna kanuni ya msingi inagombaniwa katika mgomo huu wa madaktari ulioanza tena baada ya kusitishwa kwa muda wa wiki tatu. Kwamba je wananchi wa Tanzania watatawaliwa jinsi ili watawala wanataka au jinsi wanavyotaka wao kutawaliwa? Kwamba, serikali inaweza kufanya lolote na kutenda lolote bila kuulizwa, kuhojiwa na kupingwa na wananchi wake? Je, wananchi wanalazimika kukubali na kupiga magoti ya kuitikia pale “serikali” inaposema jambo moja lifanyike hata kama jambo hilo linaonekana linapingana na maslahi ya wananchi hao? Ndugu zangu, tunachoshuhudia sasa hivi ni wananchi wa Tanzania wakisimama kudai watawaliwe ipasavyo!
Mgomo huu wa madaktari ni miongoni mwa migomu ya ajabu kabisa kutokea duniani! Toka mwanzo tulionesha kuwa ni mgomo ambao ungeweza kuepukika mapema sana kwa watawala kuonesha heshima, nidhamu na kujali madai ya madaktari badala ya kuyapuuzia na kuwakebehi madaktari kana kwamba Tanzania ni koloni la mafisadi! Madaktari walichohitaji kuona ni uongozi wenye kuonesha heshima, kujali, na kuyapa uzito madai ya madaktari lakini badala yake walichopewa ni dharau na kejeli na sasa wamepewa hadi ubabe!
Madaktari wetu wamegoma kama chaguo la mwisho!
Sote tunafahamu kuwa madaktari wetu wanafanya kazi katika mazingira magumu sana na vile vile tunafahamu kabisa kuwa hata katika mazingira haya magumu wanajitahidi sana kuhudumia wananchi na kuponya na kuokoa maisha ya watu wetu wengi huku wakati huo huo na wao wenyewe wakijijenga kimaisha wakati mwingine kwa kufanya vibarua vingine vitatu! Nilipoandika huko nyuma niliwahi kudokeza jinsi ya baadhi ya madaktari ambao waliamua kabisa kuachana na kazi ya kutibu na kwenda kwenye biashara zao wakitambua kuwa hata kama ni kujitolea nako kuna mipaka!
Kwa muda mrefu madaktari wamekuwa wakifanya kazi katika hali ngumu kweli – bila ya shaka siyo wao peke yao – lakini kwa namna ya pekee madaktari kazi yao inahusiana na uzima na kifo. Kwa muda huu mrefu wao madaktari na wauguzi wamejaribu kuishi na kufanya kazi katika mazingira haya bila kulalamika sana. Na tunafahamu jinsi gani tumepoteza madaktari wengi kwenda nje ya nchi kutafuta maisha bora zaidi na hawa wachache waliopo bado wanafanya kazi katika mojawapo ya uwiano mkubwa kabisa wa daktari na wagonjwa. Inakisiwa katika Tanzania daktari mmoja anahudumia watu 30,000-50,000 kutegemeana na mahali.
Inapofika madaktari kugoma ujue kuwa hali imekuwa ngumu sana na kwa kweli ni lazima tuoneshe shukrani ya pekee na heshima ya pekee kwao kwa kukubali na kufanya kazi katika mazingira magumu hivi na hata kukubali kurudi kazini Ikumbukwe kuwa mgomo huu ulianza mwanzoni kabisa kwa sababu ya watawala kupuuzia madai ya madaktari.
Kwa muda mrefu – kusema ukweli kuanzia 2006 – serikali imekuwa ikitoa ahadi ya “tunashughulikia” kila suala la maslahi na madai ya madaktari yalipokuwa yanatolewa. Hili si kwa madaktari tu limekuwa kweli hata kwa walimu na wafanyakazi wa kada nyingine. Baada ya kuvurugika kwa mgomo wa 2006 ambao mimi niliupinga kwa sababu moja kubwa – serikali mpya ndio ilikuwa imeingia madarakani – watawala wetu walifikiria kuwa sasa wamepata uhuru wa kutawala wapendavyo.
