Jul 13, 2013

Nurdin: Twite alitumwa kumuua Nsajigwa Yanga

 

KIRAKA Nurdin Bakari aliyeachwa na Yanga baada ya mkataba wake kumalizika amefichua siri baada ya kutamka kwamba Mbuyu Twite alisajiliwa na viongozi wa Yanga ili aje kumaliza kipaji cha Shadrack Nsajigwa.
Twite alisajiliwa na Yanga akiwa njiani kutua Simba ambapo mchezaji huyo amekuwa akipendelea sana kucheza beki ya kati lakini imemilikiwa na Kelvin Yondani na Nadir Cannavaro.
Twite alikabidhiwa namba ya Nsajigwa ambaye Yanga imemuonyesha mkono wa kwaheri kwa madai kwamba ameshuka kiwango na tayari Lipuli ya Iringa imemsajili kama kocha.
Nurdin alisema; “Hivi unajua Mbuyu (Twite) ni viongozi waliamua tu kumsajili bila kulishirikisha benchi la ufundi. Ndiyo maana unamwona anachezeshwa beki wa kulia badala ya beki wa kati,”alisema Nurdin aliyewahi kuichezea Simba na AFC ya Arusha.
Lakini viongozi wa Kamati ya Usajili wa Yanga wamesisitiza kwamba mchezaji huyo alikuwa chaguo la kocha Ernest Brandts ambaye amewahi kufanya naye kazi akiwa APR ya Rwanda.
Nurdin alisema baada ya Nsajigwa kutakiwa na Simba msimu wa 2011 na baadaye dili ikashindika alianza kuwekewa mizengwe: “Baada ya Nsajigwa kumalizana na viongozi wa Yanga, tulidhani yameisha. Fitna zilianza na kumletea mabeki wengi kwa lengo la kumshinikiza kocha awe anamweka benchi,” alisema Nurdin na kuongeza kuwa beki wa kwanza aliyesajili kwa nia ya kumpoteza Nsajigwa alikuwa Taita (Godfrey) kutoka Kagera Sugar.
“Lakini alishindwa kumweka benchi, baada ya kuona malengo yao hayajatimia walimletea tena beki mwingine Juma (Abdul) kutoka Mtibwa Sugar na baadaye akaja Mbuyu lengo lao likatimia.”
Nurdin pia amepinga vikali kutemwa kwa straika Hamis Kiiza na kipa Juma Kaseja.
Akizungumza na Mwanaspoti jijini Dar es Salaam katika mahojiano maalumu nyumbani kwake Tabata, Nurdin alisema: “Unajua hawa viongozi wa Simba na Yanga wana chuki zao tu binafsi, mimi bado naamini Kaseja (Juma) ndiye kipa bora kwa Tanzania. Pia, ana nafasi ya kuendelea kuichezea Simba na kwa mafanikio makubwa.”
“Kama unataka kuchukiwa na viongozi wa timu hizi mbili dai chako, kwa jinsi namfahamu Kaseja ni mtu ambaye hataki kuburuzwa. Ni mtu ambaye yupo mstari wa mbele kudai haki yake. Nafikiri ndiyo yaliyomkuta kama ilivyo kwangu.”
“Kaseja bado atabaki kuwa kipa bora na hakuna anaweza kupinga hilo. Sidhani kama atakosa timu ya kuichezea. Ni mtu anayelijenga vizuri jina lake kisoka. Kwa upande wa Kiiza, nafikiri anastahili kudai kuongezwa mshahara na dau la kusaini mkataba mpya anafanya kazi na inayoonekana. Kwanini wanashindwa kuthamini mchango wake na kumpa kile anachostahili,” alihoji.
“Mbona Haruna (Niyonzima) alitaka na kuboreshewa masilahi yake, iweje inashindikana kwa Kiiza mpiganaji, kuna tatizo?  Viongozi wa timu hizi mbili wanachangia kwa kiasi kikubwa kuharibu maendeleo ya soka katika klabu hizi mbili kubwa. Hawana malengo endelevu,”alisisitiza mchezaji huyo mwenye rasta.

chanzo na gazeti la mwanaspot

0 Weka maoni yako hapa:

Post a Comment

COMMENT HAPA