Na kweli kwa karibu miaka sita wametawala wapendavyo; bila mashinikizo bila kusukumwa. Kwa muda wote huo tumewaacha watawala na kuamua kufanya watakalo. Upinzani pekee ambao wameupata umetoka kwenye vyama vya siasa zaidi na siyo kwa wafanyakazi. Hili ndilo kosa kubwa zaidi la utawala wetu wa leo. Kwamba, wanafikiria upinzani pekee nchini ni wa kisiasa na ndio maana hata hivi sasa baadhi yao hawaamini kabisa kuwa mgomo huu umetokana na sababu zake zenyewe na unasukumwa na wahusika wenyewe na siyo wanasiasa.
Watawale wapendavyo au watutawale ipasavyo
Tatizo la mfumo wowote wa utawala wa kifisadi (a corrupt political regime) ni kuwa unafikia mahali unaamini kuwa unaweza kutawala upendavyo. Ndivyo ilivyokuwa kwa utawala lwa Hosni Mubarak, ndivyo ilivyokuwa kwa Bashir Al-Assad, ndivyo ilivyokuwa kwa Milosevic, ndivyo ilivyokuwa kwa kina Augustino Pinochet na watawala wengine wa mrengo wa kifisadi.
Msingi wa kutawala “wapendavyo” ni imani kuwa wao ndio walioumbwa na waliopendelewa na mbingu kutawala milele na kuwa hakuna mtu mwenye haki wala sababu ya kuwapinga, kuwahoji, au kuwakatalia. Katika utawala wa namna hiyo watawala wanataka watumie fedha za umma wapendavyo bila kuulizwa, walindane bila kugombezwa na wakandamize wanyonge bila kukatazwa!
Kimsini utawala wa kifisadi kama ulivyo utawala wa kiimla hujenga ndani yake mbegu za maamgamizi yake. Tunachoshuhudia sasa hivi nchini ni kuanza kuchipuka kwa mbegu hiyo kwani kwa miaka kadhaa sasa ufisadi umepandwa, umemwagiliwa maji, umekua na kuzaa matunda. Sasa wamekuja watu wanataka kuukata na hapa patakuwa pachungu. Patakuwa pachungu kwa sababu wapo wanaonufaika na utawala wa kifisadi. Wapo wanaokula na kusaza matunda ya ufisadi. Maslahi ya hawa ni kuona kuwa utawala uliopo unaacha “upumue”.
Wakati wowote linatokea kundi linalotoa changamoto kwa utawala uliopo na kuufanya utawala huo uonekane katika udhaifu wake watetezi watajitokeza. Watajitokeza kujaribu kutumia kila mbinu kuonesha kuwa utawala uliopo umefanya yote mazuri na unahitaji “muda kidogo” ili “kushughulikia” matatizo yanayolalamikiwa. Naam! Watetezi hawa wataita watu majina, wataanzisha ugomvi na watafanya hivyo wengine wakiamini kuwa wakitetea vizuri zaidi labda na wao watakuja kusogezwa karibu zaidi katika meza ya ufisadi – kama watakaa kwenye viti au pembeni wao haiwajalishi sana!
Madaktari wetu wameonesha kile ambacho kilikuwa kinakuja nacho ni kukataa kutawaliwa wapendavyo watawala. Unajua watawala hawapendi kubughudhiwa kabisa wanapotawala wapendavyo. Hawataki kuulizwa wala kukosolewa na wanapokoselewa wanaweka masharti ya jinsi gani wakosolewe na kuulizwa! Hawataki kuoneshwa mapungufu na udhaifu wao na wakioneshwa huja juu na kudai – tena kwa haraka sana – “kwani mazuri yetu hamuyaoni!?”
Madaktari wamekataa kuona nchi inatawaliwa wapendavyo watawala. Tukumbuke mojawapo ya vitu vilivyotuudhi wengi ni kuwa wakati serikali inasema haina fedha za kuwalipa madaktari maslahi bora wabunge waliamua kujiongezea posho nono ati kwa sababu “maisha ni magumu kule Dodoma”. Hili lilikuwa tusi na limebakia kuwa tusi kwani inaonekana baadhi yao hadi hivi sasa hawaoni kabisa tatizo la wao kudai zaidi huku serikali yao ikiwanyima wengine kile wanachodai zaidi! Hawa watawala wanaona kama wameonewa na wengine kuona kuwa yeyote anayewapinga hawatakii mema!
Mgomo huu unahusu kanuni kubwa zaidi
Ndugu zangu, mgomo huu unahusiana na kanuni kubwa zaidi. Na hakuna kosa kubwa ambalo serikali itafanya kama kuamua kuleta madaktari wa kigeni ili kuwaonesha madaktari wetu kuwa hawana thamani. Naamini hili litakuwa ni tusi la mwisho na msumari wa mwisho kusababisha mgomo mkubwa wafanyakazi nchini! Mgomo huu haukupaswa kabisa kufika hapa; Kikwete ameamua kupuuzia na akiliachilia hili mikononi mwa Waziri Mkuu mtu ambaye hajaunda baraza la mawaziri wala hana uwezo wa kuliwajibisha.
Yote haya yamefika kwa sababu Kikwete haamini kuwa alipaswa –mara moja – kuwafukuza kazi watendaji wote wakuu wanne wa wizara hiyo; kwanza kwa sababu ya kuhusika kwao kwa kusababisha mgomo na pili kutokana na kashfa mbalimbali ambazo zimetokea kwenye wizara hiyo. Madaktari wamekuwa wakilalamika kwa muda mrefu kuhusu matatizo hayo; kuna barua nyingi tu kwenda kwa Katibu Mkuu kiongozi, na Ikulu ambazo zimeanisha migongano kati ya viongozi hao wakuu. Lakini Kikwete kwa kuogopa kuonekana serikali yake ina matatizo ameendelea kuwakumbatia viongozi hawa wabovu na walioshindwa.
Matokeo yake ni mgomo huu ambao kwa kweli kabisa unastahili kuungwa mkono na Watanzania. Watawala inawapasa kutambua kuwa hawawezi kuendelea kutawala wapendavyo. Haiwezekani polisi waendelee kuua wananchi bila kujali (with impunity) halafu wananchi wakija kucharuka siku moja serikali ione inaonewa! Kuna mistari haipaswi kuvukwa na kwenye hili la madaktari na mawaziri kuna mstari umevukwa mstari ambao hauwezi kurudishwa isipokuwa kwa kujiuzulu au kufukuzwa kazi kwa uongozi wa juu wa wizara hiyo pamoja na kufanyia mabadiliko makubwa ya kimuundo.
Katika sakata hili madaktari wamechukua uamuzi mgumu zaidi kuliko maamuzi ya sekta nyingine yoyote ya kutaka viongozi wazembe wawajibishwe ili kwamba kiongozi atakayeshika uongozi katika wizara hiyo ajue kabisa kuwa siyo wizara ya kuchezea, siyo wizara ya kuzemba na siyo wizara ya kuongozwa kwa ubabe, kejeli, dharau na uzandiki. Wanaweza kuchezea sehemu nyingine lakini linapokuja suala la afya za wananchi wetu hakuna wa kuonewa huruma.
Ni matumaini yangu kuwa serikali itaamua mara moja kuwaachisha kazi watu hawa wanne ili kuokoa maisha ya maelfu ya Watanzania na kurudisha heshima katika fani za tiba nchini na hatimaye kuanza kwa mabadiliko (reform) ya sekta hiyo ili hatimaye kuboresha afya nchini.
Endapo mgomo huu utaendelea hata kwa siku moja zaidi mwenye kosa siyo Waziri Mkuu Pinda – kwani hajaunda baraza la mawaziri na hana uwezo wa kumfukuza waziri yeyote – bali itakuwa ni Rais mwenyewe ambaye ndiye amewawekea kinga viongozi hawa. Endapo mgomo huu utaendelea kwa siku nyingi ya ziada na kusababisha madhara zaidi wananchi wanayo haki kabisa ya kuanza kuandamana kutaka Rais mwenyewe awajibike – hata kujiuzulu – kwa sababu kama hadi hivi sasa hajaona uzito wa tukio haiwezekani kumfanya aone huko mbeleni.
Watanzania wanastahili kutawaliwa ipasavyo na siyo kutawaliwa wapendavyo watawala. Hili ndilo kiini hasa cha mgomo wa madaktari. Ni kujitambua sisi kama watawaliwa tunataka tutawaliwe vipi. Je watu wawili wanaweza kubebwa na kuonewa huruma kuliko watu elfu? Je, kuhofia kutengeneza mazoea ya wananchi kushinikiza serikali kunatosha kufanya watawala wahofie kuamua sasa? Madaktari wamesema tunastahili kutawaliwa ipasavyo kwa gharama yoyote ile. Hili ni somo gumu sana kulifuzu.
chanzo na fikira pevu jamii forums

0 Weka maoni yako hapa:
Post a Comment
COMMENT HAPA